read

Aya 93-94: Kumzulia Uwongo Mwenyezi Mungu

Maana

Na ni nani dhalimu mkubwa kuliko yule amzuliaye uwongo Mwenyezi Mungu.

Kumzulia Mwenyezi Mungu uwongo ni kumtengenezea mambo ambayo hayana chimbuko katika Qur’an wala Hadith au katika misingi ya akili. Na hayo yanakuwa kwa mambo yafuatayo:

• Kuhalalisha aliyoyaharamisha Mwenyezi Mungu au kuharamisha aliyoyahalalisha.

• Kumsingizia Mwenyezi Mungu, kwa makusudi, yale asiyokuwa nayo au kumfanyia washirika au kuwa ana watoto na mabinti.

• Kudai Utume kwa asiyekuwa Mtume. Hilo ameliashiria Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwa kauli yake: Au mwenye kusema: Nimeletewa Wahyi; na hali hakuletewa Wahyi wowote. Jumla hii inaungana na ile ya Amzuliaye Mwenyezi Mungu uwongo.’ Ni katika mlango wa kuunganisha mahsusi kwenye ujumla.

Na yule asemaye: Nitateremsha kama alivyoteremsha Mwenyezi Mungu.Yaani mlaanifu huyu anadai kuwa ana uwezo wa kutunga Kitab kitakachofanana na Qur’an katika utukufu wake. Imesekana kuwa mtu huyo ni Abdullah bin Sa’d bin Abu Sarh. Wengine wamesema ni Nadhr bin Harith.

Kwa ufupi ni kwamba kila mwenye kumnasibishia Mwenyezi Mungu kitu chochote bila ya kutegemea kauli ya Mwenyezi Mungu na ya Mtume au misingi ya akili basi huyo ni mzushi, mwongo mkubwa na anayestahiki shutuma na adhabu.

Na lau ungewaona madhalimu wanavyokuwa katika mahangaiko ya mauti na Malaika wamewanyooshea mikono.

Mahangaiko ya mauti ni maumivu ya kukata roho.

Wafasiri wametofautiana katika makusudio ya kunyoosha mikono ya Malaika. Je, makusudio ni kunyoosha kiuhakika wakati mtu anapokata roho, au ni fumbo tu la kufananisha vituko vya mauti?

Sisi hatuoni haja yoyote ya mzozo huu. Kwa sababu akili haikatai kuweko Malaika wala kuwa na mikono wanaoinyoosha au ndimi za kuzungumzia. Kwani Wahyi umelieleza hilo, kwa hiyo ni wajibu kuamini. Msingi huu wanautegemea Maulama wote Waislamu katika kuthibitisha itikadi na sharia.

Zitoeni roho zenu; leo mtalipwa adhabu ifedheheshayo kwa sababu ya yale mliyokuwa mkisema juu ya Mwenyezi Mungu yasiyokuwa ya haki, na mlikuwa mkizifanyia kiburi ishara zake.

Haya yote ni maneno ya Malaika wakiwaambia wazushi wakati wa kufa. Nayo ni lawama na shutuma kwa uzushi wao na kukana kwao haki. Kuna Hadith isemayo: “Anayekufa kiyama chake kimesimama.” Kwa sababu hii wamesema baadhi ya wajuzi kwamba mtu ana viyama viwili, kidogo ambacho ni mauti na kikubwa, ufufuo.

Shutuma za Malaika kwa anayemzulia Mwenyezi Mungu uwongo, katika Kiyama kidogo, ni onyo la vituko vya Kiyama kikubwa atakavyokumbana navyo. Imam Ali anasema: “Kifo kwa Mumin ni kama kuvua nguo chafu na kufungua minyororo na kuvaa kanzu ya kifahari na kushukia kwenye maliwazo. Ama kwa kafiri, ni kama kuvua kanzu ya kifahari na kuvaa gwanda chafu, na kutoka kwenye maliwazo kwenda kwenye vitisho na adhabu kubwa.”

Na hakika mtatujia wapweke kama tulivyowaumba kwanza.

Yaani mwanadamu atakutana na Mola wake kesho, kama alivyotoka tumboni mwa mamake hana chochote.

Afadhali angeliingia ardhini kama alivyotoka – haulizi wala haulizwi, lakini atarudi akiwa ni mwenye kuulizwa. Alhamdulilah, mwenye kuuliza ni mwadilifu hamdhulumu yeyote na atamfanyia mtu vile alivyowafanyia watu alipokuwa katika uhai wake wa kwanza. Ikiwa ni kheri basi itakuwa kheri na ikiwa ni shari basi ni shari.

Wametofautiana wanavyuoni kuhusu kufufuliwa kuwa je, ni kwa roho tu, au ni kwa roho na kiwiliwili pamoja. Dhahiri ya kauli yake Mwenyezi Mungu: kama tulivyowaumba kwanza, inafahamisha kufufuliwa kwa roho na kiwiliwili kwa sababu vyote viwili vimeumbwa pamoja.

