Aya 4-6: Kukana Hoja Za Mwenyezi Mungu
Lugha
Imeelezwa katika Tafsiri Razi: Wamesema baadhi: Karne ni miaka sitini. Wengine wakasema ni sabini. Wengine wakasema ni thamanini. Lililo karibu zaidi na ufahamu ni kwamba si yenye kukadiriwa kwa muda fulani kwa zaidi au kupungua, bali makusudio ni watu wa kila zama. Wakimaliza muda mwingi husemwa: Imekwisha karne. Dalili ya hilo ni kauli yake Mtume mtukufu (s.a.w.w): "karne bora ni karne yangu." Misingi ya itikadi ni mitatu, Tawhid, Utume na Ufufuo. Aya tatu zilizotangulia zimeelezea Tawhid na dalili zake na Aya hii inaelezea Utume na hali ya wanaoukanusha.
Na haiwafikii ishara yoyote katika ishara za Mola wao ila wanaipinga.
Makusudio ya ishara hapa ni hoja mkato ya kuweko Mwenyezi Mungu na umoja wake, ufufuo na Utume wa Muhammad. Maana ni kuwa makafiri wanakataa dalili ya haki na wanaipinga bila ya kuichunguza. Lau wangelikuwa ni watafutaji ukweli wangeliangalia dalili na kuzingatia maana yake. Ama kukataa na kuipinga kabla ya kuichunguza ni inadi na ujuba.
Hakuna Udikteta Ardhini Wala Mbinguni
Wametofautiana wafasiri katika kuainisha makusudio ya hoja waliyoipinga na kuidharau. Je, ni Qur'an au muujiza mwingineo katika miujiza ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.).? Au ni miujiza ya Mitume wote? Nimegundua wakati nikifuatilia tofauti hizi kuwa Aya hii tunayoifasiri na mfano wake katika Qur'an zimekusanya maana ambayo wafasiri wameji- himu kuisherehesha (kuifafanua).
Aya imekusanya dalili kwamba Uislamu unasimamia uhuru wa akili na kutoa maoni na kwamba si haki kwa yeyote, vyovyote awavyo kumtaka mwingine akubali maneno yake hivi hivi tu kwa upofu na bila ya dalili. Hata Muumba wa ulimwengu, ambaye neno lake ni tukufu, hawalazimishi waja wake kumwamini yeye na vitabu vyake, bila ya dalili.
Mwenyezi Mungu Mtukufu anasimamisha hoja kwa kila anayoyasema na kuyatolea mwito na kumtaka kila mwenye akili kuichunguza na kuangalia vizuri maana yake. Mwenyezi Mungu katika hilo ametukuka kabisa - ni kama kila mjuzi anayechunga haki; hata kama ukiwa mbali mshabaha wa Muumba na kiumbe.
MwenyeziMunguMtukufuanasema:
أَوَلَمْ يَتَفَكَّرُوا فِي أَنْفُسِهِمْ ۗ مَا خَلَقَ اللَّهُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا إِلَّا بِالْحَقِّ {8}
Na akasema:
أَفَلَمْ يَنْظُرُوا إِلَى السَّمَاءِ فَوْقَهُمْ كَيْفَ بَنَيْنَاهَا وَزَيَّنَّاهَا وَمَا لَهَا مِنْ فُرُوجٍ {6}
Na akasema tena:
كَذَٰلِكَ نُفَصِّلُ الْآيَاتِ لِقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ {24}
Aya hizi na nyinginezo, zinafahamisha kwa dalili mkato kuwa yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu huleta dalili na hoja kwenye mwito wa haki na kutoa mwito wa kuzifikiria vizuri na kuzichunguza.
Akipinga yule asiyeamini ila yale anayoyataka yeye, basi yeye peke yake ndiye mwenye jukumu la kukanusha kwake na kupinga kwake.
Wameikadhibisha haki ilipowafikia; kwa hiyo zitawafikia habari za yale waliyokuwa wakiyafanyia mzaha.
Mtu anaweza kujitia kutoijua haki bila ya kuitilia umuhimu, na kutoiamini, lakini akawa haiungi mkono wala kuipiga vita; kama ilivyo kwa mtu asiyejali mambo.
Au anaweza kuwa katika msimamo wa mwenye kuikadhibisha. Huyu ni mwenye kiburi, ikiwa atakadhibisha na huku anajijua. Ama akiikadhibisha na kuidharau, basi huyo ni mwenye kuipiga vita.
Wa kwanza kosa lake ni hafifu kuliko wa pili kwa sababu yeye anafanana na mtu asiyepiga kura.Wa pili naye dhambi yake ni hafifu kuliko watatu kwa sababu yeye ameitia kura yake kwa waongo. Ama wa tatu amekadhibisha na akadhihirisha harakati dhidi ya haki, naye ndiye aliyekusudiwa kukemewa na kupewa kiaga, na kwamba yeye atakutana na malipo ya inadi yake na istihzai yake.
Je hawaoni vizazi vingapi tulivyoviangamiza kabla yao? Tuliwamakinisha katika nchi tusivyowamakinisha nyinyi.
Waarabu wa kijahiliya walikuwa wakijua mengi kuhusu watu wa Ad, Thamud, Lut na wengineo, na katika misafara yao walikuwa wakiona athari zao wakizishuhudia na kuzizungumzia. Walikuwa wakijua kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwaangamiza kwa sababu wao walikadhibisha haki waliyokuja nayo Mitume yao kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Aya hii inawahusu wale waliomkadhibisha Muhammad (s.a.w.) kuwa wazingatie kuangamia kwa vizazi vilivyo pita. Nao walikuwa na milki na nguvu wasizokuwa nazo hao wanaoambiwa - Waarabu wa kijahiliya.
Tukawapelekea mvua nyingi.
Yaani mvua inayoleta mavuno na kuwamiminia riziki.
Na tukaifanya mito inapita chini yao.
Ni fumbo la rutuba na mavuno mengi.
Kisha tukawaangamiza kwa dhambi zao
Mali na nguvu hazikuwafaa kitu.
Na tukaanzisha baada yao karne nyingine.
Mwenye akili ni yule mwenye kupata funzo kutokana na wengine kabla ya mwengine kupata funzo kutoka kwake.
وَلَوْ نَزَّلْنَا عَلَيْكَ كِتَابًا فِي قِرْطَاسٍ فَلَمَسُوهُ بِأَيْدِيهِمْ لَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا إِنْ هَٰذَا إِلَّا سِحْرٌ مُبِينٌ {7}
وَقَالُوا لَوْلَا أُنْزِلَ عَلَيْهِ مَلَكٌ ۖ وَلَوْ أَنْزَلْنَا مَلَكًا لَقُضِيَ الْأَمْرُ ثُمَّ لَا يُنْظَرُونَ {8}
وَلَوْ جَعَلْنَاهُ مَلَكًا لَجَعَلْنَاهُ رَجُلًا وَلَلَبَسْنَا عَلَيْهِمْ مَا يَلْبِسُونَ {9}
وَلَقَدِ اسْتُهْزِئَ بِرُسُلٍ مِنْ قَبْلِكَ فَحَاقَ بِالَّذِينَ سَخِرُوا مِنْهُمْ مَا كَانُوا بِهِ يَسْتَهْزِئُونَ {10}
قُلْ سِيرُوا فِي الْأَرْضِ ثُمَّ انْظُرُوا كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الْمُكَذِّبِينَ {11}