read

Aya 59-62: Hazina Ya Siri Iko Kwake

Maana

Na ziko kwake funguo za ghaibu; hakuna aijuaye ila Yeye; anajua kilicho nchi kavu na kilicho baharini; na halianguki jani ila analijua wala punje katika giza la ardhi; wala kibichi au kikavu, ila kimo katika Kitab kidhihirishacho.

Yaani Mwenyezi Mungu anajua ulimwengu, yaliyotokea na yatakayotokea yote, ya kimada au ya kimaana. Ujuzi wake haufungiki na wakati, mahali au kuwa katika hali fulani kinyume na hali nyingine. Kwa sababu ujuzi wake ni wa kidhati si wa kuchuma; na dhati yake si ya wakati na mahali; wala haibadiliki kwa kubadilika matukio na hali.

Katika Hadith imeelezwa: “Hakika hazina za siri ni tano:” Na Qura’n inasema:

إِنَّ اللَّهَ عِنْدَهُ عِلْمُ السَّاعَةِ وَيُنَزِّلُ الْغَيْثَ وَيَعْلَمُ مَا فِي الْأَرْحَامِ ۖ وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ مَاذَا تَكْسِبُ غَدًا ۖ وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ بِأَيِّ أَرْضٍ تَمُوتُ ۚ {34}

“Hakika ujuzi wa Saa (Kiyama) uko kwa Mwenyezi Mungu. Naye huteremsha mvua, na anayajua yaliyo katika matumbo ya uzazi; na nafsi yoyote haijui itachuma nini kesho na nafsi yoyote haijui itafia nchi gani. (31:34)

Mwanafalsafa, Mulla Sadra anasema: “Vitu vyote vizima (kamili) au mafungu vinatiririka kutokana naye, naye ni msingi wa kila kilichopo, kiakili au kihisia na kwa kuwaza au kwa kuona. Na mtiririko wake kutokana naye hauepukani kuwa wazi mbele yake.”

Allama Hilli anasema: “Kila kilichopo kisichokuwa Mwenyezi Mungu ni chenye kuwezekana, chenye kutegemezwa kwake. Atakuwa ni mwenye kukijua, ni sawa kiwe chote au baadhi; na ni sawa kiwe ni chenye kusimama hicho chenyewe au kwa kutegemea kingine, na ni sawa kiwe kiko machoni au mawazoni.
Kwa sababu kupatikana picha katika mawazo ni katika mambo yenye kuwa vilevile; kwa hiyo yanamtegemea Yeye. Na ni sawa picha hiyo ya mawazo iwe ni jambo lilioko au lisilokuwapo, linalowezekana au lisilowezekana. Ujuzi wake hauepukani na kitu chochote kiwezekanacho na kisichowezekana.”

Naye ndiye anayewafisha usiku.

Kufa na mauti ni maneno mawili yenye maana moja katika kawaida ya ufahamu, nako ni kukosa uhai. Matamko yote mawili hutumiwa katika usingizi kimajazi. Kwa vile viungo hupumzika kufanya kazi kwa sababu ya usingizi. Na katika maana hayo ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

اللَّهُ يَتَوَفَّى الْأَنْفُسَ حِينَ مَوْتِهَا وَالَّتِي لَمْ تَمُتْ فِي مَنَامِهَا ۖ فَيُمْسِكُ الَّتِي قَضَىٰ عَلَيْهَا الْمَوْتَ وَيُرْسِلُ الْأُخْرَىٰ إِلَىٰ أَجَلٍ مُسَمًّى ۚ{42}

“Mwenyezi Mungu huziua roho wakati wa mauti yake na zile ambazo hazijafikiwa na mauti katika usingizi. Basi huzizuia zile alizozipitishia mauti, na huzirudisha zile nyingine mpaka wakati uliowekwa…” (39:42)

Yaani Mwenyezi Mungu anakata mawasiliano ya roho na mwili, kwa dhahiri na kwa hali halisi, wakati wa kufa na kuzizuia kwake. Uhusiano huu anaukata kwa dhahir, sio kwa hali halisi, wakati wa kulala; na wakati wa kuamka uhusiano huu unarudia kama ulivyokuwa na kubaki hadi wakati uliowekewa kufa kikweli. Kwa hiyo mwenye kulala ni maiti hai.

Makusudio ya kufa katika Aya hii ni mauti ya kimajazi. Imam Ali (a.s) anasema: “Roho ya mtu hutoka wakati wa kulala na kubaki miale yake mwilini. Kwa miale anaota ndoto. Akizinduka roho hurudi mara moja.”

Na anayajua mlichokifanya mchana kisha huwafufua humo.

Humo ni mchana; na maana ya kuwafufua ni kuwaamsha usingizini. Wafasiri wamesema kuwa maneno haya ni dalili ya ufufuo na Kiyama. Kwa sababu usingizi unafanana na mauti, na kuamka kunafanana na kufufuka baada ya mauti.

Kisha kwake yeye ndiyo marejeo yenu; kisha awaambiye mliyokuwa mkiyafanya ya kheri na ya shari, katika usiku na mchana.

