read

Aya 84 – 90: Na Tukampa Is-Haq Na Yaq’ub

Maana

Mwenyezi Mungu (swt) katika Aya hizi ametaja Mitume 18 akiwemo Ibrahim. Baadhi akawaashiria kwa baba zao, vizazi vyao na ndugu zao. Na amewasifu wote kwa hisani, wema na uongofu, na kwamba yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu amewaneemesha Mitume waliotajwa kwa hekima na Unabii na baadhi yao akawaneemesha kwa kuteremshiwa Kitab.

Makusudio katika hayo ni kutoa hoja Muhammad (saw) kwa Waarabu kwamba babu yao ni Ibrahim na wanawe wengi walikuwa wenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu.

Vilevile Mtume afuate nyayo za Mitume waliotangulia katika kulingania kwa Mwenyezi Mungu na kuvumilia adha. Huu ndio muhtasari wa madhumuni ya Aya hizi saba.

Uko wazi usiohitaji ubainifu wa kurefusha na ufafanuzi, lakini baadhi ya wafasiri wamekataa ila kurefusha, wakatoka nje ya maudhui ya Tafsir kufikia ambako hakuna uhusiano wowote na maisha.

Ni vizuri ifahamike kuwa majina ya Mitume yaliyotajwa katika Aya hayakuja kwa mpangilio wa wakati au ubora; kama ambavyo wametajwa kwa njia ya mifano tu.

Na tukampa Is-haq na Yaqub

Dhamir ya ‘tukampa’ inamrudia Ibrahim. Is-haq ni mwanawe wa kumzaa na mama yake ni Sara. Yaqub ni mwana wa Is-haq, na mwana wa mwana ni mwana. Mwenyezi Mungu anasema:

فَبَشَّرْنَاهَا بِإِسْحَاقَ وَمِنْ وَرَاءِ إِسْحَاقَ يَعْقُوبَ {71}

“Basi tukambashiria Is-haq na baada ya Is-haq ni Yaqub.” (11:71)

Kila mmoja Is-haq na Yaqub tulimuongoza .

Na Nuh tulimwongoza zamani kwani yeye ni wa zamani kuliko Ibrahim.

Na katika kizazi chake.

Dhamir inamrudia Nuh, yaani na kizazi cha Nuh, kwa sababu ndiye wa karibu kutajwa. Imesemekana kuwa inamrudia Ibrahim.

Daud na Suleiman na Ayyub na Yusuf na Musa na Harun.

Yaani wote hawa tumewaongoa kama tulivyomwongoza Nuh, Is-haq na Yaqub.

Na kama hivyo tunawalipa wafanyao mema.

Kwa sababu Mwenyezi Mungu (SWT) anamlipa mwema kwa wema, awe Mtume au sio Mtume; kama anavyomlipa mwovu kwa amali yake awe mweupe au mweusi.

Na Zakariya na Yahya na Isa na Ilyas.

Hawa vilevile ni katika aliowaongoza Mwenyezi Mungu,

Wote ni katika watu wema.

Na kila mwenye kutumia kipawa chake kwa kheri yake na kheri ya watu basi yeye ni mwema na mtengenevu.

Hasan Na Husein Ni Wana Wa Mtume

Anasema Razi katika Tafsir yake kuhusu Aya hii: “Hakika Aya hii inafahamisha kuwa Hasan na Hussein ni katika kizazi cha Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw).
Kwa sababu Mwenyezi Mungu amemjaalia Isa ni katika kizazi cha Ibrahim, ingawaje yeye amenasibiana na Ibrahim kwa upande wa mama tu. Vilevile Hasan na Hussein ni katika kizazi cha Mtume wa Mwenyezi Mungu ingawaje wananasibika na Mtume kwa mama. Inasemekana kuwa Abu Jafar Al-Baqir, aliitolea dalili Aya hii mbele za Hajjaj bin Yusuf.”

