read

Aya 124: Ahadi Yangu Haiwafikii Waovu

Lugha

Makusudio ya kujaribiwa hapa ni kukalifishwa. Makusudio ya maneno ni amri na makatazo ikiwa ni pamoja na kukalifishwa kumchinja mwanawe. Makusudio ya kuyatimiza ni kutii.

Maana

Na Mola wake alipomjaribu Ibrahim kwa matamko naye akayatimiza.

Ibrahim Al-khalil (a.s.) ni baba wa Mitume. Dini tatu (Uislamu, Ukristo na Uyahudi) zinakubali na kuthibitisha Utume wake. Washirikina wa Kiarabu wakijitukuza kwa kunasibika kwao na mwanawe Ismail (a.s.) na kwa kutumikia kwao Al-Kaaba, na kuihami, ambayo imejengwa na Ibrahim na mwanawe Ismail (a.s.).1 Mwenyezi Mungu anabainisha kwamba Yeye alimwamrisha Ibrahim baadhi ya taklifa, kama vile kumchinja mwanawe, akawa mwaminifu mwenye kutekeleza amri na kuitii. Mwenyezi Mungu amemsifu Ibrahim kuwa mtekelezaji aliposema:

وَإِبْرَاهِيمَ الَّذِي وَفَّىٰ {37}

“Na Ibrahim aliyetekeleza (ahadi).”(53:37)

Akasema: hakika mimi nimekufanya Imam wa watu

Hii ni bishara kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa Ibrahim, ya kumfadhilisha na Uimamu tangu mwanzo na bila ya yeye kuomba, ikiwa ni malipo ya Ikhlasi yake na utekelezaji wake, na pia kujitolea kwake mhanga.

Akasema na katika kizazi changu pia.

Haya ni matakwa na dua kutoka kwa Ibrahim (a.s.) kwamba Mwenyezi Mungu aneemeshe baadhi ya kizazi chake, kama alivyomnemeesha yeye. Kwa sababu neno ‘katika’ hapa ni kufahamisha baadhi. Hapa yanadhihiri mapenzi ya mzazi kwa mwanawe, kwa vile alivyotaka Ibrahim wema kwa baadhi ya kizazi chake na wala asijitakie yeye mwenyewe peke yake.

Akasema: Ahadi yangu haiwafikii madhalimu.

Kauli hii ni kumwitika Ibrahim maombi yake ya kufanywa Maimam baadhi ya kizazi chake kwa masharti ya kuwa wawe kama yeye; watekelezaji ahadi na wacha Mungu. Kwa sababu kazi ya Imamu ni kuzuia maasi, vipi awe yeye ndiye mwasi.

Sioni kauli inayofahamisha zaidi uadilifu wa Imamu na huruma yake kwa raia kuliko kauli ya Imam Ali (A.S) alipokuwa ni khalifa wa Waislamu: “Umma hivi sasa unaogopa dhulma ya viongozi wake na mimi nahofia kuwadhulumu raia zangu.”

Kiongozi anaogopa kuwadhulumu raia; mwenye nguvu anaogopa kuwadhulumu wanyonge; tena mtu mwenye nguvu ambaye hajali mauti. Yaani imekuwa yule mwenye utawala anahofia juu ya raia zake ambapo ingekuwa kinyume; kama ilivyozoeleka! Ni jambo ambalo si la kawaida.

Uimamu Na Fikra Ya Isma

Neno Imam (kiongozi) hutumika katika maana nyingi kama vile: njia, kwa sababu inamwongoza mwendaji kwenye makusudio yake. Pia lina maana ya anayoyafuata mtu kumwongoza au kumpotosha, Mwe-nyezi Mungu anasema:

وَجَعَلْنَاهُمْ أَئِمَّةً يَهْدُونَ بِأَمْرِنَا{73}

“Na tukawafanya ni maimamu wanaoongoza kwa amri yetu...”(21:73)

Katika Aya nyingine amesema:

وَجَعَلْنَاهُمْ أَئِمَّةً يَدْعُونَ إِلَى النَّارِ ۖ{41}

“Na tukawafanya ni maimamu waitao katika moto...” (28:41)

Mtu anakuwa Imam, ikiwa anafuatwa katika jambo fulani, na anakuwa Maamum ikawa yeye ndiye anayefuata.

Hayo ni kwa mujibu wa lugha. Ama kwa mujibu wa dini na sharia, ni kwamba neno Imam linatumiwa kwa anayeongoza swala, lakini katika maana hayo hutumiwa kwa kuunganishwa na neno jingine; kama vile Imam wa Ijumaa na jamaa. Ikiwa ametajwa Imam tu, bila ya neno lolote jingine, basi litatumika kwa maana mbili:

Kwanza, kwa maana ya Utume. Hiyo ni daraja ya juu zaidi ya Uimamu. Pili, kwa maana ya Wasii wa Mtume.

Imam kwa maana ya Utume na Imam kwa maana ya wasii, anakuwa ni mwenye kufuatwa katika kila kitu, naye hamfuati yeyote wakati wa Uimamu wake. Uimamu kwa maana ya Utume unahitajia nukuu (nassi) kutoka kwa Mwenyezi Mungu kupitia kwa Roho mwaminifu.

