Aya 108-109: Je Mnataka Kumuuliza Mtume Wenu
Maana
Je, mnataka kumuuliza Mtume wenu kama alivyoulizwa Musa zamani?
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kuwaambia waumini msijali kwa kupingwa ufutaji wa hukumu za dini yenu, kwa sababu mambo yote yako chini ya uweza wake Mwenyezi Mungu, na Ndiye anayewachagulia lililo na maslahi kwa ajili yenu na wengineo; baada ya kuwambia haya, aliwaambia mwataka nini kutoka kwa Mtume wenu Muhammad (s.a.w.) na hali amewajia na dalili za kutosha? Mwataka kumdodosa kama walivyofanya Mayahudi kwa Musa kwa kumuuliza yasiyofaa kuulizwa? Mtu anaweza kuwa na shaka na akataka dalili ya kukinaisha kuondoa shaka yake. Ama kutaka jabali liwe dhahabu, hiyo itakuwa ni ukaidi na kiburi. Basi enyi waumini msiwe wakaidi wenye kutakabari.
Na anayebadilisha imani kwa ukafiri, hakika amepotea njia iliyo sawa.
Kila mwenye kuwa na msimamo safi wa kutafuta dalili za kiakili kwa kutaka kuthibitisha haki, huyo ni muumini wa haki. Na kila mwenye kuwa na msimamo wa kiburi kudadisi na kutaka mambo yasiyoingia akilini basi huyo ni mpinzani wa haki. Na asiyetegemea aliyokuja nayo Muhammad (s.a.w) na kutaka zaidi, atakuwa amechagua inadi na kufuru juu ya imani.
Wengi miongoni wa watu wa kitabu wanatamani lau wangewarudisha nyinyi muwe makafiri baada ya kuamini kwenu, kwa sababu ya husuda iliyomo nafsini mwao.
Kila mtu anapendelea watu wawe kwenye dini yake. Mwanafalsafa mmoja anasema: “Siku nzuri kwangu ni ile ninayomuona anayeniafiki yuko kwenye rai yangu.” lakini Mayahudi walikuwa wakifanya juhudi kubwa ya kuwafitinisha Waislamu, kuwatoa kwenye dini yao ya Kiislamu na kuwarudisha kwenye dini yao ya kijahili ya kwanza, si kwa lolote bali ni kwa uhasidi. Ingawaje wao wanaweza kuwa Waislamu, kama walivyofanya wengine, lakini wao walihofia biashara zao na faida zao za pombe, kamari na uasherati.
Mayahudi walitaka kuwavunja Waislamu siku ya vita vya Uhud kwa kumlia njama Mtume. Imeelezwa kuwa baada ya tukio la Uhud walikuwa wakiwaita vijana wa Kiislamu majumbani mwao na kuwapatia pombe pamoja na kuwahadaa na mabinti zao, kama wanavyofanya leo na kila siku; kisha wanawatia shaka Waislamu kuhusu Qur’an na Utume wa Mtume mtukufu (s.a.w.).
Mtume alihisi mipango hii ya hatari akawakataza wasihudhurie kwenye vikao vya mambo ya upuuzi, akitilia mkazo kukataza zina, pombe, kamari na nyama ya nguruwe. Wakajizuilia Waislamu kwenda kwenye majumba ya Wayahudi waliyoyafungua kwa lengo lao hilo, ambayo hivi sasa yanajulikana kama Baa na Casino.
Baada ya kuwapambanukia haki.
Yaani Mayahudi walijaribu kuwarudisha Waislamu kwenye kufuru na upotevu pamoja na kujua Uislamu kuwa ndio dini ya haki na kwamba ushirikina na kuukana Utume wa Muhammad ni batili. Haya si kwa Mayahudi tu, kwani wako watu wengi hukanusha haki na kuipinga sio kwa lolote isipokuwa ni kwa vile haiafikiani na tamaa zao. Kwa sababu ya kupelekwa na mapenzi na manufaa yake na wala sio kwa dini na akili. Amirul Mumini anasema: “Vita vya akili mara nyingi viko kwenye tamaa.”
Basi sameheni na muwache mpaka Mwenyezi Mungu alete amri yake.
Yaani achaneni nao hivi sasa wala msiwaingilie kuwatia adabu mpaka Mwenyezi Mungu awaamrishe hilo; kwani mambo yana wakati wake. Tafsiri nyingi zinasema kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) aliwaamrisha Waislamu kuachana nao mpaka iliposhuka kauli yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.):
قَاتِلُوا الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِاللَّهِ وَلَا بِالْيَوْمِ الْآخِرِ{29}
NaAya nyenginezo zavita.
Razi amesema: “Imam Muhammad Baqir (a.s.) anasema: Hakika Mwenyezi Mungu hakumwamrisha Mtume wake vita mpaka aliposhuka Jibril na kauli yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.):
أُذِنَ لِلَّذِينَ يُقَاتَلُونَ بِأَنَّهُمْ ظُلِمُوا ۚ وَإِنَّ اللَّهَ عَلَىٰ نَصْرِهِمْ لَقَدِيرٌ {39}
Kuikhalifu Haki
Mambo yote ya maisha miongoni mwa kufuru, ulahidi, uovu, kuvunjwa heshima na ufisadi. Vile vile dhuluma, utaghuti, vita na ufukara, yote hayo yanasababishwa na kitu kimoja - kuihalifu haki. Lau watu wote, si kadhi peke yake, wangelichunga haki, wangeliishi wote kwa amani na raha. Kauli yake Mwenyezi Mungu:
فَمَاذَا بَعْدَ الْحَقِّ إِلَّا الضَّلَالُ ۖ{32}
Ni kuonyesha hakika hii.
Ni kweli kuwa haki haikosi watetezi wakati wowote ule, lakini ni wachache. Lau haki ingelipata watetezi kama ilivyo batili, basi ulimwengu wote ungelikuwa katika uzuri na amani. Bali lau kila mtu angeliitaka haki yake na akatekeleza wajibu wake, tusingeliona dhulma wala batili hata athari yake.
Mwenyezi Mungu ameisimamishia haki dalili za kuongoza kwenye hiyo haki. Hayo yanatolewa dalili na maumbile, kitabu chake Mwenyezi Mungu na kutokana na Mtume Mtukufu.
Vile vile watu watakatifu wa nyumba ya Mtume aliowaweka sawa na Qur’an; kama ilivyoelezwa katika Hadith thaqalayn ambayo ameipokea Muslim katika Sahih yake. Mwenye kuipinga dalili hii hali anajua atakuwa amempinga Mwenyezi Mungu na Mtume wake; sawa na walivyofanya Mayahudi na washirikina.
وَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَآتُوا الزَّكَاةَ ۚ وَمَا تُقَدِّمُوا لِأَنْفُسِكُمْ مِنْ خَيْرٍ تَجِدُوهُ عِنْدَ اللَّهِ ۗ إِنَّ اللَّهَ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ {110}