Mwenye Tafsir Al-Manar anasema: “Ninasema katika mlango wa Hadith Abu Bukra kwa Bukhari, iliyo Marfu’. (Hakika mwanangu, huyu ni Sayyid) yaani Hassan. Na neno mwanangu, kwa Waarabu, halitajwi kwa watoto wa binti. Na Hadith ya Umar katika Kitab Ma’rifatu Sahaba cha Abu Naim, iliyo marfu’; (kuwa kila mtoto wa Adam ukoo wao unatokana na baba yao, isipokuwa watoto wa Fatima, mimi ndiye baba yao na ni ukoo wao). Watu wakazoea haya, wakawa wanasema kuhusu watoto wa Fatima kuwa ni watoto wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) na ni kizazi chake na Ahlu bait (watu wa nyumbani) wake.”

Maana ya maneno haya ni kuwa watoto wa Fatima (as) si watoto wa Mtume wa Mwenyezi Mungu kilugha, lakini ni watoto wake kisharia, kutokana na kauli ya Mtume ‘mimi ni baba yao na ukoo wao.’ Vilevile ni watoto wake kimazoweya, kwa sababu watu walizoweya kuwaita kuwa ni watoto wa mtume.

Wamekongamana kwa kauli moja maulama wa Sunni na Shia kwamba sharia inatangulia ufahamisho wa matamko kimazowea na kilugha; na kwamba mazoea yanaitangulia lugha. Kwa sababu, mwenye hekima huzungumza na watu kwa lile wanalolifahamu haraka sio kwa lile lililoandikwa katika kamusi za lugha.

Likija neno katika Aya au Hadith, na tukakuta Tafsir maalum ya maana yake katika Qur’an au Hadith, basi tamko hilo litachukuliwa katika maana haya maalum; na huitwa maana ya kisharia na kupuuzwa ile ya kilugha na kimazoea. Ikiwa hatukupata maana maalum, basi tutalichukulia kwa maana wanayoifahamu watu; na huitwa maana ya mazoea. Wakitolifahamu watu kwa maana hayo, basi itachukuliwa maana yake kutoka kwenye kamusi za lugha.

Kwa hiyo basi maana ya sharia yanakuwa katika ngazi ya kwanza, ya mazoea katika ngazi ya pili na ya kilugha katika ngazi ya tatu. Na imethibiti kisharia na kimazoea kuwa Hassan na Hussein ni watoto wa Mtume wa Mwenyezi Mungu. Hivyo ikapuuzwa maana ya kilugha. Kwa sababu lugha inahukumiwa na sharia na mazoea.

Ama siri ya kuwa Hasan na Husein ni wana wa Mtume ingawaje si wanawe kilugha, ataipata mpekuzi katika sifa za hao wawili na hulka zao. Inamtosha mwenye kufanya utafiti wa sera ya Hasan kuwa Muawiya bin Abu Sufian hakupata wasaa wa Ufalme aliokuwa nao na huku Hassan bado yu hai. Na inamtosha mwenye kutafiti sera ya Hussein kwamba Yazid bin Muawiya dunia ilimzonga kwa kuweko Husein, kama ilivyomzonga baba yake, Muawiya kwa kuweko Hasan.

Na Ismail na Al-yasaa na Yunus na Lut. Vilevile tuliwaongoa.

Na kila mmoja tulimfadhilisha juu ya walimwengu wote katika zama zake.

Na katika baba zao na vizazi vyao na ndugu zao.

‘Katika’ hapa ni ya kubaadhisha; yaani baadhi yao Kwa sababu katika vizazi vyao na ndugu zao walikuwako makafiri; bali Isa na Yahya hawakuwa na kizazi.

Na tukawachagua na kuwaongoza katika njia iliyonyooka.

Sifa hizi ni utanguluzi wa kauli yake Mwenyezi Mungu:

Huo ni uongozi wa Mwenyezi Mungu. Kwa huo humwongoza amtakaye katika waja wake.

Yaani uongozi ambao ni wajibu kufuata ni ule waliokuja nao Mitume, wala hafuati mwongozo huu ila aliyepewa tawfiki na Mwenyezi Mungu.
Na kama wangeshirikisha, bila shaka yangeliporomoka yale waliyokuwa wakiyatenda.

Yaani hawa Mitume pamoja na ubora wao na utukufu wao wa vyeo, lau ingelitokea kufanya chembe ya kitu inayofahamisha shirk, basi bila shaka yangelibatilika yale waliyokuwa wakiyatenda na kuwa ni bure tu.

