read

Bismillah

Tamko hili tukufu ni nembo maalum ya Waislamu. Kwalo Wanaanzia maneno na vitendo vyao vyote; na iko kwenye daraja ya pili baada ya shahada mbili.

Ama wasiokuwa Waislamu, huanza: Kwa jina Lako ewe Mwenyezi Mungu Kwa jina Lake Mtukufu, kwa jina la Mwenye kuanza, na Mwenye kuishiliza au Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu n.k.

Huondolewa hamza katika neno ism katika Bismillahi, linapotamkwa na kuandikwa kwa sababu ya kutumiwa sana. Na, huondolewa hamza kwa kutamkwa, na sio kwa kuandika mahali pengine; kama vile sabbihisma rabbikal-aala na Uqsimu billah.

Tamko Allah (Mwenyezi Mungu) lina maana ya Mwenye kuabudiwa kwa haki, ambaye husifika na sifa zote za utukufu na ukamilifu, wala hakisifiwi kwa sifa hiyo kitu kingine chochote.

Inasemekana kuwa Mwenyezi Mungu ana jina moja Tukufu, na kwamba atakayelijua, basi atamiminikiwa na heri na atakuwa na miujiza. Lakini sisi tunaamini na kuitakidi kwamba kila jina la Mwenyezi Mungu ni tukufu; yaani huyo Mwenyezi Mungu ni Mtukufu. Kwa sababu haiwezekani kabisa kuufanya upande mmoja ni bora kuliko upande mwingine, kuboresha kutaleta ushirika na kuzidi; na ambaye hana mfano wa kitu chochote, hawezi kushirikiana na yeyote katika kitu.

Neno Rahman (Mwingi wa Rehema) ni sifa. Limechukuliwa kutoka katika Rahma (Rehema). Maana yake kwa upande wa Mwenyezi Mungu ni kufanya hisani na kwa upande wa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, lina maana ya upole wa moyo.

Limezoeleka kutumiwa kwa maana ya dhati yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.), likawa ni katika majina mema ya Mwenyezi Mungu.

Mwenyezi Mungu anasema:

قُلِ ادْعُوا اللَّهَ أَوِ ادْعُوا الرَّحْمَٰنَ ۖ أَيًّا مَا تَدْعُوا فَلَهُ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ ۚ{110}

“Sema! Muombeni (kwa jina la) Mwenyezi Mungu, au muombeni (kwa jina la) Mwingi wa rehema; kwa jina lolote mnalomwita (itafaa), kwani ana majina mema”. (17:110)

Neno Rahim (Mwenye kurehemu) vile vile, ni sifa. Limechukuliwa kutoka katika neno Rahma. Wafasiri wengi wametofautisha kati ya matamko haya (Rahman na Rahim) kwamba Rahman ni rehema yenye kuenea kwa muumini na kafir; na Rahim ni rehema yenye kuwahusu waumini peke yao. Wakasema: Ewe Mwingi wa Rehema katika dunia na Akhera na ewe Mwenye Kurehemu akhera tu. Ama mimi nasema: Ewe Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu katika dunia na akhera.

Mwenyezi Mungu anasema:

أَهُمْ يَقْسِمُونَ رَحْمَتَ رَبِّكَ ۚ{32}

“Je, wao wanaigawa rehema ya Mola wako?” (43:32)

Kwa ujumla maana ya “Bismillaahir rahmani rahim” ni kwamba wewe unaanza kitendo chako kwa kumtaka msaada ambaye rehema Yake imekienea kila kitu na kusajili katika nafsi yako kwamba unayoyafanya ni kwa jina lake, sio kwa jina lako wala kwa jina la mwingine yeyote asiyekuwa Yeye. Si kama vile anavyosema mtumishi wa serikali kuwaambia raia: “Kwa jina la taifa ninawaambia kadhaa…”

Bismillah inafahamisha kwamba kitendo unachofanya ni halali hakina shaka ya haramu. Kama kitendo ni haramu na ukakifanya kwa Bismillaah, basi utakuwa umeasi mara mbili kwa mpigo. Kwanza, ni kuwa kitendo chenyewe ni haramu. Pili, ni kuwa umesema uongo kwa kukinasibisha na Mwenyezi Mungu. Ametakasikia Mwenyezi Mungu na hayo kabisa.

