read

Aya 71-73: Sema: Je: Tuwaabudu Wasiokuwa Mwenyezi Mungu?

Maana

Sema: Je, tuwaabudu wasiokuwa Mwenyezi Mungu ambao hawatun- ufaishi wala kutudhuru?

Mtume (s.a.w.) aliwalingania washirikina katika kumwabudu Mwenyezi Mungu; nao wakamtaka aabudu masanamu yao. Inasemekana kwamba walitoa rai ya kuwa waabudu nao waungu wao na wao waabudu naye Mola wake.

Kwa vyovyote itakavyokuwa ni kwamba Mwenyezi Mungu (swt) alimwamrisha, katika Aya hii, kuwaambia kwa kukanusha, vipi tuache kumwabudu Mwenyezi Mungu anayenufaisha na kudhuru na tuabudu wale wasiojiweza wao wenyewe kujinufaisha au kujikinga na madhara?

Na turudishwe nyuma baada ya Mwenyezi Mungu kutuongoza.

Kurudi nyuma ni neno linalotumiwa kwa mtu aliyeiacha haki akafuata batili.

Kama yule ambaye mashetani wamempoteza; akiwayawaya katika ardhi. Anao marafiki wanaomwita kwenye uongofu: Njoo kwetu.

Huu ni mfano anaoutoa Mwenyezi Mungu kwa aliyekataa Tawhid na kwenda kwenye ushirikina au ulahidi. Kwa ufupi nikuwa mfano wa mtu huyu ni kama mfano wa mtu aliyekuwa katika msafara unakwenda kwa amani na salama.

Akauacha na akafuata njia yake jangwani bila ya mwelekeo wowote; kama ambaye amezungwa na mashetani. Basi wenzake wakamhurumia na kumwita: ‘Njoo kwetu, hii ndiyo njia ya uongofu’, lakini asiwajibu kwa kubabaika kwake. Ikawa mwisho wake ni balaa na maangamivu.

Sema: Mwongozo hasa ni mwongozo wa Mwenyezi Mungu .

Muundo huu wa kiubainifu unafahamisha kuwa mwongozo wa Mwenyezi Mungu haungiliwi na shaka yoyote; kama ambavyo unafahamisha kuwa mwongozo ni wa Mwenyezi Mungu peke yake katika kila kitu – katika itikadi sharia maadili na hali. Itikadi yoyote au fikra yoyote au kazi yoyote isiyokutana na mwongozo wa Mwenyezi Mungu basi ni ujinga na upotevu.

Na tumeamrishwa tusilimu kwa Mwenyezi Mungu, Mola wa viumbe vyote.

Hii ni katika kutaja mahsusi baada ya ujumla. Kwa sababu mwongozo wa Mwenyezi Mungu unaingia katika kila aliloamrisha Mwenyezi Mungu na kulikataza. Makusudio ya kuuhusisha Uislamu ni kukumbusha utukufu wake.

Na simamisheni swala.

Kwani hakuna mwongozo wala Uislam ila kwayo; ndiyo nguzo ya dini, ikikubaliwa hukubaliwa mengine na ikikataliwa hukataliwa mengine.

Na mcheni yeye Mwenyezi Mungu Mola wa walimwengu. Ameamrisha Mwenyezi Mungu (swt) takua baada ya kuamrisha swala. Kwa sababu hakuna swala wala imani sahihi bila ya takua. Kumwabudu Mwenyezi Mungu kweli ni kwenda kwenye njia yake na kumtii katika hukumu zote, sio baadhi tu.

Naye ndiye ambaye kwake mtakusanywa.

Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Na itakuja kila nafsi pamoja na mwendeshaji na shahidi” (50:21). Mwendeshaji atakayeiendesha hadi mahshar (watakapokusanya watu) na shahidi atakayeishuhudilia kwa yale yaliyoandaliwa kwa siku hii.

Naye ndiye aliyeziumba mbingu na ardhi kwa haki.

Haki hapa ni ishara ya kuwa ulimwengu una kanuni zinazouhukumu na desturi inayokwenda nao kwa mpangilio bila ya mkorogano wowote. Hii ni dalili fasaha ya kuweko mpangaji wa mambo na atakayeilipa kila nafsi ililochuma.

Na siku anayosema ‘kuwa’ basi huwa. Kauli yake ni haki.

Katika maneno haya kuna kukadiriwa, kutangulizwa, na kuwekwa nyuma. Asili yake ni hivi: Kauli yake ni haki siku anapokiambia kitu kuwa, huwa. Maana yake ni kuwa kauli ya Mwenyezi Mungu inakuwa tu; na hudhihirika wazi hilo siku anapokiambia kitu kuwa, kikawa. Ni sawa aliyasema haya siku alipoanza kuumba viumbe au siku atakapowarudisha.

