read

Dibaji

SifanjemazotezinamstahikiMwenyeziMungu Mola waviumbe.

Baada Ya Hayo

Mimi nimetunga mfululizo wa vitabu vidogo vidogo katika itikadi na misingi yake. Nimevitunga kulingana na mfumo na mantiki ya kizazi cha kisasa, ambacho hakiamini kitu ila kile kinachokitaka na chenye kuafikiana na malezi yake na maendeleo yake.

Alhamdulillah Mwenyezi Mungu amejaalia tawfiki na kufaulu kwa mfululizo huo na umerudiwa kuchapishwa mara nyingi.

Kimsingi ni kuwa kila kazi inayoafikiana na hekima na lengo inayolikusudia, Mwenyezi Mungu huipa ufanisi na tawfiki. Hakika tawfiki inatokana na Mwenyezi Mungu, hakuna shaka, lakini Mwenyezi Mungu amekataa kupitisha mambo isipokuwa kwa njia yake na desturi yake.

Kuandika juu ya karatasi tu, sio sharti la kufaulu katika kitu chochote; isipokuwa kufaulu ni kumridhisha na kumpendeza msomaji kile atakachokisoma.

Msomaji naye hawezi kuridhia kitabu chochote, isipokuwa kiwe kwa ajili yake na sio kwa ajili ya mwandishi. Na huko kuridhia kunampa nguvu mwandishi kuendelea. Hapo ndipo msomaji na mwandishi wanapoathiriana.

Kwa vyovyote ilivyo, kuenea kwa mfululizo huo wa vitabu vidogo vidogo kumenipa nguvu ya kutunga vitabu vikubwa na vipana; kama vile: Maalimu Falsafatil Islamiya, Alfiqhu Ala Madhahibil Khamsa, Fadhail Imam Ali n.k. Mwenyezi Mungu naye akavifanyia vitabu hivi kama alivyofanyia vile vingine. Nikapata msukumo wa kutunga Fiqhul Imam Jaffar Assadiq katika juzuu sita kubwa; nacho kikawa kama vingine vilivyotangulia.

Kwa hiyo vikanipa msukumo wa kutunga kitabu kikubwa na kitukufu, Tafsir ya Qur`an ambayo nimeiita Tafsir Al -Kashif. Kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu na nguvu Zake, vile vile kwa tawfiki Yake na fadhila Zake, imetimia juzuu hii ninayowaletea.

Ndani yake mna Sura mbili kamili za Al-Fatiha na Al-Baqara. Sijui kama uhai utaniruhusu nione natija ya lile nililojitolea mhanga, au kwamba kudra itafanya kinyume? Na kama ikitimia Tafsir Al-Kashif je, itakuwa na mafanikio, kama ilivyokuwa kwa tungo nilizozitunga, ya kutoa matunda? Je, itazaa kitabu kingine baada yake kama ilivyokuwa kwa Fiqh?

Hayo ni maswali ambayo hapana ajuaye jawabu lake isipokuwa Mwenye tamko la kwanza na Mwenye uwezo wa juu.

وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ مَاذَا تَكْسِبُ غَدًا ۖ وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ بِأَيِّ أَرْضٍ تَمُوتُ ۚ {34}

“Na nafsi yoyote haijui itachuma nini kesho, wala nafsi yoyote haijui itafia ardhi gani. (31:34)

Hata hivyo kuamini kwangu ukweli huu hakunizuii kuendelea na juhudi zangu. Kwa sababu, vile vile ninaamini kwamba azma yangu ya kujitahidi ina athari kubwa katika kuhakikisha yale ninayoyataka. Imani hii inanipa msukumo wa kutoa juhudi zangu zaidi, kwa kuogopa kupoteza fursa.

Kwa hivyo basi, nitaendelea kuandika na kuwa na ndoto ya kutimia na kufaulu mpaka kufa. Yeye peke yake ndiye ambaye atasimamisha nishati yangu. Nami nitaendelea kutoa juhudi zangu muda wote ule ambao mauti yatakuwa yako mbali nami.

Natamani sana yanijie mauti huku nikiwa ninaandika kulingania kwenye haki na uadilifu. Bali mapendeleo yangu ni kuingia peponi ili niweze kusoma na kuandika, nikiwa sina mawazo mengine yoyote ya kunishughulishi, nitakuwa sina mawazo ya kushughulikia familia na kadhalika.

Mara nyingi sana hunijia swali hili: Kama nikiingia peponi nitakuwa mvivu? Je, itawezekana nisome na niandike? Halafu hujijibu: Ndio, huko kuna yanayofurahiwa na macho na yanayopendwa na nyoyo; hata kama moyo unapenda kusoma na kuandika. Kisha linanijia swali jingine: Nimwandikie nani na watu wote wa peponi ni wakamilifu?

