Aya 90 – 92: Pombe Na Kamari
Maana
Enyi mlioamini! Hakika pombe na kamari na mizimu na mburuga ni uchafu katika kazi ya shetani.
Tumezungumzia kwa ufafanuzi kuhusu pombe na kamari katika kufasiri Aya Juz.2 (2:219). Na kuhusu mizimu na Mburuga katika Aya ya 3 ya Sura hii tuliyonayo. Mwenyezi Mungu (s.w.t) amenasibisha kwa shetani kunywa pombe, kucheza kamari, kuabudu masanamu na kuagulia kwa mburuga. Kwa sababu Shetani ndiye anayapendekeza na kuwaghuri watu kwayo.
Basi jiepusheni nayo ili mpate kufaulu.
Dhamiri ya jiepusheni nayo inarudia uchafu. Hiyo ni amri ya kujiepusha; na amri inafahamisha wajibu, hasa wakati wa kubainisha sababu. Na ameibainisha hapo kuwa sababu ya kujiepusha ni kufaulu. Hata kama kusingekuwa na dalili ya kuharamishwa pombe zaidi ya kuwekwa sawa na kuabudu sanamu, ingelitosha. Sikwambii tena kama tukiunganisha na (2:219,7:32), Hadith Mutawatir na Ijmai ya Waislamu tangu wakati wa Mtume (saw) mpaka siku ya mwisho.
Hakika Shetani anataka kuwaingizia uadui na bughudha baina yenu kwa pombe na kamari na kuwazuia kumkumbuka Mwenyezi Mungu na kuswali.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutilia mkazo uharamu wa pombe na kamari, na akakulinganisha na kuabudu masanamu na akakujaalia ni uchafu unaotokana na adui wa mtu, na tena akabainisha kuwa njia ya kujiepusha ni kufaulu, baada ya yote haya. Anaonyesha Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwamba kwenye mambo mawili hayo kuna uharibifu mara mbili:
1. Wa kijamii - kutoelewana pamoja na kuleta chuki na undani baina ya watu.
2. Wa kidini - kuzuia kumkumbuka Mwenyezi Mungu na ibada zake. Kisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) akataka watu wakome kunywa pombe na kucheza kamari kwa ibara fasaha kabisa Basi je mtakoma?
Uislamu unahimiza kwa mahimizo yote kuwa mtu aungane na Muumba wake na jamii yake, na kwamba mtu mbele ya Mungu na mbele ya watu, awe mwenye kuridhiwa na kuheshimiwa.
Na mtiini Mwenyezi Mungu na mtiini Mtume kwa kuacha pombe na kamari na mengineyo yaliyoharamishwa.
Na tahadharini isije ikawapata adhabu ya Mwenyezi Mungu, kama mkihalifu amri yake na amri ya Mtume wake. Imam Aliy (a.s) anasema: "Mwenye kuinasihi nafsi yake zaidi ya watu (wote) ni yule anayemtii Mola wake zaidi yao. Na mwenye kuihadaa nafsi yake zaidi ya watu (wote) ni yule mwenye kuasi zaidi yao."
Na mkikengeuka basi jueni kuwa ni juu ya Mtume wetu kufikisha tu (ujumbe) waziwazi.
Naye ametekeleza kikamilifu, akasimamisha hoja na kutoka katika jukumu la kufikisha. Atakayehalifu ni yeye peke yake na jukumu lake.
لَيْسَ عَلَى الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ جُنَاحٌ فِيمَا طَعِمُوا إِذَا مَا اتَّقَوْا وَآمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ ثُمَّ اتَّقَوْا وَآمَنُوا ثُمَّ اتَّقَوْا وَأَحْسَنُوا ۗ وَاللَّهُ يُحِبُّ الْمُحْسِنِينَ {93}