Aya 78-79: Wako Miongoni Mwao Wasiojua Kusoma
Maelezo
Na wako miongoni mwao wasiojua kusoma.
Yaani katika Mayahudi kuna wale waliokuwa hawakusoma; hawajui chochote katika dini ya Mwenyezi Mungu na kwamba mambo yao zaidi ni ya kudhania dhania tu, bila ya kutegemea elimu.
Kimsingi ni kwamba ingawa maelezo haya yamekuja kwa sababu ya Wayahudi, lakini shutumu inamwendea kila mjinga.
Tafsiri Ina Misingi Na Kanuni
Katika Aya hii kuna dalili wazi kwamba haifai kufasiri Qur’an na Hadith kwa kudhania na kukisia, bali hapana budi lazima mfasiri awe na elimu ya kanuni za tafsiri na misingi yake, na kuchunga kanuni hizi katika kubainisha makusudio ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa kujihadhari na kuwazulia.
Sharti la kwanza la kufaa kufasiri ni kujua kusoma na kuandika; kisha hujua elimu za Kiarabu kwa aina zake zote, ambazo ni kujua msamiati, Sarfa, Nahw, Bayan, Fiqh na misingi yake. Vile vile kujua elimu ya Tawhid na kuongeza elimu nyingine ambazo zitamsaidia katika kufasiri baadhi ya Aya. Yote haya mfasiri anaweza kuyajua kwa kuwaendea wenye kuhusika nayo.
Basi ole wao wanaoandika kitabu kwa mikono yao.
Hapa Mwenyezi Mungu anamkemea kila anayemnasibishia yale asiyokuwa nayo kwa ajili ya kuchukua thamani kwa shetani. Si lazima thamani iwe ni mali (pesa) tu; inaweza kuwa ni kupata jaha au chochote katika anasa za kidunia.1
Mwenyezi Mungu amekariri makemeo mara tatu katika Aya moja kwa kutilia mkazo kwamba kumzulia yeye Mwenyezi Mungu na Mtume ni katikamaasimakubwanayenyeadhabukali;kamaalivyosemamahali pengine. “Ole wenu msimzulie uwongo Mwenyezi Mungu asije akawafutilia mbali kwa adhabu. Na ameruka utupu anayezua uwongo.” (20:61)
Mwanachuoni Hawezi Kuhukumu Kwa Matukio
Tunadokeza kwa mnasaba huu kwamba mwanachuoni, kwa namna yoyote atakavyokuwa na elimu, ni juu yake kutomnasibishia chochote Mwenyezi Mungu na Mtume wake na kwamba kitu hicho kinatoka katika Lawh Mahfudh. Akitoa fatwa kwa uhalali au uharamu; au kuhukumia kitu kuwa ni haki; au kufasiri Aya au Hadith, basi ni juu yake kuifanya hukumu yake hiyo, fatwa yake au tafsiri yake kuwa ni rai yake tu. Inaweza kuwa ni makosa au sawa.
Hapo ndio atakuwa anakubaliwa msamaha mbele ya Mwenyezi Mungu kama akijitahidi kadiri ya uwezo wake.
Lakini kama hakujitahidi sana au amejitahidi sana, lakini akasema kuwa kauli yake hiyo ni kauli ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi atakuwa ni sawa na wale wanaomzulia Mwenyezi Mungu uwongo, ajapokuwa ni mwanachuoni wa wanachuoni. Kwa sababu mwanachuoni hatoi fatwa ya kweli wala hukumu ya kweli, bali anaitikadi tu kuwa ni haki. Huu ndio msingi wa kwamba yeye sio maasum.
وَقَالُوا لَنْ تَمَسَّنَا النَّارُ إِلَّا أَيَّامًا مَعْدُودَةً ۚ قُلْ أَتَّخَذْتُمْ عِنْدَ اللَّهِ عَهْدًا فَلَنْ يُخْلِفَ اللَّهُ عَهْدَهُ ۖ أَمْ تَقُولُونَ عَلَى اللَّهِ مَا لَا تَعْلَمُونَ {80}
بَلَىٰ مَنْ كَسَبَ سَيِّئَةً وَأَحَاطَتْ بِهِ خَطِيئَتُهُ فَأُولَٰئِكَ أَصْحَابُ النَّارِ ۖ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ {81}
وَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ أُولَٰئِكَ أَصْحَابُ الْجَنَّةِ ۖ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ {82}
- 1. Wamethibitisha wenye kuhusika na historia ya lugha na ada zake kwamba Tawrat ya sasa, ambayo Wayahudi wanaitakidi kuwa iliteremshwa na Mwenyezi Mungu kwa Musa, imetungwa. W atafiti wametoa hakika hii kutokana na muundo wa lugha ulivyo na ustawi wa kijamii na wa kisiasa ambao uko kinyume na Tawrat. Tutarudia kueleza maudhui haya kwa upana zaidi Inshallah.