read

Aya 74-79: Ibrahim Na Baba Yake Na Watu Wake

Maana

Na Ibrahim alipomwambia baba yake Azar: Unawafanya masanamu kuwa waungu? Hakika ninakuona wewe na watu wako mko katika upotofu ulio wazi.”

Dhahiri ya Aya inafahamisha waziwazi kuwa Azar ni baba hasa wa Ibrahim Khalil (a.s.); na kwamba alikuwa mshirikina muabudu masanamu; na kwamba Ibrahim alimkataza ushirikina na akamlingania kwenye Tawhid. Huu ndio ufahamisho wa Aya unaofahamika mara moja kwenye fahamu ya
mjuzinamjinga,bilayakuweko ufafanuzi autafsir.

Pamoja na hayo wafasiri wamerefusha maneno na wakatofautiana kuwa je, Azar ni baba hasa wa Ibrahim au ni baba yake kimajazi.

Tofauti hii inazalisha tofauti nyingine kuwa je mababa na mababu wote wa Muhammad (s.a.w) waliamini Mungu mmoja na wala haifai kuweko mshirikina hata mmoja, au inawezekana kuweko washirikina na wapwekeshaji? Baadhi ya maulama wametunga vitabu maalum vya hilo tu.

Shia wanasema baba na mababu zake wote Muhammad ni wapwekeshaji Mungu kutokana na Hadith isemayo: “Niliendelea kugura kutoka migongo ya watakatifu mpaka kwenye mifuko ya uzazi ya watakatifu hadi akan- itoa Mwenyezi Mungu kwenye ulimwengu wenu huu.”
Wakasema kuwa baba hasa wa Ibrahim anaitwa Tarik na kwamba Azar ni ndugu wa baba yake au babu yake wa upande wa mama yake, amepewa jina la baba kimajazi tu.1

Al-Alusi anasema, “Kundi kubwa la Sunni pia wanasema hivyo.” Lakini mwenye Tafsir Al-manar na Razi wanasema: “Sunni hawaafikiani na Shia kwenye rai yao hii na wanasema inawezekana kuweko washirikina au walahidi katika mababu wa Mtume.”

Dhahiri ya Qur’an iko pamoja nao, hasa kauli yake Mwenyezi Mungu:

وَاذْكُرْ فِي الْكِتَابِ إِبْرَاهِيمَ ۚ إِنَّهُ كَانَ صِدِّيقًا نَبِيًّا {41}

إِذْ قَالَ لِأَبِيهِ يَا أَبَتِ لِمَ تَعْبُدُ مَا لَا يَسْمَعُ وَلَا يُبْصِرُ وَلَا يُغْنِي عَنْكَ شَيْئًا {42}

“Na mtaje Ibrahim katika Kitab. Hakika yeye alikuwa mkweli sana, Nabii. Alipomwambia baba yake: Ee baba yangu! Kwa nini unaabudu visivyosikia na visivyoona na visivyokufaa chochote.” (19: 41-42).

Kwa vyovyote iwavyo hakuna faida ya mzozo huu, kwa sababu hauna uhusiano wowote na itikadi ya Kiislamu. Kwa sababu linalotakikana kwa Mwislamu ni kuamini Utume wa Muhammad (saw) na Isma yake na kwamba yeye ni bwana wa Mitume na ni wa mwisho wao. Ama kuamini kuwa baba na mababu zake wote ni wapwekeshaji Mwenyezi Mungu, na kwamba Azar ni ami wa Ibrahim na sio baba yake. Yote haya si chochote katika itikadi ya Kiislamu.

Na namna hii tukamwonyesha Ibrahim ufalme wa mbingu na ardhi.

Makusudio ya ‘namna hii’ ni kuwa Mwenyezi Mungu (swt) kama ambavyo alimfichulia Ibarahim upotevu wa watu wake wa kuabudu kwao masana- mu, pia alimfunulia maajabu ya mbingu na ardhi ili atoe dalili, kwa ustadi wa nidhamu yake na ufundi wa utengenezwaji wake, juu ya kuweko Mwenyezi Mungu, umoja wake na utukufu wake na awe miongoni mwa wenye yakini.

Aya hii inafahamisha mambo mawili:

1. Itikadi ya Uislamu inaismamia uhuru wa rai na akili. Kwa sababu Mwenyezi Mungu (swt) hakuwajibisha mtu kumwamini ila baada ya kumwekea hoja na akataka afanye uchunguzi.

2. Kuwa dalili aliyoiweka juu ya kuweko kwake ni nyepesi na sahali kufahamiwa na watu wote bila ya kuhitaji juhudi wala sayansi au falsafa. Yatosha mtu kuangalia maajabu ya ulimwengu na utaratibu wake ili aweze kuongoka kwa Muumbaji wake na mtegenezaji wake.

Na usiku ulipomwingilia, akaona nyota, alinena: Hii ni Mola wangu.

