read

Aya 183-184: Kafara Na Moto

Maana

Wale ambao wamesema: Hakika Mwenyezi Mungu ametuahidi kuwa tusimwamini Mtume yeyote, mpaka atuletee kafara itakayoliwa na moto.

Kila mwongo anadai kuwa ni mkweli, na anaupamba uongo wake kwa uzushi na tuhuma, hata wale wanaotajirika kwa vita na kuvichochea ili viwanda vyao vifanye kazi, wanadai kuwa wanawaua watu wasio na makosa, watoto na wanawake ili kuleta amani. Haya ndiyo mantiki ya kila mpinga haki na uadilifu kwa kuhofia chumo lake na manufaa yake.

Kwa hiyo hakuna geni kwa Mayahudi kumzulia Mwenyezi Mungu na kumwambia Muhammad (s.a.w.) kuwa hatukuamini, kwa sababu Mwenyezi Mungu ametuamrisha kutomsadiki anayedai Utume mpaka atuonyeshe muujiza wa kutoa kafara yetu na iteketezwe na moto utokao mbinguni. Na Mayahudi waliomwambia Muhammad kauli hii, ndio hao hao waliosema kufuru ya kuwa Mwenyezi Mungu ni fukara na wao ni matajiri.

Sema: Hakika waliwajia Mitume kabla yangu kwa hoja waziwazi na kwa hayo mliyosema basi mbona mliwaua kama mu wa kweli?

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anamwamrisha Mtume wake Mtukufu kuwakatalia maneno yao na kuwajibu kwa matukio ya kihistoria kwa kuwaambia, wakale wenu waliwataka Mitume waliotangulia muujiza huu muutakao nyinyi, wa kushuka moto kutoka mbinguni, akaudhihirisha Mwenyezi Mungu, lakini pamoja na hayo hawakuwaamini, bali waliwaua. Na nyinyi mko radhi na vitendo vya wa kale wenu. Walivyokuwa wao ndiyo mlivyo nyinyi kwa inadi. Lau mngelikuwa mwatafuta ukweli, mngelimwamini Muhammad (s.a.w.) baada ya kuwaletea hoja ya Utume wake.

Kama wakikukadhibisha, basi hakika wamekadhibishwa Mitume kabla yako waliokuja na hoja zilizo wazi wazi na vitabu vya waadhi na kitabu chenye mwanga.

Msemo unaelekezwa kwa Mtume Mtukufu (s.a.w.), lengo lake ni kumpa moyo kwa masaibu yaliyowapata wenzake waliotangulia. Sera yao ilikuwa ni kukabiliana na kupingwa na wenye inadi katika watu waovu, kama wana wa Israil na wanao- fanana nao, hata ingawaje walionyesha hoja kwa kila mkadhibishaji na mpinga haki.

Makusudio ya hoja zilizo waziwazi ni miujiza iliyo wazi inayofahamisha ukweli wa waadhi; mawaidha ya Mtume na hekima zao, na kitabu chenye mwanga ni Tawrat, kwa yanayomuhusu Muhammad na sifa zake.
Na kwa kuwa Aya zilikuwa zikibainisha mambo yao. Basi hao ndio waliosema: Mwenyezi mungu ni fukara na kwamba Mwenyezi Mungu amewaahidi wasimwamini Mtume mpaka awajie na kafara

كُلُّ نَفْسٍ ذَائِقَةُ الْمَوْتِ ۗ وَإِنَّمَا تُوَفَّوْنَ أُجُورَكُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۖ فَمَنْ زُحْزِحَ عَنِ النَّارِ وَأُدْخِلَ الْجَنَّةَ فَقَدْ فَازَ ۗ وَمَا الْحَيَاةُ الدُّنْيَا إِلَّا مَتَاعُ الْغُرُورِ {185}

Kila nafsi itaonja mauti. Na bila shaka mtatekelezewa malipo yenu siku ya Kiyama. Mwenye kuepushwa na moto akatiwa peponi, basi huyo amefuzu. Na hayakuwa maisha ya dunia ila ni starehe idanganyayo.

لَتُبْلَوُنَّ فِي أَمْوَالِكُمْ وَأَنْفُسِكُمْ وَلَتَسْمَعُنَّ مِنَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ مِنْ قَبْلِكُمْ وَمِنَ الَّذِينَ أَشْرَكُوا أَذًى كَثِيرًا ۚ وَإِنْ تَصْبِرُوا وَتَتَّقُوا فَإِنَّ ذَٰلِكَ مِنْ عَزْمِ الْأُمُورِ {186}

Kwa hakika mtapata misuko suko katika mali zenu na nafsi zenu na mtasikia udhia mwingi kutoka kwa wale waliopewa Kitabu kabla yenu na kwa washirikina. Na mkisubiri na mkamcha mungu basi hayo ni miongoni maazimio.