read

Aya 92: Mali Ndio Sababu Ya Ugomvi

Hamtapata wema mpaka mtoe katika vile mnavyovipenda, na chochote mna- chokitoa, basi Mwenyezi Mungu anakijua.
Makusudio ya wema hapa, ni utukuzo wa Mwenyezi Mungu na fadhila kwa mja wake. Zimetangulia tafsir za Aya kadha kuhusu kutoa. Lakini Aya hii imetofautiana kabisa na Aya zingine zinazoelezea maudhui haya.

Kwa sababu, haitosheki na kuamrisha kutoa tu, kama Aya nyinginezo, bali imeunganisha baina ya kupata mtu daraja ya juu mbele za Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwa kujitolea anavyovipenda. Kwa hiyo ibada isiyokuwa ya kujitolea, haikurubishi kwa Mwenyezi Mungu - kwa mujibu wa Aya hii - isipokuwa ikiambatana na kujitolea katika njia ya Mwenyezi Mungu.

Kwa hivyo basi, kauli yake Mwenyezi Mungu; "Hamtaufikia wema mpaka mtoe katika vile mnavyovipenda," ni tafsiri na ubainufu wa kila Aya na Riwaya inayohimiza kufanya amali kwa ajili ya kupata radhi ya Mwenyezi Mungu na kujikurubisha kwake hali ya kuwa ni ufafanuzi kwamba, kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu hakupatikani wala hakutapatikana ila kwa kujitolea mtu nafsi yake na mali yake anayoipenda. Ni kama kwamba Imam Ali (a.s.) alichukua kutokana na Aya hii, kauli yake: "Hapana haja ya Mungu kwa ambaye katika nafsi yake na mali yake hakuna fungu la Mungu."

Kutoa ni kugumu na hasa mali ambayo ndiyo mgomvi anayeipambanua imani ya asili. Mali ilikuwa na inaendelea kuwa ni yenye kuabudiwa na mamilioni ya watu. Watu wengi wanawazishwa na shetani kwamba wao wanamwabudu Mwenyezi Mungu (s.w.t.), kumbe kwa hakika wanaabudu pesa, lakini wenyewe hawatambui.

Kuna kisa kimoja kwamba Iblis, kabla ya kuanzishwa mfumo wa pesa, alikuwa na shughuli kubwa sana ya kuwapoteza watu na kuwaepusha na ibada ya Mwenyezi Mungu wawe waabudu sanamu. Kwa hiyo ikawa hana raha usiku na mchana. Baada ya kupita masiku, ukaja mfumo wa pesa ndipo Ibilisi akapumua, akafurahi sana, akaandaa hafla ya taarabu, akawa anacheza huku ameweka Dirham kwenye jicho moja na Dinar kwenye jichojengine. Akasema: (kuziambia pesa hizo) “mmenipumzisha sasa, sitojali kama watu wanawaabudu nyinyi au wataabudu masanamu.”

Kisa hiki kiwe ni cha kweli au uongo au hata kama ni katika vigano, lakini ni picha ya kweli. Kwa sababu hakuna tofauti kati ya kuabudu mali na kuabudu masanamu, kila moja inamwepusha mtu na Mungu na haki.

Bali kuabudu mali kuna athari mbaya zaidi, na kuna madhara zaidi. Kwa sababu, mara nyingi sana mali ndio kiini cha matamanio na ni chimbuko la ufisadi. Wale waliozihaini nchi zao wamefanya hivyo kwa sababu ya pesa. Na wale waliowapiga vita Mitume na watu wema na kuibadilisha dini na sharia ya Bwana wa Mitume, walifanya hivyo baada ya kupata chochote.

Kadiri nitakavyotia shaka, lakini siwezi kutia shaka kuwa walahidi na waabudu masanamu ambao hawakuzifanyia hiyana nchi zao wala kuwafanyia njama watu wema, kuwa ni bora mara elfu, kuliko mwenye kufunga, kuswali, kuhiji na kutoa zaka lakini anapanga njama pamoja na maadui kuuza nchi na riziki za waja.

Kwa hiyo hapana ajabu kwa mtu kupata daraja mbele ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwa kujitolea kwa mali, ambapo kutokana na kutoa huku kunaonyesha haki kuwa juu ya batili na akhera juu ya ulimwengu.

Unaweza kuuliza kuwa, mbona kauli yake Mwenyezi Mungu "Hamtapata wema mpaka mtoe katika vile mnavyovipenda." Kwa dhahiri inafahamisha kuwa pepo haipati ila yule aliye nazo atakayejitolea vizuri katika mali, ambapo watu wengi hawamiliki chochote.

Jibu: Msemo katika Aya tukufu unamhusu mwenye nacho. Ama asiyekuwa nacho, yeye ndio anapasa achukue sio kutoa, bali yeye ni sehemu mojawapo ya kutolea hiyo mali.

Zaidi ya hayo ni kwamba, ambao wanapigana jihadi kwa nafsi zao, wana cheo zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu kuliko wale ambao wanapigana jihadi kwa mali zao. Kwa sababu, kuitoa nafsi ni ukomo wa kutoa.
Kama ambavyo Aya imefahamisha, kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu kumedhaminiwa na kutoa na kujitolea. Basi vile vile imefahamisha kwamba, mali ni chim- buko la kheri na ni njia ya kumtii Mwenyezi Mungu; kama ambavyo pia ni kiini cha matamanio na ni ya kumridhisha shetani. Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w) anasema: "Mwenye kuitafuta dunia kwa ajili ya kujilimbikizia na kujifaharisha atakutana na Mwenyezi Mungu akiwa amekasirika. Na mwenye kuitafuta kwa kujistahi na kuichunga nafsi yake, atakuja siku ya Kiyama uso wake ukiwa kama mbalamwezi."

Imam Ali (a.s.) anasema: "Hakupewa yeyote kitu katika dunia ila hupungua fungu lake katika akhera." Mmoja wa waliokuwepo akasema: 'Sasa sisi tunaitafuta dunia (Itakuaje?)' Imam akasaili: "Mnaifanyia nini?" Akajibu: 'Kujikimu mimi, wanangu na kutoa sadaka na kuhiji.' Imam akasema: "huku si kutafuta dunia, bali ni kutafuta Akhera."

كُلُّ الطَّعَامِ كَانَ حِلًّا لِبَنِي إِسْرَائِيلَ إِلَّا مَا حَرَّمَ إِسْرَائِيلُ عَلَىٰ نَفْسِهِ مِنْ قَبْلِ أَنْ تُنَزَّلَ التَّوْرَاةُ ۗ قُلْ فَأْتُوا بِالتَّوْرَاةِ فَاتْلُوهَا إِنْ كُنْتُمْ صَادِقِينَ {93}

Kila chakula kilikuwa halali kwa wana wa Israil ila alichojiharamishia Israil mwenyewe kabla ya kuteremshwa Tawrat. Sema: Leteni Tawrat muisome mkiwa ni wakweli.

فَمَنِ افْتَرَىٰ عَلَى اللَّهِ الْكَذِبَ مِنْ بَعْدِ ذَٰلِكَ فَأُولَٰئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ {94}

Basi wenye kumzulia uongo Mwenyezi Mungu baada ya hayo, basi hao ndio madhalimu.

قُلْ صَدَقَ اللَّهُ ۗ فَاتَّبِعُوا مِلَّةَ إِبْرَاهِيمَ حَنِيفًا وَمَا كَانَ مِنَ الْمُشْرِكِينَ {95}

Sema: Amesema kweli Mwenyezi Mungu. Basi fuateni mila ya Ibrahim aliyeshikamana na haki; wala hakuwa katika washirikina