Aya 30 – 33: Mola Wako Alipowaambia Malaika
Makusudio ya majina katika kauli yake Mwenyezi Mungu: Na Mwenyezi Mungu akamfundisha Adam majina ya (vitu) vyote, ni maana ya majina, nayo ni ya vitu vya ulimwengu na sifa zake. Mwenye Majmaul-Bayan anasema: “Hakika majina bila ya maana hayana faida wala kuonyesha ubora wake.”
Imam Sadiq (a.s.) Aliulizwa kuhusu hayo majina akasema: “Ni milima na mabonde.” Kisha akaonyesha busati lililokuwa chini yake akasema: “Hili ni miongoni mwayo”, yaani kila kitu mpaka busati hili pia.
Malaika
Hakuna njia ya kuwajua Malaika na hakika yao kwa hisia na majaribio wala kwa akili na kukisia au kwa kitu chochote isipokuwa kwa njia ya wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kupitia midomoni mwa Mitume yake. Mwenye kukanusha wahyi kimsingi haifai kumzungumzia habari ya Malaika kwa hali yoyote. Kwa sababu wao ni tawi na wahyi ni asili (shina). Ikiwa hapana budi kulumbana naye basi ni lazima iwe ni kuhusu fikra ya wahyi na kuswihi kwake tu.
Hapa hatukusudii kulumbana na anayekanusha wahyi, kwa vile tumekwishafafanua; isipokuwa tunamwambia yule mwenye kukanusha: “Si haki kulazimisha rai yako juu ya yule mwenye kuamini wahyi; kama si hivyo basi ingelijuzu kwake kulazimisha rai yake kwako. Kama ukimwambia mwenye kuamini wahyi kuwa imani yake ni batili kwa vile yeye hategemei majaribio, atakujibu kwamba kuamini kwako kuwa wahyi ni batili vilevile hakukutegemea kwenye majaribio, kwa sababu kukanusha kwako na uthibitisho wa mwenye kuamini, maudhui yake ni mamoja, nayo ni wahyi. Ikiwa majaribio, hayathibitishi wahyi pia hayaukanushi.
Kwa maneno mengine kuamini kutokuwepo ghaibu ni sawa na kuamini kuwepo, yote mawili ni ghaibu katika ghaibu. Kimsingi ni kwamba ghaibu haifai kuipinga kwa ghaibu.”
Sartre, mwandishi na mwanafalsafa mashuhuri wa Kifaransa akiwajibu wanao-amini maada alisema: “Nyinyi mnapokanusha kuwepo Mwenyezi Mungu ndio mnafafanua ghaibu kwa ukamilifu, kama wanaoamini mifano ambao wanakubali kuwepo kwa Mwenyezi Mungu. Hakika yakini ya kimaada ya kukanusha ghaibu, inategemea dalili ile ile anayoitegemea mwenye kuamini kuswihi ghaibu. Kwa hivyo basi imebainika kwamba imani ya kimaada inajipinga yenyewe.”1
Khalifa
Makusudio ya Khalifa katika Aya ni Adam, baba wa watu na kila mtu aliyeko na atakayekuwako katika kizazi chake wakati wowote na mahali popote. Wajihi wa kumwita Khalifa ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alimpa nafasi ya kuchukua hatamu za uongozi wa ardhi hii na kutafuta yaliyomo ndani yake miongoni mwa nguvu na manufaa na kufaidika nayo.
Katika kauli ya Malaika: “Utaweka humo watakaofanya uharibifu na kumwaga damu.”
Inaonyesha kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) aliwafahamisha Malaika kwa njia fulani kabla ya kumuumba Adam, kwamba lau binadamu atakuwa katika ardhi hii angeliasi kwa ufisadi na kumwaga damu. Kutokana na hali hiyo ndio wakaona ajabu vipi Mwenyezi Mungu amlete ambaye atamuasi na wao wanamtukuza kwa sifa zake na kumtaja kwa utakatifu wake?
