Aya 176-178: Wanaokimbilia Ukafiri
Maana
Wala wasikuhuzunishe wale wanaokimbilia ukafiri, hakika hao hawatamdhu- ru kitu Mwenyezi Mungu.
Yametangulia maelezo kuwa washirikina walikusanya makundi, wakaandaa jeshi la kumpiga vita Mtume (s.a.w.) na wanafiki walikuwa wakiwasaidia na wakiwapangia njama waislamu.
Katika Aya hii Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewataja wanafiki na washirikina kuwa ni waasi na wanafanya bidii kuipinga haki na kuipiga vita. Na Mtume (s.aw.) alikuwa akihuzunika na kuona uchungu kutokana na vitendo vyao hivi. Ndipo Mwenyezi Mungu Mtukufu akamwambia: Usihuzunike, wao hawatakudhuru na chochote wewe, wala Waislamu na dini ya Mwenyezi Mungu, na kwamba njama zao hizo zitapotea tu. Ama dini itakuwa na utukufu. Na kweli hazikupita siku nyin- gi Mwenyezi Mungu akaumakinisha uislamu Mashariki na Magharibi kwa watu ambao jana walikuwa wakikimbilia kuupiga vita.
Mwenyezi Mungu anataka asiwawekee fungu lolote huko akhera. Nao wana adhabu kubwa.
Huu ndio ukweli wa kila mwenye kuendelea na upotevu mpaka akafa. Unaweza kuuliza, kuwa dhahiri ya Aya inaonyesha kuwa shari inatokana na Mwenyezi Mungu, kwa sababu , adhabu ya Jahannam ni shari, na Mwenyezi Mungu amewatakia hiyo adhabu, itakuwaje?
Jibu: ni kweli kuwa Mwenyezi Mungu amewatakia adhabu, lakini ni baada ya kustahili, kwa sababu yeye Mwenyezi Mungu (s.w.t.) aliwaamrisha kuamini na akawakataza kukufuru na akawaachia hiyari. Hivyo wakachagua ukafiri badala ya imani. Maana yake ni kwamba washirikina na wanafiki ndio waliosababisha adhabu. Baada ya wao kusababisha kwa hiyari yao, ndipo Mwenyezi Mungu akawatakia adhabu sawa na hakimu anayemtakia kifungo mwenye hatia baada ya kufanya makosa.
Hakika wale walionunua ukafiri kwa imani, hawatamdhuru kitu Mwenyezi Mungu.
Neno 'walionunua' linafahamisha hiyari. Kwa sababu mnunuzi anachagua bidhaa na kuridhia anachokichukua badala ya thamani. Na kafiri ameridhia ukafiri badala ya imani, ndipo akastahili adhabu kali.
Unaweza kuuliza: kwa nini Mwenyezi Mungu amelikariri neno 'hawatamdhuru Mwenyezi Mungu kitu' katika Aya mbili, kuna siri gani?
Jibu: makusudio ya Aya ya kwanza ni makafiri wa kiquraishi walioandaa jeshi la kumpiga Mtume (s.a.w.) na wale wanafiki waliokuwa wakiwasaidia. Aya ya pili, makusudio yake ni kila kafiri kuanzia wa mwanzo hadi wa mwisho, awe mpiga vita au la.
Kwa hiyo Aya ya kwanza inakuwa ni mahsusi, na ya pili ni kutaja kiujumla. Mara nyingi inakuwa hivi katika maneno ya watu ambao husema "Fulani amecheza kamari akajimaliza na kila mwenye kufanya hivyo ataangamia."
Wala wasidhanie kabisa wale waliokufuru kwamba muda tunaowapa, ni heri kwa nafsi zao. Hakika tunawapa muda na wanazidi tu katika (kufanya) dhambi na wana wao adhabu idhalilishayo.
Umri wa mtu ni kama mali yake, akiitumia vizuri yeye, kwa watu wake na pia kwa watu wengine au jamaa zake wanaohitaji, basi atarudiwa na heri na wema. Kila mali yake inapozidi ndiyo kunavyozidi kutoa kwake na ndipo wema wake unavyozidi. Na kama akiitumia vibaya na kuitoa katika maasi, basi humrudia mabaya, na kila inavyozidi na kukuwa ndivyo anavyozidi uasi na ufisadi.
