Aya 33 – 37: Tunajua Kuwa Yanakuhuzunisha
Maana
Hakika tunajua kwamba yanakuhuzunisha yale wanayoyasema.
Msemo unaelekezwa kwa Mtume (s.a.w.). Dhamir ya ‘wanayoyasema’ inawarudia wale waliomkadhibisha Mtume (saw).
Ama yale wanayoyasema bali waliyasema hasa, ni yale yaliyoashiriwa na Mwenyezi Mungu (s.w.t):
ثُمَّ تَوَلَّوْا عَنْهُ وَقَالُوا مُعَلَّمٌ مَجْنُونٌ {14}
قَالَ الْكَافِرُونَ إِنَّ هَٰذَا لَسَاحِرٌ مُبِينٌ {2}
Na mengineyo.
Basi hakika hao hawakukadhibishi wewe, lakini madhalimu wanakataa ishara za Mwenyezi Mungu.
Kila mwenye kumpiga vita mwenye haki, basi ameipiga vita haki yenyewe, na kila mwenye kumdharau Mtume kwa kuwa yeye anachukua risala ya aliyemtuma, basi atakuwa amemdharau yule aliyemtuma na sio Mtume mwenyewe.
Washirikina wa Makka walikuwa wakimwita Muhammad (saw) mkweli mwaminifu, kabla ya Utume. Alipowaletea risala ya Mwenyezi Mungu na kuwasimamishia hoja, walimpiga vita na wakamwita mwendawazimu, mchawi nk.
Kwa hiyo kumkadhibisha kwao huku na hali hii, ni kukadhibisha risala ya Mwenyezi Mungu na hoja zake. Hakuna linalofahamisha hilo kwa dalili zaidi ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Hakika wale wanaokubai, kwa hakika wanambai Mwenyezi Mungu; mkono wa Mwenyezi Mungu uko juu ya mikono yao” (48:10)
Na hakika walikadhibishwa Mitume kabla yako, wakavumilia juu ya kukadhibishwa na kuudhiwa, mpaka ikawafikia nusura yetu.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) anamwambia Mtume wake ikiwa watakukadhibisha, basi wamekadhibishwa Mitume kabla yako na wakaudhiwa katika kufikisha risala yake, wakavumilia juu ya maudhi mpaka ikawajia nusura. Kwa hiyo nawe vumilia kama walivyovumilia; na Mwenyezi Mungu atakunusuru kama alivyowanusuru.
Huu ndio mzunguko wa maisha – mvutano baina ya kheri na shari na haki na batili. Ni muhali kwa mpigania haki asipate maudhi kutoka katika maadui wa haki. Vilevile haki haiwezi kushinda ila wapatikane watakaoi- nusuru wavumilivu katika jihadi ya haki na wainunue kwa nafsi zao, watu wao na mali zao.
Ni desturi ya Mwenyezi Mungu, wala huwezi kupata mabadiliko katika desturi ya Mwenyezi Mungu. Hii ndio maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
Na hakuna wa kubadilisha maneno ya Mwenyezi Mungu.
Wala sijui wakati ambao wabatilifu wamekuwa na nguvu kuliko wakati huu tunaoishi. Wameweka vituo vya kijeshi kila mahali, vituo vya kuharibu, silaha kali za kumaliza watu na kubomoa. Wanatawala nyenzo za wananchi wadhaifu, mabenki, magazeti, uchapishaji na usambazaji. Mpaka yule mtu aliye mwaminifu mwenye ikhlasi anajikuta ametupwa hawezi kutoa makala huru au kutangaza haki kupitia kwenye Idhaa. Lakini mhaini, popote atakapoelekea atapata mapokezi na kutukuzwa.1
Na bila shaka zimekujia baadhi ya habari za Mitume hao.
Yaani tumekusimulia kabla yale yaliyowapata Mitume kutokana na watu wao na jinsi walivyovumilia katika kukadhibishwa na maudhi, na kwamba mwisho ushindi ulikuwa wao.
Na desturi hii itakupitia wewe, kama iliyowapita wao, wala hakuna mwenye kubadilisha maneno ya Mwenyezi Mungu.
Na ikiwa ni makubwa kwako huku kukataa kwao, basi kama unaweza kutafuta njia ya chini kwa chini katika ardhi au ngazi kwendea mbinguni na kuwaletea ishara.