Samahani kwa kuiachia kalamu iandike hayo; au kwa usahihi zaidi, kuiacha dhati yangu kujieleza. Kwa kweli mimi ni mtu wa kawaida tu, ambaye ni vigumu kumtenganisha na dhati yake na ambaye inakuwa vigumu kujizuia kuyaelezea yaliyo katika pango la moyo wake, wakati inapopatikana fursa ya kujieleza.

Kizazi Cha Kisasa

Kila kitu kina sababu ya kutokea kwake, ni sawa kiwe ni cha kimaumbile, kama vile tufani na tetemeko; au cha kijamii, kama vile ujinga na ufukara; au kiwe ni katika mambo ya moyoni, kama vile imani na kufuru.

Hakuna kitu chochote kinachotokea kwa sadfa bila ya sababu yoyote, au bila ya mipangilio yoyote. Nitayafafanua maelezo haya kwa swali na jibu lifuatalo:

Kwa nini kizazi cha sasa hakijishughulishi na misimamo ya kidini kama kilivyokuwa kizazi kilichopita? Vijana wengi wa kileo wameachana na ibada na mazingira ya kidini; bali imekuwa uzito sana kwao kusikiliza mawaidha na nasaha za kidini; hata msimamo mzuri wa kiutu - kama udugu, usawa, amani, kusaidiana, ukweli na uadilifu - haumo katika nyoyo zao kabisa. Inapotokea kuuzungumzia basi wanauzungumzia katika ndimi zao tu, sio katika nyoyo zao; ila ikiwa kuna manufaa ya kibinafsi.

Jibu ni kuwa, mataifa ya Kiislamu ya Kiarabu na yasiyokuwa ya Kiarabu yalikuwa hayategemei misingi yoyote wala misimamo yoyote ila ile iliyotokana na Kitabu cha Mwenyezi Mungu (s.w.t.) na Sunna ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.), sio iliyotokana na ujamaa au ubepari, wala demokrasia au ubaguzi. Hakuna kitu chochote walichotegemea isipokuwa wahyi wa Mwenyezi Mungu.

Humo ndimo mlimochukuliwa misingi ya itikadi, adabu, tabia na njia za taaluma. Vile vile kanuni na hukumu zinazotumiwa katika mahakama na mambo mengine ya kibinafsi na ya kijamii, yalitoka humo.

Kwa hiyo, ndio maana yakawa mafundisho ya dini yako wazi katika bongo za watu wengi; wakawa wanayajua yanayotakiwa na sharia na yanayokatazwa. Yule aliyekuwa akiishi maisha ya dini alikuwa ndio tegemeo la wote na ndio mahali pa amana zao. Na, yule mbaye hana dini hakuaminiwa au kutegemewa katika jambo lolote. Yaani misimamo ya kijamii ilikuwa ni misimamo ya kidini. Yeyote anayetoka katika msimamo huo, anakuwa ametoka katika usalama.

Kisha siku zikapita, yakatokea mapinduzi kutoka nchi za Kimagharibi, wakavamia miji ya Kiislamu. Kwanza kabisa walielekea kwenye sharia ya Qur`an, wakaiondoa katika mahakama. Badala yake wakaleta kanuni za Kifaransa na za Kiingereza. Wakaondoa mafunzo ya kidini katika taaluma. Wakaanzisha majumba ya ufuska; kama vile mabaa, vilabu vya usiku pamoja na kila kitu ambacho waliona kingeweza kuondoa itikadi na maadili.

Kwa hiyo athari za Qur`an na Sunna za Mtume zikafichika katika maisha ya kijamii. Hata lugha ya Kiarabu pia ilipatwa na kile kilichopatwa na dini. Ndio kikawa kizazi hiki hakijishughulishi na dini wala maadili mema. Hiyo ni natija ya ufisadi waliokulia na kulelewa nao. Na kama kawaida, hali hiyo ilienea.

Kwa hiyo ni makosa kukitenga kizazi na jamii yake na malezi yake. Hawakukosea wale waliosema: “Panapofuka moshi hapakosi moto”

Dawa

Unaweza kuniuliza: Umeelezea ugonjwa, sasa dawa yake ni nini?

Kwa kweli jibu la swali hili si la kujibiwa na msomi mmoja tu; hapana budi zikutane akili kubwa zenye ikhlas. Kwa sababu, tabia na ada zikiingia katika kizazi na zikabaki kwa muda mrefu, huwa zimemea. kazi rahisi kuzing`oa. Kwa vile zinafanya kazi katika nafsi, kama zinavyofanya kazi athari za kisayansi.

Kuzibadilisha kunahitaji juhudi na jihadi ndefu, zenye mashaka; kama juhudi aliyoifanya Mtume (s.a.w.) katika kubadilisha ada za kijahiliya na itikadi zao. Kuna Hadith zinazoonyesha hayo; kama ile inayosema: “Uislamu ulianza katika hali ya ugeni na utarudi katika hali ya ugeni, kama ulivyoanza.”

