read

Aya 80 – 83: Je, Mnanihoji Juu Ya Mwenyezi Mungu

Lugha

Neno ‘hoja’ linatumika kwa maana ya dalili zenye kuthibitisha haki; na hutumiwa kwa maana yale anayoyatolea hoja mdai kuthibitisha madai yake.

Maana

Na watu wake wakamhoji.

Baada ya Ibrahim kuwapatia watu wake hoja inayoingia akilini kutokana na mantiki ya kiakili na kimaumbile, na kuthibitisha uharibifu na ibada yao ya mizimu na nyota, baada ya yote hayo nao walileta hoja zao dhaifu. Wakasema miongoni mwa waliyoyasema:

وَجَدْنَا آبَاءَنَا لَهَا عَابِدِينَ {53}

Tumewakuta baba zetu wakiyaabudu.” (21:53)

Ndipo Ibrahim akawajibu kwa kusema:

Je, mnanihoji juu ya Mwenyezi Mungu na hali yeye ameniongoza?

Yaani ni hoja gani hizi kuhusu Mwenyezi Mungu na hali yeye ameniongoza kumjua kutokana na nafsi yangu na ulimwengu. Imetangulia katika sura hii Aya ya 71:

قُلْ إِنَّ هُدَى اللَّهِ هُوَ الْهُدَىٰ ۖ{71}

“Mwongozo hasa ni mwongozo wa Mwenyezi Mungu” (6:71)

Ambao hauna shaka yoyote, vinginevyo ni ujinga na upotevu. Ama kuhofisha waungu wao alikujibu kwa kusema:

Wala siogopi wale mnaowashirikisha naye wasiokuwa Mwenyezi Mungu. Kwa sababu hawadhuru wala hawanufaishi, hawoni wala hawasikii, Isipokuwa Mola wangu akitaka chochote kwa kuniangushia sanamu kichwani kwangu linivunje fuvu, au kimondo cha nyota kitakachoniunguza.

Mola wangu ana wasaa wa kujua kila kitu. Kwa hiyo siogopi kuwa nitapatwa na jambo lolote baya bila ya kujua yeye au kutaka.

Je, hamkumbuki kuwa miungu yenu si chochote na kwamba Mwenyezi Mungu peke yake ndiye mwenye kudhuru na kunufaisha. Kwa sababu yeye ni Muumbaji wa kila kitu.

Nitaogopaje hao mnaowashirikisha, na hali nyinyi hamwogopi kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kile ambacho hakukiteremshia dalili kwenu?

Makusudio ya mliowashirikisha ni masanamu na nyota mnaoziabudu. Maana nikuwa mnataka niwaogope waungu wenu walioumbwa wanaoshindwa na nyinyi hamwogopi madai yenu ya kumfanyia Mungu washirika, madai ambayo ni uzushi usiokuwa na hoja wala dalili!

Kwa maneno mengine, Ibrahim aliwaambia je, mnanihofisha kwa wale wasiokuwa na uwezo, na nyinyi mmejiamini na kumfanyia uzushi yule mwenye nguvu na uwezo kwa wote?

Basi kundi gani katika mawili haya linastahiki kupata amani kama nyinyi mnajua?

Kundi linalomwamini Mwenyezi Mungu mwenye nguvu, mwenye kushinda, au linaloamini udhaifu ulio dhalili?

Wale walioamini na hawakuchanganya imani yao na upotevu, hao ndio watakaopata amani na ndio walioongoka.

Huu ni ubainifu wa kundi lililookoka katika makundi mawili na kwamba wao ndio waliomfanyia ikhlasi Mwenyezi Mungu katika imani yao na hawakuchanganya na imani hii kushirikisha katika itikadi wala katika kutii hawaa za kiumbe yeyote awaye. Hawa peke yao ndio waliosalimika, wenye kuongoka.

Na hiyo ndiyo hoja yetu tuliyompa Ibrahim juu ya watu wake.
Yaani hizo ndizo hoja ambazo tumemtia ilham Ibrahim , zinazoingia bon- goni ambazo aliwahshinda nazo Ibrahim watu wake. Aya hii ni dalili wazi kwamba Mitume na wale wanaoongozwa na mwongozo wao katika maulama, ni maneno ya Mwenyezi Mungu na ubainifu wake; na kwamba kuwapinga ni kumpinga Mwenyezi Mungu hasa; kama ilivyoelezwa katika Hadith.