Ndipo Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akawabainishia hekima ya kuumbwa mtu na kwamba huko ni kuandaa kujulisha lile wasilolijua na uharibifu wake katika ardhi hauwezi kuondoa faida ya kupatikana kwake. Hapo Malaika wakatosheka na wakatii.2
Kwa hivyo Mwenyezi Mungu Mtukufu hakumuumba mwanaadamu ili afanye maasi na maovu, bali amemuumba kwa ajili ya elimu na amali yenye manufaa na akamkataza ufisadi na madhara. Akikhalifu na kuasi basi huadhibiwa kadri anavyostahiki.
Aya hii inafahamisha kwamba elimu na yanayoambatana nayo, ina cheo kikubwa mbele za Mwenyezi Mungu na Malaika wake, kwa sababu Mwenyezi Mungu amefanya bora kumuumba mtu kwa ajili ya elimu na maarifa na alipowaonyesha hilo, Malaika walitoa udhuru kwa kusema: Utakatifu ni wako hatuna elimu isipokuwa ile uliyotufundisha.
Ikiwa lengo la kuumbwa mtu ni elimu na amali, basi mwenye kuiacha atakuwa ameivunja hekima ya kuwepo.
Naogopa kusema kuwa lau Malaika wakati huo wangejua athari ya mabomu ya kitonoradi (Nuclear) na mabomu ya sumu (Napalm) waliyotumia Wamarekani huko Vietnam, basi wasingelikinai kabisa...
Namuomba msamaha Mwenyezi Mungu ambaye anajua vile tusivyovijua sisi wenyewe.
Somo Wazi
Somo ambalo ni lazima tufaidike nalo katika majibizano ya Mwenyezi Mungu na Malaika wake, ni kwamba mtu, vyovyote atakavyofikia katika elimu, nguvu na ukubwa, hawezi kuepuka kufanyiwa majibizano, malumbano na kushauriwa. Mwenyezi Mungu mwenyewe tu aliye mtukufu alitoa nafasi kwa Malaika ajadiliane nao na kujibizana ambako kunafananana upinzani; na wao hawakujizuia na hilo, bali walijitia ushujaa wa elimu. Mwenyezi Mungu akawachukulia upole katika kuwajibu na kuwabainishia dalili kwa upole wakakubali kwa kuridhia na kukinai, sio kwa kukemewa.
Pia Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akafungua mlango wa majibizano pamoja na Iblis mwenye laana ambaye alijibizana naye kwa kusema: “Umeniumba kwa moto na yeye umemuumba kwa udongo...”, kama yatakavyokuja maelezo.
Basi ni juu ya wale wanaojiona kuwa hawawezi kupingwa wachukue faida ya somo hili la wazi. Wakijitoa na kujibiwa watakuwa wanajifanya juu zaidi ya Mwenyezi Mungu, bila ya kujua. Anasema Amirul Muminin Ali (a.s.): “Msinich-anganye na watu wenye kujifanya wala msinidhanie kuwa nitaona uzito kwa haki niliyoambiwa wala kujifanya mkubwa. Kwani mwenye kuona uzito wa haki anayoambiwa au uadilifu atakaoonyeshwa, basi kuyafanya hayo mawili itakuwa uzito zaidi kwake. Msijizuwie na haki iliyosemwa au ushauri wa uadilifu.” (Nahjul-Balagha, Khutba Na. 213)
وَإِذْ قُلْنَا لِلْمَلَائِكَةِ اسْجُدُوا لِآدَمَ فَسَجَدُوا إِلَّا إِبْلِيسَ أَبَىٰ وَاسْتَكْبَرَ وَكَانَ مِنَ الْكَافِرِينَ {34}
- 1. Angalia kifungu cha Sartre na madhehebu ya kimaada katika kitabu chetu Falsafatul- Mabdai W al-Maad, tulichokitunga kuwajibu wenye Falsafa ya kimaada.
- 2. Inasemekana kuwa katika ardhi walikuwepo watu kabla ya Adam wetu, na kwamba wao walifanya uharibifu kisha wakaangamia wote na Malaika walikuwa wakilijua hilo.