Kwa hivyo, hauwezi kuepukana na ugeni wake na kutulia katika kurudi kwake, isipokuwa kwa kiongozi kama Mtume Muhammad (s.a.w.) na Masahaba kama Wahajiri na Ansari. Mwenyezi Mungu hashindwi kufanya Qur`an, sharia yake na maadili yake kuwa ndiyo inayotawala leo. Lakini ni juu yetu kufanya juhudi kadiri ya uwezo wetu, wala tusingoje muujiza wa mbinguni.

Na kazi ambayo tunaiweza kuifanya, nionavyo mimi, ni: Kwanza, tuitilie mkazo dini katika mashule, hasa Qur`an, kuisoma, kuihifadhi na kuifasiri. Kwani hiyo ndiyo msingi. Kama wasimamizi wakikataa kufundisha dini katika mashule na watakataa tu, basi ni juu yetu kuanzisha Shule za kibinafsi kwa ajili ya lengo hilo tu. Tuanzishe Shule hizi kutokana na mamillioni yanayotolewa sabili kwa wanavyuoni wakubwa na wengine

Wala sijui kama kuna kazi nyingine bora zaidi ya kutumia pesa hizo kuliko kufufua na kuyaeneza mafundisho ya dini.

Pili, kila mmoja katika watu wa dini atekeleza wajibu wake kwa ikhlasi, baada ya kujiandaa kuwa kiongozi mwenye mwamko, anayejua namna ya kuwakinaisha vijana, kuwa dini ndio chimbuko la msimamo ulio sawa, ambalo litawapa maisha mema zaidi.
Tatu, kuufafanua uhakika wa dini, kuufanya mwepesi kufahamika na kuutangaza kwa vitabu, hotuba, makala na matoleo kadhaa. Tumthibitishie mjinga na mwenye shaka kuwa Uislamu kwa sharia na maadili yake, unatosheleza kabisa mahitaji ya mwanadamu ya kiroho na ya kimaada; na unaweza kutatua matatizo yake; na kwamba una lengo la kumfanya afaulu katika dunia yake na akhera yake.

Msomaji atapata dalili ya hayo katika tafsiri hii ambayo inaunganisha dini na maisha, na ambayo imeshughulikia zaidi upande wa ubinadamu kuliko kushughulikia ufasaha wa maneno.

Mfasiri

Tafsiri, kilugha, ina maana ya kubainisha. Na, katika istilahi ina maana ya elimu inayotafiti maana ya maneno ya Qur`an na yanavyohusika.

Ili mfasiri awe na ubainifu katika ambayo yanamstahiki Mwenyezi Mungu, hana budi kuwa na maandalizi yafuatayo:-

Elimu za kiarabu kwa nyanja zake zote, elimu ya Fiqh na Misingi (usul) yake, Hadith na elimu ya Tawhid. Na miongoni mwa maandalizi hayo, kama wanavyoona wengine, ni elimu ya Tajwid na elimu ya kisomo cha Qur`an.

Kuna kitu kingine anachokihitajia mfasiri ambacho ni muhimu na kikubwa kuliko chochote katika walivyovitaja wafasiri katika utangulizi wa tafsiri zao. Kwa sababu, ndio msingi wa kwanza wa kufahamu maneno yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.); Wala sijamwona yeyote aliiyekielezea.

Kitu chenyewe ni kuwa, maana ya Qur`an hawezi kuyafahamu na hatayafahamu kwa uhakika wake na kujua ukubwa wake, isipokuwa yule mwenye kuyahisi ndani ya moyo na akili yake. Pia imani yake ichanganyike na maana ya Qur’an pamoja na damu yake na nyama yake.

Hiyo ndiyo siri iliyo katika kauli ya Amirul Muminin, Ali (a.s.): Hiyo ni Qur`an iliyonyamaza na mimini Qur`an inayotamka.

Vilevile imenijia yakini wakati nikiendelea na tafsiri kwambamfasiri yeyote asiyeleta fikra mpya, ijapokuwa moja tu, katika tafsiri yake yote, basi atakuwa hana akili ya mwamko, isipokuwa ana akili ya kusoma tu. Anamchorea mwingine yale anayoyasoma, kama inavyoonekana picha ya kitu katika kioo vile ilivyo kwa rangi na umbo.

Hiyo ni kwa sababu maana ya Qur’an yako ndani sana kiasi ambacho yeyote hawezi kuyafikia kwa vyovyote vile atakavyokuwa na elimu na fahamu; isipokuwa atagundua yale ambayo maarifa yake yanayamudu. Atakaposimama mfasiri aliyetangulia pale alipofikia, kisha akaja mwingine akafuata nyayo zake bila ya kuzidisha chochote ijapokuwa hatua moja tu, basi atakuwa ni kama kipofu kamili anayetegemea fimbo tu; anapoikosa anabakia pale alipo.

