read

Aya 135-138: Na Wakasema: Kuweni Mayahudi Au Manaswara

Maana

Na wakasema: Kuweni Mayahudi au Wakristo mtaongoka.

Dhamiri katika “wakasema” inawarudia watu wa Kitabu; maana yake walisema Mayahudi kuweni Mayahudi mtaongoka kwa sababu uongofu, wanavyodai wao, unatokana na wao tu peke yao. Na Wakristo nao walisema hivyo hivyo.
Mwenyezi Mungu anamwambia Mtume wake Mtukufu Muhammad (s.a.w.): “Sema bali (tunashika) mila ya Ibrahim.” Yaani hatuwafuati Mayahudi wala Wakristo, bali tunafuata mila ya Ibrahim. Tumeyataja yanayoelekeana na haya katika Aya ya 111-113 ya sura hii .

Mjadala Wa Kimantiki

Huenda mtu akasema: Mayahudi wamedai kuwa na haki, Wakristo nao wakadai kuwa na haki, na Muhammad (s.a.w.) naye aka-sema bali Ibrahim ndiye mwenye haki sio Mayahudi wala Wakristo; na kauli zote hizi ni madai. Sasa basi ikiwa itafaa kwa Mayahudi na Wakristo kutumia mantiki haya yasiyofaa, basi itakua haifai kuyafa-nanisha kwa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake; Je, kuna njia gani?

Jibu: Makusudio ya: “Bali (tunashika) mila ya Ibrahim” ni kuyabatilisha madai ya Mayahudi na kuwanyamazisha, na wala sio kuthibitisha uhakika hasa. Inawezekana mtu kuipinga hoja ya mtesi wake kwa kitu ambacho sio hoja yake bali ni hoja iliyo mfano wake; kama vile kuyavunja madai ya Wakristo kwa Adamu ambaye hana baba; pale waliposema kwamba Masih ni Mungu, kwa sababu hana baba. Na Adam naye hana baba, lakini hawamwiti Mungu. Aina hii ndiyo inayoitwa ‘mjadala wa kimantiki.’ Kwa hiyo njia ya kuwanyamazisha Mayahudi na Wakristo ambayo tunayo ni:-

Mayahudi na Wakristo wanahitalifiana kidini na kiitikadi. Kila kundi linalikufurisha kundi jingine, lakini wakati huo huo wanaafikiana juu ya usahihi wa dini ya Ibrahim. Kwa dhahiri kabisa ni kwamba Ibrahim hakuwa Yahudi wala Mkristo bali aliacha dini za upotefu akashikamana na dini ya haki na hakuwa katika washirikina. Hakuwa Yahudi kwa vile hakusema kuwa Uzayr ni mtoto wa Mungu, wala hakumfananisha Mwenyezi Mungu; kama walivyodai kwamba Mwenyezi Mungu ni mzee mmoja mwenye mvi za kichwani na kidevuni. Vile vile Ibrahim hakuwa Mkristo kwa sababu hakusema Masih ni mtoto wa Mungu kwa vile hilo ni shirk.

Maadam Mayahudi na Wakristo wanaikubali dini ya Ibrahim, basi inawalazimu wawe ni wenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu, bali pia wanalazimika wahiji Al-Ka’aba tukufu; kama alivyokuwa Ibrahim akiitakidi na kufanya, na kama alivyoitakidi Muhammad na kufanya; na wao hawakumpwekesha Mwenyezi Mungu wala hawakuhiji. Kwa hiyo wao ni waongo; na Muhammad ni mkweli na mwaminifu juu ya dini ya Mwenyezi Mungu na mila ya Ibrahim.

Kwa maneno mengine ni kwamba kushikamana na lile lililoafiki ambalo ni dini ya Tawhid aliyokuwa nayo Ibrahim na aliyonayo Muhammad hivi sasa, ni bora kuliko kuchukua lile lenye hitilafu ambalo ni Uyahudi na kumfananisha kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu, na Ukristo na utatu wake.

Semeni: Tumemwamini Mwenyezi Mungu. Yaani semeni enyi Waislamu. Na yale tuliyoteremshiwa ambayo ni Qur’an.

Na yale yaliyoteremshwa kwa Ibrahim nazo ni sahifa za Ibrahim; Inasemekana zilikuwa kumi.

Na Ismail na Is-hak.

Hao ni watoto wa Ibrahim. Ismail ndiye mkubwa kuliko Is-hak; mama yake ni Hajar na mama wa Is-hak ni Sara.

Yaqub ni mtoto wa Is-hak. Hao wote hawakuteremshiwa sahifa, isipokuwa ziliteremshwa kwa Ibrahim, lakini inafaa kusema kuwa zimeteremshiwa wote kwa kuangalia kwamba wao walikuwa wakiabudu na kulingania kutokana na sahifa hizi; sawa na vile inavyofaa, kwa sisi Waislamu kusema: tumeteremshiwa Qur’an, kwa vile tunaamini na kufanya amali kutokana nayo na tunailingania.

