read

Aya 46-49: Akichukua Mwenyezi Mungu Kusikia Na Kuona

Maana

Sema: Mwaonaje kama Mwenyezi Mungu akichukuwa kusikia kwenu na kuona kwenu na akaziziba nyoyo zenu, ni nani Mungu mwingine isipokuwa Mwenyezi Mungu awezaye kuwaletea tena?

Mtu ni usikizi, uoni na moyo. Lau haya yanamwondokea, basi hatakuwa ni chochote, mnyama atakuwa ni bora kuliko yeye. Hakuna mwenye shaka kwamba Mwenyezi Mungu anaweza kuvichukua hivyo, kwa sababu Yeye ndiye aliyeviumba. Makusudio ya ishara hii ni kuwakumbusha Mwenyezi Mungu Makafiri kuwa wanaowafanya waungu asiyekuwa yeye hawatawakinga na madhara wala hawatawaletea manufaa:

وَإِذَا أَرَادَ اللَّهُ بِقَوْمٍ سُوءًا فَلَا مَرَدَّ لَهُ ۚ {11}

“Na Mwenyezi Mungu anapowatakia watu adhabu hakuna cha kuzuia” (13:11)

Tazama jinsi tunavyozikariri ishara, kisha wao wanapuuza.

Yaani tumesimamisha hoja juu yao zinazofuatiwa na hoja kwa mifumo mbali mbali, ili wawaidhike na wazingatie. Tukawaondolea nyudhuru zote ili waamini. Lakini dalili hizo mkato hazikuwadishia ila kuendelea na ukafiri, dhuluma na inadi.

Sema: Mwaonaje ikiwafikia adhabu ya Mwenyezi Mungu kwa ghaflaau kwa dhahiri nani wataangamizwa isipokuwa watu waliodhulumu?

Mara ya pili anawapa mawaidha na kuwatishia kuwaletea adhabu ambayo hawataweza kuikinga; ni sawa ingewajia ghafla kwa namna wasiyoijua au kwa wazi wazi kwa namna ya kuwa tayari nayo. Mara hii katika Aya hii anawaonya Mwenyezi Mungu na kuwapa onyo ili waiogope adhabu kabla ya kutukia kwake, na waelekee kwenye uongofu wao, lakini nyoyo zao zikasusuwaa na wala wasipondokee kwenye haki na uongofu.

Na hatutumi Mitume ila na waonyaji.

Hii ndiyo kazi ya Mtume, anawapa bishara watiifu na kuwaonya waasi. Kazi hii, pamoja na urahisi wa ufafanuzi wake na kueleweka kwake, lakini ndiyo kazi yenye mashaka makubwa na nzito. Kwa sababu inagusa maisha ya mataghuti moja kwa moja, na kuyaingilia masilahi yao na manufaa yao.
Mwishilio wa kazi ya Mtume ni kulipwa wema mwenye kuamini na kufanya matendo mema, na kuadhibiwa mwenye kukufuru na kuzikadhibisha ishara za Mwenyezi Mungu.

Na wenye kuamini na wakafanya wema, basi haitakuwa hofu juu yao wala hawatahuzunika.

Kwa sababu mwenye makosa ndiye anayehofia na kuhuzunika. Ama asiye na hatia huwa katika amani na utuvu.

Na wale waliokadhibisha ishara zetu itawagusa adhabu kwa sababu ya walivyokuwa mafasiki.

Ufasiki ni zaidi ya ukafiri. Kila kafiri ni fasiki, sio kila fasiki ni kafiri. Makusudio ya ufasiki hapa ni ukafiri, kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: Waliokadhibisha ishara zetu.

لْ لَا أَقُولُ لَكُمْ عِنْدِي خَزَائِنُ اللَّهِ وَلَا أَعْلَمُ الْغَيْبَ وَلَا أَقُولُ لَكُمْ إِنِّي مَلَكٌ ۖ إِنْ أَتَّبِعُ إِلَّا مَا يُوحَىٰ إِلَيَّ ۚ قُلْ هَلْ يَسْتَوِي الْأَعْمَىٰ وَالْبَصِيرُ ۚ أَفَلَا تَتَفَكَّرُونَ {50}

Sema: Siwaambii kuwa ninazo hazina za Mwenyezi Mungu, wala sijui ghaibu; wala siwambii mimi ni Malaika; sifuati ila ninayopewa Wahyi. Sema: Je, kipofu na mwenye kuona wako sawa? Je, hamfikiri?

وَأَنْذِرْ بِهِ الَّذِينَ يَخَافُونَ أَنْ يُحْشَرُوا إِلَىٰ رَبِّهِمْ ۙ لَيْسَ لَهُمْ مِنْ دُونِهِ وَلِيٌّ وَلَا شَفِيعٌ لَعَلَّهُمْ يَتَّقُونَ {51}

Na waonye kwayo wale wanaoogopa kwamba watakusanywa kwa Mola wao. Hawana mlinzi wala mwombezi isipokuwa yeye ili wapate kuwa na takua.

وَلَا تَطْرُدِ الَّذِينَ يَدْعُونَ رَبَّهُمْ بِالْغَدَاةِ وَالْعَشِيِّ يُرِيدُونَ وَجْهَهُ ۖ مَا عَلَيْكَ مِنْ حِسَابِهِمْ مِنْ شَيْءٍ وَمَا مِنْ حِسَابِكَ عَلَيْهِمْ مِنْ شَيْءٍ فَتَطْرُدَهُمْ فَتَكُونَ مِنَ الظَّالِمِينَ {52}

Wala usiwafukuze wale wanaomwomba Mola wao asubuhi na jioni kwa kutaka radhi yake; si juu yako hisabu yao hata kidogo, wala hisabu yako si juu yao hata kidogo, kwamba uwafukuze na uwe miongoni mwa madhalimu.

وَكَذَٰلِكَ فَتَنَّا بَعْضَهُمْ بِبَعْضٍ لِيَقُولُوا أَهَٰؤُلَاءِ مَنَّ اللَّهُ عَلَيْهِمْ مِنْ بَيْنِنَا ۗ أَلَيْسَ اللَّهُ بِأَعْلَمَ بِالشَّاكِرِينَ {53}

Na namna hii tumewajaribu wao kwa wao ili waseme: Je, hao ndio ambao Mwenyezi Mungu amewafadhili miongoni mwetu? Kwani Mwenyezi Mungu hawajui wanaoshukuru?

وَإِذَا جَاءَكَ الَّذِينَ يُؤْمِنُونَ بِآيَاتِنَا فَقُلْ سَلَامٌ عَلَيْكُمْ ۖ كَتَبَ رَبُّكُمْ عَلَىٰ نَفْسِهِ الرَّحْمَةَ ۖ أَنَّهُ مَنْ عَمِلَ مِنْكُمْ سُوءًا بِجَهَالَةٍ ثُمَّ تَابَ مِنْ بَعْدِهِ وَأَصْلَحَ فَأَنَّهُ غَفُورٌ رَحِيمٌ {54}

Na wanapokufikia wale wanaoamini ishara zetu waambie: Amani iwe juu yenu (Assalam alaykum), Mola wenu amejilazimisha rehema. Ya kwamba atakayefanya miongoni mwenu uovu kwa ujinga, kisha akatubu baada yake na akatengenea. Basi yeye ndiye mwingi wa maghufira mwenye kurehemu.

وَكَذَٰلِكَ نُفَصِّلُ الْآيَاتِ وَلِتَسْتَبِينَ سَبِيلُ الْمُجْرِمِينَ {55}

Namna hii tunazieleza ishara na ili njia ya wakosefu ibainike.