Nimepata rai nyingi na itikadi za hapa na pale wakati nilipokuwa nafasiri. Kwa kweli tafsiri imesahihisha fikra zangu nyingi za zamani. Nimekuwa na yakini kwamba hapana imani bila ya takua pepo haipati isipokuwa mwenye kujitahidi na akajitoa mhanga katika njia ya haki na kwamba hakuna msingi wowote katika misingi ya Kiislamu au tawi lolote katika matawi ya Kiislamu - katika kumwamini Mwenyezi Mungu au hukumu ndogo katika sharia - isipokuwa inafungamana na maisha.

Vile vile nimeyakinisha kuwa wengi wa wale ambao hawaujui Uislamu na makusudio yake ni wale wanaojinaki na Uislamu; na mengi ambayo atayakuta msomaji wakati wa kupekuwa kurasa za Tafsir hii, nimeyahusisha hayo katika vifungu mbali kwa vielelezo vyake.

Kwa kweli sijui kama kuna kazi ngumu na nzito kama kufasiri maneno ya Mwenyezi Mungu. Sio kazi rahisi kueleza matakwa yake Mwenyezi Mungu. Lakini jambo la kutia moyo, nikuwa mfasiri hufasiri maana ya Qur`an na makusudio yake kulingana na alivyofahamu yeye, sio kulingana na ilivyo hasa; sawa na mujtahid wa Fiqh ambaye hulipwa thawabu akifutu sawa na husamehewa akikosea, bali hupata thawabu, hata akikosea, kwa sababu ya juhudi yake na kutokuwa mvivu.

Mwito Wa Qur’an

Mwenye kufuatilia Aya za Qur’an tukufu, akazingatia maana yake, atazikuta zina mfungamano mmoja tu katika kanuni zake zote na misingi yake. Vile vile katika sura zake na Aya zake. Mfungamano huu ni ule mwito wa kuwapa watu maisha mema yenye uadilifu, ustawi na amani. Mwenyezi Mungu anasema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اسْتَجِيبُوا لِلَّهِ وَلِلرَّسُولِ إِذَا دَعَاكُمْ لِمَا يُحْيِيكُمْ ۖ {24}

“Enyi mlioamini mwitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume anapowaita katika yale yatakayowapa uhai.” (8:24)

Mwito wa Mwenyezi Mungu na Mtume kwenye maisha, una mfumo wake na nguzo zake maalum zinazousimamia Mwenyezi Mungu ameupanga mfumo wa kulingania kwa kumwambia Mtume wake mtukufu (s.a.w.):

ادْعُ إِلَىٰ سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ ۖ وَجَادِلْهُمْ بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ ۚ {125}

Waite kwenye njia ya Mola wako kwa hekima na mawaidha mazuri na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora.(16:125)

Makusudio ya hekima na mawaidha mazuri ni kuuambia moyo na akili, na kuuonyesha viumbe vya aina yake na vya ajabu. Mwenyezi Mungu anasema:

سَنُرِيهِمْ آيَاتِنَا فِي الْآفَاقِ وَفِي أَنْفُسِهِمْ حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَهُمْ أَنَّهُ الْحَقُّ ۗ {53}

Tutawaonyesha ishara zetu zilizo katika upeo wa mbali na katika nafsi zao mpaka iwabainikie kwamba haya ni kweli.(41:53)

Vile vile kuwahadharisha wapinzani na mwisho mbaya, na huwaonyesha mfano wa umma uliotangulia; kama alivyofanya Nabii Shuaib aliposema:

وَيَا قَوْمِ لَا يَجْرِمَنَّكُمْ شِقَاقِي أَنْ يُصِيبَكُمْ مِثْلُ مَا أَصَابَ قَوْمَ نُوحٍ أَوْ قَوْمَ هُودٍ أَوْ قَوْمَ صَالِحٍ ۚ وَمَا قَوْمُ لُوطٍ مِنْكُمْ بِبَعِيدٍ {89}

“Na enyi watu wangu! Kukhalifiana nami kusiwapelekee kuwasibu kama yaliyowasibu watu wa Nuh au watu wa Hud au watu wa Swaleh. Na watu wa Lut si mbali nanyi.(11:89)

Wakiendelea na inadi yao, na ikiwa hakuna dalili zaidi za kutoa, basi achana nao. Mwenyezi Mungu anasema:

فَإِنَّمَا عَلَيْكَ الْبَلَاغُ وَعَلَيْنَا الْحِسَابُ {40}

“Na kama wakikuhoji, basi sema nimeusalimisha uso wangu kumwelekea Mwenyezi Mungu na walionifuata…. (3:20)

Ama nguzo zamwitowa maisha mema,nihizizifuatazo:-

1. Hakika mtu hakupatikana kibahati tu, bila ya makusudio yoyote: Na Mwenyezi Mungu amewaumba kisha atawafisha. (16:70)

2. Mwenyezi Mungu hakumwacha mtu bure bure tu, ajihukumilie kimapenzi yake, bali amemuwekea njia ya sawasawa, ambayo haijuzu kuikengeuka: Mwenyezi Mungu anasema:

