Aya 111-113: Na Walisema Hataingia Peponi
Lugha
NenoHudlinatokananaHaidlenye maanayakutubianakurudikwenye haki. Na neno Naswara tumelifafanuakatikakufasiriAya ya 62.
Maana
Na walisema: Hataingia peponi ila aliye Myahudi au Mnaswara (Mkristo).
Mwenye Majmau anasema: Hii ni kufupisha maneno: Kukadiria kwake ni kama kusema hivi: “Husema Myahudi: Hataingia peponi ila aliye Myahudi, na husema Mkristo: Hataingia peponi ila aliye Mkristo.” Imekadiriwa hivi kwa sababu inajulikana kwamba Mayahudi hawakubali kuwa Wakristo wataingia peponi. Kwa hivyo tukafahamu kuwa yameunganishwa maneno kwa kufupiliza maneno bila ya kuharibu maana, kwani umashuhuri wa hali unatosha kuwa ni ubainifu.
Ulanguzi Wa Pepo
Inadhihiri kutokana na Aya hii tukufu kwamba Mayahudi na Wakristo wanaamini nadharia ya ulanguzi tangu zamani na kwamba nadharia hiyo kwao inaingia pia kwenye neema za dunia na akhera.
Vile vile imedhihiri kwamba ulanguzi wa pepo unahusika na watu wa dini. Kwa misingi hiyo ndio likawa kanisa linauza cheki za msamaha kwa waasi na wenye dhambi kwa pesa. kanisa likachuma mali nyingi sana, lakini lilizidisha makosa na kueneza ufisadi. Miongoni mwa mambo yanayoandikwa kwenye cheki hiyo ya msamaha ni: “Unafungwa mlango ambao wataingia wenye makosa kwenye adhabu na mateso na unafunguliwa mlango wa kwenda kwenye pepo ya furaha; na hata ukiendelea kuishi muda mrefu neema hii itabaki bila ya kubadilika mpaka ifikie saa yako ya mwisho, kwa jina la Baba na Mwana na la Roho Mtakatifu.”
Hayo ni matamanio yao tu.
Ni matamanio yao ambayo ni mengi sana. Miongoni mwayo ni kwamba Waislamu warudi kuwa makafiri na maadui zao waadhibiwe na kwamba pepo ni yao peke yao.
Sema: Leteni dalili zenu, kama nyinyi ni wasema kweli.
Madai yote huhitaji dalili na vile vile kila dalili ya kinadharia inahitaji dalili mpaka iishie kwenye asili yenye kuthibitika kimsingi. Maana ya kuthibiti kwake ni kuafikiana wote wenye akili kuhusu usahihi wake wala visipingane vitu viwili; kama ilivyo asili hii “Kila madai yanahitaji dalili” isipokuwa ikiwa madai yenyewe ni ya kimsingi, kwani mwenye kudai madai ya kimsingi yaliyo wazi hayawezi kuitwa madai; kwa sababu madai huhitaji dalili; na madai ya kimsingi yanakuwa pamoja na dalili yake haiepukani nayo. Kwa hivyo huwezi kumuuliza dalili mwenye kusema: “Kumi ni zaidi ya moja.”
Katika Tafsir Al-Manar anasema katika kutaja Aya hii kwamba wahenga wa Kiislamu walio wema walikuwa na asili hii ya kuonyesha dalili juu ya wanayosema na wakitaka dalili kwa watu kwa wanayoyadai. Lakini waliokuja baadaye walio waovu - kama asemavyo mwenye Al-Manar - wameifanya kinyume Aya; wamewajibisha kufuata tu na kuharamisha dalili ila kufanya kwa kufuata tu. Wamezuia kufanya amali kwa kauli ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakawajibisha kufanya amali kwa kauli ya fulani.
Si hivyo! Yeyote anayeuelekeza uso wake kwa Mwenyezi Mungu kwa nafsi yake hali anatenda mema basi ana malipo yake kwa Mola wake.
