Aya 12 – 16: Amejilazimishia Rehema
Maana
Sema: Ni vya nani vilivyomo ardhini na mbinguni? Useme ni vya Mwenyezi Mungu.
Mwenyezi Mungu alimwamrisha Mtume wake mtukufu kuwauliza Washirikina wa Kiarabu: Ni nani anayemiliki mbingu na ardhi? Kisha akamwamrisha kuwajibu kuwa ni Mwenyezi Mungu peke yake, yeye ndiye Mfalme wa wafalme.
Inawezekana kuwa yeye ndiye muulizaji na mwenye kujibu. Kwa sababu mwulizaji na mwenye kuulizwa wanaafikiana na jawabu. Kwani Washirikina wa Kiarabu walikuwa wakiamini kuwa Mwenyezi Mungu ni Muumba wa ulimwengu na ndiye mwenye kumiliki: “Ukiwauliza ni nani aliyeumba mbingu na ardhi na akalitiisha jua na mwezi? Bila shaka watasema: Mwenyezi Mungu. Basi wapi wanakogeuzwa?” (29:61)
Unaweza kuuliza maadamu mambo yako hivyo, basi kuna faida gani ya kuuliza?
Jibu: Makusudio ya swali na jibu lake ni kumvuta mbishani akiri uwezekano wa kufufuliwa, na kusimamisha hoja juu yake. Kwa sababu ikiwa yeye ndiye Muumbaji wa ulimwengu na ndiye mwenye kuumiliki, basi anaweza kuumaliza na kuurudisha tena.
Amejilazimishia rehema.
Ameirudia Mwenyezi Mungu (s.w.t) jumla hii katik Sura hii Aya 54.
Wafasiri wanasema Mwenyezi Mungu amejiwabishia rehema kwa wajibu wa fadhila na ukarimu. Na sisi tunaamini kuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye fadhila na ukarimu; wakati huo huo tukiamini kuwa rehema yake ni natija ya kujitosheleza na kila kitu na kuwa kila kitu kinamhitajia yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Kwa sababu kiumbe kwa tabia yake anahitajia usaidizi wa Muumbaji na rehema zake kwa uhitajio wa sababu kwenye ilichokisababisha.
Kwa hiyo basi, rehema ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake haiepukani na dhati yake Mwenyezi Mungu na ukamilifu wake. Hivyo basi maana ya Amejilazimishia rehema yanakuwa kwamba rehema yake inalazimiana na dhati yake takatifu; sawa na ulivyo uweza na ujuzi.
Hakika atawakusanya Siku ya Kiyama.
Mkusanyiko huu vilevile ni lazima; ndio maana Mwenyezi Mungu Mtukufu akausifu kwa kusema: Isiyo na shaka, kwa sababu Siku hiyo atalipizwa kisasi aliyedhulumiwa kwa aliyemdhulumu na atalipwa mwovu mfano wa uovu wake, na mwema atalipwa zaidi ya mfano.
Lau si Siku hii, haki ingelikwenda bure na mwenye nguvu ndio angelikuwa mwenye amri na wala sio Muumbaji wa ulimwengu.
Wale ambao wamezitia hasarani nafsi zao, basi wao hawaamini hawaamini.
Zamakhshari anasema: “Makafiri wamechagua hasara, kwa hiyo hawataamini.” Zamakhshari ni katika Mu’tazila wasemao mtu ana hiyari, halazimishwi.
Razi naye akasema; “Mwenyezi Mungu ndiye aliyejaalia hasara yao kwa hiyo hawakuamini.” Razi ni katika Ashaira wasemao mtu analazimishwa hana hiyari. Wengine wamesema hawakuamini Makafiri kwa ajili ya kufuata baba zao.
Tuonavyo sisi ni kuwa Aya inaashiria kwenye hakika ya mtu na kwamba mtu ni nafsi yake na mwili wake, na kila kimoja katika viwili hivyo kinamkamilishia mwenzake na kwamba mtu hatakuwa na maisha sahihi mpaka avitumikie vyote viwili.
Mwenye kufanya amali kwa ajili ya roho tu bila mwili, au kwa mwili tu bila ya roho, basi amepata hasara na mwenye kupata hasara hiyo hawi na amani yoyote.
Ni vyake vilivyotulia katika usiku na mchana; naye ndiye asikiaye na ajuaye.
Yaani yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye mwenye kumiliki kila kitu.