أَيَحْسَبُ الْإِنْسَانُ أَنْ يُتْرَكَ سُدًى {36}

Hivi anadhani kuwa mtu ataachwa bure bure tu!” (75:36)

فَوَرَبِّكَ لَنَسْأَلَنَّهُمْ أَجْمَعِينَ {92}

عَمَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ {93}

Naapa kwa Mola wako tutawauliza wote yale waliyokuwa wakiyatenda.” (15: 92-93)

3. Amani na kuchunga nidhamu. Mwenye kuiharibu na akafanya uharibifu katika nchi ataadhibiwa adhabu kali duniani, na katika akhera atakua na adhabu. Mwenyezi Mungu anasema:

إِنَّمَا جَزَاءُ الَّذِينَ يُحَارِبُونَ اللَّهَ وَرَسُولَهُ وَيَسْعَوْنَ فِي الْأَرْضِ فَسَادًا أَنْ يُقَتَّلُوا أَوْ يُصَلَّبُوا أَوْ تُقَطَّعَ أَيْدِيهِمْ وَأَرْجُلُهُمْ مِنْ خِلَافٍ أَوْ يُنْفَوْا مِنَ الْأَرْضِ ۚ ذَٰلِكَ لَهُمْ خِزْيٌ فِي الدُّنْيَا ۖ وَلَهُمْ فِي الْآخِرَةِ عَذَابٌ عَظِيمٌ {33}

Hakika malipo ya wale wanaopigana na Mwenyezi Mungu na Mtume wake na kufanya uovu katika nchi, ni kuuawa au kusulubiwa au kukatwa mikono yao kwa mabadilisho au kuhamishwa katika nchi; hii ndio fedheha yao katika dunia na akhera watapata adhabu kubwa. (5:33)

4. Amaninanidhamuhaiwezikuwakonawalahaitakuwakoikiwa kila mtu hatachunga heshima yake na uaminifu wake. Kwa sababu jamii njema, kwa mujibu wa Qur’an, ni ile isiyokuwa na mbegu ya ufisadi hata moja. Mwenyezi Mungu anasema:

أَنَّهُ مَنْ قَتَلَ نَفْسًا بِغَيْرِ نَفْسٍ أَوْ فَسَادٍ فِي الْأَرْضِ فَكَأَنَّمَا قَتَلَ النَّاسَ جَمِيعًا وَمَنْ أَحْيَاهَا فَكَأَنَّمَا أَحْيَا النَّاسَ جَمِيعًا ۚ{32}

“Mwenye kumuua mtu bila ya yeye kuua mtu au kufanya ufisadi katika nchi, basi ni kama amewaua watu wote; na mwenye kumwacha hai basi ni kama amewaacha hai watu wote.”(5:32)

Hiyo ni kwamba hakika ya utu inakuwa kwa kila mmoja. Mwenye kumfanyia ubaya mmoja, atakuwa amewafanyia ubaya wote na mwenye kumfanyia wema mmoja, atakuwa amewafanyia wema wote.

Kusema kwake Mwenyezi Mungu: “Mwenye kuua mtu bila ya yeye kumuua mwingine au kufanya ufisadi katika nchi”, ni kuonesha kuwa kila mtu ana heshima yake ya kiutu, mpaka aivunje mwenyewe kwa kufanya kosa litakalovunja heshima yake hiyo.

5. Utangamano kati ya watu unakuwa juu ya misingi ya kuchunga heshima kwa kila mtu bila ya kubagua kati ya mwanamume au mwanamke, mweusi au mweupe na tajiri au maskini, katika mila yoyote aliyo nayo. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameuthibitisha ubainifu huu kwa ibara fupi:

وَلَقَدْ كَرَّمْنَا بَنِي آدَمَ{70}

“Hakika tumemtukuza mwanaadamu...(17:70)

6. Kuamini Mwenyezi Mungu, Utume wa Muhammad (s.a.w.), siku ya mwisho na mengineyo, ni katika misingi ya dini na matawi yake, wala sio kuwa ni bendera ya dini inayopeperushwa na Qur’an. Kila msingi katika misingi ya Uislamu na kila hukumu katika hukumu zake, zina matunda na amali yenye manufaa. Mwenyezi Mungu amekukutanisha kumwamini yeye na amali njema katika Aya kadhaa. Ama kuamini Utume wa Muhammad (s.a.w.) ni kuamini utu na wema wake. Mwenyezi Mungu anasema:

وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا رَحْمَةً لِلْعَالَمِينَ {107}

Na hatukukutuma isipokuwa uwe rehema kwa walimwengu.” (21: 107)

Ama kuingia peponi, kunafungamana zaidi na jihadi na amali njema katika maisha haya. Mwenyezi Mungu anasema:

