Sura Ya Pili: Al – Baqarah
Amesema mwenye Majmaul-Bayan kwamba sura hii yote imeshuka Madina, isipokuwa Aya ya 281.
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ
الم {1}
ذَٰلِكَ الْكِتَابُ لَا رَيْبَ ۛ فِيهِ ۛ هُدًى لِلْمُتَّقِينَ {2}
الَّذِينَ يُؤْمِنُونَ بِالْغَيْبِ وَيُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنْفِقُونَ {3}
وَالَّذِينَ يُؤْمِنُونَ بِمَا أُنْزِلَ إِلَيْكَ وَمَا أُنْزِلَ مِنْ قَبْلِكَ وَبِالْآخِرَةِ هُمْ يُوقِنُونَ {4}
أُولَٰئِكَ عَلَىٰ هُدًى مِنْ رَبِّهِمْ ۖ وَأُولَٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ {5}
Aya 1-2: Mianzo Ya Baadhi Ya Sura
Alif Lam Mim
Wamehitalifiana wanavyuoni kuhusu makusudio ya mwanzo huu na ya mianzo ya sura nyingine inayofanana na hii mfano: Alif Laam Miim Raa, Kaaf Haa Yaa A’yn Swaad na Haa Miim. Imesemekana kuwa herufi hizo ni katika elimu ya ghaibu ambayo Mwenyezi Mungu hakuidhihirisha kwa yeyote.
Lakini sidhani kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anaweza kuwaambia watu jambo asilotaka walijue. Zaidi ya hayo Mwenyezi Mungu amewakemea wale ambao hawaifikiri vizuri Qur’an, aliposema:
أَفَلَا يَتَدَبَّرُونَ الْقُرْآنَ أَمْ عَلَىٰ قُلُوبٍ أَقْفَالُهَا {24}
Pia imesemekana mianzo hii ni majina ya sura; vilevile imesemwa ni majina ya Mwenyezi Mungu, aidha ikasemwa kuwa ni ya Muhammad (s.a.w.) nk.
Lakini linaloelekea zaidi ni kauli inayosema kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) baada ya kuwaambia wapinzani walete mfano wa Qur’an, au sura kumi, au moja; na wakashindwa, ndipo akataja herufi hizi. Yaani, kitabu hiki ambacho ni muujiza, hutokana na herufi hizi ambazo hata watoto na wajinga pia wanazitumia, lakini nyinyi mmeshindwa.
Kwa hivyo kushindwa kwenu ni dalili wazi kwamba kuna siri, na siri yenyewe ni kuwa hii Qur’an ni wahyi wa kidini sio usanii wa kidunia.
Qur’an Na Sayansi
Kauli yake Mwenyezi Mungu: Ni uwongozi kwa wamchao Mwenyezi Mungu, ni dalili wazi kwamba Qur’an si kitabu cha elimu ya Historia, wala Falsafa, au elimu ya Fizikia au ya Hesabu; isipokuwa ni kitabu cha elimu ya uongofu wa mwana-adamu katika dunia na akhera, au sema Qur’an ni kitabu cha dini, maadili, itikadi na sharia.
Kama utauliza: “Ikiwa Qur’an ni kitabu cha dini, mbona basi kuna Aya zinazohusu mambo ya kilimwengu; kama vile
وَالشَّمْسُ تَجْرِي لِمُسْتَقَرٍّ لَهَا ۚ…وَالْقَمَرَ قَدَّرْنَاهُ مَنَازِلَ…
Jibu: Lengo la Aya hizi sio kutubainishia hali ya maumbile kwa undani wa kielimu - kwani hilo limeachiwa akili na majaribio yake - isipokuwa lengo la kwanza la kutajwa Aya hizo ni kwamba, kujua ulimwengu na nidhamu yake kutatuongoza kujua kuwa kuna Mungu, na kwamba huu ulimwengu haukupatikana kibahati tu bila ya kukusudiwa; kama wanavyodai watu wa kimaada. Bali ulipatikana kwa matakwa ya kihekima.
MwenyeziMungu amelibainisha hilokatikaAyaisemayo:
سَنُرِيهِمْ آيَاتِنَا فِي الْآفَاقِ وَفِي أَنْفُسِهِمْ حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَهُمْ أَنَّهُ الْحَقُّ ۗ{53}
Yaani, tutawafafanulia makafiri - kwa vile watakavyoufahamu ulimwengu kutokana na mipangilio mizuri ya Mwenyezi Mungu - kuwa wao wako katika upotevu.
Qur’an inapotoa mwito wa kuangalia ulimwengu, inasema kwa lugha iliyo wazi kuwa dalili za ulimwengu ni hoja ya kweli na ni dalili yenye nguvu zaidi juu ya kuwapo Mungu, kuliko kitu chochote.