Na Uimamu kwa maana ya wasii hauna budi kuwa ni kwa nukuu kutoka kwa Mwenyezi Mungu kupitia kwa ulimi wa Mtume wake mtukufu. Sharti ya nassi hiyo ni kuwa kwa jina na kwa mtu maalum, sio kwa sifa na kwa tamko la ujumla; kama ilivyo kwa Mujtahid na hakimu wa sharia (kadhi). Bali ni lazima iwe ni kwa nukuu mahsus isiyokubali taawil au uwezekano wa kinyume.

Kuanzia hapa ndio inabainika kwamba kutumia neno Imam peke yake kwa asiyekuwa Mtume au Wasii ni jambo la kuangaliwa vizuri na sio mbali kuwa ni haramu, sawa na kutumia neno Wasii wa Mtume kwa asiyekuwa Imam Massum.

Vyovyote iwavyo, kauli ya Imam huyu - awe Mtume au Wasii - ni kauli ya Mwenyezi Mungu; uongozi wake ni wa Mwenyezi Mungu; hukumu yake ni hukumu ya Mwenyezi Mungu ambayo haina kinyume. Yeyote mwenye kudai kitu bila ya kuthibitisha kwa nukuu inayomuhusu basi huyo ni mzushi mwongo.

Bora ya niliyoyasoma katika sifa ya Imam ni kauli ya Imam mtukufu Zainul-abidiin (a.s.) katika Sahifa Sajjadiyya: “Ewe Mwenyezi Mungu! Hakika wewe umeitia nguvu dini yako kila wakati kwa Imam uliyemweka kuwaelimisha waja wako; na ni mnara katika miji yako baada ya kuiunganisha kamba yake na yako. Na ukawajaalia ni nyenzo ya radhi zako. Na umefaradhisha kutiiwa na ukahadharisha kuasiwa; umeamrisha kufuatwa maamrisho yake na kuachwa makatazo yake na kutotanguliwa na mtangulizi yeyote au kubaki nyuma naye yeyote. Yeye ni ngome ya wanaotafuta hifadhi na ni pango la Waislamu: Ni tegemeo la waumini na ni fahari ya Mola wa viumbe vyote.”

Hizo ndizo sifa za ambaye amechaguliwa na Mwenyezi Mungu kuwa Imam kwa waja wake. Kimsingi ni kwamba Uimamu wa Utume na ule wa Uwasii unahitajia Isma (kuhifadhiwa na dhambi) haiwezekani bila ya hivyo, kwa sababu kipofu hawezi kumwongoza kipofu mwenzake. Mwenye uchafu na ambaye ana haddi (adhabu) hawezi kumfanyia haddi mwingine.

Wamelitolea daili hilo Shia Imamiya kwa kauli yake Mwenyezi Mungu:

Hakika mimi nimekufanya Imam wa watu.

Kwamba Uimam hauwi ila kwa kufanywa na Mwenyezi Mungu. Hilo linatiliwa nguvu na ombi la Nabii Ibrahim kwa Mwenyezi Mungu kufanywa Maimamu katika kizazi chake.

Ikiwa Uimamu ni kwa kufanywa na Mwenyezi Mungu (s.w.t.) utakuwa unatokana na nukuu kutoka kwake.

Vile vile wametolea dalili Shia, kauli Yake Mwenyezi Mungu:“Ahadi yangu haiwafikii madhalimu.”

Kwamba ni wajibu kupatikana Isma kwa Mtume na Wasii. Njia ya kutolea dalili ni kuwa Mwenyezi Mungu amewabainishia wazi wazi kuwa Yeye hautoi Uimamu kwa dhalimu; na dhalimu ni yule aliyefanya madhambi katika maisha yake kwa namna yoyote ile, hata kama atatubia baada yake, lakini jina hili litakuwa limempitia. Kwa hivyo mwenye kuwa na hilo hawezi kuwa Imam.

Inatokea sadfa mtu mwengine asiyekuwa Ali kukua katika malezi ya ushirikina na uchafu, kuabudu masanamu, kuzama katika uchafu wa kijahilia na wala asitamke shahada mbili ila baada ya kuyashiba masanamu na kuyasujudia.

Kwa upande mwingine Mwenyezi Mungu akataka Ali bin Abi Twalib akulie katika malezi ya Mtume yaliyo na usafi; na Mtume amtengeneze kulingana na matakwa ya Mwenyezi Mungu na kuyaangusha masanamu kutoka kwenye hadhi yake na kuyatupa chini ya miguu ya Muhammad (s.a.w.)

Hapa kuna swali tunalolitoa kwa kila mwenye akili mwenye kuchunga haki, ili ajijibu yeye mwenyewe kwa akili yake; nalo ni hili:

Mtu asiyejua kutumia vizuri, amerithi mali kutoka kwa baba yake, ikabidi awe na msimamizi atakayemlinda na kumuhifadhia mali yake. Sasa kukawa na utatanishi wa kumpa usimamizi mtu ambaye hakuwahi kumwasi Mwenyezi Mungu katika uhai wake, si kwa dhambi dogo au kubwa, au apewe usimamizi mtu aliyewahi kumwasi Mwenyezi Mungu kwa muda mrefu akiwa amekwisha baleghe, kisha akatubia; je tumchague yupi?