Tunamuinua kwa vyeo yule tumtakaye.

Utaipata Tafsir yake katika Juz 28 (58:11.) inshaallah Sababu ya kuinuliwa mtu kwa Mwenyezi Mungu ni imani na elimu, na kila moja katika hayo ina daraja ya juu na ya juu zaidi. Ibrahim alifikia ile ya juu zaidi mpaka akawa rafiki wa Mwenyezi Mungu (Khalilullah).

Hakika Mola wako ndiye mwenye hekima, Mjuzi.

Mwenye hekima aliyetakata na mchezo na matamanio, anajua anayostahiki kila mtu katika daraja na vyeo.

وَوَهَبْنَا لَهُ إِسْحَاقَ وَيَعْقُوبَ ۚ كُلًّا هَدَيْنَا ۚ وَنُوحًا هَدَيْنَا مِنْ قَبْلُ ۖ وَمِنْ ذُرِّيَّتِهِ دَاوُودَ وَسُلَيْمَانَ وَأَيُّوبَ وَيُوسُفَ وَمُوسَىٰ وَهَارُونَ ۚ وَكَذَٰلِكَ نَجْزِي الْمُحْسِنِينَ {84}

Na tukampa Is-haq na Yaqub Kila mmoja tulimuongoza. Na Nuh tulimwongoza zamani. Na katika kizazi chake Daud na Suleiman na Ayyub na Yusuf na Musa na Harun. Na kama hivyo tunawalipa wafanyao mema.

وَزَكَرِيَّا وَيَحْيَىٰ وَعِيسَىٰ وَإِلْيَاسَ ۖ كُلٌّ مِنَ الصَّالِحِينَ {85}

Na Zakariya na Yahya na Isa na Ilyas; wote ni katika wema.

وَإِسْمَاعِيلَ وَالْيَسَعَ وَيُونُسَ وَلُوطًا ۚ وَكُلًّا فَضَّلْنَا عَلَى الْعَالَمِينَ {86}

Na Ismail na Al-yasaa na Yunus na Lut; na kila mmoja tulimfadhilisha juu ya walimwengu wote

وَمِنْ آبَائِهِمْ وَذُرِّيَّاتِهِمْ وَإِخْوَانِهِمْ ۖ وَاجْتَبَيْنَاهُمْ وَهَدَيْنَاهُمْ إِلَىٰ صِرَاطٍ مُسْتَقِيمٍ {87}

Na katika baba zao na vizazi vyao na ndugu zao na tukawachagua na kuwaongoza katika njia iliyonyooka.

ذَٰلِكَ هُدَى اللَّهِ يَهْدِي بِهِ مَنْ يَشَاءُ مِنْ عِبَادِهِ ۚ وَلَوْ أَشْرَكُوا لَحَبِطَ عَنْهُمْ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ {88}

Huo ni uongozi wa Mwenyezi Mungu. Kwa huo humwongoza amtakaye katika waja wake. Na kama wangelishirikisha bila shaka yangeliporomoka yale waliyokuwa wakiyatenda.

أُولَٰئِكَ الَّذِينَ آتَيْنَاهُمُ الْكِتَابَ وَالْحُكْمَ وَالنُّبُوَّةَ ۚ فَإِنْ يَكْفُرْ بِهَا هَٰؤُلَاءِ فَقَدْ وَكَّلْنَا بِهَا قَوْمًا لَيْسُوا بِهَا بِكَافِرِينَ {89}

Hao ndio tuliowapa Kitab na hukumu na utume. Kama hawa wakiyakataa, basi tumekwisha yawakilisha kwa watu wasioyakataa.

أُولَٰئِكَ الَّذِينَ هَدَى اللَّهُ ۖ فَبِهُدَاهُمُ اقْتَدِهْ ۗ قُلْ لَا أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ أَجْرًا ۖ إِنْ هُوَ إِلَّا ذِكْرَىٰ لِلْعَالَمِينَ {90}

Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu amewaongoza, basi fuata mwongozo wao. Sema: Siwaombi ujira juu ya haya. Haikuwa hiyo ila ni mawaidha kwa waimwengu wote.