كَمَا بَدَأْنَا أَوَّلَ خَلْقٍ نُعِيدُهُ ۚ وَعْدًا عَلَيْنَا ۚ إِنَّا كُنَّا فَاعِلِينَ {104}

“Kama tulivyoanza umbo la awali tutalirudisha tena. Ni ahadi iliyo juu yetu, hakika sisi ni watendaji.” (21:104)

Na mmeacha nyuma yenu yale tuliyowapa.

Mtu atarudi ardhini akiwa ameacha watu wake, marafiki mali na ufalme.
Na hatuwaoni waombezi wenu pamoja nanyi ambao mlidai ni washirika (wa Mwenyezi Mungu) kwenu.

Kama vile masanamu, nyota na mengineyo mliyokuwa mkiyaabudu na kuwatawalisha wafisadi na wapotevu.

Kwa hakika yamekatika (mahusiano) baina yenu.

Yaani hamna mawasiliano yoyote ya duniani.

Na yamewapotea mliyokuwa mkidai katikamadaiyauwongokwawale mliowafikiria kuwa ni
washirika au waombezi mbele yake, na yamepotea matumaini yenu baada ya kufichuka uhakika; na mwema ni yule atakayefuzu kupata radhi za Mwenyezi Mungu na maghufira yake.

إِنَّ اللَّهَ فَالِقُ الْحَبِّ وَالنَّوَىٰ ۖ يُخْرِجُ الْحَيَّ مِنَ الْمَيِّتِ وَمُخْرِجُ الْمَيِّتِ مِنَ الْحَيِّ ۚ ذَٰلِكُمُ اللَّهُ ۖ فَأَنَّىٰ تُؤْفَكُونَ {95}

Hakika Mwenyezi Mungu ndiye mpasuaji mbegu na kokwa. Humtoa aliye hai katika maiti na ni mtoaji wa maiti katika aliye hai huyo ndiye Mwenyezi Mungu basi mnageuzwa wapi?

فَالِقُ الْإِصْبَاحِ وَجَعَلَ اللَّيْلَ سَكَنًا وَالشَّمْسَ وَالْقَمَرَ حُسْبَانًا ۚ ذَٰلِكَ تَقْدِيرُ الْعَزِيزِ الْعَلِيمِ {96}

Ndiye mpambazuaji wa asubuhi; ameufanya usiku kuwa mapumziko na utulivu, na jua na mwezi (kwenda) kwa hesabu. Hayo ndiyo makadirio ya Mweye nguvu, Mjuzi.

وَهُوَ الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ النُّجُومَ لِتَهْتَدُوا بِهَا فِي ظُلُمَاتِ الْبَرِّ وَالْبَحْرِ ۗ قَدْ فَصَّلْنَا الْآيَاتِ لِقَوْمٍ يَعْلَمُونَ {97}

Na yeye ndiye aliyewafanyia nyota ili muongoke kwazo katika viza vya bara na baharini. Hakika tumezifafanua ishara kwa watu wanaojua.

وَهُوَ الَّذِي أَنْشَأَكُمْ مِنْ نَفْسٍ وَاحِدَةٍ فَمُسْتَقَرٌّ وَمُسْتَوْدَعٌ ۗ قَدْ فَصَّلْنَا الْآيَاتِ لِقَوْمٍ يَفْقَهُونَ {98}

Na Yeye ndiye aliyewaanzisha nyinyi kutokana na nafsi moja. Pako mahali pa kutulia na pa kupita njia. Hakika tumezifafanua ishara kwa watu wanaofahamu.

وَهُوَ الَّذِي أَنْزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَخْرَجْنَا بِهِ نَبَاتَ كُلِّ شَيْءٍ فَأَخْرَجْنَا مِنْهُ خَضِرًا نُخْرِجُ مِنْهُ حَبًّا مُتَرَاكِبًا وَمِنَ النَّخْلِ مِنْ طَلْعِهَا قِنْوَانٌ دَانِيَةٌ وَجَنَّاتٍ مِنْ أَعْنَابٍ وَالزَّيْتُونَ وَالرُّمَّانَ مُشْتَبِهًا وَغَيْرَ مُتَشَابِهٍ ۗ انْظُرُوا إِلَىٰ ثَمَرِهِ إِذَا أَثْمَرَ وَيَنْعِهِ ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكُمْ لَآيَاتٍ لِقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ {99}

Naye ndiye aliyeteremsha maji kutoka mbinguni na kwayo tunatoa mimimea ya kila kitu. Kisha tukatoa kutokana nayo kijani. Tukatoa ndani yake punje zilizopandana. Na katika mitende yakatoka kwenye makole yake mashada yaliyo karibu. Na bustani za miza bibu na mizaituni na miko-mamanga. Yanayofanana na yasiyofanana. Angalieni matunda yake yanapozaa na kuiva kwake. Hakika katika hayo kuna ishara kwa watu wanaoamini.