read

Aya 134 – 136: Sifa Za Wamchao Mwenyezi Mungu

Maana

Mwenyezi Mungu amewasifu wanaomcha Yeye kwa sifa ambazo ni njema na ni bora hata kwa asiyemwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho, sifa hizo ni kama hizi zifuatavyo:

I. Ambao Hutoa Katika Raha Na Shida

Utajiri hauwafanyi kuwa na pupa na tamaa ya mali na kufanya ubahili. Wala ufakiri hauwakatishi tamaa wakajiona kuwa wao wanastahiki kuchukua zaidi kuliko kutoa. Bali katika hali zote mbili kwao ni sawa wanatoa kiasi wanavyoweza. Hadith inasema: "Toeni sadaka japokuwa ni upande wa tende."

II. Na Wazuiao Ghadhabu

Hakuna kitu kifahamishacho zaidi nguvu ya imani na akili kubwa kuliko mtu kuimiliki nafsi yake na kuzuia ghadhabu. Ikiwa kumeza ghadhabu kuna uchungu na mashaka ya nafsi, lakini ni kinga ya masaibu mengi na matatizo. Imam Ali (a.s.) katika kumuusia mwanawe, Imam Hasan (a.s.), anasema: "Meza ghadhabu, kwani mimi sikuona kinywa chenye utamu wa matokeo na ladha ya athari kuliko hicho."

III. Na Wenye Kusamehe Watu

Kumsamehe aliyekufanyia uovu kunashinda sana kuzuia ghadhabu. Kwa sababu mtu mara nyingi anaidhiki nafsi yake na kuzuia ghadhabu yake kwa msukumo fulani wa masilahi yake kama kujiepusha kujiingiza katika matatizo, ama kusamehe makosa ya watu huko ndiko kufanya hisani kuliko safi kabisa. Imam Ali (a.s.) anasema: "Ikiwa unamuweza adui yako, ujaalie msamaha wako ndio shukurani ya kuwa na uwezo huo."

IV. Na Mwenyezi Mungu Huwapenda Wafanyao Hisani

Hisani inapatikana katika kila lenye manufaa ya kimaada au kimaana, iwe nyingi au chache, hata kama ni kusema: "Njia ni hii."

Sheikh Al-Maraghi, katika kufasiri Aya hii, anasema: "Ametaja Baihaqi kwamba, mjakazi wa Ali bin Husein (a.s.) alikuwa akimtilia maji ili atawadhe kwa ajili ya Swala. Birika ikamtoka mkononi na ikavunjika. Ali akainua kichwa chake; yule mjakazi akasoma Aya: "Na wazuiao ghadhabu."

Akasema: "Nimezuia ghadhabu yangu."Akasoma tena mjakazi: "Na wenye kusamehe watu." Akasema: "Mungu akusamehe."

Mjakazi akaongeza: "Na Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao hisani." Akasema: "Nimekuacha huru kwa ajili ya Mwenyezi Mungu."

V. Na Ambao Wakifanya Jambo Ovu Au Wakidhulumu Nafsi Zao Humkubuka Mwenyezi Mungu Na Kuomba Msamaha Wa Dhambi Zao

Uovu ni kama kuingilia haki za wengine, nako ni kuovu zaidi na kukubwa. Kujidhulumu nafsi yake mtu, sio kuingilia haki za wengine, lakini kunaweza kuwa ni kuovu; kama vile ukafiri. Kwa hiyo kukutaja baada ya kutaja uovu ni katika hali ya kutaja ujumla baada ya kutaja mahsusi.

Kwa vyovyote iwavyo, ni kwamba Mwenyezi Mungu husamehe madhambi yote na hughufiria kila dhambi; iwe kubwa au ndogo. Kwa sharti yakutaka msamaha; yaani toba ya kweli. Yaani hakika Mwenyezi Mungu (s.w.t.) humsamehe mwenye kutubu na akajing'oa kutoka kwenye dhambi. Ama mwenye kung'angania kufanya dhambi naye akiwa anajua kuwa ni dhambi, hawezi kughufiriwa na Mwenyezi Mungu.
Maana yake ni kwamba mwenye kufanya uovu kwa kutojua ubaya wake, basi ni mwenye kusamehewa.

Hao malipo yao ni Msamaha.

Mfano wa Aya hii umeshapita katika Sura ya Baqara Aya 25 na 266.

قَدْ خَلَتْ مِنْ قَبْلِكُمْ سُنَنٌ فَسِيرُوا فِي الْأَرْضِ فَانْظُرُوا كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الْمُكَذِّبِينَ {137}

Hakika zimepita desturi nyingi kabla yenu, basi tembeeni katika nchi na muone ulikuwaje mwisho wa wale waliokadhibisha.

هَٰذَا بَيَانٌ لِلنَّاسِ وَهُدًى وَمَوْعِظَةٌ لِلْمُتَّقِينَ {138}

Huu ni ubainifu kwa watu na mwongozo na mawaidha kwa wamchao.