read

Aya 93-95: Wana Wa Israil Na Chakula

Maana

Kila chakula kilikuwa halali kwa wana wa Israel.

Aya hii kwa ufupi inasimulia kwamba, Aya nyingi zinaonyesha wazi kuwa Muhammad (s.a.w) na walio pamoja naye wako kwenye mila ya Ibrahim; wanamwamini Mwenyezi Mungu na aliyoteremshiwa Ibrahim, Ismail, Is-haq,Yakub na kizazi chake. Vile vile Musa, Isa na Mitume wengineo.

Maana yake kwa dhahiri ni kwamba, kila lililokuwa haramu katika dini ya Mitume hiyo basi ni haramu katika dini ya Kiislamu. Mayahudi walikuwa wakiitakidi kuwa nyama ya ngamia na maziwa yake ni haramu katika dini ya Mitume iliyotajwa. Wakamwona Muhammad anaihalalisha na kwamba, uhalalishaji huo unapingana na kauli yake kuwa yeye yuko kwenye mila ya Ibrahim, na kwamba yeye anaamini alichoteremshiwa Ibrahim na Mitume walio baada yake.

Kwa kutegemea madai haya, wakatangaza na kueneza habari kwa makusudio ya kutia ila na kuleta shaka katika Uislamu kwamba Muhammad anajipinga mwenyewe. Anahalalisha chakula kilichokuwa haramu katika mila ya Ibrahim, na wakati huo huo anadai kwamba yuko katika mila ya Ibrahim.

Ndipo Mwenyezi Mungu akawajibu kwa kusema: "Kila chakula kilikuwa halali kwa wana wa Israel." Yaani Ibrahim na waliomfuata, hawakuharamisha nyama ya ngamia na maziwa yake, bali kila chakula kilikuwa halali kwao. Na mayahudi ni wakadhibishaji na ni wazushi katika kuwanasibishia Mitume kuwa ndio wenye kuharamisha.

Ila alichojiharamishia Israil mwenyewe.

Israel ni Yakub bin Is-haq bin Ibrahim. Alikuwa hatumii baadhi ya vyakula kwa sababu zake zinazomhusu yeye tu, si kwa sababu ya kuharamishiwa na Mwenyezi Mungu.

Ni kama mtu akiamua kutovuta sigara kwa sababu za kiafya n.k. Lakini alipojizuia ikawa ni desturi ya Wana wa Israil kumfuata baba yao katika yale aliyojizuilia mwenyewe na hilo lilikuwa kabla ya kuteremshwa Tawrat.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametaja hivyo, kwa sababu aliwaharamishia vitu vingi baada ya Tawrat kutoka na dhambi walizozifanya; kama asemavyo Mwenyezi Mungu: "Basi kwa dhuluma ya Mayahudi tuliwaharamishia vitu vizuri walivyohalalishiwa, na kwa sababu ya kuzuilia kwao njia ya Mwenyezi Mungu kwa wingi" (4:160).

Ama aina ya vitu walivyoharamishiwa baada ya kuteremshwa Tawrat vimetajwa na Aya hii: "Na kwa wale walio mayahudi tuliharamisha kila(mnyama) mwenye kucha, na katika ng’ombe na kondoo tukawaharamishia mafuta yao isipokuwa yale iliyobeba migongo yao au matumbo au ile iliyogandamana na mifupa. Tuliwalipa hivyo kwa uasi wao. "Na hakika sisi ndio wa kweli."(6:146) Ufafanuzi zaidi utakuja mahali pake.

Kwa ujumla ni kuwa Waislamu wameafikiana kwa kauli moja kwamba asili ya kila kitu ni halali mpaka ithibiti kinyume chake.

Sema: Leteni Tawrat muisome mkiwa ni wenyewe kusema kweli.

Hii ni kujadiliana na mayahudi kwamba walete Tawrat ambayo ndiyo wanayoitegemea waisome kadamnasi, wakiwa wanasema kweli katika madai yao ya uharamu wa ngamia au wengineo. Lakini wao baada ya pambano hili waliingia gizani na hawakuwa na ushujaa wa kuileta Tawrat, kwa sababu wao walikuwa wana yakini kabisa na ukweli wa Mtume (s.a.w) na uongo wao.

Mwenye kumzulia uongo Mwenyezi Mungu baada ya hayo.

Yaanibaadayakudhihirihojanakusimamadaliliyahaki.

Basi hao ndio madhalimu.

Kwa sababu wamepotea na kuwapoteza wengine kwa kuing'ang'ania na kuipinga haki.

Sema: amesema kweli Mwenyezi Mungu.

Kwamba kila chakula kilikuwa halali kwa wana wa Israil na kwamba Muhammad ni Mtume wa haki.

Basi fuateni mila ya Ibrahim aliyeshikamana na haki.

Hapana budi kuashiria kwamba Muhammad (s.a.w) alikuwa katika mila ya Ibrahim na mila ya Mitume yote katika itikadi na misingi. Ama katika sharia alikuwa ni tofauti, ingawaje sharia zote zinasimamia masilahi, lakini masilahi yanatofautiana kulingana na hali ya mazingira na mnasaba.

Kuafikiana sharia katika kuhalalisha chakula, hakuwezi kukulazimisha kuwa sharia moja katika pande zote.

Vyovyote iwavyo, ni kwamba makusudio ya Aya tulizozifafanua ni kuwakadhibisha mayahudi yale waliyowasingizia Mitume katika kuharamisha baadhi ya vyakula.

إِنَّ أَوَّلَ بَيْتٍ وُضِعَ لِلنَّاسِ لَلَّذِي بِبَكَّةَ مُبَارَكًا وَهُدًى لِلْعَالَمِينَ {96}

Hakika nyumba ya kwanza waliyowekewa watu ni ile iliyoko Makka yenye kubarikiwa na mwongozo kwa viumbe.

فِيهِ آيَاتٌ بَيِّنَاتٌ مَقَامُ إِبْرَاهِيمَ ۖ وَمَنْ دَخَلَهُ كَانَ آمِنًا ۗ وَلِلَّهِ عَلَى النَّاسِ حِجُّ الْبَيْتِ مَنِ اسْتَطَاعَ إِلَيْهِ سَبِيلًا ۚ وَمَنْ كَفَرَ فَإِنَّ اللَّهَ غَنِيٌّ عَنِ الْعَالَمِينَ {97}

Mna humo ishara zilizo wazi: Mahali aliposimama Ibrahim. Na mwenye kuingia humo huwa katika amani; Na ni haki ya Mwenyezi Mungu juu ya watu kuhiji nyumba hiyo kwa mwenye kuweza njia ya kuiendea. Na atakayekufuru, basi Mwenyezi Mungu si muhitaji wa viumbe.