Hukumu

Kwa upande wa Shia Imamiya, Bismillah ni sehemu ya sura na wamewajibisha kuisoma kwa sauti katika swala ambayo ni wajibu kusoma Alhamdu na sura kwa sauti; kama vile swala ya Asubuhi (Al-fajr) na rakaa mbili za mwanzo za swala ya Maghrib na Isha. Ni Sunna kusoma kwa sauti katika swala ambayo haisomwi kwa sauti kama vile swala ya Adhuhuri na Alasiri.

Hanafi na Maliki wamesema kuwa inajuzu kuiacha Bismillaah katika swala, kwa sababu si sehemu ya sura. Shafi na Hambali wamesema ni sehemu ya sura; ispokuwa Hambal wamesema kuwa isisomwe kwa sauti wakati wowote wa swala.

Shafi nao kwa upande wao, wakasema isomwe kwa sauti katika swala ya Asubuhi (Al-fajr) na rakaa mbili za Maghribi na Isha. Hapa kauli ya Shafi na Hambal haziko mbali na kauli ya Imamiya.

Kwa ujumla ni kwamba herufi hizi za Bismillah zinatengeneza jina la Mwenyezi Mungu Mtukufu na sifa Zake. Hutamkwa na kuandikwa kama maneno mengine, lakini lina heshima na hukmu mahsusi. Haijuzu kuliandika juu ya karatasi, au kwa wino, kalamu au kitu chochote kilicho najisi. Vile vile haijuzu kuligusa bila ya twahara.

Wataalamu wa Fiqhi wa Kiimamiya wamefutu kwamba mwenye kuutupa msahafu makusudi katika uchafu, kuupiga teke, kuupasua kwa dharau, au kuufanyia kitu chochote kinachoonyesha dharau, basi amekuwa kafiri aliyeritadi.

Msemaji mmoja amesema kuwa Sura ya Fatiha imekusanya maana yote ya Qur’ran, na kwamba Bismillah imekusanya maana yote ya Fatiha, na herufi Ba katika Bismillah imekusanya maana yote ya Bismillah. Hatimaye herufi Ba inakuwa imekusanya maana yote ya Qur’an.

Msemaji huyu ni kama yule anayejaribu kuuingiza ulimwengu pamoja na ardhi yake na mbingu yake katika yai bila ya kulikuza yai hilo au kuufanya mdogo ulimwengu!

Nembo Ya Uislamu

Nilisoma makala katika gazeti la Al-Jumhuriyya la Misri la tarehe 21 Aprili 1967 yaliyoandikwa na Dhiyau Rayis, kwamba yeye alisoma makala katika jarida la fasihi la mwandishi mashuhuri wa Kiarabu akisema “(Huyo mwandishi) alipokuwa Uingereza, aliwahi kubishana vikali na msomi mmoja Mwingereza kuhusu Uislamu na Ukristo.

Akasema yule Mwingereza kupingana na Waislamu wote: “Mimi ninaifupisha misingi yote ya Kikristo kwa neno moja tu, ‘Upendo’. Je unaweza wewe Mwislamu kuleta tamko linalokusanya misingi ya Kiislamu?” Yule mwandishi akajibu: “Ndio neno hilo ni ‘Tawhid’.

