read

Aya 54 – 57: Musa Alipowaambia Watu Wake

Lugha

Manna ni kitu fulani kinachonata mithili ya asali, na Salwa ni tombo (aina ya ndege wa jamii ya kware, kama kuku).

Maelezo

“Na Musa alipowaambia watu wake. Enyi watu wangu! Hakika nyinyi mumejidhulumu kwa kumfanya kwenu Ndama (kuwa ni Mungu). Basi tubuni kwa Muumba wenu.”

Maana yoyote inayofahamika kwa kusikia tu haihitaji tafsiri, bali kuifasiri na kuisherehesha ni ufedhuli tu! Na Aya hii iko katika hali hiyo.

Na jiueni

Makusudio ya kujiua yako wazi, ni kujitoa roho: wala hapana haja ya kufasiri vingine, kwa maana ya kuhalifu mapenzi na kuidhalilisha nafsi kwa kukiri dhambi na makosa au kumwabudu sana Mwenyezi Mungu; kama ilivyosemwa. Makusudio ya kujiua hapa, ni baadhi wawaue wengine. Kwa hivyo yule ambaye hakurtadi dini yake kwa kuabudu ndama ndio atamuua yule aliyertadi dini yake. Sawa na kusema kwake Mwenyezi Mungu: ...Mnapoingia katika majumba jitoleeni salamu.... (24:61)
Na vile vile kusema kwake:”...Wala msijikejeli: yaani msikejeliane (49:11)

Amesema Tabrasi katika Majmaul-Bayan kwa upande wa Shia, na Razi katika Tafsir Al-Kabir, kwa upande wa Sunni, kuwa Mwenyezi Mungu aliijaalia toba yao ni huko kujiua, sio kwamba wajiue baada ya kutubia. Hukumu hii ina mfano wake katika sharia ya Kiislamu, pale ulipozingatia kuua kuwa ni hadi na adhabu ya kosa la kurtadi. Hilo tutalieleza katika kifungu cha kurtadi kinachofuatia.

Zinaendelea Aya kueleza maovu ya Waisrail:

Na mliposema: Ewe Musa! Hatutakuamini mpake tumwone Mungu waziwazi

Wakati Musa alipowaendea na Tawrat, baadhi yao walisema:

“Hatuamini kuwa kitabu hiki kinatoka kwa Mungu mpaka tumwone kwa macho; bila ya kizuwizi chochote kati yetu sisi na Yeye; na atueleze ana kwa ana kuwa Yeye amekutuma na kitabu hiki.”

Sijui kama wale wanaokanusha kuwepo Mwenyezi Mungu wakati huu, kwa kuwa tu hawajamuona kwa wazi, wanategemea Waisrail na inadi yao? Au vipi?

Mayahudi walimwambia Musa: “Hatutakuamini mpaka tumwone Mungu.” Hawa wa sasa nao wanasema: “Hakuna chochote chenye kupatiana isipokuwa kile tunachoweza kukiona kwa jicho, kukigusa kwa mkono, kukinusa kwa pua au kukionja kwa mdomo.”

Hivyo ndivyo inavyokaririka historia ya picha ya upinzani wa haki katika kila kizazi.

Yakawanyakua mauti ya ghafla na hali mwalizania

Yaani adhabu kutoka mbinguni iliwapata wale waliomwambia Musa hatukuamini mpaka tumwone Mungu wazi wazi, wakaangamizwa mbele ya macho ya wale wasiopinga.

Kisha tukawafufua baada ya kufa kwenu ili mpate kushukuru.

Baadhi ya wafasiri kama vile Muhamad Abduh, katika tafsiri Al-Manar, amesema: “Hakika Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hakuwarudishia uhai mara ya pili baada ya kuchukuliwa na ukelele; na kwamba makusudio ya kufufuliwa kwao ni kizazi chao kuwa kingi.”

Wengine wakasema kuwa sio hivyo, hayo hayafahamiki kutokana na dhahiri yake ilivyo, na kwamba waliorudishwa ni wale wale waliouliwa na ukelele. Na hii ndiyo sawa, kwani hapana sababu inayolazimisha taawil, madamu kurudishwa kuwa hai kunawezekana kiakili.

Na hilo lilimtokea Uzair, kama inavyofahamisha Aya: Akasema: Mwenyezi Mungu atauhuisha vipi (mji) huu baada ya kufa kwake? Mwenyezi Mungu Akamfisha kwa miaka mia, kisha akamfufua.... (2:259)

Kimsingi, lililotokea haliwezi kuwa muhali. Kwa hakika inaonyesha kwamba makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu: “Yakawanyakua mauti ya ghafla,” na kauli yake “tukawafufua” ni wale waliokuwa wakati wa Musa waliosema: “Mpaka tumwone Mungu waziwazi.”

