Aya 144-148: Hakuwa Muhammad Ila Ni Mtume
Maana
Hakuwa Muhammad ila ni Mtume wamekwishapita Mitume kabla yake. Je, akifa au akiuliwa mtarudi nyuma?
Aya hii inaashiria tukio maalum ambalo ni vita vya Uhud; limekwishaelezwa. Kwa ufupi ni kuwa Mtume (s.a.w) aliwaamrisha wapiga mishale wasiondoke kwenye mlima kwa hali yoyote ile, ni sawa wawe waislamu wameshinda au wameshindwa.
Lakini kundi kubwa la wapiga mishale walipoona kushindwa kwa washirikina katika muhula wa kwanza, waliziacha sehemu za nyuma za waislamu bila ya ulinzi na kuharakia nyara. Kwa hiyo washirikina wakawarudia waislamu: wengi wao wakauwawa na Mtume kujeruhiwa vibaya. Mnadi akanadi kuwa Muhammad
ameuawa, watu wakamkimbia Mtume na akabakiwa na wachache tu, akiwemo Ali bin Abi Talib na Abu Dajana Al-ansari. Masahaba wengine wakasema: "Hatupati mtu wa kututakia amani kwa Abu Sufian?" wengine wakasema: "Lau Muhammad angelikuwa Mtume asingeuawa, rudieni dini yenu ya kwanza."
Qur'an imewakaripa walioshindwa, wenye shaka shaka ikiwaambia kuwa Muhammad ni Mtume aliye binadamu tu, anayefikisha risala ya Mola wake kwa waja wake, na anapofikisha, basi umuhimu wake umekoma. Na ujumbe wake haufungamani na utu wake wala haufi kwa kufa kwake, bali utabaki kwa kubakia Mwenyezi Mungu asiyekufa; sawa na Mitume wengine ambao walikufa au kuuwawa na ujumbe wao na mafunzo yao kubakia. Kwa maneno mengine, mwito haufi kwa kufa anayeutoa mwito huo; na misingi haiondoki kwa kuondoka watu.
Mfano mzuri wa hakika hii ni yale yaliyoelezwa katika Tafsir Tabari kwamba mtu mmoja katika Mujahirina alimpitia mtu mwengine katika Ansari akiwa ametapakaa damu. yule Muhajir akasema: "Je, wajua kuwa Muhammad ameuawa?" Ansari akasema: "Ikiwa ameuwawa tayari amekwisha fikisha ujumbe, basi ipi- ganieni dini yenu."
Katika hiyo hiyo Tabari na vinginevyo imeelezwa kuwa Anas bin Annadhr alimpitia Umar bin Khattab na Talha bin Ubaidullah na watu wengine katika Muhajir na Ansar wakiwa wamesalimu amri. Anas akawaambia: "Mbona mmekaa? wakasema: Muhammad ameuawa. Akasema: Ikiwa Muhammad ameuawa, lakini Mola wa "Muhammad hakuuawa, na mtayafanyia nini maisha baada ya Muhammad. Basi piganieni lile alilopigania na kufeni kwenye lile alilolifia."
Kisha akaendelea kusema: "Ewe Mola wangu! Hakika mimi nakuomba msamaha na waliyoyasema hawa na ninajitenga na waliyokuja nayo." Kisha akaukamata barabara upanga wake akapigana mpaka akauawa. (radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie)
Ibn Al-Qayyim Al-Jawziy katika juzuu ya pili ya Zadul-Ma'ad uk. 253 anasema: Tukio la Uhud lilikuwa ni utangulizi na lawama kuhusu mauti ya Muhammad (s.a.w).
Mwenyezi Mungu anawazindua na kuwakaripia kwa kurudi nyuma kwao, iwapo Mtume wa Mwenyezi Mungu atakufa au kuuwawa. Mwenye Tafsir Al-Manar akimnukuu mwalimu wake Sheikh Muhammad Abduh anasema: Neno 'mtarudi nyuma' linaenea katika kurtadi kwa kuacha dini na kuacha kuipa nguvu haki." Kisha akaongezea mwenye Al-Manar kwa kusema: hivi ndivyo ilivyo.
Kwa hiyo basi, kurudi nyuma kulikokusudiwa katika Aya hii hakuishii kwenye Tawhid peke yake, bali kunaenea kuacha kazi ya haki aliyoiusia Mtume (s.a.w). Haya yanatiliwa nguvu na yaliyoelezwa katika Sahihi Bukhari Jz 9 kitabul-Fitan kwamba Mtume atasema siku ya kiyama: "Ewe Mola wangu! (Hao) ni sahaba zangu." Naye ataambiwa "Wewe hujui walizuwa nini baada yako."
