read

Aya 56-58: Sifuati Hawaa Zenu

Maana

Sema: Nimekatazwa kuwaabudu wale mnaowaomba badala ya Mwenyezi Mungu.

Katika Aya iliyotangulia Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameashiria njia ya wenye makosa. Katika Aya hii anaibainisha njia hiyo; kumwabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu.

Sema: Sifuati hawaa zenu, maana hapo nitapotea na sitakuwa miongoni mwa walioongoka.

Kwa sababu kuomba kwao hakuna asili yoyote ila hawaa na upotevu, sasa vipi atafuata Mtume Mtukufu?

Sema Hakika mimi ninayo dalili wazi itokayo kwa Mola wangu, nanyi mmeikadhibisha.

Yaani ninamwabudu Mwenyezi Mungu kwa ujuzi na nyinyi mnamkanusha; na mnaabudu masanamu kwa ujinga. Kwa mantiki gani mjuzi amfuate mjinga? Na mwenye batili amwongoze mwenye haki?

Sina haraka kwa mnayoyataka.

Mtume alipowatolea mwito wa kuamini walisema: “Tuletee mvua ya mawe kutoka mbinguni au tuletee adhabu kali.”

Ndipo Mwenyezi Mungu akamwamrisha aseme: Sina haraka. Bali yako kwa Mwenyezi Mungu anaiteremsha wakati anaotaka wala mimi sina uwezo wa kuitanguliza au kuichelewesha.

Hapana hukumu ila ya Mwenyezi Mungu katika kuteremsha adhabu na kuitanguliza au kuiahirisha. Anasimulia yaliyo kweli.

Yaani anasema kweli: Naye ni mbora wa wanaohukumu, hadhulumu yeyote katika hukumu yake.

Sema: Lau ningelikuwa nayo mnayotaka haraka katika adhabu, basi shauri lingekwisha baina yangu na baina yenu kwa kuangamizwa mwenye kudhulumu katika nyinyi.

Na Mwenyezi Mungu anawajua zaidi madhalimu.

Huharakisha au kuchelewesha adhabu kulingana na vile inavyopitisha hekima yake.

وَعِنْدَهُ مَفَاتِحُ الْغَيْبِ لَا يَعْلَمُهَا إِلَّا هُوَ ۚ وَيَعْلَمُ مَا فِي الْبَرِّ وَالْبَحْرِ ۚ وَمَا تَسْقُطُ مِنْ وَرَقَةٍ إِلَّا يَعْلَمُهَا وَلَا حَبَّةٍ فِي ظُلُمَاتِ الْأَرْضِ وَلَا رَطْبٍ وَلَا يَابِسٍ إِلَّا فِي كِتَابٍ مُبِينٍ {59}

Na ziko kwake funguo za ghaibu; hakuna azijuaye ila Yeye; anajua kilichomo nchi kavu na kilichomo baharini; na halianguki jani ila analijua wala punje katika giza la ardhi; wala kibichi au kikavu, ila kimo katika Kitab kinachobainisha.

وَهُوَ الَّذِي يَتَوَفَّاكُمْ بِاللَّيْلِ وَيَعْلَمُ مَا جَرَحْتُمْ بِالنَّهَارِ ثُمَّ يَبْعَثُكُمْ فِيهِ لِيُقْضَىٰ أَجَلٌ مُسَمًّى ۖ ثُمَّ إِلَيْهِ مَرْجِعُكُمْ ثُمَّ يُنَبِّئُكُمْ بِمَا كُنْتُمْ تَعْمَلُونَ {60}

Naye ndiye anayewafisha usiku. Na anakijua mlichokifanya mchana kisha huwafufua humo ili muda umalizike. Kisha kwake yeye ndiyo marejeo kwenu; kisha awaambiye mliyokuwa mkiyafanya.

وَهُوَ الْقَاهِرُ فَوْقَ عِبَادِهِ ۖ وَيُرْسِلُ عَلَيْكُمْ حَفَظَةً حَتَّىٰ إِذَا جَاءَ أَحَدَكُمُ الْمَوْتُ تَوَفَّتْهُ رُسُلُنَا وَهُمْ لَا يُفَرِّطُونَ {61}

Naye ndiye mwenye nguvu za kushinda juu ya waja wake. Na huwapelekea waangalizi. Hata mmoja wenu yakimjia mauti wajumbe wetu humfisha nao hawazembei.

ثُمَّ رُدُّوا إِلَى اللَّهِ مَوْلَاهُمُ الْحَقِّ ۚ أَلَا لَهُ الْحُكْمُ وَهُوَ أَسْرَعُ الْحَاسِبِينَ {62}

Kisha watarudishwa kwa Mwenyezi Mungu, Mola wao wa haki. Hakika hukumu ni yake, naye ni mwepesi kuliko wote wanaohisabu.