read

Aya 40 – 45: Sema Niambieni

Maana

Sema: niambieni, kama ikiwafikia adhabu ya Mwenyezi Mungu au ikiwafikia ile Saa, je, mtamuomba asiyekuwa Mwenyezi Mungu ikiwa nyinyi ni wakweli?

Mwenyezi Mungu (s.w.t) anamwamrisha Mtume wake awaambie washirikina: Niambieni kama ikiwafikia adhabu, kama ile iliyoteremshiwa wale waliokadhibisha Mitume yao; au yakiwafikia maumivu makubwa ya mauti na vitisho vya Kiyama, je katika hali hii, mtayaita masanamu na mizimu mliyokuwa mkiabudu na kudai kuwa itawaondolea fazaa na adhabu?

Makusudio ya Aya hii ni kuwa Makafiri kesho watajivua na yale waliyokuwa wakiyaabudu na kukimbilia kwa Mwenyezi Mungu baada ya kuwabainikia kuwa hakuna hila wala nguvu ila kwa msaada wake Yeye tu peke yake bila ya kuwa na mshirika.

Mwenyezi Mungu Na Maumbile

Bali yeye tu ndiye mtakayemuomba.

Baada ya kuwauliza kuwa mtamwomba asiyekuwa Mwenyezi Mungu siku ya vituko vikubwa, amelithibithisha jibu kwa kusema kwake: (Bali yeye tu ndiye mtakayemuomba).

Hilo ndilo jibu linaloaminiwa na kujibiwa na umbile ambalo Mwenyezi Mungu amewaumbia watu, katika dunia na akhera. Na sio maana ya umbile la Mwenyezi Mungu kuwa mtu atamtambua Muumba hivi hivi tu bila ya dalili. Hapana! Kama ni hivo basi kusingelitokea mtu yeyote wa kumkanusha Mwenyezi Mungu.

Hakika maana ya umbile hili ni kuwa Mwenyezi Mungu amempa mtu maandalizi ya kufahamu dalili zinazofahamisha kuweko Mwenyezi Mungu, na dalili hizi haepukani nazo kwa hali yoyote. Anayekufuru anakufuru kwa kuzembea na kupuuza kwa kuepuka kuchunguza dalili na hoja. Kwa hiyo ndipo akastahiki adhabu kwa kupuuza huko.

Kwani hakuna tofauti kabisa katika mtazamo wa akili, baina ya mwenye kuacha kufanya amali, kwa makusudi, na huku anajua; na yule mwenye kuiacha haki akafuta batili kwa kutojua lakini ana uwezo wa kujua na kupambanua uongufu na upotevu, lakini akaacha kwa kupuuza na kudharau.

Inawezekana maandalizi hayo yakajificha nyuma ya pazia la kufuata maelezo na matamanio; sawa na linavyojificha jua nyuma ya mawingu, ikafikiriwa kwa yule asiyejua sitara hizo kuwa yeye amemkana Mwenyezi Mungu kwa kukosa dalili na dalili iko katika dhati yake na maumbile yale ambayo amemuumbia Mwenyezi Mungu. Na siku ya Kiyama sitara hii iliyozuka itaondoka na kudhihiri hakika iliyo wazi wala hakutasalia nafasi ya shaka na ukanusho.

Atawaondolea mnayomuomba akitaka.

Yaani nyinyi washirikina mtaacha siku ya Kiyama, kuomba masanamu mliyokuwa mkiyaabudu duniani na mtamwomba Mwenyezi Mungu peke yake, wakati hakika ya kila jambo itakapodhihiri.

Na mtawasahau mnaowashirikisha.

Yaani nyinyi washirikina siku ya Kiyama mtaacha kuyaomba masanamu mliyokuwa mkiyaabudu duniani na kumwomba Mwenyezi Mungu peke yake wakati itakapodhihiri hakika ya kila kitu.

Kwa hakika tulipeleka (Mitume) kwa umma zilizokuwa kabla yako; kisha tukawatia katika shida na madhara ili wapate kunyenyekea.

Hakika Mwenyezi Mungu (s.w.t) hawaadhibu waja wake ila baada ya kuwapelekea mjumbe atakayewaongoza kwenye njia ya uongofu. Kama hawakuongoka anawapa fursa ili wajirudi wenyewe, na kuwatia katika mtihani kwa mabalaa ili wanyenyekee na watubie, lakini wao waling’ang’ania maasi; kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Aya inayofuatia hii.