Hadith nyingine katika Hadith za Bukhari inasema: "…wewe hujui walibadilisha nini baada yako?" "Hapo nitasema: Basi kuangamia ni kwa mwenye kuibadilisha (dini yake) baada yangu." Hakuna mwenye shaka kwamba makusudio ya kubadil- isha hapa ni kuiacha sunna yake na kuhalifu kauli zake na sharia yake.
Na atakayerudi nyuma hatamdhuru kitu Mwenyezi Mungu
bali atajidhuru mwenyewe kwa kujiingiza katika machukivu na adhabu ya Mwenyezi Mungu.
Na mwenyezi Mungu atawalipa wenye kushukuru
Ibnul-Qayyim katika Zadul-Ma'ad uk. 254 anasema: "Na wenye kushukuru ni wale waliojua thamani ya neema wakathibiti nayo mpaka wakafa au kuuawa.
Ilidhihiri athari ya lawama hii na yakahukumu maneno hayo siku alipokufa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w), akartadi mwenye kurtadi kwa kurudi nyuma.
Ajali Haina Kinga
Na nafsi haiwezi kufa ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu - kama ilivyoandikwa ajali yake.
Aya hii iko katika maana ya Aya isemayo: "…Utakapofika muda wao hawatakawia hata saa moja wala hawatatangulia." (7:34)
Maana ni kuwa uhai na kifo viko mikononi mwa Mwenyezi Mungu na kwamba ajali imepangwa katika muda maalum anaoujua yeye; haiharakishwi wala haikawizwi. Ni sawa iwe sababu yake ni upanga, maradhi, uzee au mengineyo.
Imam Ali (a.s.) anasema: "Ajali inatosha kuwa ni mlinzi."Akasema tena: "Ajali ni ngome imara." Katika Aya hii kuna mahimizo ya Jihadi, kwa sababu ajali ipo tu. Na wala hakuna yeyote atakayekufa kabla ya kufikilia ajali yake. Hata akijipeleka kwenye maangamizi.
Unaweza kuuliza: tunavyoshuhudia ni kuwa mauti yana sababu maalum: kama vile kuuliwa, kufa maji, majanga na mengineyo. Je hili si linakanusha kuwa ajali imepangwa kwa ujuzi wake Mwenyezi Mungu?
Hilo amelijibu Sheikh Muhammad Abduh - kama ilivyo katika Al-Manar - kwamba hakuna sababu za mauti zaidi ya ajali iliyokadiriwa na Mwenyezi Mungu. Kwani janga linaweza kuenea, lakini akafa kijana mwenye nguvu na akabaki mkongwe dhaifu.
Ni majanga mangapi yaliyomwacha huyu ya kamuua yule. Na kama ingelikuwa sababu hizi zinawaenea wote, basi ingelithibiti athari yake kwa wote, bila ya kubakisha hata mmoja.
Swali la pili: Kama ni hivyo basi inatakikana muuaji asiwe na majukumu mbele ya Mwenyezi Mungu. Lakini Mwenyezi Mungu anasema: "Na Mwenye kumua Muumin kwa kukusudia, basi malipo yake ni Jahannam, humo atadumu na Mwenyezi Mungu amemghadhibikia na amemlaani na amemwandalia adhabu kubwa (4:93).
Jibu: Mwenye kuuawa amekufa kwa muda wake, na mwenye kuuwa anastahili adhabu, kwa sababu amefanya lililokatazwa na Mwenyezi Mungu hali alikuwa anaweza kujiepusha nalo na kumwacha aliyemuua, afe na sababu nyingine. Kwa maneno mengine ni kuwa hapa kuna mambo mawili:
1. Kila mwenye kufanya jambo la haramu kwa makusudi, ana jukumu.
2. Mwenye kufanyiwa makosa ana muda wake maalum.Kwa hiyo hapo yamekuja mambo mawili katika maudhui moja, lakini kila moja lina hukumu yake na athari yake.
Na anayetaka malipo ya dunia tutampa humo na anayetaka malipo ya akhera tutampa huko: na tutawalipa wenye kushukuru.