Kwa hiyo, kauli haiwahusu Mayahudi waliokuwa na mtume, msemo umeelekezwa kwao kwa kuangalia kuwa wanatokana na kizazi kilichosema hivyo.

Tukawatilia kivuli cha mawingu na tukawateremshia Manna na Salwa.

Hayo yaliyotokea wakati Waisrail walipotoka Misri wakahangaika katika jangwa la Sinai, kusikokuwa na majengo; wakamlalamikia Musa kwa joto la jua; Mwenyezi Mungu akawaneemesha kwa wingu lililowafunika na kuwakinga na joto la jua kali. Vile vile Mwenyezi Mungu akawaneemesha kwa Manna na Salwa ili wale.

Yatakuja maelezo katika tafsiri ya Aya ya 60 kuwa maji yaliwabubujikia kutoka katika jiwe alilolipiga Musa kwa fimbo yake.

Inashangazakuonabaadhiyawafasiri,wakifasiriyalealiyoyanyamazia Mwenyezi Mungu kuyabainisha; kama vile idadi ya waliojiua kwa toba ya kuabudu ndama, kuwa ni watu elfu moja; vile vile walionyakuliwa kuwa ni watu sabini.

Ama kuhusu Manna, wanadai kila mtu alikuwa akipata pishi moja na kwamba Salwa ilikuwa ikishuka kutoka mbinguni ikiwa moto moto huku ikifuka moshi, na mengineyo ambayo hayana kauli yoyote iliyopokewa au kudhaniwa.

Imethibiti Hadith kutoka kwa Mtume mtukufu (s.a.w.): “Hakika Mwenyezi Mungu amenyamazia mambo si kwa kusahau, ni kwa kuwaonea huruma, kwa hiyo msijikalifishe nayo.”
Katika Nahjul-Balagha amesema Imam Ali (a.s.): “Hakika Mwenyezi Mungu amewafaradhisha faradhi msizipoteze, na amewawekea mipaka msipetuke; na ameyakataza mambo basi msifanye; na ameyanyamazia mambo si kwa kusahau, basi msijikalifishe (nayo).”

Na hawakutudhulumu sisi, lakini wamejidhulumu wenyewe.

Kukanusha dhulma kwa Mwenyezi Mungu ni sawa na kukanusha kuwa na watoto na mshirika; yaani kumwepusha kabisa na hilo; sawa na kumwambia mseja kuwa hana mtoto.

Ama kujidhulumu kwa Mayahudi ni kwa sababu ya usafihi wao na kuzikanusha neema za Mwenyezi Mungu ambaye hanufaiki na twaa ya mwenye kumtii wala hayamdhuru maasi ya mwenye kuasi na madhara ya uasi yanamrudia mwasi. Anasema Ali bin Abu Twalib (a.s.): “Ewe mwanadamu ukiona Mola wako anaendelea kukuneemesha nawe unamwasi, basi mhadhari.”

Kwa ufupi Aya hizi zinaonyesha ibada ya Waisrail kwa ndama, kutubia kwao kwa kujiua na kutaka kwao kumwona Mwenyezi Mungu. Vile vile kuangamia kwao na kufufuliwa kwao, kufunikwa na kiwingu na kulishwa Manna na Salwa.. Tutaelezea kisa cha Nabii Musa na Waisrail katika surah ya Maida (5) Inshallah. Waliposema kumwambia Musa:

فَاذْهَبْ أَنْتَ وَرَبُّكَ فَقَاتِلَا إِنَّا هَاهُنَا قَاعِدُونَ {24}

...Basi nenda wewe na Mola wako mkapigane sisi tutakaa hapa” (5:24)

Hilo ni tamko linaloonyesha ukhabithi na uduni wa Mayahudi.

Wa kwanza waliogundua uhabithi na uduni wao ni watu wa Firaun ambao waliwachinja watoto wao wa kiume na kuwaacha wa kike.

Kumwona Mwenyezi Mungu

Kutokana na Aya tukufu: “Mpaka tumwone Mungu waziwazi” tutaonyesha mzozo uliopo katika madhehebu ya Kiislamu na tofauti zao kuwa akili inajuzisha kuonekana Mwenyezi Mungu kwa macho au la! Wamesema Ash’ari (Sunni): “Hakika kuonekana Mungu kwa macho kunawezekana kiakili, kwa sababu Yeye yuko na kila kilichopo kinawezekana kuonekana.”

