read

Aya 25 – 26: Nyoyo Zao Zina Pazia

Maana

Na miongoni mwao wako wanaokusikiliza, na tumezitia pazia nyoyo zao wasije kuyafahamu na mna uziwi masikioni mwao.

Mwenyezi Mungu anamwambia Mtume wake katika Aya hii, baada ya kumwamrisha kuwambia hoja zinazowasimamia. Maana ni kuwa kundi katika hawa wapinzani wanamsikiliza Mtume, nao wanasoma Qur’an, lakini wao hawanufaiki nayo wala hawanufaiki na dalili na hoja nyinginezo.

Kwa sababu wao tangu mwanzo waling’anga’ania inadi na kiburi, mpaka kung’angania huko kukapofua akili zao zisione haki na kukatia uziwi kwenye masikio yao.

Unaweza kuuliza: Dhahiri ya Aya inaonyesha kuwa Mwenyezi Mungu ndiye aliyezipofua nyoyo zao akatia uziwi masikio yao. Kwa nini basi wastahiki shutuma na adhabu na hali ya kuwa wamelazimishwa hawana hiyari?

Jibu: Kwa vile nyoyo za wapinzani hazikuitambua Qur’an na kunufaika nayo, na masikio yao hayakuisikiliza kwa usikizi wa kufahamu na kuzingatia, imesihi kusema, kimajazi, kwamba nyoyo zao zimefumba na katika masikio yao mna uziwi.

Na kwa vile Mwenyezi Mungu (s.w.t) ndiye aliyeumba nyoyo na masikio, imesihi kunasibisha upofu na uziwi kwake yeye kimajazi vilevile.

Ama kulingana na hali halisi ilivyo ni kuwa washirikina ndio wenye jukumu. Kwa sababu wao waliipinga haki kwa kutaka wenyewe. Yamekwishatangulia maelezo ya hayo katika Juz. 1(2:7)

Ni vizuri kuashiria kuwa Aya hii inafahamisha kwa uwazi kwamba Uislam hauna mfano na chochote kwa ulivyo; bali kwa natija zake na athari zake. Kwa hiyo usikizi na uoni ni utekelezaji wa akili, na akili ndiyo inayopanga matendo. Ikiwa kitendo hakikufanyika, basi usikizi na uoni utakuwa hauna maana yoyote; kwa dhahiri au si kwa dhahiri.

Kwa maneno mengine katika Uislamu, mambo yote ya ndani na ya nje, na ya ardhini na ya angani ni nyenzo za manufaa ya watu katika kupangilia maisha yao na kutatua matatizo yao. Imam Ali (as) anasema: “Anadai kwamba yeye anamtaraji Mwenyezi Mungu.

Amesema uwongo kwa nini matarajio yake hayaonekani katika vitendo vyake, na kila mwenye kutarajia (Mwenyezi Mungu) hujulikana matarajio yake katika vitendo vyake.”

Na wakiona kila Ishara hawaiamini

Muhammad (saw) alifichua hakika ya waongo katika watu wapendao mali na jaha. Wakataharuki na kuhisi hatari ya masilahi yao wakakimbilia kukadhibisha na wakasema kuhusu Aya za Mwenyezi Mungu kuwa ni ngano za watu wa kale, na hali wao wana yakini kwamba Qur’an hii ni mwongozo, lakini wakawa wanaitia njia za shaka shaka na makosa ili wawatumie watu kutokana na upotevu wao na ubatilifu; sawa na wanavyofanya leo watu wa serikali ovu na kanuni za dhuluma.

Na wanamkatazia na wenyewe wanajitenga naye.

Dhamiri ya neno nao inawarudia wale waliopinga haki kwa kupupia masilahi yao. Dhamiri ya wanamkatazia na kujiweka mbali naye, inamrudia Muhammad (saw).

Waongo walikataza watu wasimfuate Muhammad (saw) na wakampinga, vilevile walijaribu kumtesa na wakakusanya majeshi kwa ajili ya kumpiga vita. Si kwa lolote ila ni kwamba yeye amefichua mabaya yao.