Baadhi ya wenye hekima wamesema: “Mwenyezi Mungu ana vitabu viwili: Kitabu kinachosomwa na kitabu cha akili, ambacho ni ulimwengu.”
Ni kweli kuwa Qur’an inahimiza kusoma sayansi na kila elimu itakayompa binadamu ufanisi. Lakini kuhimiza ni kitu kingine na kuwa ni kitabu cha elimu hiyo ni kitu kingine. Katika ambayo yanatia nguvu na kuunga mkono kwamba Qur’an ni kitabu cha uongofu, sharia, na maadili mema, na kwamba Qur’an imeteremshwa kwa lengo hili, ni kauli yake Mwenyezi Mungu:
هَٰذَا بَصَائِرُ مِنْ رَبِّكُمْ وَهُدًى وَرَحْمَةٌ لِقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ {203}
Amesema tena:
كِتَابٌ أَنْزَلْنَاهُ إِلَيْكَ لِتُخْرِجَ النَّاسَ مِنَ الظُّلُمَاتِ إِلَى النُّورِ{1}
Na Mtume mtukufu (s.a.w.) anasema: “Hakika hapana jingine, nimetumwa kutimiza tabia njema”. “Na amesema Amirul Muminin (a.s.) katika hotuba ya 174, ya Nahjul-Balagha: “Hakika Qur’an ni dawa ya ugonjwa mkubwa sana wa kufuru, unafiki na upotevu.”
Kwa maneno haya tunapata tafsiri ya Aya isemayo:
وَنُنَزِّلُ مِنَ الْقُرْآنِ مَا هُوَ شِفَاءٌ وَرَحْمَةٌ لِلْمُؤْمِنِينَ ۙ وَلَا يَزِيدُ الظَّالِمِينَ إِلَّا خَسَارًا {82}
Kama utauliza mara ya pili: Unasemaje kuhusu Aya hii. “Hatukupuuza kitabuni kitu chochote”, (6:38) si inafahamisha kuwa katika Qur’an kuna elimu zote?
Jawabu: Kutosha kila kitu huwa ni kulingana na mahitaji. Ukisema: Nyumba hii ina kila kitu; itafahamika kwamba ina mahitaji ya mwenye kukaa humo. Kama ukisema: Kitabu cha Fiqh kina kila kitu, itafahamika kuwa mna masuala yote ya kifiqh.
Qur’an ni kitabu cha dini. Kwa hiyopale Mungu aliposema. “Hatukupuza kitabuni kitu chochote, maana yake ni kila kinachoambatana na heri ya mtu na uongofu wake.
Swali la tatu: “Unasemaje kuhusu vitabu hivi vyenye majina kama: Qur’an na Sayansi, Uislamu na tiba ya kisasa, na vingenevyo?”
Jibu: Kwanza kabisa, kila anayejaribu kulinganisha kati ya uvumbuzi wa kielimu wa kisasa au wa kizamani na Qur’ani, atakuwa anajaribu jambo lisilowezekana. Kwa sababu elimu ya binadamu ina mpaka kulingana na nguvu yake ya kiakili; na Qur’an ni elimu ya Mwenyezi Mungu ambayo haina mpaka. Itakuwaje kitu kilicho na mpaka kiafikiane na kisichokuwa na mpaka?
Pili, elimu ya binaadamu inaingiliwa na makosa. Kwa sababu inakuwa ni dhana na makisio; inakosea na kupata. Mara ngapi tumewaona wataalamu wakikongamana juu ya nadharia fulani na kudai kuwa ni kweli mia kwa mia; kisha wao wenyewe au wale watakaokuja baada yao wanagundua kuwa ni makosa mia kwa mia? Qur’an ni yenye kuhifadhiwa na makosa. Itakubalika vipi kuoanisha chenye makosa na kile kisicho na makosa? Kisha je tuendelee kugeuza Qur’an kila yanapogeuka makisio ya elimu na nadharia zake? Hapana.
Ndio!Hapanaubayakujisaidianaugunduziwakielimukatikakufahamu baadhi ya Aya, lakini kwa sharti ya kutoufanya huo ugunduzi kuwa ni kipimo cha ukweli na kusihi Qur’an, bali hata kutozifanya hizo elimu kuwa ndio nyezo za kufahamu siri ya Qur’an na kufahamu hekima ya baadhi ya hukumu zake.
Inawezekana kuwa hili ndilo lililowafanya watungaji kutunga vitabu kama: Qur’an na Sayansi n.k.
Vyovyote iwavyo, sisi tuna yakini kwamba tuna hoja zenye nguvu katika dini yetu, na tuna dalili za kutosha juu ya ukweli wake; hatuna haja kabisa na vilivyo kwa wengine. Bali tunaamini kwamba wengine ndio walio na haja kwetu katika hilo.
