read

Aya 63 – 67: Ni Nani Anayewaokoa

Maana

Sema: Ni nani anyewaokoa katika viza vya nchi kavu na baharini? Mnamwomba kwa unyenyekevu na kwa sauti ndogo.

Viza vya nchi kavu na baharini ni fumbo la shida na machungu anayoyapata mwanadamu katika mambo yote anayoyafanya bara na baharini; nasi tunaongezea (katika ufafanuzi wetu)‘angani’ baada ya kuwa katika zama za anga, ambako ni hatari zaidi kuliko nchi kavu na baharini.

Maana ni kuwa Ewe Mtume! Waulize Washirikina na Walahidi, ni nani wanayemkimbilia kumwomba katika saa ya dhiki na kumnyenyekea katika siri na dhahiri. Je, wanamkimbilia Mwenyezi Mungu au wanawakimbilia wanaowaabudu asiyekuwa Mungu?

Tumesema katika kufasiri Aya ya 41 katika Sura hii kwamba umbile la mtu linamtambua Muumbaji wake, lakini pazia ya kufuata na hawaa inauzuia mwanga wake machoni. Wakati wa shida inaondoka pazia hii na hutamka mtu kwa umbile lake safi. Hakuna yeyote anayeokoka na shida hii vyovyote alivyo, hata mwenye afya huogopa maafa na kuhofia mwisho mbaya, akiwa ana akili. Imam Ali (as) anasema: “Mwenye shida sana hahitaji dua zaidi kuliko yule asiye na shida ambaye hasalimiki na balaa.”

Kama akituokoa na haya, hakika tutakuwa miongoni mwa wanaoshukuru.

Yaani wanamfanyia ikhlasi Mwenyezi Mungu peke yake wakati wa shida na hofu na wanatoa ahadi wao wenyewe kuwa watampwekesha Mwenyezi Mungu na kumshukuru, kama akiwaokoa na viza vya nchi kavu na baharini. Mara tu wanaposalimika na kuwa katika starehe wanamshirikisha na kufanya ufisadi. Elimu imethibitisha kuwa udhaifu wa utu na matakwa yake unakwenda na hali; sawa na yalivyo maji hufuata rangi ya chombo yalimowekwa.

Sema: Mwenyezi Mungu huwaokoa katika hayo na katika kila mashaka.

Kwa hiyo ilikuwa ni juu yenu kuzitukuza neema za Mwenyezi Mungu na kuzishukuru.

Kisha nyinyi mnamshirikisha.

Lakini baada ya kuwaneemesha kwa kuokoka mmebadilisha neema ya Mwenyezi Mungu kwa ukafiri na shirki.

Sema: Yeye ndiye awezaye kuwaletea adhabu kutoka juu yenu.

Au kutoka chini ya miguu yenu, kama mitetemeko na kudidimizwa ardhini.

Au awavuruge (muwe) makundi.

Yaani awachanganye-changanye na kuwafanya vikundi vinavyopondana visivyokuwa na msimamo; au amfanye mmoja wenu awe katika vita na ugomvi pamoja na nafsi yake, aridhie jioni yale yaliyomkasirisha asubuhi na kinyume, hali yake igongane wala asiwe na msimamo.

Na awaonjeshe baadhi yenu jeuri ya wenzao.

Yaani mpigane wenyewe kwa wenyewe.

Tazama jinsi tunavyozieleza ishara kwa njia mbali mbali ili wapate kufahamu.

Mwenyezi Mungu (swt) anasimamisha hoja na dalili zilizo wazi juu ya haki, kwa hisia akili na maono, na anapiga mifano ya kila aina kwa mbinu mbali mbali ili waijue haki waifuate, na batili wajiepushe nayo; na atakayehalifu basi hoja imemsimamia na atastahiki adhabu.

Na watu wako wameikadhibisha nayo ni haki

Msemo unaelekezwa kwa Mtume, dhamiri ya wameikadhibisha inarudia kwa Qur’an inayotamka dalili na hoja na adhabu ya mwenye kuikadhibisha.

Sema: Mimi si kuwakilishwa juu yenu.

Bali ni mtoa bishara na mwonyaji anayefikisha aliyotumwa na kumwachia Mwenyezi Mungu mambo ya hisabu na adhabu.

Kila habari ina wakati maalum.

Inawezekana Tafsir ya ‘mahali maalum’. Maana ni kuwa kila habari anayoitekeleza Mwenyezi Mungu ina wakatiau mahali maalum bila ya kuhalifu.

Na punde mtajua wakati wa kutokea kwake. Hili ni kemeo na kiaga kwa kukadhibisha haki.

وَإِذَا رَأَيْتَ الَّذِينَ يَخُوضُونَ فِي آيَاتِنَا فَأَعْرِضْ عَنْهُمْ حَتَّىٰ يَخُوضُوا فِي حَدِيثٍ غَيْرِهِ ۚ وَإِمَّا يُنْسِيَنَّكَ الشَّيْطَانُ فَلَا تَقْعُدْ بَعْدَ الذِّكْرَىٰ مَعَ الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ {68}

Na unapowaona wanaoziingilia Aya zetu basi jitenge nao mpaka waingie katika mazugumzo mengine. Na kama shetani akikusahaulisha, basi usikae baada ya kukumbuka pamoja na watu madhalimu.

وَمَا عَلَى الَّذِينَ يَتَّقُونَ مِنْ حِسَابِهِمْ مِنْ شَيْءٍ وَلَٰكِنْ ذِكْرَىٰ لَعَلَّهُمْ يَتَّقُونَ {69}

Wala si juu ya wale wenye takua hesabu yao hata kidogo, lakini ni mawaidha ili wapate kuwa na takua.

وَذَرِ الَّذِينَ اتَّخَذُوا دِينَهُمْ لَعِبًا وَلَهْوًا وَغَرَّتْهُمُ الْحَيَاةُ الدُّنْيَا ۚ وَذَكِّرْ بِهِ أَنْ تُبْسَلَ نَفْسٌ بِمَا كَسَبَتْ لَيْسَ لَهَا مِنْ دُونِ اللَّهِ وَلِيٌّ وَلَا شَفِيعٌ وَإِنْ تَعْدِلْ كُلَّ عَدْلٍ لَا يُؤْخَذْ مِنْهَا ۗ أُولَٰئِكَ الَّذِينَ أُبْسِلُوا بِمَا كَسَبُوا ۖ لَهُمْ شَرَابٌ مِنْ حَمِيمٍ وَعَذَابٌ أَلِيمٌ بِمَا كَانُوا يَكْفُرُونَ {70}

Na waache wale walioifanya dini yao ni mchezo na upuuzi na yamewadanganya maisha ya dunia. Na wakumbushe kwayo, isije nafsi yoyote ikafungwa kwa sababu ya yale iliyoyachuma. Haina mlinzi wala mwombezi isipokuwa Mwenyezi Mungu. Na hata ikatoa kila fidia haitapokelewa. Hao ndio waliofungwa kwa sababu ya yale waliyoyachuma. Watapata kinywaji cha maji ya moto sana na adhabu chungu kwa sababu ya waliyokuwa wakiyakanusha.