Baada ya Rayis kunakili mazungumzo haya akasema: “Jawabu halikuwa sawa.” Akataja sababu kadhaa za kutomwafiki kwake, kisha akasema: “Lau swali hili ningeulizwa mimi, ningelijibu kuwa ni ‘Rehema.’ Akatoa dalili kwa Aya nyingi na Hadith nyingi, akianzia na Bismillahir rahmanir rahim mpaka Aya inayosema:

وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا رَحْمَةً لِلْعَالَمِينَ {107}

“Nasi hatukukutuma ila uwe rehema kwa walimwengu.” (21:107)

Amesema kweli Rayis kwamba jawabu la yule mwandishi halikuwa sawa. Lakini hata yeye Rayis pia jawabu lake halikuafiki, kwa kuchagua neno ‘rehema’. Kwa sababu hakuzidisha kitu katika aliyoyasema Mwingereza. amechukua neno ‘upendo’ na kulifasiri rehema. Kwa hiyo Uislamu unakuwa hautofautiani na Ukristo.

Lau mimi ningelikuwa pamoja na yule mwandishi, ningelijibu kwa neno unyoofu’. (msimamo) Kwa sababu ni neno lenye kukusanya unyoofu katika itikadi tawhidi, vitendo, maadili, hukumu, na mafundisho yote yaliyo na rehema mapenzi na kusaidiana. Rehema ni moja katika misingi ya Kiislamu na sio Uislamu kamili; kama vile ambavyo tawhidi ni msingi katika misingi ya Uislamu na sio misingi yake yote.

Unyoofu ndio kipimo sahihi cha ukamilifu ambao mtu aweza kuufikilia wema wa dunia na Akhera. Ndio maana tunakariri katika swala zetu usiku na mchana: “Tuongoze njia iliyonyooka.” Mwenyezi Mungu amesema kumwambia Mtume wake mtukufu (s.a.w.):

فَاسْتَقِمْ كَمَا أُمِرْتَ وَمَنْ تَابَ مَعَكَ وَلَا تَطْغَوْا ۚ إِنَّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ {112}

“Endelea na unyoofu kama ulivyoamrishwa, (wewe) na wale wanaoelekea (kwa Mwenyezi Mungu) pamoja nawe; wala msiruke mipaka.. Hakika Yeye anayaona mnayoyatenda.(11:112)

Amesema tena:

إِنَّ الَّذِينَ قَالُوا رَبُّنَا اللَّهُ ثُمَّ اسْتَقَامُوا تَتَنَزَّلُ عَلَيْهِمُ الْمَلَائِكَةُ أَلَّا تَخَافُوا وَلَا تَحْزَنُوا وَأَبْشِرُوا بِالْجَنَّةِ الَّتِي كُنْتُمْ تُوعَدُونَ {30}

“Hakika wale waliosema: Mola wetu ni Mwenyezi Mungu kisha wakafuata unyoofu, hao Malaika huwateremkia (wakiwaambia): Msiogope wala msihuzunike, na furahini kwa Pepo mliyokuwa mkiahidiwa.(41:30)

Hakuna kitu kinachofahamisha zaidi kwamba unyoofu ni muhimu, kuliko neno la Ibilisi aliyelaaniwa:

قَالَ فَبِمَا أَغْوَيْتَنِي لَأَقْعُدَنَّ لَهُمْ صِرَاطَكَ الْمُسْتَقِيمَ {16}

Basi nitawakalia (waja wako) katika njia yako iliyonyooka...(7:16)

Kuna Hadith tukufu inayosema kuwa Sufyan Thaqafi alimwambia Mtume: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Niambie neno ambalo sitamuuliza mtu mwingine baada yako milele.” Mtume wa Mwenyezi Mungu akamwambia:”Sema nimemwamini Mwenyezi Mungu, kisha ufuate njia iliyonyooka.”

Kwa ufupi maana ya unyoofu ni kuwa ndani ya mipaka ya Mwenyezi Mungu bila ya kukengeuka na haki kwa kuifuata batili na kuacha uongofu na kuwa katika upotevu. Vile vile kuwa kwenye njia iliyonyooka, njia ya (wale) ambao Mwenyezi Mungu amewaneemesha, sio ya wale walioghadhibikiwa wala waliopotea.