Aya hii ni mfano wa kauli yake Mwenyezi Mungu kumwambia Mtume wake Mtukufu:
فَلَا تَذْهَبْ نَفْسُكَ عَلَيْهِمْ حَسَرَاتٍ ۚ إِنَّ اللَّهَ عَلِيمٌ بِمَا يَصْنَعُونَ {8}
Aya zote hizi mbili zinatoa picha jinsi Mtume (saw) alivyokuwa akipata jakamoyo na uchungu kutokanana upinzani wa washirikina kwa mwito wake. Yaliyompata Mtume kutoka kwa watu wake ni yale yanayoondoa upole wa mpole. Lakini yeye akavumilia na kuwa na matumaini; wala hakuwaapiza bali aliwaombea, akisema: “Ewe Mola wangu! Wasamehe watu wangu, hakika wao hawajui.”
Pamoja na hayo yote alikuwa akihisi uchungu kwa kufuru zao. Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia kwa Aya hii, ili kumpoza na kumwon- dolea matumaini na aachane nao; kisha angoje kidogo, aone vile utakavyokuwa mwisho wa wakadhibishaji.
Na kama Mwenyezi Mungu angelitaka, bila shaka angeliwakusanya kwenye uongofu.
Razi anasema kuwa: “Hii inafahamisha kuwa yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu hataki makafiri waamini, bali anataka kuwabakisha kwenye ukafiri.
Lakini hii itakuwa ni dhuluma hasa, na Mwenyezi Mungu hawadhulumu waja. Usahihi wa maana ya jumla hii, ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) hataki kumlazimisha yeyote katika kumwamini, bali anamwachia hiyari yake baada ya kumsimamishia hoja kwa dalili na ubainifu. Lau angelitaka waja wake waamini kwa kusema ‘kuwa ikawa’, basi asingelikufuru yeyote katika wao. Lakini hekima yake Mwenyezi Mungu Mtukufu ilita- ka ajiingize katika mambo ya watu kama mwamrishaji na mwenye kutoa nasaha, si kama Muumba mwenye nguvu.
Umetangulia ufafanuzi katika Juz. 1 (2:26)
Basi usiwe miongoni mwa wajinga.
Atakuwaje Mtume Mtukufu miongoni mwa wajinga na hulka zake ni hulka za Qur’an?
Msemo huu umefaa kuelekezwa kwa mtukufu wa viumbe, kwa vile unato- ka kwa Muumba wa viumbe na sio kwa kwa aliye kama yeye.
Wanaokubali ni wale tu wanaosikia. Na wafu Mwenyezi Mungu atawafufua kisha watarejeshwa kwake.
Aya hii ni mfano wa Aya isemayo:
إِنَّكَ لَا تُسْمِعُ الْمَوْتَىٰ وَلَا تُسْمِعُ الصُّمَّ الدُّعَاءَ إِذَا وَلَّوْا مُدْبِرِينَ {80}
Maana ni kuwa: Ewe Muhammad! Wale unaopupia waonyeke hawakusikii kwa kufahamu na kuzingatia. Kwa sababu kupenda dunia kumewafanya kama wafu, na wafu haitakikani kuwaambia chochote; bali wanaachwa na mambo yao mpaka siku ya kiyama, watakapoiona adhabu ambayo hawataweza kuikimbia.
Na husema: Kwa nini hakuteremshiwa ishara kutoka kwa Mola wake?
Utauliza vipi wanasema hivi na hali Mwenyezi Mungu amemteremshia Muhammad (s.a.w.) ishara na hoja kadhaa na ubainifu.
Jibu: Makusudio ya ishara hapa ni muujiza ule walioutaka wao kuwa ni sharti la wao kumwamini Muhammad (saw); hawakusudii muujiza unaomkinaisha mwenye kuitafuta haki. Lau wangeliutaka huo wasingelisema hivyo.
Sema: Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye uweza wa kuteremsha ishara yoyote, ile wanayotaka, lakini yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu haiteremshi kwa kuitikia matakwa na hawaa zao; isipokuwa anateremsha miujiza kulingana na inavyopitisha hekima Yake.
Lakini wengi wao hawajui, kuwa anateremsha miujiza kulingana na hekima Yake na sio hawa za watu.
وَمَا مِنْ دَابَّةٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا طَائِرٍ يَطِيرُ بِجَنَاحَيْهِ إِلَّا أُمَمٌ أَمْثَالُكُمْ ۚ مَا فَرَّطْنَا فِي الْكِتَابِ مِنْ شَيْءٍ ۚ ثُمَّ إِلَىٰ رَبِّهِمْ يُحْشَرُونَ {38}
وَالَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا صُمٌّ وَبُكْمٌ فِي الظُّلُمَاتِ ۗ مَنْ يَشَإِ اللَّهُ يُضْلِلْهُ وَمَنْ يَشَأْ يَجْعَلْهُ عَلَىٰ صِرَاطٍ مُسْتَقِيمٍ {39}
- 1. Kumbuka wakati huo anaouzngumzia mwandishi ni 1967. Je, hivi sasa hali ikoje? – Mtarjumu