Hii ni kuyakomesha madai kwamba pepo ni yao peke yao. Maana ni kuwa kila anayemwamini Mwenyezi Mungu kwa kumsafia nia katika amali zake bila ya kuichanganya na shirk; wala ria, basi yeye ni katika wenye kutukuzwa kwa Mwenyezi Mungu kwa sababu yeye hapotezi malipo ya mwenye kutenda wema. Ama kauli yake na hali anatenda mema, ni ishara kwamba. Kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu kunatokana na amali njema sio mbaya, kwa sababu Mwenyezi Mungu hatiiwi pale anapoasiwa.
Na Mayahudi walisema: Manaswara hawana chochote na Manaswara walisema: Mayahudi hawana chochote.
Mwenye Majmaul-Bayan amesema akimnukuu Ibn Abbas kwamba Wakristo wa Kinajran walibishana na Mayahudi mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) Myahudi mmoja akasema: “Hamna chochote nyinyi.” Akajibiwa na Mkristo: “Mayahudi hawana chochote,” ndipo ikashuka Aya hii ikisajili kauli ya vikundi vyote viwili.
Dini Ya Maslahi Kwa Mayahudi Na Wakristo
Ni maarufu kwamba Wakristo wanaeleza kwa uwazi kwamba Mayahudi na kizazi chao ndio waliohusishwa na kumsulubu Yesu. Pamoja na hayo yote Baba mtakatifu wa Roma alifanya juhudi za kufa na kupona mnamo mwaka 1965 za kuwatakasa Mayahudi wa sasa na wa kizazi kijacho. Ikabidi kugongana na kanisa la Mashariki. Na gharama za mkutano zilifikia dola milioni ishirini.
Lengo la kwanza na la mwisho la mkutano huo ni siasa tu ya kuipa nguvu dola ya Israil na kuyapa nguvu makao yake katika Palestina na siasa yake ulimwenguni. Kwa usahihi zaidi ni kuupa nguvu ukoloni na kuweka nguvu zake katika mashariki kwa ujumla na hasa katika miji ya kiarabu. Hii inafahamisha kwamba dini kwa baadhi yao ni manufaa ya kimada.1
Na hali wote wanasoma Kitabu
Yaani Mayahudi wana Tawrat ambayo inaelezea habari njema za kuja Isa na kukubali Utume wake. Vile vile Wakristo wana Injil inayomtambua Musa na Tawrat yake. Kwa hivyo Mayahudi na Wakristo wako katika hukumu ya taifa moja, kwa sababu dini yao ni moja na kati ya Tawrat na Injil, ni fungu la kuitimiza nyingine. Lakini pamoja na hayo wamekufurishana.
Waislamu Vilevile Wanakufuishana
Ikiwa Mayahudi na Wakristo wako katika hukumu ya taifa moja, kwa sababu tu Tawrat inamtambua Isa na Injil inatambua Musa, basi bora zaidi ni Sunni na Shia wawe taifa moja kwa uhakika kabisa.
Kwa sababu kitabu chao ni kimoja ambacho ni Qur’an moja wala sio viwili, na Mtume wao ni mmoja ambaye ni Muhammad sio Muhammad wawili. Sasa imekuwaje wengine wawakufurishe ndugu zao katika dini?
Na Mayahudi walisema: Manaswara hawana chochote na Manaswara walisema: Mayahudi hawana chochote na hali wote wanasoma kitabu.
Lau tukiangalia maana tuliyoyabainisha ya Aya hii na wafasiri wote wakaafikiana; kisha tukaikisia na Mwislamu anayemkufurisha ndugu yake Mwislamu, basi hali ingelikuwa mbaya zaidi ya mara elfu kuliko Mayahudi na Wakristo.
Mayahudi waliwakufurisha Wakristo na Wakristo wakawakufurisha Mayahudi. Na hali wote wanasoma kitabu. Yaani Tawrat na Injil. Sasa itakuaje Mwislamu amkufurishe ndugu yake Mwislamu na hali naye anasoma Qur’an? Basi na wamwogope Mwenyezi Mungu wale wanaopinda ndimi zao kwa kusoma kitabu na nyoyo zao hazijui maana yake na makusudio yake.
Na hivi ndivyo wale wasiojua wasemavyo mfano wa kauli yao.