Tamko la Aya linaenea kwa mambo yote na mfumo wa maneno unahusu jihadi. Maana yake ni kuwa mwenye kupigana kwa kutafuta faida na ngawira, si kwa kutaka thawabu za Mwenyezi Mungu na akauliwa, basi atakuwa amepata hasara ya dunia na akhera. Na kama akisalimika na jeshi likapata ngawira, atapata fungu lake na hatapata chochote katika thawabu za Mwenyezi Mungu, kama akipigana kwa kuinusuru haki na kuinyanyua dini atachukua fungu lake la ngawira na atastahiki malipo na thawabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Vilevile hata akikusudia mambo mawili pamoja, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "…Na kuna miongoni mwa watu asemaye: Mola wetu! Tupe katika dunia, na katika akhera hana sehemu yoyote. Na miongoni mwao yuko anayesema: Mola wetu! Tupe mema duniani na katika akhera (utupe) mema na utukinge na adhabu ya moto. Hao ndio wenye fungu katika waliyoyachuma na Mwenyezi Mungu ni mwepesi wa kuhisabu." (2:200-202)
Jihadi inaweza kuchukuliwa na makusudio mawili pamoja: dunia na akhera kinyume na Saumu, Swala, Hijja na Zaka. Kwa sababu hayo yote ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu pekee yake ambayo yanaharibiwa hata na mchanganyiko mdogo.
Kila Mtu Ana Alilolinuia
Mwenye kufuatilia Aya za Mwenyezi Mungu (s.w.t.) na Hadith za Mtume Wake (s.a.w) ataona kuwa nia ina athari kubwa katika kuhukumu kauli na vitendo vya watu. Mwenyezi Mungu anasema: "Anayetaka malipo ya duniani tutampa…"
Akasema tena: "Anayetaka (dunia) ipitayo upesi, tutamharakisha humo tunayoyataka… na anayetaka akhera na akizifanyia juhudi amali zake na hali ya kuwa ni mu'min, basi hao juhudi yao ni yenye kushukuriwa." (17: 18-19).
Vilevile amesema: "Siku ambayo haitafaa mali wala watoto, isipokuwa mwenye kuja na moyo safi." (26: 88-89). Katika Hadith tukufu imesemwa hivi: "kila mtu ana alilonuia…watu watafufuliwa kulingana na nia zao…. hakika amali (zote huzingatiwa) kwa nia… Nia ya mtu ni bora kuliko vitendo vyake."
Wala hapana ajabu, kwani moyo ndio msingi. Mapigo yake ndiyo yanayopeleka uhai wa mtu na kuzimika kwake ndiko kuzimika uhai, ndipo mahali pa imani na ukanushaji, hofu na matarajio, mapenzi na chuki, ushujaa na woga, ikhlas na unafiki, kukinai na tamaa na mengineyo katika mambo mazuri na mabaya.
Hadith Qudsi inasema: "Haikunikunjua ardhi yangu wala mbingu yangu lakini moyo wa mja wangu mumin umenikunjua.” Yaani umetambua ukubwa wa Mwenyezi Mungu.
Vitendo vyote hutendwa na kutengenezwa na moyo, kwa sababu ndio asili yake. Kwa hivyo basi mtu anaweza kujichagulia njia yake yeye mwenyewe kwa kuchgua malengo yake, kheri na shari anayachagua kuanzia mwanzo hadi mwisho, kama ambavyo sisi tunaweza kumhukumu kwa malengo anayojichaguliya mwenyewe.
Watu wa nadharia (ya upatikanao) wanasema: haiwezekani kumhukumu mtu ila baada ya kupita hatua ya mwisho katika hatua za maisha yake.. maana yake ni kuwa wanalazimisha kutopitisha hukmu ila kwa waliokufa tu. Ama walio hai hawahukumiwi au kulaumiwa. Ingawaje hawa wanaodai hivyo akiwemo kiongozi wao Sartre, wanawahukumu walio hai.
Unaweza kuuliza: Mara nyingi umeeleza - katika sehemu mbali mbali - kwamba vinavyozingatiwa ni vitendo na kwamba hakuna imani ila kwa takua na amali njema. Na haya si yanapigana na kauli yako ya hapa kwamba inayozingatiwa ni nia na malengo?
Jibu: Nia, tunayoikusudia hapa ni nguvu ya msukumo na azimio linalotia mkazo ambalo haliepukani na kitendo. Hilo limeelezwa na Aya isemayo: "... Na anayeita- ka akhera na akazifanyia juhudi amali zake…" (17:19).