Imamiya na Mu’tazila wamesema; “Haijuzu kuonekana Mwenyezi Mungu kwa macho katika hali yoyote ile, si duniani wala akhera, kwa sababu Yeye si umbo hata akaonekana, wala haingii katika umbo wala upande fulani.”

Baada ya akili kuthibitisha kutoonekana, wamechukulia kwamba ataonekana kiakili sio kwa macho na kwa hakika ya imani sio ya viungo vya mwili, kwa mujibu wa alivyosema mwanafalsafa mkubwa na mashuhuri, Muhammad bin Ibrahim Shirazi, maarufu kwa jina la Mulla Sadra.

Katika aliyoyatolea dalili Mulla Sadra kuhusu kutoonekana, ni kauli yake: “Kuhisi kitu ni hali inayozuka kwa kile kinachohisi kikikutanishwa na kinachohisiwa kilichozuka. Hivyo basi, kulazimisha kitu ambacho hakikuzuka kuwa kinahisiwa ni kama kulazimisha kitu kisicho na upande kuwa kina upande.”

Kauliyakehii-kamaninavyoona-nikwambajichohaliwezikuonakitu isipokuwa kwa sharti mbili: Liwe linaweza kuona na kiwe kile kinachoangaliwa kinaweza kuonekana kwa jicho.

Hilo ni jambo la msingi; likikosa jicho uwezo wa kuona, au kikiwa kitu hakina uwezo wa kuonekana; itakuwa kuona hakuko. Jicho ni dogo na duni zaidi kuweza kuona dhati tukufu; kama vile ambavyo, Mwenyezi Mungu ni mkubwa wa kuonekana na jicho.

Nilipokuwa nasoma ibara hii, tukufu akili yangu ilienda kwa mwanafalsafa wa Kiingereza John Luk, anayesema kuwa: kitu kina sifa yake ya kwanza yenye kukithibitikia, ambayo haipambanuki nayo, ni sawa mtu aitambue au asiitambue; kama vile vitu vinavyosimamisha kitu hicho.

Vile vile kuna sifa ya pili ambayo haiwezi kuepukana na kuhisiwa au kujulikana; kama rangi, sauti na ladha. Rangi siyo sifa ya kitu, kama inavyoonekana, isipokuwa ni mawimbi ya kimwangaza yanayohusika kati ya kitu na jicho; kama wasemavyo wataalamu.

Vile vile sauti ni mawimbi ya kihewa; na ladha isingekuweko kama si mdomo. Kwa hiyo ladha inahitilafiana kwa uzima wa mdomo na ugonjwa. Kwa ufupi anataka kueleza kuwa hakuna rangi bila ya jicho; wala sauti bila ya sikio; au ladha bila ya mdomo.

Hakuna mwenye kutia shaka kwamba nuru ya Mwenyezi Mungu imezidi mawimbi ya kimwanga na mengineyo. Kwa hivyo yakikosekana mawimbi haya, ndio kumekosekana kuona.

وَإِذْ قُلْنَا ادْخُلُوا هَٰذِهِ الْقَرْيَةَ فَكُلُوا مِنْهَا حَيْثُ شِئْتُمْ رَغَدًا وَادْخُلُوا الْبَابَ سُجَّدًا وَقُولُوا حِطَّةٌ نَغْفِرْ لَكُمْ خَطَايَاكُمْ ۚ وَسَنَزِيدُ الْمُحْسِنِينَ {58}

Na tuliposema: Ingieni mji huu na kuleni humo maridhawa popote mpendapo na ingieni katika mlango (wake) kwa kunyenyekea na semeni: ‘Tusamehe.” Tutawasamehe makosa yenu na tutawazidishia wale wafanyao mazuri.

فَبَدَّلَ الَّذِينَ ظَلَمُوا قَوْلًا غَيْرَ الَّذِي قِيلَ لَهُمْ فَأَنْزَلْنَا عَلَى الَّذِينَ ظَلَمُوا رِجْزًا مِنَ السَّمَاءِ بِمَا كَانُوا يَفْسُقُونَ {59}

Wakabadilisha wale walio dhulumu kauli isiyokuwa ile waliyoambiwa. Na ndipo tukateremsha juu ya wale waliodhulumu adhabu kubwa mbinguni kwa sababu ya ufuska waliokuwa wakiufanya.