Umri nao ni hivyo hivyo. Mtu hufikilia wema kama akifanya amali nzuri na unakuwa ni sababu ya uovu wake, kama akifanya uovu. Hiyo ndiyo desturi ya Mungu kwa kijamii. Kila desturi iliyozoeleka inayojulikana kimaumbile au kijamii, basi ni desturi ya Mwenyezi Mungu katika viumbe vyake.
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amepitisha desturi yake kwa makafiri na watu wote. Amewapa muda kwa kurefusha umri ili mtu ajichagulie mwenyewe, kheri au shari. Lakini kafiri akaghurika kwa kupewa muda na akajiachia katika upotevu.
Kwa hiyo ikawa natija ya kupewa kwake muda, ni uovu wake na adhabu yake. Kinyume na Mumini, Mwenyezi Mungu akichelewesha ajali yake kheri yake huzidi na wema huwa mwingi. Bali mwenye kufanya wema katika sehemu iliyobakia katika umri wake, hataadhibiwa kwa dhambi zake zilizopita, kama ilivyoelezwa katika Hadith tukufu.
Kwa hali hiyo basi, inatubainikia kuwa herufi Lam katika neno liyazdaadu ni ya mwishilio, sio ya sababu, yaani wanazidi tu na sio 'ili' wazidi.
Kafiri Na Amali Njema
Unaweza kuuliza: baadhi ya makafiri hufanya kheri kwa ajili ya kheri, na kila umri wao unavyozidi ndivyo wanavyozidi kuwanufaisha watu kwa elimu zao na juhudi zao zilizo nzuri kabisa. Je, hii haipingani na kauli yake Mwenyezi Mungu, na wanazidi tu, katika dhambi?
Jibu: Mfumo wa Aya unakusudia dhambi tu, na kuwa wao kwa upande huu wanazidi ukafiri, na wala sio katika hali zote, kwani huenda wakawa ni wema kati- ka baadhi ya matendo yao.
Swali la pili: Je kafiri akifanya wema na kuwanufaisha watu, atapata thawabu, au wema wake huo ni sawa na kutofanya chochote?
Jibu: Mtu kwa mtazamo wa imani na matendo (amali), atakuwa katika mojawapo ya hali nne zifuatazo: -
1. Kuamini na kutenda amali njema, hali hii inafuatana na kauli ya Mwenyezi Mungu: "Hakika wale wanaosema mola wetu ni Mwenyezi Mungu, kisha wakawa na msimamo, wao huteremkiwa na Malaika (na kuwaambia): msiogope wala msihuzunike na furahieni pepo mliyokuwa mkiahidiwa." (41:30)
2. Kutomuamini Mwenyezi Mungu na kutofanya amali njema, hawa ni katika wale ambao: "Shetani amewatawala, kwa hivyo akawasahaulisha kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Hao ndio kundi la shetani ni lenye kupata hasara." (58:19)
3. Kuamini bila ya kufanya amali njema, hawa ni katika wanachama wa shetani kama wale waliotangulia. Lau angelikuwa ni mumin wa kweli, basi zingeonekana alama za imani. Mtume (s.a.w.) anasema: "Hakuna inayookoa isipokuwa amali. Lau ningeasi ningeliangamia." Ama ikiwa amali yake njema imechanganyika na mbaya na akatubia, basi atakuwa katika Aya isemayo: "Na wako wengine waliokiri dhambi zao, wakachanganya vitendo vizuri na vingine vibaya. Huenda Mwenyezi Mungu akapokea toba zao. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kusamehe mwenye kurehemu." (9:102)
4. Kufanya amali njema bila ya kuamini, kama kafiri amlishaye mwenye njaa au amvishaye aliye uchi, atengenezaye barabara, kujenga nyumba za mayatima, au hospitali, kwa njia ya kheri ya kibinadamu. Imesemekana amali yake hii, kuwepo kwake na kutokuwepo ni sawa tu. Kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu: "Hakika Mwenyezi Mungu anawakubali wamchaye tu." (5:28)
Hapa Tunajibu hivi:
Kwanza: Makusudio ya kauli ya Mwenyezi Mungu: "Hakika Mwenyezi Mungu huwakubalia wamchaye tu," sio kuwa mtu akimwasi Mwenyezi Mungu katika jambo fulani, basi hamkubalii akimtii katika jambo jingine. Kama ni hivyo basi wasingekubaliwa isipokuwa waliohifadhiwa kutotenda dhambi (Maasum) tu, jambo ambalo linapingana na uadilifu wake na hekima yake.