أَمْ حَسِبْتُمْ أَنْ تَدْخُلُوا الْجَنَّةَ وَلَمَّا يَعْلَمِ اللَّهُ الَّذِينَ جَاهَدُوا مِنْكُمْ وَيَعْلَمَ الصَّابِرِينَ {142}

Je mnadhani mtaingia peponi na hali Mwenyezi Mungu hajawajua wale waliopigania jihadi dini ya Mwenyezi Mungu miongoni mwenu na kuwajua waliofanya subira? (3:142)

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اسْتَجِيبُوا لِلَّهِ وَلِلرَّسُولِ إِذَا دَعَاكُمْ لِمَا يُحْيِيكُمْ ۖ{24}

“Enyi ambao mmeamini mwitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume anapowaita katika yale yatakayowapa uhai...” (8:24)

Hii ni dalili wazi kwamba mwito wowote ambao hauna muungano wowote wa maisha, basi sio wa dini. Na mwenye kuunasibisha kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, atakuwa ameizulia uwongo dini.Kwa misingi hii, ndipo nikajaribu kufasiri Aya za Qur’an tukufu na kuifafanua kwa ufafanuzi ufuatao:-

Njia

Makusudio ya njia hapa ni udhibiti anaokwenda nao mtungaji, bila ya kukengeuka. Kwani kazi yoyote ambayo haina njia ni shaghalabaghala tu, itakayoongozwa na migongano.

Njia niliyofuata katika tafsiri hii, inafungamana na kudhibiti mambo yafuatayo:-

1. Nimeitazama Qur’an kwa mtazamo kuwa hakika yake na sera yake ni kitabu cha dini na uongozi, kutengeneza na kuweka sharia inayolenga kuwapa watu wote maisha yaliyo katika misingi iliyosalimika, inayoongozwa na amani na uadilifu na iliyojaa furaha na wema. Hayo nimetangulia kuyaeleza.

2. Baadhi ya wafasiri wa kwanza walijishughulisha zaidi na lugha, wakarefusha maneno katika kubainisha siri ya matamko na wakaweka maswali; mfano: Kwa nini imetajwa wau na wala isitajwe fa au kwa nini amesema mafasiki na wala asiseme madhalimu, n.k. Kisha wakajibu majibu yasiyo na umuhimu. Mimi sikuingilia jambo hili.

Ikiwa kila tafsiri imepondokea upande fulani, basi mimi nimepondokea kwenye namna ya kumkinaisha msomaji kwamba dini kwa misingi yake yote na matawi yake pamoja na mafunzo yake mengine, ina lengo la kumpatia mtu heri na heshima na kwamba mwenye kukengeuka lengo hili, atakuwa ameikengeuka hakika ya dini na njia ya maisha yaliyonyooka.

Ili kuweza kulifikia lengo langu hili, nimejaribu kwa juhudi zangu zote kuleta ufafanuzi mwepesi na ulio wazi, atakaoweza kuufahamu msomaji kwa kiwango chochote atakachokuwa.

Kwa vile zama walizoishi wafasiri wa zamani hazikuwa zama za kudharauliwa dini, sharia yake na misimamo yake kama ilivyo sasa, ndio maana wafasiri hao walijishughulisha zaidi na fasihi kuliko kumkinaisha msomaji kuwa dini ni msimamo ulio sawa sawa. Kwa hiyo lugha ya tafsiri ya zama hizo sio ya zama hizi.

Hakika tafsiri ni fani kamili inayokwenda na wakati. Ndio maana mimi nimeielekeza tafsiri yangu katika kukinaisha kizazi cha kisasa kuwa dini inakwenda sambamba na maisha.

Lakini hiyo haimaanishi kuwa mimi nimeghafilika na upande wenye kunufaisha, ambao umeonyeshwa na wafasiri wakubwa, la!

Isipokuwa nimeufupisha upande huo na kuuonesha kwa uwazi zaidi, hata nimeonyesha rai yangu ndani yake hasa katika masuala nyeti ya kifalsafa; mfano: Kulazimishwa watu au kuwa na hiyari, uongofu na upotevu, Uimamu na Isma ya Mitume.

Pia shafaa, mwenye madhambi makubwa, hisabu ya kaburi na mengineyo.

Vilevile mara nyingi nimehusisha kifungu maalum cha lugha, kwa ajili ya kutafsiri misamiati ambayo si maarufu. Mara nyingine nimeweka kifungu kingine cha irabu kwa ajili ya kubainisha hukumu za Kinahw (sarufi) kwa tamko lenye utatanishi, ijapokuwa wafasiri wa kisasa hawakujishughulisha nalo, lakini mimi nimeangalia matakwa ya baadhi ya wasomaji wa nahw, ingawaje ni wachache.

Ama usanii wa methali za maneno, elimu ya usemaji, ulinganishaji na uunganishaji, nimemwachia Zamakhshari katika Kash-Shaf, Al-Andalusi katika Bahrul-Muhit, na wengineo.