Na Wajukuu.

Hao ni wajukuu wa Yaqub kutokana na watoto wake kumi na wawili; Ni kama makabila ya Kiarabu katika uzao wa Ismail. Katika kizazi hicho kuna mitume wengi; kama vile Daud, Suleiman, Yahya, Zakariya. Vile vile waumini wengine ambao walifanya ibada kutokana na sahifa za Ibrahim (a.s.).

Na waliyopewa Musa na Isa

Ni Taurat na Injil na pia wengine waliyopewa Manabii. Kama Zaburi aliyoteremshiwa Daud.

Hatutofautishi baina ya yeyote katika hao.

Yaani tunawaamini wote, wawe na kitabu au la. Sisi sio kama Mayahudi na Wakristo ambao wanaamini baadhi na kukanusha baadhi, bali wote kwetu ni sawa katika kuukubali utume wao. Kimsingi ni kwamba kuwaamini wote ni wajibu kwa njia ya ujumla, na wala hatukukalifishwa kuwajua kwa upambanuzi ila baada ya ubainifu kutoka katika Qur’an, au Hadith.

Basi wakiamini kama mnavyoamini nyinyi itakuwa kweli wameongoka.

Yaani wakiamini imani sahihi ambayo ni Tawhid yenye kutakata na aina yoyote ya shirk, na pia wakiwakubali Mitume wote akiwemo Muhammad; kama vile wanavyofanya Waislamu kwa Mitume wote bila ya kuwabagua wengine, wakifanya hivyo, basi watakuwa wameongoka. Wala maksudio sio kuwa waamini dini mfano wa dini ya Kiislam. Kwa sababu Uislamu hauna cha kufananisha.

Na wakikengeuka basi wao wamo katika upinzani tu.

Yaanikila anayeipinga hakianakuwa amejitoakundinina kujitofautisha.

Basi Mwenyezi Mungu atakutoshea

Kwani vitimbi viovu vinawapata wenyewe. Kwa ufupi ni kwamba Uislamu unakataa ubaguzi, unatoa mwito wa kusaidiana kwa misingi ya kheri na uadilifu, unaikubali haki popote ilipo na unawataka wafuasi wake wafungue nyoyo kwa watu wote kwa mapenzi na Ikhlasi.

Huu ni) upakaji rangi wa Mwenyezi Mungu.

Ni dini ya haki ambayo inautwaharisha moyo na akili kutokana na uchafu; na wala sio kuzama katika maji, (ya kubatiza) kama wanavyofanya Wakristo.

Muhyiddin Ibnul-Arabi katika tafsir yake anasema: “Hakika kila mwenye madhehebu na itikadi anapambika na itikadi yake, dini na madhehebu yake. Wenye kuabudu kutokana na mila wanapambika na pambo la kiongozi wao. Na wenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu wanapambika na pambo la Mwenyezi Mungu ambalo hakuna pambo zuri zaidi ya hilo na wala hakuna jengine baada yake!”

قُلْ أَتُحَاجُّونَنَا فِي اللَّهِ وَهُوَ رَبُّنَا وَرَبُّكُمْ وَلَنَا أَعْمَالُنَا وَلَكُمْ أَعْمَالُكُمْ وَنَحْنُ لَهُ مُخْلِصُونَ {139}

Sema: Je mnahojiana nasi juu ya Mwenyezi Mungu? Na hali yeye ni Mola wetu na Mola wenu? Na sisi tuna vitendo vyetu, nanyi mna vitendo vyenu; na sisi tunamfanyia Ikhlas yeye.

أَمْ تَقُولُونَ إِنَّ إِبْرَاهِيمَ وَإِسْمَاعِيلَ وَإِسْحَاقَ وَيَعْقُوبَ وَالْأَسْبَاطَ كَانُوا هُودًا أَوْ نَصَارَىٰ ۗ قُلْ أَأَنْتُمْ أَعْلَمُ أَمِ اللَّهُ ۗ وَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّنْ كَتَمَ شَهَادَةً عِنْدَهُ مِنَ اللَّهِ ۗ وَمَا اللَّهُ بِغَافِلٍ عَمَّا تَعْمَلُونَ {140}

Au Mnasema kuwa Ibrahim na Ismail na Is-haq na Yaqub na wajukuu (zake) walikuwa Mayahudi au Manaswara? Sema: Je, nyinyi mnajua zaidi au Mwenyezi Mungu? Na ni nani dhalimu mkubwa kuliko yule afichaye ushaidi alio nao utokao kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika na hayo mnayoyafanya.

تِلْكَ أُمَّةٌ قَدْ خَلَتْ ۖ لَهَا مَا كَسَبَتْ وَلَكُمْ مَا كَسَبْتُمْ ۖ وَلَا تُسْأَلُونَ عَمَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ {141}

Huo ni umma uliokwishapita. Utapata uliyoyachuma nanyi mtapata mliyoyachuma wala hamtaulizwa waliyokuwa wakifanya.