Kwa hakika historia ya binadamu haitapata dini yenye utengeneo zaidi ya dini ya Kiislamu, wala kitabu chenye kunufaisha zaidi ya kitabu chake, au Mtume mtukufu zaidi ya Mtume wake.
Na yule ambaye hakuongoka kwa dalili za Qur’an na mwito wake wa maisha mema, basi hataweza kukinaishwa na ugunduzi wa kisayansi wa sasa au wa zamani.
Kuna kitu nilichokifikiria ambacho huenda kikapunguza machovu ya msomaji kuhusu majibu ya yule anayejaribu kuilinganisha Qur’an na ugunduzi wa sayansi; kama ifuatavyo:
Uzayr alipita katika mji uliokufa, akiwa na punda wake, chakula chake na kinywaji chake akastaajabu na kusema:
أَنَّىٰ يُحْيِي هَٰذِهِ اللَّهُ بَعْدَ مَوْتِهَا ۖ فَأَمَاتَهُ اللَّهُ مِائَةَ عَامٍ{259}
Mwenyezi Mungu akataka kuuondoa mshangao wake. Akamfisha miaka mia. Chakula na kinywaji alichokuwa nacho, kilibakia katika hali yake bila ya kuharibika katika muda wote huo.
KishaMwenyeziMunguakamfufuanaakatakakumwonyeshamiujiza yake ya ajabu, akamwambia:
فَانْظُرْ إِلَىٰ طَعَامِكَ وَشَرَابِكَ لَمْ يَتَسَنَّهْ ۖ{259}
Hebu angalia msomaji! Je, chakula cha Uzayr kilikuwa katika jokofu (friji)? Swali hili linamhusu mwenye kuilinganisha Qur’an na elimu ya kisasa.
Hakuna anayetia shaka kwamba jokofu hili ambalo lilihifadhi chakula na kinywaji kwa muda wa miaka mia, pengine linaweza kuwa ni sampuli ya mwaka 2000, na wala siyo ya mwaka 1967.
Ndio! Inawezekana kulinganisha sayansi na kufahamu maana ya Qur’an tukufu; hasa kwa upande wa nadharia ya relativity (uwiano).
Kwa vile kufahamu kunahusika na upande fulani katika maana yake, na kunatofautiana na hali ya anayesoma au anayesikiliza.
Kama mtu akisema kuwa tofauti hii haihusiki na Qur’an peke yake, kwa sababu nadharia ya uwiano ni ya jumla, isiyokubali kuhusishwa, tutajibu: Hiyo ni sawa, lakini maana ya Qur’an yamejiandaa na hilo. Na hili linatilia nguvu maelezo yetu kwamba mtu mwenye kuganda na kauli za wafasiri bila ya kuongeza kitu, atakuwa na akili ya kusoma tu, lakini sio akili ya mwamko.
Basi twamuomba Mwenyezi Mungu azijaalie fahamu zetu katika Aya zake kuwa ni za mwamko na sio fahamu za kunakili.
Wamchao Mwenyezi Mungu
Maana ya neno kucha (takua) kilugha ni kujichunga na kitu chochote. Na maana yake kisheria ni kujikinga na hasira za Mwenyezi Mungu na adhabu Yake, kujikinga na kuuacha wajibu na kutenda haram. Amesema Amirul Mumini Ali (a.s.): “Kumcha Mwenyezi Mungu ndio msingi wa tabia njema.” Wengine wamesema kumcha Mwenyezi Mungu ni kuwa Mwenyezi Mungu asikuone na lile alilokataza na kutoacha alilokuamrisha.
Kumcha Mungu ndiko kunakomfanya mtu kuwa bora mbele ya Mwenyezi Mungu. Qur’an inasema:
إِنَّ أَكْرَمَكُمْ عِنْدَ اللَّهِ أَتْقَاكُمْ ۚ{13}
Unaweza kuuliza, ikiwa wenye kumcha Mungu ni wenye kuongoka, basi wana haja gani ya kuongozwa? Je mwanachuoni anahitaji wa kumfundisha?
Jibu: Hakika mwalimu hufundisha wanafunzi wote wajinga na wenye akili, lakini wale wanaonufaika na mwalimu ni wale wenye akili wanaojitahidi ambao mwisho wao utakuwa ni kufaulu. Kwa hivyo ni sawa tukisema kuwa mwalimu ni wa wenye kufaulu. Vile vile Qur’an tukufu imewaeleza watu wote, lakini wanaonufaika nayo ni wale waumini wenye kumcha Mungu. Mwenyezi Mungu anasema: “Na wale wanaokubali kuongoka Mwenyezi Mungu anawazidishia uongofu.” (47:17)