Kwa maneno mengine ni kuwa kauli ya Mwenyezi Mungu ndiyo kitendo chake katika kupatikana kitu bila ya kitu, na katika kukirudisha jinsi kilivyokuwa baada ya kuharibika na kuchangukana.

Na ufalme ni wake siku itakapopulizwa parapanda.

Kupulizwa parapanda ni fumbo la kufufuliwa walio makaburini. Na maana ya ufalme wa ufufuo huu ni kwamba yeye ndiye anayerudisha wafu kwenye uhai.

Masufi

Mjuzi wa ghaibu na yanayoonekana.

Ghaibu ni mambo ya siri yaliyojificha, kama vile Malaika, ufufuo na mambo anayoyaficha mtu nafsini mwake. Na dhahiri ni yale yanay- oonekana kidhahiri, kama vile ardhi, mbingu na anayoyafanya mtu wazi wazi.

Haya kwa binadamu ni sawa; ama kwa Mwenyezi Mungu hakuna ghaibu si katika mbingu wala ardhi. Hata hivyo masufi wanadai kuwa nafsi zao zinafichua ghaibu. Ibn Al-Arabi, katika Futuhatil- makkiya mlango wa 302, anasema: “Hakika watu wa Mwenyezi Mungu wana macho wanayoonea na masikio wanayosikizia na nyoyo wanazofahamia na ndimi wanazosemea; si macho haya wala masikio au nyoyo na ndimi hizi. Kwa macho hayo wanaona na kwa masikio hayo wanasikia na kwa nyoyo hizo wanafahamu na kwa ndimi hizo wanasema na maneno yao yanapatia…”

Naye ndiye mwenye hekima mwenye habari.
Yeye tu peke yake hana mshirika katika kupangilia mamabo ya viumbe vyake kulingana na heima yake na katika kujua siri zote. Basi hebu naa- muogope Mwenyezi Mungu yule anayedai kuwa ana nyoyo mbili, ndimi mbili, macho mane na masikio mane.

وَإِذْ قَالَ إِبْرَاهِيمُ لِأَبِيهِ آزَرَ أَتَتَّخِذُ أَصْنَامًا آلِهَةً ۖ إِنِّي أَرَاكَ وَقَوْمَكَ فِي ضَلَالٍ مُبِينٍ {74}

Na Ibrahim alipomwambia baba yake Azar: Unawafanya masanamu kuwa waungu? Hakika ninakuona wewe na watu wako mko katika upotofu ulio wazi.

وَكَذَٰلِكَ نُرِي إِبْرَاهِيمَ مَلَكُوتَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَلِيَكُونَ مِنَ الْمُوقِنِينَ {75}

Na namna hii tukamwonyesha Ibrahim ufalme wa mbingu na ardhi ili awe katika wenye yakini.

فَلَمَّا جَنَّ عَلَيْهِ اللَّيْلُ رَأَىٰ كَوْكَبًا ۖ قَالَ هَٰذَا رَبِّي ۖ فَلَمَّا أَفَلَ قَالَ لَا أُحِبُّ الْآفِلِينَ {76}

Na usiku ulipomwingilia, akaona nyota, alinena: Hii ni Mola wangu. Ilipotua akasema: Sipendi wanaotua.

فَلَمَّا رَأَى الْقَمَرَ بَازِغًا قَالَ هَٰذَا رَبِّي ۖ فَلَمَّا أَفَلَ قَالَ لَئِنْ لَمْ يَهْدِنِي رَبِّي لَأَكُونَنَّ مِنَ الْقَوْمِ الضَّالِّينَ {77}

Na alipouona mwezi unachomoza alisema: Huu ni Mola wangu. Ulipotua alisema: Asiponiongoza Mola wangu, hakika nitakuwa katika watu waliopotea.

فَلَمَّا رَأَى الشَّمْسَ بَازِغَةً قَالَ هَٰذَا رَبِّي هَٰذَا أَكْبَرُ ۖ فَلَمَّا أَفَلَتْ قَالَ يَا قَوْمِ إِنِّي بَرِيءٌ مِمَّا تُشْرِكُونَ {78}

Na alipoliona jua linachomoza alisema: Hili ndilo Mola wangu. Hili ni kubwa kabisa. Lilipotua alisema: Enyi watu! Mimi simo katika hayo mnayoyashirikisha.

إِنِّي وَجَّهْتُ وَجْهِيَ لِلَّذِي فَطَرَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ حَنِيفًا ۖ وَمَا أَنَا مِنَ الْمُشْرِكِينَ {79}

Hakika mimi nimeuelekeza uso wangu kwa yule aliyeziumba mbingu na ardhi. Hali ya kuwa nimeacha dini za upotevu, tena mimi si katika washirikina.