Inatosha kuwa ni dalili ya kuhifadhiwa na madhambi (Isma) kwa Ahlul Bait (a.s.) kutokana na alivyowatolea ushahidi Mwenyezi Mungu aliposema:

إِنَّمَا يُرِيدُ اللَّهُ لِيُذْهِبَ عَنْكُمُ الرِّجْسَ أَهْلَ الْبَيْتِ وَيُطَهِّرَكُمْ تَطْهِيرًا {33}

“Hakika Mwenyezi Mungu anataka kuwaondolea uchafu enyi watu wa nyumba ya Mtume na kuwatakasa kabisa kabisa.” (33:33)

Tumezungumzia Isma kwa ufafanuzi katika kufasiri Aya ya 39 kifungu cha Isma ya Mitume na kifungu cha Ahlul Bait: Tafad-hali rejea, kwani kifungu hiki ni ukamilisho wa vifungu hivyo vilivyopita.
Fikra ya Isma (kuhifadhika na makosa) haihusiki na Shia tu. Masunni pia wameizungumzia, akini wao wanaijaalia kwa umma, wakitegemea Hadith ambayo haikuthibiti kwa Shia, nayo ni “Umma wangu hauwezi kukusanyika juu ya jambo la upotovu.”

Wakristo nao wanasema Baba mtakatifu ana Isma. Wakomunisti wamesema Marx na Lenin pia wana Isma. Makabaila wa Syria nao wamesema iko Isma kwa Antony Saada, na wanachama wa Ikhwanul- Muslimin (ndugu wa Kiislamu) wamesema Hassan Al-Banna anayo Isma. Huko China, hivi leo ninapoandika tafsir hii ni mwaka 1967, mamilioni ya watu wanaamini kuwa Mao Tse Tung ana Isma na wanajizatiti kwa mafunzo yake.

Wakomunisti; tuliowataja wakitofautiana huwa wanatofautiana katika kauli za viongozi na makusudio, sio katika wajibu wa kuwafuata na kuwafanya viongozi; sawa na vile wanavyohitlafiana Waislamu katika tafsir ya Qur’an au Wakristo katika tafsir ya Injil.

Yeyote atakayeihuisha Isma kwa Mashia peke yao, basi atakuwa ni mmoja kati ya hawa wawili. Ama atakuwa ni mjinga mwenye kughafilika au mzushi mwenye njama.

وَإِذْ جَعَلْنَا الْبَيْتَ مَثَابَةً لِلنَّاسِ وَأَمْنًا وَاتَّخِذُوا مِنْ مَقَامِ إِبْرَاهِيمَ مُصَلًّى ۖ وَعَهِدْنَا إِلَىٰ إِبْرَاهِيمَ وَإِسْمَاعِيلَ أَنْ طَهِّرَا بَيْتِيَ لِلطَّائِفِينَ وَالْعَاكِفِينَ وَالرُّكَّعِ السُّجُودِ {125}

Na tulipoifanya ile nyumba (Al-Kaa’ba) iwe mahali pa kuendewa na watu na mahala pa amani. Na pafanyeni alipokuwa akisimama (Maqamu) Ibrahim ni mahali pa kuswalia. Na tuliagana na Ibrahim na Ismail kuwa: Itakaseni nyumba yangu kwa ajili ya wale wenye kutufu na wenye kujitenga huko kwa ibada na wanaorukuu na kusujudu.

وَإِذْ قَالَ إِبْرَاهِيمُ رَبِّ اجْعَلْ هَٰذَا بَلَدًا آمِنًا وَارْزُقْ أَهْلَهُ مِنَ الثَّمَرَاتِ مَنْ آمَنَ مِنْهُمْ بِاللَّهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۖ قَالَ وَمَنْ كَفَرَ فَأُمَتِّعُهُ قَلِيلًا ثُمَّ أَضْطَرُّهُ إِلَىٰ عَذَابِ النَّارِ ۖ وَبِئْسَ الْمَصِيرُ {126}

Na aliposema Ibrahim: Ewe mola wangu! Ufanye mji huu uwe wa amani na uwaruzuku wakazi wake matunda wale wanaomwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho katika wao. Akasema Mwenyezi Mungu: Na mwenye kukufuru nitamstarehesha kidogo; kisha nitamsukumiza katika adhabu ya moto napo ni mahali pabaya kabisa pa kurejea.
  • 1. Mwenye Bahrul Muhit amesema: “Ibrahim ni babu wa thalathini na moja wa Muhammad; naye ni Ibrahim bin Tarih, bin Najur bin Sarugh, bin Arghu, bin Faligh bin Abir ambaye ni Mtume Hud. Naye alizaliwa katika ardhi ya Ahwaz.”