read

Aya 103: Lau Wangeamini

Maelezo:

Baada ya Mwenyezi Mungu kuyaorodhesha maasi ya Mayahudi na kampeni zao mbaya dhidi ya Muhammad (s.a.w.), amesema kuwa ukafiri wao huu na upinzani wao hautawafaa kitu.

Lau wangelimwamini Muhammad, kama ilivyowaamrisha Tawrat yao, wangelistarehe na kupata daraja ya juu kwa Mwenyezi Mungu.

Amirul Mumini anasema: “Hakika kumcha Mungu ni ngome yenye nguvu na uovu ni ngome dhalili, haiwakingi watu wake wala haimhifadhi mwenye kuikimbilia.

Fahamuni kuwa kumcha Mungu (takuwa) kunavunja uti wa mgongo wa makosa na hupatikana malengo kwa yakini”.

Uchawi Na Hukumu Yake

Mafaqihi wa Kishia wamezungumzia sana kuhusu uchawi, na wamerefusha maneno katika kuelezea maana yake, mafungu yake, yanayowezekana na yasiyowezekana. Pia wamezungumzia kuhusu kufundisha, kujifundisha na kuutumia.

Uchawi uliozungumziwa na Qur’an ni namna fulani ya udanganyifu na hadaa, kwa kuufanya uwongo uwe haki. Mwenyezi Mungu anasema: ...Tahamaki kamba zao na fimbo zao zikaonekana mbele yake (Musa) zinakwenda mbio kwa uchawi wao. (20:66) “...Hawakuwa wenye kumdhuru yeyote kwa hayo ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu (2:102)

ImamSadiq(a.s.)amesemakwambauchawiukonamnanyingi;Kama vile wepesi na haraka na kufanya hila, kwa sababu wenye hila wamegeuza uzima kuwa ugonjwa na maana kuwa hila.

Ama mambo ya kuandika, kuzungua na kutumia azima au kutabana na mengin-eyo ambayo yamesemekana kuwa yana athari, kama kufungwa mume wakati wa ndoa kiasi cha kushindwa kumwingilia mke. Vile vile mambo ya kuzidisha mapenzi, kutia chuki kati ya watu wawili na kuwatumia malaika na mashetani katika kupiga ramli na kutopoa, yote hayo, Shahidi wa pili ameyazungumzia katika Masalik mlango wa biashara akisema kuwa: “Wanavyuoni wengi wa Kishia wanaitakidi kwamba ni mambo ya kuwazia na dhana zisizokuwa na msingi wowote; na baadhi yao wanaona kuwa ni matukio ya kweli. Na yeye ni miongoni mwa wasemao kuwa ni hakika.

Bukhari amepokea katika Sahih yake J-4, mlango wa kisa cha Iblis na Askari wake, kwamba “Mtume alirogwa mpaka akawa anaonekana kama anafanya kitu na wala hakifanyi”. Lakini hayo ameyakanusha mmoja wa Maimamu wa Kihanafi katika kitabu Ahkamul-Qur’an J-1; Uk. 55 chapa ya mwaka 1347 A.H. Vile vile Sheikh Muhammad Abduh amekanusha katika kufasiri Sura ya Falaq.

Sisi tuko pamoja na wale wanaouona uchawi kuwa hauna msingi wowote. Imam Sadiq anasema: Uchawi ni wenye kushindwa kabisa kugeuza aliyoumba Mwenyezi Mungu “...Lau mchawi angelikuwa na uwezo angelijizuwia asizeeke na pia angelijikiinga na maafa na magonjwa pia angelizuwia uzee, na ufukara.

Na kwamba uchawi ni fitina inayotenganisha watu wanaopendana na kuleta uadui kwa wanaosikilizana.” Vyovyote iwavyo, wameafikiana mafaqihi wa Kishia kwamba adhabu ya mchawi ni kuuliwa akiwa ni Mwislamu. Akiwa si Mwislamu ni kutiwa adabu ya viboko na jela, kama atakavyoona hakimu.1

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَقُولُوا رَاعِنَا وَقُولُوا انْظُرْنَا وَاسْمَعُوا ۗ وَلِلْكَافِرِينَ عَذَابٌ أَلِيمٌ {104}

Enyi mlioamini msiseme ‘Raa’ina bali semeni ‘Undhurnaa’ na sikilizeni; na makafiri wana adhabu iumizayo.

مَا يَوَدُّ الَّذِينَ كَفَرُوا مِنْ أَهْلِ الْكِتَابِ وَلَا الْمُشْرِكِينَ أَنْ يُنَزَّلَ عَلَيْكُمْ مِنْ خَيْرٍ مِنْ رَبِّكُمْ ۗ وَاللَّهُ يَخْتَصُّ بِرَحْمَتِهِ مَنْ يَشَاءُ ۚ وَاللَّهُ ذُو الْفَضْلِ الْعَظِيمِ {105}

Hawapendi waliokufuru miongoni mwa watu wa kitabu wala washirikina mteremshiwe heri kutoka kwa Mola wenu. Na Mwenyezi Mungu humhusisha kwa rehema zake amtakaye; na Mwenyezi Mungu ni mwenye fadhila kubwa.
  • 1. Mwenye kutaka ufafanuzi kuhusu uchawi na hukum yake asome kitabu Al-Jawahir mlango wa Biashara na mlango wa kisasi. Vile vile kwenye kitabu Makasib cha Sheikh Ansari. Mwenye Jawahir anasema :” sio kila Jambo geni ni uchawi, kwani elimu nyingi zina athari za ajabu; kama vile wanavyofanya wazungu wakati huu.” Hivi sasa ni mwaka 1967; miaka 121 imepita tangu alipokufa mwandishi huyu mkuu. Lau angelikuwako wakati huu asingeliona ajabu. Kwa sababu kila la ajabu hivi sasa litakuwa ni la kawaida wakati ujao.