read

Aya 95-99: Hutoa Aliye Hai Katika Maiti

Maana

Katika Aya hizi kuna mifano ya ajabu katika viumbe ambavyo anayemili- ki utengenezaji wake ni Mwenyezi Mungu peke yake. Vilevile kufahamisha kuwepo Mwenyezi Mungu na utukufu wake. Mifano imetajwa kwa mpango ufuatao:

Hakika Mwenyezi Mungu ndiye mpasuaji mbegu na kokwa.

Ukiweka mbegu ya ngano au kokwa ya tende katika ardhi itapasuka chini na juu. Upande wa chini itatoka mizizi na kushuka ardhini, na upande wa juu utatoka mti utakaorefuka hewani. Kisha ile mbegu au kokwa itapotea na mchanganyiko wote kuwa kitu kimoja, sehemu moja itakuwa ardhini na nyingine itakuwa kwenye hewa.

Hakuna mwenye shaka kwamba kazi yote hii inategemea sababu zake za kimaumbile; kama vile mchanga, maji, jua na hewa, lakini vyote hivyo vinaishia kwa Mwenyezi Mungu peke yake, kwa sababu yeye ndiye aliyeumba maumbile, msababishaji wa sababu na mpatishaji wa mada ya kwanza kwa neno ‘Kuwa’ na ikawa.

Uhai Umetoka Wapi?

Humtoa aliye hai katika maiti na ni mtoaji wa maiti katika aliye hai.

Si ajabu kuzalika kitu hai kutoka kwa kilicho hai mfano wake; na kisicho na uhai kutoa kisicho na uhai. Vilevile chenye uhai kuzaa kisicho na uhai, au kinyume chake.

Msemaji mmoja alisema: “Uhai unazalikana kutokana na nguvu ya asili ya maumbile.” Tumwulize msemaji huyu: Ni nani aliyeifanya ipatikane asili hiyo, nguvu zake na utendaji kazi wake? Ikiwa msukumano tu unatosha kuleta uhai bila ya kuweko msaada wa Mwenyezi Mungu, basi kwa nini wanasayansi wameshindwa kutengeneza uhai kama vile watengenezavyo vyombo vya jikoni na mengineyo; pamoja na kuwa wamejaribu wakaleta msukumano; lakni baada ya kukata tamaa walisema kwamba kutengeneza uhai ni kuzito kuliko kumrudisha mzee utotoni.

Hebu tuchukulie kuwa wao wanajiona watafaulu katika kutengeza chembehai , je , wamefaulu kutengeza mdudu mdogo tu?.

Tuache binadamu na ubongo wake na wanyama na maumbile yao ya ajabu na tupige mfano wa hawa wadudu tunaowaogopa na kupiga madawa kuwauwa. Baadhi ya wataalamu wa wadudu wanasema hivi: “Baadhi ya wadudu wanaishi katika nyuzi joto 50 chini ya sifuri; wengine wanaishi nyuzi joto hizi hizi juu ya sifuri, wengine katika hewa ya sumu na wengine katika visima vya mafuta, na wana utaratibu mzuri sana katika maisha yao na kazi zao.”

Ikiwa mwanaadamu anaweza kugundua satalaiti, maroketi na akili za Elktroni, lakini hawezi kabisa kutengeza bawa la mbu au chembe moja ya mbawa zake. Akili ya binadamu ni kubwa lakini ukubwa wake ni wenye kuhemewa mbele ya uweza wa ajabu ulioumba mbu na chungu na nyuki!

Yote hayo yako wazi, Lakini msiba mkubwa ni kuwa tumejisahau, hatujiangalii sisi wenyewe na uwazi wa uweza wa Mwenyezi Mungu mwenye hekima. Kama tukiangalia tutazidi imani kwa kiwango kikubwa kwa muumba aliye mkubwa. Tunachohitajia ni imani na imani yetu inahitajia akili kwa sababu imani bila ya akili ni kama uso bila macho.

Ndiyo, tunahitaji kuamini uweza wa Mwenyezi Mungu ili tufasiri yale yaliyoshinda akili za mabingwa, ambazo zimeshindwa kufasiri maumbile ya uhai. Na wengi wenye akili hizo wanakimbilia kwenye kitu kilicho nyuma ya maumbile. Uwezo wenye hekima na ujuzi, wanaufasiri kwa kusema kuwa ni asili ya uhai, huyo ndiye Mwenyezi Mungu basi mmegeuzwa wapi?