Isipokuwa makusudio ya Aya kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hakubali isipokuwa amali safi isiyokuwa na uchafu wowote wa kidunia na kwamba mwenye kufanya tendo lolote kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu na kwa kheri basi atatosheka na aliyemfanyia.
Hakuna mwenye shaka kwamba mwenye kufanya kheri kwa ajili ya kheri na ubinadamu, basi amefanya kheri hiyo kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ni sawa awe amekusudia hivyo au la. Na mwenye kufanya amali kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, basi malipo yake yako kwa Mwenyezi Mungu.
Ama makusudio ya 'hapana dhambi zaidi ya ukafiri' ni kuwa ukafiri ni dhambi kubwa na kwamba dhambi yoyote kadiri itakavyokuwa kubwa haishindi ukafiri. Lakini hili - la kuwa ukafiri ni dhambi kubwa - ni jambo jingine, na malipo ya wema ni jambo jingine.
Pili: Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ni mwadilifu, katika jumla ya uadilifu wake ni kwamba mwema na muovu hawako sawa bali mwema ana malipo yake na mwovu ana malipo yake. Wala sio lazima malipo ya mtenda mema asiyekuwa mu'min yawe akhera. Inawezekana yakawa duniani kwa kuondolewa madhara na balaa, kama asemavyo Mtume (s.a.w.): "Kufanya wema ni kinga ya mambo maovu."
Na pia sio kuwa malipo ya akhera ni pepo tu, inawezekana kuwa ni kwa kupunguziwa adhabu, au kutokuwa na adhabu wala malipo kama ilivyo hali ya A'raf.
Kwa ufupi ni kuwa mtu atalipwa kwa vitendo vyake, vikiwa ni kheri basi atalipwa kheri na vikiwa ni shari atalipwa shari. Kafiri anastahili adhabu kutokana na ukafiri wake, na huenda akafanya kheri kwa ajili ya kheri akastahiki malipo mema. Kila tendo lina hisabu.
Ndio, ni kweli sisi hatujui aina ya malipo atakayolipwa mtenda wema asiyekuwa mu'min. Pia hatujui ni lini na wapi, duniani au akhera. Haya yanategemezewa kwenye ujuzi wa Mwenyezi Mungu na hekima Yake. Na kuyapanga hayo ni kama kushirikiana na Mwenyezi Mungu katika elimu yake. Basi na amwogope Mwenyezi Mungu mwenye kumwamini. Kwa mnasaba huu tutataja maneno ya Sayyid Kadhim mwenye kitab U'rwathul- Wuthqa mlango wa waqf, maswala ya sharti ya niya ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu. Ninamnuku:
"Inawezekana kusema kwamba, thawabu zinathibiti kwa matendo mema, hata kama hayakusudiwa kwa ajili ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu. Kwa sababu anayeyatenda anastahiki kusifiwa kwa wenye akili, hata kama hakukusudia kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu. Basi ikiwa hivyo, sio mbali kustahiki fadhila kuto- ka kwa Mwenyezi Mungu mtukufu."
Kwa hiyo mwanachuoni huyu mkubwa anasema wazi kwamba inawezekana mtu kulipwa malipo mema kwa vitendo vizuri hata kama hakukusudia radhi ya Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo kutakuwa na uwezekano mkubwa zaidi kupewa malipo mema anayekusudia njia ya kheri na ubinadamu. Imekwishaelezwa mara nyingi kwamba akili haikatai kuwa yawezekana mwenye dhambi aneemeshwe kwa fadhila za Mwenyezi Mungu, isipokuwa linalokataliwa na akili ni kuadhibiwa na Mwenyezi Mungu yule asiyestahili adhabu.
مَا كَانَ اللَّهُ لِيَذَرَ الْمُؤْمِنِينَ عَلَىٰ مَا أَنْتُمْ عَلَيْهِ حَتَّىٰ يَمِيزَ الْخَبِيثَ مِنَ الطَّيِّبِ ۗ وَمَا كَانَ اللَّهُ لِيُطْلِعَكُمْ عَلَى الْغَيْبِ وَلَٰكِنَّ اللَّهَ يَجْتَبِي مِنْ رُسُلِهِ مَنْ يَشَاءُ ۖ فَآمِنُوا بِاللَّهِ وَرُسُلِهِ ۚ وَإِنْ تُؤْمِنُوا وَتَتَّقُوا فَلَكُمْ أَجْرٌ عَظِيمٌ {179}