Watu wa Ibrahim walikuwa wakiabudu nyota badala ya Mwenyezi Mungu. Akataka kuwavuta kidogo kidogo kwenye haki na kuwaelekeza kwenye mantiki ya kiakili na kimaumbile kwa upole na ulaini. Akangoja mpaka usiku ulipoingia na kufunga giza, akaona nyota wanazoziabudu. Akasema kwa kuigiza madai yao: ‘Huyu ni Mola wangu’. Wakamwamini, lakini ilipotua na kupotea pambizoni, akili zao zilizinduka na mtazamo wao ukaona kuwa Mwenyezi Mungu habadiliki wala kugeuka na wala hifichwi na chochote.

Na alipouona mwezi unachomoza alisema kwa kutaka kuwavuta:

Huu ni Mola wangu, kwa sababu ni mkubwa na una mwangaza zaidi kuliko ule wa kwanza.

Ulipotua alisema: Asiponiongoza Mola wangu, hakika nitakuwa katika watu waliopotea.

Anaashiria kuwa yeye bado hajatulizwa nafsi yake na nyota hizii; na kwamba yeye bado hajaongoka kwenye njia na akamtaka Mwenyezi Mungu amwokoe.

Na alipoliona jua linachomoza alisema: Hili ndilo Mola wangu. Hili ni kubwa kabisa. Lilipotua alisema: Enyi watu wangu! Mimi simo katika hayo mnayoyashirikisha.

Jaribio la kwanza, la pili na la tatu yamepita na shaka ikabakia kama ilivyokuwa. Kwa hiyo hapana budi kujiepusha na kuabudu nyota.

Kwani hazistahiki kuabuduiwa wala kutukuzwa. Baada ya kutangaza kujitoa kati- ka waungu wao aliuelekeza moyo wake kwa Muumba wa ulimwengu na akasema:

Hakika mimi nimeuelekeza uso wangu kwa yule aliyeziumba mbingu na ardhi, hali ya kuwa nimeacha dini za upotevu, tena mimi si katika washirikina.

Hii ndiyo natija ya utafiti na kufikiria katika kitu chochote miongoni mwa vitu vya ulimwengu huu. Mtazamo mmoja tu, wa kuangalia sura yoyote katika sura za ulimwengu huu, lazima utapelekea kwenye yakini ya mkato kuwa Mwenyezi Mungu pekee yake ndiye Muumba wa mbingu na ardhi.

وَحَاجَّهُ قَوْمُهُ ۚ قَالَ أَتُحَاجُّونِّي فِي اللَّهِ وَقَدْ هَدَانِ ۚ وَلَا أَخَافُ مَا تُشْرِكُونَ بِهِ إِلَّا أَنْ يَشَاءَ رَبِّي شَيْئًا ۗ وَسِعَ رَبِّي كُلَّ شَيْءٍ عِلْمًا ۗ أَفَلَا تَتَذَكَّرُونَ {80}

Na watu wake wakamhoji. Akasema: Je, mnanihoji juu ya Mwenyezi Mungu na hali yeye ameniongoza? Wala siogopi wale mnaowashirikisha naye; isipokuwa Mola wangu akitaka kitu. Mola wangu ana wasaa wa kujua kila kitu. Je, hamkumbuki.

وَكَيْفَ أَخَافُ مَا أَشْرَكْتُمْ وَلَا تَخَافُونَ أَنَّكُمْ أَشْرَكْتُمْ بِاللَّهِ مَا لَمْ يُنَزِّلْ بِهِ عَلَيْكُمْ سُلْطَانًا ۚ فَأَيُّ الْفَرِيقَيْنِ أَحَقُّ بِالْأَمْنِ ۖ إِنْ كُنْتُمْ تَعْلَمُونَ {81}

Nitaogopaje hao mnaowashirikisha, na hali nyinyi hamwogopi kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kile ambacho hakukiteremshia dalili kwenu? Basi kundi gani katika mawili haya linastahiki kupata amani kama nyinyi mnajua?

الَّذِينَ آمَنُوا وَلَمْ يَلْبِسُوا إِيمَانَهُمْ بِظُلْمٍ أُولَٰئِكَ لَهُمُ الْأَمْنُ وَهُمْ مُهْتَدُونَ {82}

Wale walioamini na hawakuchanganya imani yao na upotevu, hao ndio watakaopata amani na ndio walioongoka.

وَتِلْكَ حُجَّتُنَا آتَيْنَاهَا إِبْرَاهِيمَ عَلَىٰ قَوْمِهِ ۚ نَرْفَعُ دَرَجَاتٍ مَنْ نَشَاءُ ۗ إِنَّ رَبَّكَ حَكِيمٌ عَلِيمٌ {83}

Na hiyo ndiyo hoja yetu tuliyompa Ibrahim juu ya watu wake. Tunamuinua kwa vyeo yule tumtakaye. Hakika Mola wako ndiye mwenye hekima, Mjuzi.
  • 1. Zimekuja Hadith Mutawatir kwamba Abdul Mutwalib, babu wa Mtume (saww) aliapa kuwa akiruzukiwa watoto kumi atamchinja mmoja wao na kwamba kura ilimwangukia Abdullah, baba wa Muhammad (saw). Haya yanapingana na kuwa mababu zake Mtume wote walikuwa kwenye dini ya Ibrahim.