Na hawaangamizi ila nafsi zao na hawatambui.

Walitaka kuufanyia vitimbi Uislamu na Mtume wake, balaa ikawafikia wao, walipoangamia baadhi yao siku ya Badr wengine wakajisalimisha wakiwa madhalili na wanyonge siku ya kutekwa Makka. Huu ndio mwisho wa kila mwenye kuzama na kung’ang’ania dhuluma na inadi.

وَلَوْ تَرَىٰ إِذْ وُقِفُوا عَلَى النَّارِ فَقَالُوا يَا لَيْتَنَا نُرَدُّ وَلَا نُكَذِّبَ بِآيَاتِ رَبِّنَا وَنَكُونَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ {27}

Na ungeliona watakapoonyeshwa moto wakawa wanasema. Laiti tungerudishwa (duniani) wala hatutakadhibisha ishara za Mola wetu na tutakuwa katika wanaoamini.

بَلْ بَدَا لَهُمْ مَا كَانُوا يُخْفُونَ مِنْ قَبْلُ ۖ وَلَوْ رُدُّوا لَعَادُوا لِمَا نُهُوا عَنْهُ وَإِنَّهُمْ لَكَاذِبُونَ {28}

Bali yamewadhihirikia waliyokuwa wakiyaficha zamani. Na kama wangalirudishwa, bila shaka wangeyarudia yale waliyokatazwa na hakika wao ni waongo.

وَقَالُوا إِنْ هِيَ إِلَّا حَيَاتُنَا الدُّنْيَا وَمَا نَحْنُ بِمَبْعُوثِينَ {29}

Na kusema: Hakuna kingine ila maisha yetu ya dunia, wala sisi hatutafufuliwa.

وَلَوْ تَرَىٰ إِذْ وُقِفُوا عَلَىٰ رَبِّهِمْ ۚ قَالَ أَلَيْسَ هَٰذَا بِالْحَقِّ ۚ قَالُوا بَلَىٰ وَرَبِّنَا ۚ قَالَ فَذُوقُوا الْعَذَابَ بِمَا كُنْتُمْ تَكْفُرُونَ {30}

Na ungeliona watakaposimamishwa mbele ya Mola wao, Akasema: Je, si kweli haya? Watasema: Kwa nini? Tunaapa kwa Mola wetu. Atasema: Basi onjeni adhabu kwa sababu ya yale mliyokuwa mkiyakataa.

قَدْ خَسِرَ الَّذِينَ كَذَّبُوا بِلِقَاءِ اللَّهِ ۖ حَتَّىٰ إِذَا جَاءَتْهُمُ السَّاعَةُ بَغْتَةً قَالُوا يَا حَسْرَتَنَا عَلَىٰ مَا فَرَّطْنَا فِيهَا وَهُمْ يَحْمِلُونَ أَوْزَارَهُمْ عَلَىٰ ظُهُورِهِمْ ۚ أَلَا سَاءَ مَا يَزِرُونَ {31}

Hakika wameshahasirika wale waliokadhibisha kukutana na Mwenyezi Mungu, na wamefuzu wale waliomwamini, mpaka itakapowajia ghafla saa (Kiyama) watasema: Oo! Majuto yetu juu ya yale tuliyoyapuuza! Nao watabeba mizigo yao migongoni mwao. Angalieni! Ni mabaya mno wanayoyabeba.

وَمَا الْحَيَاةُ الدُّنْيَا إِلَّا لَعِبٌ وَلَهْوٌ ۖ وَلَلدَّارُ الْآخِرَةُ خَيْرٌ لِلَّذِينَ يَتَّقُونَ ۗ أَفَلَا تَعْقِلُونَ {32}

Na maisha ya dunia si kitu ila mchezo na upuzi. Na hakika nyumba ya akhera ni bora zaidi kwa wenye takua. Basi je hamtii akili?