Basi mbona wasinyenyekee ilipowafikia adhabu yetu? Lakini nyoyo zao zilikuwa ngumu na shetani akawapambia waliyokuwa wakiyafanya.

Mwenyezi Mungu, ambaye zimetukuka sifa zake, anasema kuwa wao hawakunyenyekea ilipowafikia shida duniani wala hawakumdhalilikia Mwenyezi Mungu kwa kuacha inadi yao, bali waling’ang’ania ukafiri, na shetani akawa nyuma yao akiwapambia upotevu na ufisadi.

Aya hii inafahamisha kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) anamkubali kila anayekimbilia kwake, hata kama kukimbia kwake ni kwa vikwazo vya shida na balaa. Hivi ndivyo alivyo aliye mkarimu na adhimu. Hamnyimi mwenye kuomba wala hamkatishi tamaa, kwa namna yoyote lengo na msukumo wake utakavyokuwa.

Basi waliposahau yale waliyokumbushwa tuliwafungulia milango ya kila kitu mpaka walipofurahia yale waliyopewa tuliwakamata kwa ghafla; na mara wakawa wenye kukata tamaa.

Aliwaonya kwanza kwa kauli kupitia kwa Mitume. Pili, kwa vitendo alipowapa mtihani kwa shida na madhara.

Waliponga’ang’ania ukafiri na inadi aliwafungulia milango ya riziki na raha, ili kuwasimamishia hoja na kuwavuta kidogo kidogo kwa neema baada ya mtihani wa nakama.

Walipofurahia raha na kuzidi kiburi na wala wasielekee kwenye uongofu, basi Mwenyezi Mungu aliwaadhibu kwa namna wasiyofikiria, wakajuta kwa kuzembea na wakakata tamaa ya kuokoka.

Kwa ufupi ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) mara nyingine aliwapa dhiki na mara nyingine furaha kwa kupenda waongoke; sawa na afanyavyo mzazi kumhurumia mwanawe akitaka atengenekewe.
Lakini wala hawakushukuru raha wala kuwaidhika na balaa. Wakang’olewa wote asibakie yeyote katika wao, ili wapate funzo watakaokuja baada yao.

Ikakatwa mizizi ya watu waliodhulumu; na sifa njema ni za Mwenyezi Mungu Mola wa viumbe vyote.

Kwa sababu ya kuwaneemesha kwake waumin na kuwanusuru na watu wa kufuru na ufisadi.

قُلْ أَرَأَيْتُمْ إِنْ أَخَذَ اللَّهُ سَمْعَكُمْ وَأَبْصَارَكُمْ وَخَتَمَ عَلَىٰ قُلُوبِكُمْ مَنْ إِلَٰهٌ غَيْرُ اللَّهِ يَأْتِيكُمْ بِهِ ۗ انْظُرْ كَيْفَ نُصَرِّفُ الْآيَاتِ ثُمَّ هُمْ يَصْدِفُونَ {46}

Sema: Mwaonaje kama Mwenyezi Mungu akichukua kusikia kwenu na kuona kwenu na akaziziba nyoyo zenu, ni nani Mungu mwingine isipokuwa Mwenyezi Mungu awezaye kuwaletea tena? Tazama jinsi tunavyozikariri ishara, kisha wao wanapuuza.

قُلْ أَرَأَيْتَكُمْ إِنْ أَتَاكُمْ عَذَابُ اللَّهِ بَغْتَةً أَوْ جَهْرَةً هَلْ يُهْلَكُ إِلَّا الْقَوْمُ الظَّالِمُونَ {47}

Sema: Mwaonaje ikiwafikia adhabu ya Mwenyezi Mungu kwa ghafla au kwa dhahiri nani wataangamizwa isipokuwa watu waliodhulumu?

وَمَا نُرْسِلُ الْمُرْسَلِينَ إِلَّا مُبَشِّرِينَ وَمُنْذِرِينَ ۖ فَمَنْ آمَنَ وَأَصْلَحَ فَلَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ {48}

Na hatutumi Mitume ila niwabashiri na waonyaji. Na wenye kuamini na wakafanya wema, basi haitakuwa hofu juu yao wala hawatahuzunika.

وَالَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا يَمَسُّهُمُ الْعَذَابُ بِمَا كَانُوا يَفْسُقُونَ {49}

Na wale waliokadhibisha ishara zetu itawagusa adhabu kwa sababu ya walivyokuwa mafasiki.