Kwa ufupi ni kwamba kila mtu anakufa kwa kwisha siku zake zilizoandikwa, kisha Mwenyezi Mungu atamfufua baada ya mauti, sawa na anavyomwamsha usingizini; kisha ailipe kila nafsi ilichokichuma na wao hawatadhulumiwa.

Ikiwa mtu atasema: Kwa nini Aya imehusisha kulala usiku na kufanya kazi mchana ambapo mtu mara nyingine hulala mchana na akafanya kazi usiku? Tutamwambia Aya imekuja katika hali iliyo aghlab.

Naye ndiye mwenye nguvu za kushinda juu ya waja wake.

Inatosha kuwa amewazidi nguvu kwa vile wanadamu wanakuja katika maisha haya kwa nguvu na wanayaacha kwa nguvu. Imam Ali (a.s.) anasema: “Hakuna chochote isipokuwa mmoja mwenye kushinda nguvu ambae kwake ni marejeo ya mambo yote yaliyoanza umbile lake bila ya kujiweza na yatakayokwisha bila ya kujizuia.”

Na huwapelekea waangalizi.

WatunzajihaoniMalaika.MwenyeziMunguMtukufuanasema:

وَإِنَّ عَلَيْكُمْ لَحَافِظِينَ {10}

كِرَامًا كَاتِبِينَ {11}

يَعْلَمُونَ مَا تَفْعَلُونَ {12}

“Na hakika mna waangalizi. Watukufu wenye kuandika. Wanajua mnayoyatenda.” (82:10-12)

Nasi tunaamini hayo, kwani Wahyi umeyaelezea na akili haiyakatai. Katika maneno ya Mwenyezi Mungu au ya Mtume haukuja ubainifu wa sifa za hao waandishi na maandishi; na akili hailazimishwi kufanya utafiti na kuuliza. Kwa hiyo tunayaacha katika ujuzi wake Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Ama kufananisha waandishi na polisi wa siri; kama ilivyo katika Tafsir Al- manar na Maraghi, ni kama kufananisha ghaibu na yanayoonekana na kufananisha mbingu na ardhi ambazo zina tofauti kubwa.

Hata mmoja wenu yakimjia na mauti, wajumbe wetu humfisha nao hawazembei.

Utapata Tafsir yake katika Sura (32:11) Inshallah. Hayo vilevile ni katika mambo ya ghaibu yanayowezekana kiakili na yaliyothibiti Ki-Wahyi; sawa na watunzaji wanaoandika.

Kisha watarudishwa kwa Mwenyezi Mungu, Mola wao wa haki ili wahukumiwe kwa hukumu Yake.

Hakika hukumu ni yake, naye ni mwepesi wa wanaohisabu.

Anahisabu, anahukumu na anatekeleza katika muda mchache sana. Kwa sababu haki iko wazi, hukumu itapitishwa na malipo yameandaliwa na kila kitu kitatimia kwa kutaka tu.

قُلْ مَنْ يُنَجِّيكُمْ مِنْ ظُلُمَاتِ الْبَرِّ وَالْبَحْرِ تَدْعُونَهُ تَضَرُّعًا وَخُفْيَةً لَئِنْ أَنْجَانَا مِنْ هَٰذِهِ لَنَكُونَنَّ مِنَ الشَّاكِرِينَ {63}

Sema: Ni nani anyewaokoa katika viza vya nchi kavu na baharini? Mnamwomba kwa unyenyekevu na kwa sauti ndogo: Kama akituokoa na haya, hakika tutakuwa miongoni mwa wanaoshukuru.

قُلِ اللَّهُ يُنَجِّيكُمْ مِنْهَا وَمِنْ كُلِّ كَرْبٍ ثُمَّ أَنْتُمْ تُشْرِكُونَ {64}

Sema: Mwenyezi Mungu huwaokoa katika hayo na katika kila mashaka. Kisha nyinyi mnamshirikisha.

قُلْ هُوَ الْقَادِرُ عَلَىٰ أَنْ يَبْعَثَ عَلَيْكُمْ عَذَابًا مِنْ فَوْقِكُمْ أَوْ مِنْ تَحْتِ أَرْجُلِكُمْ أَوْ يَلْبِسَكُمْ شِيَعًا وَيُذِيقَ بَعْضَكُمْ بَأْسَ بَعْضٍ ۗ انْظُرْ كَيْفَ نُصَرِّفُ الْآيَاتِ لَعَلَّهُمْ يَفْقَهُونَ {65}

Sema: Yeye ndiye awezaye kuwaletea adhabu kutoka juu yenu au kutoka chini ya miguu yenu; au awavuruge (muwe) makundi, na awaonjeshe baadhi yenu jeuri ya wenzao. Tazama jinsi tunavyozieleza ishara kwa njia mbali mbali ili wapate kufahamu.

وَكَذَّبَ بِهِ قَوْمُكَ وَهُوَ الْحَقُّ ۚ قُلْ لَسْتُ عَلَيْكُمْ بِوَكِيلٍ {66}

Na watu wako wameikadhibisha nayo ni haki. Sema: Mimi si kuwakilishwa juu yenu.

لِكُلِّ نَبَإٍ مُسْتَقَرٌّ ۚ وَسَوْفَ تَعْلَمُونَ {67}

Kila habari ina wakati maalum. Na punde mtajua.