read

Aya 119-120: Ukweli Wa Wakweli

Maana

Mwenyezi Mungu atasema: Hii ndiyo siku ambayo wasemao kweli utawafa ukweli. Wao watapata bustani zipitazo mito chini yake. humo watadumu milele.

Baada ya kumzungumzia Nabii Isa kwamba yeye aliwaambia watu wake mwabuduni Mwenyezi Mungu. Baada ya haya amefuatishia kuwasifu wakweli kwa ujumla na kwamba mwenye kuwa mkweli katika maisha haya atanufaika nao katika maisha ya pili na atalipwa pepo.

Mfuatilio huu ni ushahidi kutoka kwa mwenyezi Mungu juu ya ukweli wa Issa katika kauli yake na vitendo vyake; na kwamba yeye alitekeleza ujumbe wa Mola wake kwa ukamiifu. Basi mwenye kukufuru na kufanya ushirkina ni jukumu lake peke yake.

Awe radhi nao Mwenyezi Mungu na wao wawe radhi naye. Huko ndiko kufuzu kukubwa.

Radhi ya Mwenyezi Mungu kwa mja wake ni pepo na neema. Na radhi ya mja kwa Mola wake ni kufurahia yale aliyompa Mwenyezi Mungu. Razi anasema: "Katika radhi ya Mwenyezi Mungu kuna siri za ajabu ambazo kalamu zinashindwa kuzielezea, amezijaalia Mwenyezi Mungu kwa watu wake" Na hawezi kuwa yeyote ni katika watu wake ila kwa kulipa thamani, na thamani yenyewe ni kuwa nembo ya mnunuzi iwe ni "lailaha illa llah" (Hakuna Mungu ispokuwa Allah) katika kila kitu; yaani kutoikasirikia katika jambo lolote hata kama atakerezwa na msumeno; kama alivyosema bwana wa viumbe: "Ikiwa wewe hukunikasirikia basi sijali" na kama alivyosema mjukuu wake, Husein Shahid: "Radhi ya Mwenyezi Mungu ndiyo radhi yetu sisi Ahlu bait, tunavumilia mitihani yake na atulipe malipo ya wanaovumilia"

Mwenyezi Mungu ndiye mwenye ufalme wa mbingu na ardhi na vilivyomo, naye ni Muweza wa kila kitu.

Ambaye ana uweza huu na ufalme huu humpa anayemridhia bila ya hisabu.