Lengo la ishara hii ni kuzindua kuwa Mwenyezi Mungu atawafanyia watu kulingana na amali zao si kulingana na vyeo vyao, na kwa watakavy- oishilia wanapokufa, si kwa walivyoanzia uhai wao.

Hao ndio tuliowapa Kitab na hukumu na utume.

Hao, ni wale Mitume waliotangulia kutajwa. Na Kitab, ni jinsi ya Kitab inayochanganya vitabu vyote vya Mwenyezi Mungu vilivyoitangulia Qur’an, kama vile Mbao za Ibrahim, Tawrat, Zabur na Injil. Makusudio ya ‘Hukumu’ ni kujua kuhukumu na kila lile aliloliwekea sharia Mwenyezi Mungu katika halali na haramu.

Kama hawa wakiyakataa, basi tumekwisha yawakilisha kwa watu wasioyakataa.

Hawa, ni washirikina wa Kiquraish ambao wameukana Utume wa Muhammad (saw) na kumfanyia uadui. Wanayoyakataa ni Utume. Makusudio ya watu ambao hawayakanushi ni Muhajirina na Ansari1 ambao walimwamini Muhammad na wakamsaidia.

Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu amewaongoza, basi fuata mwon- gozo wao.

Hao wanaotajwa hapa ni Mitume waliotangulia kutajwa. Mwenyezi Mungu amemwamrisha Mtume wake mtukufu kufuata nyao zao katika kuilingania haki na kuvumilia adha katika njia yake.

Sema: Siwaombi ujira juu ya haya.

Kwa sababu dini haikuwekwa kuwa ni chumo na biashara.

Haikuwa hiyo ila ni mawaidha kwa walimwengu wote

Dhamir ya hiyo ni Qur’an. Maneno haya ni dalili wazi kuwa Muhammad ametumwa kwa watu, wakati wote na mahali pote.

وَمَا قَدَرُوا اللَّهَ حَقَّ قَدْرِهِ إِذْ قَالُوا مَا أَنْزَلَ اللَّهُ عَلَىٰ بَشَرٍ مِنْ شَيْءٍ ۗ قُلْ مَنْ أَنْزَلَ الْكِتَابَ الَّذِي جَاءَ بِهِ مُوسَىٰ نُورًا وَهُدًى لِلنَّاسِ ۖ تَجْعَلُونَهُ قَرَاطِيسَ تُبْدُونَهَا وَتُخْفُونَ كَثِيرًا ۖ وَعُلِّمْتُمْ مَا لَمْ تَعْلَمُوا أَنْتُمْ وَلَا آبَاؤُكُمْ ۖ قُلِ اللَّهُ ۖ ثُمَّ ذَرْهُمْ فِي خَوْضِهِمْ يَلْعَبُونَ {91}

Na hawakumkadiria Mwenyezi Mungu kwa haki ya kadri yake, waliposema: Mwenyezi Mungu hakuteremshia chochote juu ya binadamu yoyote. Sema: nani aliyekileta Kitab alichokuja nacho Musa chenye nuru na mwongozo kwa watu? Mlichokifanya nyara- ka-nyaraka, mkizidhihirisha na mkificha mengi. Na mkafundishwa msiyoyajua nyinyi wala baba zenu. Sema: Ni Mwenyezi Mungu. Kisha waache wacheze katika porojo zao.

وَهَٰذَا كِتَابٌ أَنْزَلْنَاهُ مُبَارَكٌ مُصَدِّقُ الَّذِي بَيْنَ يَدَيْهِ وَلِتُنْذِرَ أُمَّ الْقُرَىٰ وَمَنْ حَوْلَهَا ۚ وَالَّذِينَ يُؤْمِنُونَ بِالْآخِرَةِ يُؤْمِنُونَ بِهِ ۖ وَهُمْ عَلَىٰ صَلَاتِهِمْ يُحَافِظُونَ {92}

Na hiki ni kitab tulichokiteremsha, kilichobarikiwa, chenye kusadikisha yale yaliyokitangulia. Na ili uwaonye (watu wa) Ummul qura na walio pambizoni mwake. Na wale wanaoamini akhera, wanakiamini. Nao huzihifadhi Swala zao.
  • 1. Muhajirina ni wale waliohama pamoja na Mtume kutoka Makka hadi Madina na Ansar ni wale waliowakaribisha Muhajirina.