Makusudio ya wasiojua katika Aya hii ni makafiri wa kiarabu kutokana na vile wali-vyosema, sawa na Mayahudi na Wakristo kwamba wao peke yao ndio watakaoingia peponi. Qur’an imewajibu, kwanza, kwamba haki haifungamani na watu fulani tu wala na majina, isipokuwa kuingia peponi kunatokana na imani njema.
Pili, kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anamjua mwenye haki na mwenye batil na yeye atamlipa kila mmoja kwa amali yake. Basi Mwenyezi Mungu atahukumu baina yao siku ya Kiyama katika yale waliyohitalifiana.
Kila Mmoja Avutia Kwake
Unaweza kuuliza kila watu wa dini na vikundi wanadai kuwa wao wako kwenye haki na wenzao wako kwenye batili; kama walivyodai Mayahudi, Wakristo na washirikina wa kiarabu. Sasa je, vipi tutamjua mwongo na mkweli?
Kabla ya kujibu, kwanza tunaanza kuelezea hakika hii: Kila mwenye kudai haki hana budi kuwa na moja ya mambo mawili: Ama kukubaliana kabisa na rai yake tangu mwanzo na kuendelea nayo na wala asione uwezekano wa makosa wala asifuate vingine vyovyote itakavyokuwa.
Au awe anaitafuta haki kwa juhudi zake mpaka aone dalili ya kuitegemea kwa kuazimia kwamba akibainikiwa na haki kwa upande mwingine aifuate na kugeuza rai yake. Kwa sababu yeye anaitafuta haki popote na wakati wowote ilipo na itakavyokuwa.
Hapana budi kuwatofautisha wawili hawa. Wa kwanza hakuna njia ya kumkinaisha kwa hoja na mantiki ya kiakili, bali hana dawa isipokuwa kuachana naye.
Wa pili inakua wepesi kufahamiana naye. Kila mmoja wetu anajua kuwa kuna mambo ambayo yako wazi. Mfano, maisha mazuri ni raha, na ufukara ni balaa na mashaka, mapenzi ni bora kuliko kugombana, usalama ni wenye manufaa kuliko vita, elimu ni nuru na ujinga ni giza, uadilifu ndio haki na dhulma ni batili na kwamba kitu kimoja hakiwezi kuwa pamoja na kinyume chake, n.k.
Tukianza kuangalia hayo na kuyajua, kisha mtu akadai kwamba yeye ni mwenye haki kinyume cha mwingine tutampima na kumhukumu kwa hakika hizo, zikiafikiana naye atakuwa ni mkweli, vinginevyo atakuwa mwongo.
Kwa hivyo basi inatubainikia kwamba kauli ya mwenye kusema:“Kila mmoja anavutia dini yake nitatambua vipi iliyo sahihi?”, ni ya hatari na duni yenye shabaha ya kueneza vurugu na ujinga.
Lau ingekuwa ni kweli ingelipasa sehemu za kuabudu na vituo vifungwe, jambo ambalo halina msimamo wa kiakili wala kikanuni au kitabia.
La upuuzi zaidi ni kwamba kauli hiyo (nitajuaje ukweli) ni maneno ya kishairi yaliyokuja kutokana na mawazo yasiyo-kuwa na mantiki yoyote. Mwenyezi Mungu amesema kweli aliposema:
وَالشُّعَرَاءُ يَتَّبِعُهُمُ الْغَاوُونَ {224}
أَلَمْ تَرَ أَنَّهُمْ فِي كُلِّ وَادٍ يَهِيمُونَ {225}
وَأَنَّهُمْ يَقُولُونَ مَا لَا يَفْعَلُونَ {226}
وَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّنْ مَنَعَ مَسَاجِدَ اللَّهِ أَنْ يُذْكَرَ فِيهَا اسْمُهُ وَسَعَىٰ فِي خَرَابِهَا ۚ أُولَٰئِكَ مَا كَانَ لَهُمْ أَنْ يَدْخُلُوهَا إِلَّا خَائِفِينَ ۚ لَهُمْ فِي الدُّنْيَا خِزْيٌ وَلَهُمْ فِي الْآخِرَةِ عَذَابٌ عَظِيمٌ {114}
- 1. Angalia kifungu cha “Masilahi ndio sababu “katika tafsir ya Aya 96 ya Sura hii.