Unaweza kuuliza kuwa maana haya yashafahimishwa na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Aya iliyotangulia: ‘Sema ni vya nani vilivyomo ardhini na mbinguni? Useme ni vya Mwenyezi Mungu.’ Kuna wajihi gani wa kukaririka huku?
Wafasiri wamejibu kuwa Aya ya kwanza imeeleza viumbe kwa wakati na hii ni kwa mahali; navyo ni vyombo viwili vya kila kiumbe, iwe ni kwa kimaada au kimaana (kimwili au kiroho). Kwa hiyo ukapatikana ujumla na maana kwa Aya zote mbili; na akafuatishia Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwa sifa mbili za usikizi na ujuzi ili kutilia mkazo mkusanyiko wa maana hii.
Mara nyingi tumeeleza kuwa kukaririka katika Qur’an ni jambo la kawaida, lakini wafasiri wamekuwa wakijaribu kuleta kitu tu, hata kama hakuna haja.
Sema: Je nimfanye mlinzi asiyekuwa Mwenyezi Mungu?
Vipi nimtake msaada mwingine. Naye ni Muumba wa mbingu na ardhi? naye analisha na wala halishwi. Mwingine hawezi kujizuia na madhara wala kujinufaisha.
Sema: Hakika mimi nimeamrishwa niwe wa mwanzo katika wenye kusilimu.
Kwa sababu Muhammad ni mlinganiaji wa kwanza kwenye Uislamu, basi anakuwa yeye ni Mwislamu wa kwanza katika umma wake. Vinginevyo atakuwa katika wale ambao wanaamrisha na wao hawafuati amri. Hiyo haiwezekani kabisa kwa yule aliyechaguliwa na Mwenyezi Mungu kwa risala yake.
Na wala kabisa usiwe katika washirikina.
Ni muhali kuwa miongoni mwao. Maneno haya yamesihi tu kwa vile ni maelekezo kutoka kwa aliye juu kwenda kwa aliye chini; kama tulivyosema mara nyingi.
Sema: Hakika mimi ninaogopa adhabu ya siku kubwa ikiwa nita- mwasi Mola wangu.
Mtume kufanya maasia haiwezekani kutokana na cheo cha Isma. Lakini ‘kukadiria muhali si muhali.’ Lengo lake hapa ni kuthibitisha au kutilia mkazo msingi wa usawa baina ya watu wote mbele ya Mwenyezi Mungu na kwamba yeye ameumba pepo kwa anayemtii, hata kama ni mtumwa wa Kihabeshi; na akaumba moto kwa anayemwasi, hata kama ni sharifu wa Kiquiraish.
Na kumcha Mwenyezi Mungu (s.w.t) kunakuja kwa kiasi cha kujua ukubwa wake: “Kwa hakika wanaomwogopa Mwenyezi Mungu miongoni mwa waja wake ni wenye elimu tu” (35:28) na hasa Mitume.
Atakayeepushwa nayo siku hiyo, hakika (Mwenyezi Mungu) amem- rehemu na huko ndiko kufuzu kuliko wazi.
Kila mwenye kuhofia vituko vikubwa, huona uokovu kuwa ni rehema kubwa, na kufuzu ni jambo adhimu.
وَإِنْ يَمْسَسْكَ اللَّهُ بِضُرٍّ فَلَا كَاشِفَ لَهُ إِلَّا هُوَ ۖ وَإِنْ يَمْسَسْكَ بِخَيْرٍ فَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ {17}
وَهُوَ الْقَاهِرُ فَوْقَ عِبَادِهِ ۚ وَهُوَ الْحَكِيمُ الْخَبِيرُ {18}
قُلْ أَيُّ شَيْءٍ أَكْبَرُ شَهَادَةً ۖ قُلِ اللَّهُ ۖ شَهِيدٌ بَيْنِي وَبَيْنَكُمْ ۚ وَأُوحِيَ إِلَيَّ هَٰذَا الْقُرْآنُ لِأُنْذِرَكُمْ بِهِ وَمَنْ بَلَغَ ۚ أَئِنَّكُمْ لَتَشْهَدُونَ أَنَّ مَعَ اللَّهِ آلِهَةً أُخْرَىٰ ۚ قُلْ لَا أَشْهَدُ ۚ قُلْ إِنَّمَا هُوَ إِلَٰهٌ وَاحِدٌ وَإِنَّنِي بَرِيءٌ مِمَّا تُشْرِكُونَ {19}