Ili kuthibitisha kuwa lugha ya tafsiri inatofautiana kulingana na wakati, ninataja maneno ya Muhyiddin Ibn El-Arabi katika kitabu Futuhatil Makkiyya, Juzuu ya nne, mlango wa Hadhratul-hikma, kuhusu kuisoma Qur’an, ambayo yana maana ya undani kabisa na yanayoafikiana na nadharia za kisasa; hasa ile nadharia ya Uwiano (Relativity) ya Einstein, ambaye anazingatia kuwa wakati na mahali ndivyo vinavyosimamisha kitu. Anasema huyo Ibnul Arabi:

“Msomaji anasoma alichokihifadhi katika Qur'an, anakuta katika kila kisomo maana ambayo hakuyakuta katika kisomo cha kwanza pamoja na kuwa herufi zinazosomwa ni zile zile, isipokuwa matukio na hali ndivyo vipya. Kwa hivyo hapana budi maana hayo yawe mapya. Kwa sababu, wakati wa kusoma kwa kwanza sio kwa pili.”

Hapa aliposema, “hapana budi kuwa maana hayo yawe mapya, maana yake ni kuwa, kitu kinakuwa kipya kwa kuwa kipya wakati ule.”

Amesema kweli mwanafalsafa Rasil, aliposema: “Hakika watu wa zamani waligundua nadharia zilizothibitishwa na elimu kulingana na fikra na jitahadi zao; na zilikuwa ni rai za sawa; ambapo katika zama zao hizo hakukuwa na kitu zaidi ya jitihadi ya maoni.”

3. Nimeangalia hadith zinazohusu Israil ambazo zimekuja katika baadhi ya tafsiri, nikazikuta ni vigano tu. Kitu kinachofahamisha zaidi uwongo wake, ni kuzinasibisha kwa Waisrail.

Vilevile nimejipurukusha na riwaya zilizoelezea sababu za kushuka, isipokuwa chache tu. Kwa sababu, wanachuoni hawakudhibiti mategemezo yake na kupambanua kati ya dhaifu na sahihi; kama walivyofanya kwa riwaya za hukumu. Hata hizo nazo hawakuangalia sana zile za Sunna na kuchunguza kwa makini, isipokuwa katika wajib na haramu. Bali wameweka utafiti mbali katika vitabu vya Usuul.

Vilevile sikujishughulisha na pia kumshughulisha msomaji, kutaja kufungamana au kunasibiana kati ya Aya na Aya nyingine; kama walivyofanya wafasiri wengine. Kwa sababu, Qur’an haikufunuliwa kwa Mtume (s.a.w.) kwa mpigo, bali iliteremshwa kwa nyakati maalum, mara nyingine kwa kufuatana na mara nyingine kwa kuchelewa; wala sura au Aya hazikupangwa kama tunavyozisoma hivi sasa.

Qur’an, tuliyo nayo hivi sasa, ilipangwa tangu siku za Mtume (S.A.W). Mpango huu haukufuata utaratibu wa kushuka sura, wala kuwa sura ni ya Makka au Madina; vile vile hakuna tarehe ya kushuka Aya. Hivyo tunakuta Sura ya Baqarah, Al-Imran na Maida ziko mwanzo wa msahafu baada ya Sura ya Fatiha, pamoja na kuwa zimeshuka Madina. Mara nyingine tunakuta sura iliyoshuka Madina ina Aya zilizoshuka Makka.

Mwenye tafsir ya Al-Manar, akimnukuu mwalimu wake, Sheikh Muhammad Abduh, katika Juzu ya pili, ukurasa 451, chapa ya pili, anasema: “Qur’an sio kitabu cha fani cha kuwa na mlango mahsusi na makusudio fulani; isipokuwa ni kitabu cha uongozi na waadhi, inamgurisha mtu kutoka hili mpaka lile.

Na mara kwa mara inarudia kwenye utafiti wa kusudio moja, kwa ibara nyingine na namna nyingine ya ubainifu, ili asichoke mwenye kupewa mawaidha na kuongozwa.”

4. Kabla ya kitu chochote nimetegemea, katika kutafsiri Aya na kubainisha makusudio, Hadith zilizothibiti kwa Mtume (s.a.w.). Kwa sababu, ndizo zinazofasiri Qur’an na ni njia ya kujua maarifa yake.

Mwenyezi Mungu anasema:

وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانْتَهُوا ۚ{7}

Alichowapa Mtume kipokeeni na alichowakataza jiepusheni nacho.(59:7)

Ikiwa hakuna hadith, basi ninategemea dhahiri ya Aya na mpangilio wake. Kwa vile, msemaji mwenye hekima, ubainifu wake hutegemea yale anayoyafahamu yule anayemwambia kutokana na dalili zilizo wazi; kama ambavyo mwenye kuambiwa anachukua dhahiri hiyo tu, mpaka pale itakapothibitika kinyume.