Na nia hii iko katika hukmu ya kitendo, bali ni kitendo hasa, kama alivyosema Imam Jafar as-Sadiq (a.s.). kwa sababu ndiyo asili ya kitendo na ni chimbuko lake. Na asiyekusudia hatendi. Kwa hivyo basi thawabu za nia hii ni thawabu za kitendo. Ama nia ya uovu, yaani kuazimia kufanya uovu, ni haramu bila ya shaka yoyote.
Na mwenye kuazimia hayo anastahiki adhabu, lakini Mwenyezi Mungu (s.w.t.) aweza kumuondoshea adhabu hiyo - kwa hisani yake - ikiwa hatofanya alilolinuiya, hata kama alilazimika kuliacha kwa nguvu. Hivyo, katika mtazamo wa Kiislamu, nia ya kheri ni kheri hata bila ya vitendo na nia ya shari si shari bila ya kitendo.
Ni Manabii wangapi waliopigana, pamoja nao waumini wengi. Nao hawakulegea kwa yale yaliyowasibu katika njia ya Mwenyezi Mungu, wala hawakudhoofika, wala hawakudhalilika. Na Mwenyezi Mungu anawapenda wafanyao subira.
Baada ya Mwenyezi Mungu kuwapa ushindi Waislamu katika vita vya Badr, waki- wa ni wachache na wanyonge, waliona kwamba kila vita watashinda maadamu wako na Muhammad (s.a.w), hivyo kushindwa kwa siku ya Uhud kukawa ni jambo wasilolitazamia. Wakawa na yale tuliyokwisha yaeleza.
Katika Aya hii Mwenyezi Mungu (s.w.t) anawapigia mifano wale waliolegea, wakadhoofika na kudhalilika na kutokuwa na subira siku ya Uhud, anawapigia mfano na wafuasi wa Mitume waliotangulia, ambao walikuwa na subira katika Jihadi, kuuliwa, kutekwa na kujeruhiwa, nao hawakukimbia, kama mlivyofanya nyinyi wafuasi wa Muhammad (s.a.w).
Na ilikuwa ni laiki yenu muwaigize, muwe na mazingatio kwa hali zao; jambo ambalo linatakikana kwa waumini wanaopigania dini yao na itikadi yao kwa nyoyo zao.
Halikuwa neno lao, yaani wafuasi wa Mitume waliotangulia,ila ni kusema: "Ewe Mola wetu! Tughufurie dhambi zetu na kupita kwetu kiasi katika mambo yetu na uimarishe miguu yetu na utusaidie juu ya watu makafiri.
Hawakutia shaka kabisa katika dini yao na Mtume wao kama yale waliyoyafanya maswahaba wa Muhammad (s.a.w) siku ya Uhud. Hivi ndivyo anavyokuwa mu'min wa kweli, akijituhumu mwenyewe na kuona kuwa balaa zilizompata ni kwa ajili ya uzembe wake na kupetuka kwake mpaka katika amri za Mwenyezi Mungu, humuomba Mwenyezi Mungu msamaha na uongofu. Ama mu'min aliye kom- bokombo anamsukumizia Mungu na kusema: Mola wangu amenitweza.
Mwenyezi Mungu akawapa malipo ya duniani na malipo mema ya akhera, na Mwenyezi Mungu anawapenda wanaotenda wema.
Malipo ya Mwenyezi Mungu na pendo lake linatosha kuwa ni fahari na ni akiba ya akhera. Aya hii inafahamisha kwamba kunyenyekea na kujituhumu kunakurubisha kwa Mwenyezi Mungu na humwinua mwenye kunyenyekea na kumweka kwenye daraja ya juu.
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنْ تُطِيعُوا الَّذِينَ كَفَرُوا يَرُدُّوكُمْ عَلَىٰ أَعْقَابِكُمْ فَتَنْقَلِبُوا خَاسِرِينَ {149}
بَلِ اللَّهُ مَوْلَاكُمْ ۖ وَهُوَ خَيْرُ النَّاصِرِينَ {150}
سَنُلْقِي فِي قُلُوبِ الَّذِينَ كَفَرُوا الرُّعْبَ بِمَا أَشْرَكُوا بِاللَّهِ مَا لَمْ يُنَزِّلْ بِهِ سُلْطَانًا ۖ وَمَأْوَاهُمُ النَّارُ ۚ وَبِئْسَ مَثْوَى الظَّالِمِينَ {151}