AnaemaEnstein:“Hakikauoniwetuwakidinindiounaloelekezauoni wetu wa kielimu”. Ustadh Tawfiq Al-Ahkim aliongeza katika kitabu chake Fannul-adab: ‘Huku bila shaka ni kukiri dini. Hakuna mtaalamu yeyote katika waliopiata aliyesema kuhusu dini kama alivyosema huyu.”

Nasi twaongeza juu ya kauli ya Al-Hakim, kwamba siri pekee ya kukubali wataalamu wa karne ya ishirini ni kuwa uoni wa dini ndio chimbuko la uoni wa kielimu, ni kuendelea kwa elimu katika karne hii na kuwa ilikuwa nyuma katika zama zilizopita. Kila inapopiga hatua elimu ndipo dini inapozidi kupata watetezi; kama Einstein anayekubali ukuu wa dini na kuamini kuwa ni haki ambayo haiingiliwi na batili mbele yake wala nyuma yake.

Ndiye mpambazuaji wa asubuhi; ameufanya usiku kuwa mapumziko na utulivu, na jua na mwezi (kwenda) kwa hesabu.

Mwenyezi Mngu (swt) ametaja katika Aya zlizotangulia mifano ya utukufu wake kwa kupatikana uhai kwenye ardhi; na katika Aya hii ametaja mifano mitatu ya mbinguni:

1. Kuwa ameitoa asubuhi kwenye usiku, hilo ni fumbo la kupatikana mchana ambao watu wanahangaikia riziki na kupanga mambo yao.

2. Kwamba yeye Mwenyezi Mungu ameuleta usiku kwa ajli ya kutulia na kupumzika kutokana na machovu za kazi ya mchana kutwa.

Tatu, kwamba ameweka Jua na Mwezi kwa kiasi mahsusi cha haraka na polepole kwa namna ambayo ardhi inakuwa na harakati mbili: Harakati za masaa 24, hisabu ya siku moja, na harakati za mwaka, ambazo ndani yake mna misimu mine ambayo ni hisabu ya mwaka mmoja.

Mwenyezi Mngu (swt) amesema:

هُوَ الَّذِي جَعَلَ الشَّمْسَ ضِيَاءً وَالْقَمَرَ نُورًا وَقَدَّرَهُ مَنَازِلَ لِتَعْلَمُوا عَدَدَ السِّنِينَ وَالْحِسَابَ ۚ {5}

Yeye ndiye aliyelijaalia Jua kuwa mwanga na mwezi kuwa nuru na akaupimia vituo ili mjue idadi ya miaka na hisabu’ (10:5)

Utauliza: kwa hiyo basi kupatikana usiku na mchana ni natija ya mzunguko wa ardhi , basi kuna wajihi gani wa kutegemeza kwa Mwenyezi Mungu?

Jibu: kwa sababu yeye ndiye Muumba mbingu na ardhi na kwake yeye ndio mwisho wa sababu zote , kwa hali yoyote ni kuwa makusudio ya kwanza ya kila yaliyokuja katika Aya hizi ni kuwa hakuna kitu katika vitu vya ulimwengu vilivyopatikana kwa sadfa na kibahati, isipokuwa kumetokana na aliye Mjuzi, Mwenye hekima aliyekipa kila kitu umbile lake na kukikadiria.

Hayo ndiyo makadirio ya weye nguvu, Mjuzi.

Na Yeye ndiye aliyewafanyia nyota ili muongoke kwazo katika viza vya bara na baharini. Hakika tumezifafanua ishara kwa watu wanaojua.

Nyota hapa ni kutoa Jua na Mwezi kama inavyofahamika kutokana na mpangilio wa maneno. Katika kitabu Qur-an walilmul-hadith anasema bingwa wa falaki James Jentis: “Tunapotaka kujua nyumba fulani katika mji iko wapi tunauliza jina la mtaa kisha namba yake, basi ni hivyohivyo katika nyota, kwani katika hizo kuna zilizo maarufu kwa majina yake mahsusi nazo ni alama muhimu wanazozifuata mabaharia katika majahazi yao na waendeshao vyombo na wapanda wanyama. Ni misafara mingapi inyokwenda kwa ramani ya mbinguni na nyota wakati dira inapoacha kufanya kazi?”

Na Yeye ndiye aliyewaanzisha nyinyi kutokana na nafsi moja. Pako mahali pa kutulia na pa kupita njia. Hakika tumezifafanua ishara kwa watu wanaofahamu.

Nafsi iliyoumbwa kila moja kutokana nayo ni mtu wa kwanza ambaye watu wote wametokana naye ambaye ni Adam.

Tumezungumzia kwa ufafanuzi tulipofasiri Juz.4 (4:1)

Razi ametaja kauli sita katika kufasiri mahali pa kutulia na pa kupita njia.

Wafasiri wengi wamesema ‘kutulia’ ni kutulia manii katika migongo ya wanaume na ‘pa kupita njia’ kuwa katika matumbo ya uzazi ya wanawake. Katika Aya hakuna linalofahamisha hilo, wala lolote katika maana sita alizozinukuu Razi.

Imepokewa kutoka kwa Imam Sadiq (as) kwamba yeye amegawanya waumini katika mafungu mawili; mwenye kuamini imani ya kweli inayotulia mpaka kufa, ambaye maneno yake yanaafikiana na vitendo vyake, na mumini ambaye imani yake inalegalega iko kwa muda tu, inamwondoka kabla ya kufa; maneno yake yanatofautiana na vitendo vyake.

Hakika tumezifafanua ishara kwa watu wanaofahamu.

Na asiyefahamu dalili hizi za ulimwengu juu ya ukuu wa muumbaji, mwanzilishi, basi huyo ni katika wale waliokusudiwa na kauli yake Mwenyezi Mungu:

صُمٌّ بُكْمٌ عُمْيٌ فَهُمْ لَا يَعْقِلُونَ {171}

“Ni viziwi ni mabubu ni vipofu kwa hivyo hawafahamu.” (2:171)

Naye ndiye aliyeteremsha maji kutoka mbinguni na kwayo tunatoa mimea ya kila kitu.

Mvua ndio chimbuko la maji tamu, lau si hiyo ardhi ingelikuwa kame isiyo na uhai. Mwenyezi Mungu ametegemeza kushuka maji kwake yeye, kwa sababu yeye ndiye msababishaji wa sababu, kwake huanza kila kitu hata kama mzunguko utakuwa mrefu kiasi gani.

Kisha tukatoa kutokana nayo kijani.

Dhamiri ya ‘nayo’ inarudia kwenye mimea. Makusudio ya kijani ni ubichi, yaani kutokana na mmea huchipua matawi mabichi. Inasemekana kuwa maana ya kijani hapa ni ubichi zaidi.

Tukatoa ndani yake punje zilizopandana.

Dhamiri ya ‘ndani yake’ ni ndani ya hiyo kijani, yaani tunatoa mashuke katika matawi kama vile ya ngano nk, na kama mfano wa, tunda la koma-manga ambalo tembe zake zinapandana.

Na katika mitende yakatoka kwenye makole yake mashada yaliyo karibu.

Yaani ni rahisi kuyachuma au kuwa kukurubiana kwa wingi wake.

Na bustani za miabibu na mizaituni na mikomamanga.

Yaani tunatoa katika mimea aina hizi tatu. Mwenyezi Mungu amezitaja kwa njia ya kupigia mfano ambayo kutokana nazo itajulikana mingine.

Yanayofanana na yasiyofanana.

Katika mimea kuna inayofanana katika umbile na ladha na mingine haifananai.

Angalieni matunda yake yanapozaa na kuiva kwake.

Yaani zingatieni vipi linatoka tunda mwanzo, linakuwa dogo lisilo na manufaa kisha linabadilika badilika mpaka kuiva na kuwa na ladha tamu.

Hakika katika hayo kuna ishara kwa watu wanaoamini.

Makusudio ya wanaoamini siyo wale wanaoamini tu, bali ni wale wanaotikia mwito wa imani na kunufaika na dalili na hoja. Ama wenye nyoyo zilizofungwa wanazipita kama wanyama.

Kwa ufupi makusudio ya kwanza ya mifano hii ya ardhini na mbinguni ni kuleta uzindushi kuwa vitu vya ulimwengu huu na vilivyomo ndani yake vinatokana na uanzilishi na upangiliaji.

Ni muhali kuwa vimekuja kisadfa katika mtazamo wa kiakili na kimaumbile.
Hizo mbili zinahukumu kwa mkato kwamba kila liliopo limepatikana kwa matakwa na makusudio na kwa hekima ya hali ya juu anayoijua mjuzi na mjinga, wala hakuna kitu kinachobatilisha sadfa kama vile kukaririka tukio moja kila zinapokaririka sababu zake.

وَجَعَلُوا لِلَّهِ شُرَكَاءَ الْجِنَّ وَخَلَقَهُمْ ۖ وَخَرَقُوا لَهُ بَنِينَ وَبَنَاتٍ بِغَيْرِ عِلْمٍ ۚ سُبْحَانَهُ وَتَعَالَىٰ عَمَّا يَصِفُونَ {100}

Na wamemfanyia Mwenyezi Mungu washirika majini. Hali yeye amewaumba. Na wamemsingizia kuwa na wana wa kike na wa kiume bila ujuzi. Ametakasika na ametukuka juu ya hayo wanayombandikiza nayo.

بَدِيعُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ أَنَّىٰ يَكُونُ لَهُ وَلَدٌ وَلَمْ تَكُنْ لَهُ صَاحِبَةٌ ۖ وَخَلَقَ كُلَّ شَيْءٍ ۖ وَهُوَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ {101}

Mbunifu wa mbingu na ardhi. Inawezekanaje awe na mwana hali hana mke. Na ameumba kila kitu. Naye ni Mjuzi wa kila kitu.

ذَٰلِكُمُ اللَّهُ رَبُّكُمْ ۖ لَا إِلَٰهَ إِلَّا هُوَ ۖ خَالِقُ كُلِّ شَيْءٍ فَاعْبُدُوهُ ۚ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ وَكِيلٌ {102}

Huyo ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu hakuna Mola (mwingine) isipokuwa Yeye; Muumba wa kila kitu. Kwa hivyo mwabuduni yeye. Na yeye ni mtegemewa wa kila kitu.

لَا تُدْرِكُهُ الْأَبْصَارُ وَهُوَ يُدْرِكُ الْأَبْصَارَ ۖ وَهُوَ اللَّطِيفُ الْخَبِيرُ {103}

Hayamfikii macho. Bali yeye huyafikia macho. Naye ni Mpole Mwenye habari

قَدْ جَاءَكُمْ بَصَائِرُ مِنْ رَبِّكُمْ ۖ فَمَنْ أَبْصَرَ فَلِنَفْسِهِ ۖ وَمَنْ عَمِيَ فَعَلَيْهَا ۚ وَمَا أَنَا عَلَيْكُمْ بِحَفِيظٍ {104}

Hakika zimewajia busara kutoka kwa Mola wenu. Basi atakayefungua macho ni faida yake mwenyewe; na atakayeyapofua ni hasara yake mwenyewe. Nami si mtunzaji wenu.

وَكَذَٰلِكَ نُصَرِّفُ الْآيَاتِ وَلِيَقُولُوا دَرَسْتَ وَلِنُبَيِّنَهُ لِقَوْمٍ يَعْلَمُونَ {105}

Na namna hii tunazifafanua ishara na waseme umesoma. Na ili tuyabainishe kwa watu wanaojua.

عْ مَا أُوحِيَ إِلَيْكَ مِنْ رَبِّكَ ۖ لَا إِلَٰهَ إِلَّا هُوَ ۖ وَأَعْرِضْ عَنِ الْمُشْرِكِينَ {106}

Fuata uliyopewa wahyi kutoka kwa Mola wako. Hakuna Mola (mwingine) isipokuwa Yeye; na jitenge na washirikina.

وَلَوْ شَاءَ اللَّهُ مَا أَشْرَكُوا ۗ وَمَا جَعَلْنَاكَ عَلَيْهِمْ حَفِيظًا ۖ وَمَا أَنْتَ عَلَيْهِمْ بِوَكِيلٍ {107}

Na kama Mwenyezi Mungu angetaka wasingeshirikisha. Na hatukukufanya uwe mtunzaji wao wala wewe si mlinzi juu yao.