read

Aya 98-99: Kukanusha Dalili Na Ishara Za Mwenyezi Mungu

Maana

Qur'an imejishughulisha sana na watu wa Kitabu, ikawateremeshia Aya kadha wa kadha zinazowakumbusha Tawrat na Injil na kuwaaibisha, kwa sababu ya kuzigeuza; ikawajadili kwa namna nzuri na kuwaelezea makosa yao mengi na dhambi zao.

Miongoni mwa Aya hizo, ni Aya hizi mbili:
1. "Sema: Enyi watu wa Kitabu! Kwa nini mnazikanusha ishara za Mwenyezi Mungu ambazo zimefahamisha Utume wa Muhammad (s.a.w); na kwamba Al-Kaaba ndiyo nyumba ya kwanza kuwekewa watu kwa ibada, pamoja na kuwa ishara hizo na hoja hizo ziko wazi kama jua, na hawezi kuzikanusha isipokuwa mwenye kiburi."

2. "Sema: Enyi watu wa Kitabu! Kwa nini mnawazuilia njia ya Mwenyezi Mungu walioamini? Mkaitafutia kosa…" Hawakutosheka na kufanya ufisadi hao wenyewe, mpaka wakajishughulisha kuwaharibu wengine na kuwapoteza. Kwa hiyo wamechanganya upotevu na kupoteza, na ufisadi na kuwafanya wengine wawe wafisadi. Kila mfisadi anatamani na kufanya kadiri ya uwezo wake ili kuwe na mafisadi wengi kwa kutumia misingi ya Iblis aliposema: "Kwa kunihukumu kupotea, basi nitawapambia katika ardhi na nitawapoteza wote." (15:39)

Tusisahau ishara ya aina hii ya upole wa kuwaambia watu wa Kitabu, na kuwakumbusha vizuri kuwa wao ni watu wa dini na Kitabu, ili angalau waweze kusikia mawaidha na kuongoka.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنْ تُطِيعُوا فَرِيقًا مِنَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ يَرُدُّوكُمْ بَعْدَ إِيمَانِكُمْ كَافِرِينَ {100}

Enyi mlioamini! Mtakapotii kikundi katika watu wa Kitabu watawarudisha kuwa makafiri baada ya kuamini kwenu.

وَكَيْفَ تَكْفُرُونَ وَأَنْتُمْ تُتْلَىٰ عَلَيْكُمْ آيَاتُ اللَّهِ وَفِيكُمْ رَسُولُهُ ۗ وَمَنْ يَعْتَصِمْ بِاللَّهِ فَقَدْ هُدِيَ إِلَىٰ صِرَاطٍ مُسْتَقِيمٍ {101}

Na vipi mnakufuru na nyinyi mnasomewa Aya za Mwenyezi Mungu na Mtume wake mnaye? Na mwenye kushikamana na Mwenyezi Mungu basi ameongozwa katika njia iliyonyooka.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّهَ حَقَّ تُقَاتِهِ وَلَا تَمُوتُنَّ إِلَّا وَأَنْتُمْ مُسْلِمُونَ {102}

Enyi mlioamini mcheni Mwenyezi Mungu ipasavyo kumcha; wala msife isipokuwa mmekuwa waislamu.

وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا ۚ وَاذْكُرُوا نِعْمَتَ اللَّهِ عَلَيْكُمْ إِذْ كُنْتُمْ أَعْدَاءً فَأَلَّفَ بَيْنَ قُلُوبِكُمْ فَأَصْبَحْتُمْ بِنِعْمَتِهِ إِخْوَانًا وَكُنْتُمْ عَلَىٰ شَفَا حُفْرَةٍ مِنَ النَّارِ فَأَنْقَذَكُمْ مِنْهَا ۗ كَذَٰلِكَ يُبَيِّنُ اللَّهُ لَكُمْ آيَاتِهِ لَعَلَّكُمْ تَهْتَدُونَ {103}

Na Shikamaneni na kamba ya Mwenyezi Mungu nyote wala msifarikiane; na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu juu yenu mlipokuwa maadui naye akaziunganisha nyoyo zenu; hivyo kwa neema yake mkawa ndugu; na mlikuwa ukingoni mwa shina la moto naye akawaokoa nalo. Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyozibainisha Aya Zake ili mpate kuongoka.