read

Aya 68 – 70: Mpaka Waingie Katika Mazungumzo Mengine

Maana

Na unapowaona wanaoziingilia Aya zetu basi jitenge nao mpaka waingie katika mazugumzo mengine.

Yamepita maelezo yake katika kufasiri Juz.5 (4:139)

Na kama shetani akikusahaulisha, basi usikae, baada ya kukumbuka, pamoja na watu madhalimu.

Msemo unaelekezwa kwa Mtume kwa dhahiri, lakini makusudio ni kwa mwingine kwa hali halisi. Kwa sababu Mtume ni mwenye kuhifadhiwa na madhambi na makosa na kusahau (maasum). Vinginevyo basi kauli yake na vitendo vyake na uthibitisho wake usingekuwa ni hoja na dalili mkato isiyokubali mjadala wala ubishi.
Wala si juu ya wale wenye takua hesabu yao hata kidogo, lakini ni mawaidha ili wapate kuwa na takua.

Yaani si juu ya waumini wanaomcha Mwenyezi Mungu chochote katika kufuatilia makafiri ambao wanaingilia Aya za Mwenyezi Mungu, lakini wawakumbushe na wawakataze ili wajiepushe kuingilia Aya za Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Ama Aya zifuatazo zina mambo yafuatayo:

Na waache wale walioifanya dini yao ni mchezo na upuuzi na yame- wadanganya maisha ya dunia.

Kwa dhahiri amri inamwelekea Mtume na kwa hali ilivyo inamwelekea yeye na anayemfuata katika waumini. Anawaamrisha Mwenyezi Mungu (swt) waache kutangamana na wale ambao wameifanya dini yao ni mchezo na upuuzi na wala hakuwaamrisha kuwapuuza na kuacha kuwaonya. Kwa sababu kauli yake Mwenyezi Mungu:

Na wakumbushe kwayo ni amri ya kuwaonya.

Kila mwenye kuwa katika dini yoyote miongoni mwa dini na asiheshimu na kuitukuza misingi yake yote na hukumu zake zote, basi atakuwa ameifanya dini yake ni mchezo na upuzi. Mwenye kuifanyia dini chumo au akaita moja ya hukumu zake kwa namna ambayo inapelekea dharau, basi yeye atakuwa ndiye anayekusudiwa na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

Walioifanya dini yao ni mchezo na upuzi.

Hakuna mwenye kutia shaka kuwa ambaye hana dini ni bora kuliko yule anayedharau misingi yake na hukumu zake. Kwa sababu huyu alivyo hasa ni kuwa ameifanyia dini mchezo na upuzi na hiyo ndiyo dini yake.

Na wakumbushe kwayo, isije nafsi yoyote ikafungwa kwa sababu ya yale iliyoyachuma. Haina mlinzi wala mwombezi isipokuwa Mwenyezi Mungu.

Baada ya Mwenyezi Mungu (swt) kumwamrisha Mtume na waumini kutotangamana na wale walioifanyia mchezo dini yao, aliwaamrisha kuwakumbusha Qur’an wale ambao wanaingilia Aya za Mwenyezi Mungu na kucheza na dini ili wasiadhibiwe kwa yale makosa na madhambi yaliyo chumwa na mikono yao, katika siku ambayo hawatapata msaidizi wa kuwasaidia asiyekuwa Mwenyezi Mungu wala mwombezi atakayewaombea mbele ya Mwenyezi Mungu.

Na hata ikatoa kila fidia haitapokelewa.

Yaani kama ambavyo kafiri hatapata mlinzi wala mwombezi siku ya Kiyama, vilevile haitakubaliwa fidia yake kwa namna yoyote itakavyokuwa. Amesema Razi: “Mtu akifikiri namna ya adhabu kwa njia hii atakurubia kugwaya anapothubutu kumwasi Mwenyezi Mungu.”

Hao ndio waliofungwa kwa sababu ya yale waliyoyachuma. Watapata kinywaji cha maji ya moto sana na adhabu chungu kwa sababu ya waliyokuwa wakiyakanusha.

Hao ni ishara ya wale walioifanyia mchezo dini. Na kufungika kwa waliyoyachuma; yaani wamewekwa rahani na matendo yao. Ama kupata kinywaji cha maji ya moto sana, ni kubainisha adhabu ya ukafiri wao na uasi wao.

قُلْ أَنَدْعُو مِنْ دُونِ اللَّهِ مَا لَا يَنْفَعُنَا وَلَا يَضُرُّنَا وَنُرَدُّ عَلَىٰ أَعْقَابِنَا بَعْدَ إِذْ هَدَانَا اللَّهُ كَالَّذِي اسْتَهْوَتْهُ الشَّيَاطِينُ فِي الْأَرْضِ حَيْرَانَ لَهُ أَصْحَابٌ يَدْعُونَهُ إِلَى الْهُدَى ائْتِنَا ۗ قُلْ إِنَّ هُدَى اللَّهِ هُوَ الْهُدَىٰ ۖ وَأُمِرْنَا لِنُسْلِمَ لِرَبِّ الْعَالَمِينَ {71}

Sema: Je, tuwaabudu wasiokuwa Mwenyezi Mungu ambao hawatunufaishi wala kutudhuru? Na turudishwe nyuma baada ya Mwenyezi Mungu kutuongoza? Kama yule ambaye mashetani wamempoteza; akiwayawaya katika ardhi. Anao marafiki wanaomwita kwenye uongofu: Njoo kwetu. Sema: Mwongozo hasa ni mwongozo wa Mwenyezi Mungu. Na tumeamrishwa tusilimu kwa Mwenyezi Mungu, Mola wa viumbe vyote.

وَأَنْ أَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَاتَّقُوهُ ۚ وَهُوَ الَّذِي إِلَيْهِ تُحْشَرُونَ {72}

Na simamisheni Swala na mcheni yeye; naye ndiye ambaye kwake mtakusanywa.

وَهُوَ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ بِالْحَقِّ ۖ وَيَوْمَ يَقُولُ كُنْ فَيَكُونُ ۚ قَوْلُهُ الْحَقُّ ۚ وَلَهُ الْمُلْكُ يَوْمَ يُنْفَخُ فِي الصُّورِ ۚ عَالِمُ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ ۚ وَهُوَ الْحَكِيمُ الْخَبِيرُ {73}

Naye ndiye aliyeziumba mbingu na ardhi kwa haki. Na siku anayosema ‘kuwa’ basi huwa. Kauli yake ni haki. Na ufalme ni wake siku itakapopulizwa parapanda. Mjuzi wa ghaibu na yanayoonekana. Naye ndiye mwenye hekima mwenye habari.