Kama ikija Aya nyingine katika maana ya Aya ya kwanza na ikawa ina ubainifu na kuwa wazi zaidi, basi ninazitaja pamoja ili zifafanuke zaidi. Kwa vile chimbuko la Qur’an ni moja, inajitamkia yenyewe na kujiletea ushahidi.

Kama ikipingana dhahiri ya tamko pamoja na hukumu ya kiakili, basi ninaitafsiri kwa namna ambayo inaafikiana na akili, kwa kuizingatia hiyo akili kuwa ni dalili na hoja juu ya amali iliyo wajibu.

Ikiwa dhahiri ya tamko inapingana na Ijmai ya Waislamu katika nyakati zote kwenye masuala ya Kifiqh, basi huchukua Ijmai: kama kauli yake Mwenyezi Mungu:

إِذَا تَدَايَنْتُمْ بِدَيْنٍ إِلَىٰ أَجَلٍ مُسَمًّى فَاكْتُبُوهُ ۚ{282}

“Mnapowekeana deni kwa muda uliowekwa, basi iandikeni.(2:282)

Ambapo neno iandikeni limefahamisha wajibu, lakini Ijmai imesimamia juu ya kuwa kuandika deni ni sunna. Kwa hiyo hapo nimechukua kuwa ni suna na sio wajibu.

Ama kauli za wafasiri, sikuzifanya ni hoja mkataa na dalili peke yake; isipokuwa kutilia nguvu njia mojawapo, ikiwa tamko linachukua maana nyingi.

Hata hivyo wafasiri wamefanya juhudi kubwa sana za kufafanua maana ya Qur’an na siri zake, na kuonyesha lugha inayofahamika na ngeni. Wamekitafsiri kitabu cha Mwenyezi Mungu kwa juhudi ambayo haijapatikana mfano wake katika umma wa zamani au wa sasa.

Kwa hakika kuna wafasiri wakubwa na waliobobea katika fani mbali mbali za elimu ya Qur’an ambao walikuwa ni watu muhimu sana katika historia ya Kiislam. Kwa hiyo ingawaje kauli za mabingwa hao si hoja, kama kauli ya Masum, lakini zinaweza kuwa ni mwangaza juu ya maana yanayokusudiwa na kuuandaa njia ya kufahamu.

Makosa Ya Chapa

Sikumbuki kama nimewahi kusoma kitabu kilichotoka kupigwa chapa, cha zamani au cha sasa, bila ya kukuta makosa ya chapa. Nafikiri sitasoma kitabu kisichokuwa hivyo. Nimejaribu sana kuliepuka hilo katika tungo zangu, lakini sikufanikiwa.

Nilikuwa sifikirii kama ninaweza kuona makosa haya katika maandishi ya msahafu mtukufu, kama yale yaliyo katika baadhi ya chapa; kwa mfano neno yabswutu kwa Swad, badala ya yabsutu kwa sin, na katika chapa ya Tafsir Arrazi ya Misr ya mwaka 1935, Sura ya (2:146) Imeandikwa La Ya’alamuun, (hawajui) badala ya Ya’alamuun (wanajua). Mfano wa makosa haya hausameheki.

Katika Tafsir Al-Manar, chapa ya pili, Sura (2:212), imeandikwa “Fawqahum ila yawmil qiyama badala ya Fawqahum yawmal qiyama”. Hatuwezi kusema kosa hili ni kubwa zaidi kuliko lile.

Lakini mkosaji atatuletea udhuru kwa msemo mashuhuri huko kwetu JabalamilMakosa ya chapa.
Katika Tafsiri Majmau chapa ya Urfan, Sura (46:15), imeandikwa: “Hatta idha balagha arbai’na sanah badala ya: Hatta idha balagha ashuddahu arbai’na sanah.”
Kusema hivi sio kama ninajitetea kutokana na makosa ya chapa atakayoyakuta msomaji katika kitabu hiki, ijapokuwa naomba msamaha kama litatokea hili, lakini makusudio yangu hasa ni kumwambia yule atakayefungua macho yake kwenye makosa ya matamko na kuufungia macho uzuri wa maana.

Vilevile ninamwambia yule ambaye siku moja aliniambia: ‘Vitabu vyako vimejaa makosa ya chapa, kama kwamba hakuna kitu chochote katika vitabu hivyo isipokuwa makosa ya chapa tu. Wote hao ninawaambia: Mungu awasamehe na aniongoze mimi na nyinyi.

Vyovyote iwavyo, mimi ninaomba msamaha kutokana na makosa ya kifikra na ya chapa. Anasema Amirul Muminiin (AS): “Watu wote ni wapungufu wenye kuchanganyikiwa, isipokuwa yule aliyehifadhiwa na Mwenyezi Mungu”. Na Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ndiye mwenye jukumu la kunikubalia yale niliyoyapatia na kunisamehe niliyoyakosea, kwa jaha ya Mtume na kizazi chake, ziwashukie rehema na amani. (Amin).
MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYAH