Aya 91 - 92: Hawamheshimu Mwenyezi Mungu Kama Inavyotakiwa
Maana
Na hawakumkadiria Mwenyezi Mungu kwa haki ya kadiri yake , waliposema: Mwenyezi Mungu hakuteremshia binadamu chochote.
Aya hii inafahamisha kuwa katika wakati wa Mtume wa Mwenyezi Mungu kulikuwa na watu wanaokanusha wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa mtu yoyote, na wakisema kuwa Mwenyezi Mungu hakumtuma mtu yeyote kuwa mjumbe. Lakini Mwenyezi Mungu (swt) hakubainisha ni akina nani waliokanusha na kusema hivyo.
Kwa ajili hii waliotofautiana wafasiri, kuhusu waliokusudiwa katika kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu. Je, ni washirikina wa Kiarabu au Mayahudi wa Hijaz?
Kuna kundi la wafasiri waliosema kuwa ni washirikina wa Kiarabu. Kauli hii inapingwa, kwanza kuwa Mwenyezi Mungu (swt) alimwamrisha Mtume wake kuwakabili na swali hili:
Sema: Ni nani aliyekileta Kitab alichokuja nacho Musa chenye nuru na mwongozo kwa watu?
Kimsingi ni kuwa swali hili linaelekezwa kwa yule anayekubali Utume wa Musa na Tawrat; na yajulikana kuwa washirikina wa Kiarabu hawakubali Utume wa Musa na Tawrat yake; vinginevyo wangelikuwa ni katika watu wa Kitab.
Pili, ni kwamba Mwenyezi Mungu (swt) amewatahayariza wakanushaji kwa kauli yake:
Mlichokifanya nyaraka-nyaraka, mkizidhihirisha na mkificha mengi.
Yaani kuwa nyinyi mmeibadilisha Tawrat, mkadhihirisha yale yanayoafikiana na hawaa zenu na mkaficha yale yasiyoafikiana nayo. Inajulikana kuwa walioibadilisha Tawrat ni Mayahudi, sio washirikina wa Kiarabu.
Kundi jingine la wafasiri limesema kwamba waliosema kuwa Mwenyezi Mungu hakuteremsha chochote kwa mtu, ni Mayahudi. Wakatoa dalili kwa mambo mawili: Kuwa Mwenyezi Mungu alimwamrisha Mtume wake Muhammad amjibu anayesema hivi kwa Utume wa Musa na Tawrat, nalo ni jibu sahihi, kisha akatilia mkazo jibu hili kwa kuipotosha kwao Tawrat akasema: “Mlichokifanya nyaraka-nyaraka”
Kauli hii iko karibu na dhahiri ya Aya kuliko ile ya kwanza.
Na mkafundishwa msiyoyajua nyinyi wala baba zenu.
Msemo huu unaelekezwa kwa Mayahudi vilevile; na maana yake ni, vipi mnasema – Enyi Mayahudi – kuwa Mwenyezi Mungu hakuteremsha chochote kwa mtu yeyote na hali nyinyi mnaitakidi kwamba Musa ni mwanadamu na kwamba Tawrat imeteremshwa kwake? Na mmejua kutokana nayo yale mliyokuwa hamyajui nyinyi na baba zenu.
Miongoni mwayo ni kuwa nyinyi mlikuwa mkisoma katika Tawrat sifa za Muhammad kabla ya kutumwa kwake, wala hamkuwa mkimjua kwa ufafanuzi aliyekusudiwa. Mwenyezi Mungu alipomtuma na mkamjua aliyekusudiwa hasa, kwa kiburi na inadi yenu mkageuza na kuondosha yale yanayomwelezea.
Sema: Ni Mwenyezi Mungu.
Hili ni jawabu la swali lililotangulia (Sema: Ni nani aliyeteremsha Kitab alichokuja nacho Musa?
Jibu hili ndilo lenyewe hasa na halikimbiliki. Kwa sababu Mayahudi wanakiri kuwa Tawrat inatoka kwa Mwenyezi Mungu. Na kwa ajili ya kukiri kwao huku ndio inawasimamia hoja na kuwajibu kauli yao ya kuwa Mwenyezi Mungu hakuteremsha chochote kwa mtu.
Kisha waache wacheze katika porojo zao.
Yaani sema haki Ewe Muhammad, na waache Mayahudi katika batili zao wala usijishughulishe na inadi zao na ria zao.
Huku ni kuwapa onyo na kuwapa kiaga, kama ambavyo pia ni kuwadharau na kuwapuuza.
Utauliza: Mayahudi wanaukubali Utume wa Musa (a.s.) na kuteremshwa Tawrat, kama yalivyotangulia maelezo. Kwa hiyo imekuwaje Mwenyezi Mungu akawanasibishia kukanusha wahyi na Utume?
Jibu: Wao wanakanusha wahyi na Utume kwa dhahiri, kwa inadi na kiburi kwa Muhammad (saw) na si kwa undani hasa.
وَجَحَدُوا بِهَا وَاسْتَيْقَنَتْهَا أَنْفُسُهُمْ ظُلْمًا وَعُلُوًّا ۚ {14}
Mitume Wa Mwenyezi Mungu Na Wanasayansi
Wanasayansi wengi wakati huu wanaamini kuweko Mwenyezi Mungu. Kwa sababu wameona kuwa ulimwengu huu unakwenda kulingana na kanuni thabiti, na iliyowazi inayohukumu, haiepukani nao kwa hali yoyote ile.
Kwa ajili hii imewezekana kuichunguza, kuikisia na kufaidika nayo. Huku ni kuthibitika kuweko nguvu ya hali ya juu nyuma ya ulimwengu inay- ofanya uhandisi na kujenga; na nguvu hiyo ndio Mwenyezi Mungu.
Kwa maneno mengine, si lazima mtu akitaka kujua kuweko kila kitu afanye majaribio katika vyombo na kukiona kwa macho, bali inatosha kwa kujua kwa elimu isiyo na shaka na dhana, ni sawa elimu hiyo iwe imetokana na majaribio na macho au imetokana na natija ya akili ya kiasili. Mwenye fikira na uchunguzi akitaamali ulimwnengu huu kwa taamuli ya kielimu isiyo na shaka shaka, lazima atakomea kwenye kumjua Mwenyezi Mungu.
Lakini Wanasayansi waliojua kuweko Mwenyezi Mungu kwa Kisayansi, wamekanusha kuwa ana wajumbe katika watu anaowapa wahyi na wakasema: Nguvu-asili (nature) peke yake ndio Kitab cha Mwenyezi Mungu na wala sio Tawrat, Injil na Qur’an.
Sina shaka kwamba wataalam hawa, lau wangelipa somo la Qur’an wakati mdogo tu katika muda ule ule walioutoa kwa kusoma sayansi wangelikinai kuwa Mwenyezi Mungu ana vitabu viwili: Ulimwengu na wahyi. Na kwamba mtu anavihitajia vyote viwili.
Kutokana na Kitab cha ulimwengu atajua Ufalme wa Mwenyezi Mungu na kumwamini. Na kutokana na Kitab cha wahyi atajua sharia ya Mwenyezi Mungu ambayo itamwangazia njia ya maisha, kusonga mbele na kujiepusha na maangamizo na matatizo ambayo yatachelewesha safari yake ya kwenda mbele.
Mtu ameumbwa ili afanye kazi katika maisha haya, kwa hivyo basi, hapana budi kwa kila anayefanya amali kuwa na njia anayoifuata katika kufanya kazi. Kwa sababu kujifanyia mambo ovyo ovyo hakupelekei kheri yoyote. Na Mwenyezi Mungu ndiye aliyememuumba mtu, anajua siri yake na dhahiri yake, nguvu yake na udhaifu wake na yale yanayomnufaisha na kumdhuru.
Kwa hiyo basi ni lazima kuwa yeye ndiye marejeo ya kwanza ya njia ambayo inapasa mtu kuifuata katika kazi yake; sawa na ilivyo kwa mgun- duzi wa ndege na gari na mengineyo; ambapo inakuwa lazima kumrejea yeye katika kutaka kuitumia na kufaidika nayo. Kwa sababu yeye ndiye Ayajuae zaidi masilahi ya ndege na madhara yake.
Hakuna mwenye shaka kwamba kuifikisha njia ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake na kuwafahamisha kunafungika na Mitume na Manabii, kwa sababu wao ndio lugha ya Mwenyezi Mungu na ubainifu wake. Huu ndio wahyi hasa.
Anayetaka ufafanuzi na arejee kitab chetu Al-Islam wal-aql (Uislamu na akili) sehemu ya Utume na akili.
Na hiki ni kitab tulichokiteremsha, kilichobarikiwa, chenye kusadik- isha yale yaliyokitangulia.
Hii, ni Qur’an Tukufu; na maana ni kuwa kama tulivyoteremsha Tawrat kwa Musa, Vilevile tumeiteremsha hii Qur’an Kwa Muhammad (s.a.w.) nayo ina manufaa na faida nyingi kwa anayejua hukumu zake na siri zake na akazitumia.
Nayo Vilevile inasadikisha vitabu vya Mwenyezi Mungu ambavyo vimeteremshiwa Mitume wa Mwenyezi Mungu tangu zamani. Imam Ali anasema: “Jifundisheni Qur’an kwani hiyo ni mazungumuzo mazuri, na ifa- hamuni kwani hiyo ni utuvu wa nyoyo, na ifanyeni dawa kwa nuru yake kwani hiyo ni ponyo la nyoyo, na isomeni vizuri kwani hiyo ina visa vizuri.”
Na ili uwaonye (watu wa) Ummul qura na walio pambizoni mwake.
Ummul-qura (Mama wa miji) ni Makka. Imeitwa hivyo kwa sababu mna nyumba ya kwanza iliyowekwa kwa ajili ya watu kumwabudu Mwenyezi Mungu.
Wastashriki (Wataalamu wa kimagharibi juu ya mambo ya uislamu) na kabla yao Mayahudi walidai kuwa Muhammad (s.a.w.) ametumwa kwa Waarabu tu, kwa kutolea hoja Aya hii, na kusahau Aya nyingine; kama vile:
وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا رَحْمَةً لِلْعَالَمِينَ {107}
وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا كَافَّةً لِلنَّاسِ بَشِيرًا وَنَذِيرًا وَلَٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ {28}
Wamejitia purukushani na Aya hizo na hali chimbuko la Qur’an ni moja. maneno yake yanajifasiri hayo yenyewe na Aya mbili hizi ni ubainifu wa kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘Na ili uwaonye (watu wa) Ummul qura na walio pembezoni mwake.’
Na Vilevile makusudio yake ni kuanza mwito wa Uislam, mwanzo kabisa, katika mji wa mwenye mwito huo; yaani Makka.
Mpaka utakapopata wafuasi ndipo uwape bishara walio kando kando yake; kama vile mwito wowote unavyoanza, ambapo unazaliwa kisha unatembea mabara yote.
Zaidi ya hayo imethibiti riwya kwa njia ya Mutawatir kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) aliwaandikia Wafalme na viongozi wote akiwalingania kwenye Uislamu, miongoni mwao ni Mfalme Kisra wa Fursi (Iran) na Kaizari wa Roma. Wastashriki wanajua hayo, lakini baadhi yao wanaficha wanayoyajua.
Na wale wanaoamini akhera, wanakiamini.
Dhamiri ya wanakiamini inarudia Kitabu ambacho ni Qur’an. Yeyote atakayeisoma Qur’an kwa uchunguzi na kuzingatia maana hutoka na kitu.
Akiwa anamwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho, basi huzidi imani, na akiwa anamwamini Mwenyezi Mungu tu, basi ataamini wahyi na ufufuo; akiwa anamwamini Mwenyezi Mungu na ufufuo bila wahyi, basi ataamini Mitume na vitabu vya Mwenyezi Mungu, na hasa Utume wa Muhammad na Qur’an.
Akiwa anamkanusha Mwenyezi Mungu atamwamini. Kwa sababu Qur’an itamwonyesha dalili za hilo na kumhimiza kuichunguza. Nayo kwa asili yake humpeleka mtafiti, anayechunga haki, kwenye elimu.
Nao huzihifadhi Swala zao.
Ili daima wawe na mawasiliano ya kutegemewa na Mwenyezi Mungu. Ameihusisha kutaja Swala kinyume cha ibada nyinginezo kwa sababu ndiyo nguzo kubwa ya dini na inayodumisha imani. Miongoni mwa kazi za swala ni kumkataza mwenye kuswali uovu na mambo mabaya.
وَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّنِ افْتَرَىٰ عَلَى اللَّهِ كَذِبًا أَوْ قَالَ أُوحِيَ إِلَيَّ وَلَمْ يُوحَ إِلَيْهِ شَيْءٌ وَمَنْ قَالَ سَأُنْزِلُ مِثْلَ مَا أَنْزَلَ اللَّهُ ۗ وَلَوْ تَرَىٰ إِذِ الظَّالِمُونَ فِي غَمَرَاتِ الْمَوْتِ وَالْمَلَائِكَةُ بَاسِطُو أَيْدِيهِمْ أَخْرِجُوا أَنْفُسَكُمُ ۖ الْيَوْمَ تُجْزَوْنَ عَذَابَ الْهُونِ بِمَا كُنْتُمْ تَقُولُونَ عَلَى اللَّهِ غَيْرَ الْحَقِّ وَكُنْتُمْ عَنْ آيَاتِهِ تَسْتَكْبِرُونَ {93}
وَلَقَدْ جِئْتُمُونَا فُرَادَىٰ كَمَا خَلَقْنَاكُمْ أَوَّلَ مَرَّةٍ وَتَرَكْتُمْ مَا خَوَّلْنَاكُمْ وَرَاءَ ظُهُورِكُمْ ۖ وَمَا نَرَىٰ مَعَكُمْ شُفَعَاءَكُمُ الَّذِينَ زَعَمْتُمْ أَنَّهُمْ فِيكُمْ شُرَكَاءُ ۚ لَقَدْ تَقَطَّعَ بَيْنَكُمْ وَضَلَّ عَنْكُمْ مَا كُنْتُمْ تَزْعُمُونَ {94}