read

Aya 142 – 143: Thamani Ya Pepo

Maana

Je, mwadhani mtaingia peponi na hali Mwenyezi Mungu hajawajua wale waliofanya jihadi miongoni mwenu na kuwajua wale waliofanya subira?

Aya hii imefahamisha wazi wazi kwamba uislamu una mfungamano mkubwa na amali njema hapa duniani na kwamba sharti ya kwanza ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu na kufuzu kwa radhi Zake na thawabu Zake ni jihadi, kujitolea, ukweli, ikhlasi, subira na uthabiti.

Ama kujenga misikiti, sehemu za ibada, kufunga, kuswali na kusoma Qur'an na nyuradi, yote hayo na mengineyo sichochote ila ikiwa, ni nyenzo ya kazi itakayoleta manufaa kwa watu au itakayowakinga na madhara.

Aya hii tuliyonayo ambayo imefungamanisha kuingia peponi na jihadi na kuvumilia taabu zake, iko katika maana pamoja na Aya hizi zifuatazo: "Hakika Mwenyezi Mungu amenunua kwa waumini nafsi zao na mali zao kwamba wapate pepo, wanapigana katika njia ya Mwenyezi Mungu, kwa hiyo wanaua na wanauwa. Ni ahadi iliyothibiti juu yake katika Tawrat na Injil na Qur'an …" (9:111) Na

Aya nyingine ni: "Na aliye kipofu katika (dunia) hii basi katika akhera atakuwa kipofu na aliyepotea zaidi njia." (17:72) Inatosha kuwa ni dalili ya mkato ya hayo kauli yake Mwenyezi Mungu: "Na kwamba mtu hatapata ila yale aliyoyafanya. Na kwamba amali yake itaonekana. Kisha atalipwa malipo yaliyo kamili." (53: 39 - 41)

Miongoni mwa kauli za Imam Ali (a.s.) ni: "Pepo imezungukwa na machukivu na moto umezungukwa na anasa …Nafsi zenu hazina thamani zaidi ya pepo, kwa hivyo msiziuzie (kitu kingine) ila hiyo tu." Yameshatangulia maelezo katika tafsir ya Aya 155 katika Sura ya Baqara, kifungu 'Thamani ya pepo.'

Nembo Za Kidini

Nembo za kidini, ni kama sehemu za ibada na za kuswali zilizo takatifu, hilo halina shaka, bali ni dharura ya kidini, hapana budi kuwepo. Hakuna nchi yoyote au kikundi chochote ambacho kina msingi mmoja ila kitakuwa na nembo inayokionyesha kikundi hicho au nchi hiyo, na inayowaweka pamoja wafuasi wake.

Lakini nembo peke yake si chochote, bali nembo ni lazima ifuatiliwe na vitendo na athari. Kwa hiyo Swala si kurukuu na kusujudu tu, bali Swala ni ile inayoiweka nafsi ya mwenye kuswali kujitakasa na maovu, wala muungano sio kuungana kusoma tahlili na takbira, bali ni kusaidiana tukiwa na ikhlasi ya lile ambalo lina kheri ya wote.

Hivi sasa wengi wetu wamezifanya nembo za kidini ni vyombo vya kupoteza, na maficho ya miradi ya wakoloni na malengo ya uzayuni. Kwa sababu vyama vingi ambavyo vina majina ya kidini au ya kizalendo ni mashirika ya kijasusi ya nje. Na gharama zake zinatokana na faida itokayo katika mashirika ya mafuta. Lakini jambo la kutia moyo ni kuwa hayo yamefichuka kwa wote. Wenye ikhlasi hawaviamini wala hawashirikiani navyo isipokuwa wahaini wanaouza dini yao na nchi yao kwa shetani.

Kwa hakika mlikuwa mkiyatamani mauti kabla ya kuyakuta; basi mmekwisha yaona nanyi mwatizama.

Msemo unaelekezwa kwa baadhi ya Sahaba wa Mtume (s.a.w), ambao kabla ya vita vya Uhud, walikuwa wakitamani kufuzu kwa kufa shahid, lakini mambo yalipowazidia, waliogopa, wakamwachia Mtume (s.a.w) adui yake na adui yao.

Baadhi ya Riwaya zinasema kuwa miongoni mwa Masahaba walikuwako waliokuwa wakisema: vikija vita tukiwa na Mtume (s.a.w) tutapigana tu, walipotahiniwa na hilo hawakutekeleza ahadi. Ndipo Mwenyezi Mungu akawateremshia Aya hii. Makusudio ya kuona mauti ni kuona sababu zake kutoka kwenye mapambano ya mashujaa. Mwenyezi Mungu amewatahayarisha kwa Aya hii kutokana na vitendo vyao kuhalifu kauli zao.

Mabadiliko Ya Hulka Na Fikra

Kila mtu ana hali zake na mazingira yake yanayomuhusu. Hali hizi - aghlab - ndizo zinazotawala hulka na fikra zake. Kwa mfano mtu mnyonge anaiona mbaya zaidi dhulma kuliko mwenye nguvu.

Na mwenye kukulia katika mazingira ya kuabudu masanamu hawezi kuona ubaya kuyatukuza, ila akiwa si mtu wa kawaida; kama vile Muhammad bin Abdullah. Kwani yeye kimaumbile yake tu alikuwa akichukia kila desturi mbaya ya watu wake.

Mara nyingine hali ya mtu inaweza kubadilika na kuwa tajiri baada ya kuwa maskini, au kinyume chake. Basi hapo hulka zake na fikra zake zinabadilika kufuatana na mabadiliko hayo. Kwa hiyo dhati ya mtu inabakia na sifa yake ikiwa hali yake ya kijamii haikubadilika.

Aghlabu hali ikibadilika na sifa za dhati nazo hubadilika. Tumewaona watu waliokuwa wakiwalaumu matajiri na maraisi, wakati wao ni mafukara wanaoongozwa, lakini mara tu walipopata mali na cheo wakavunja ahadi na kuwa wabaya zaidi ya waliokuwa wakiwalaumu jana.

Qur'an Tukufu imetilia mkazo nadharia hii kwa Aya hii tuliyo nayo, na pia Aya nyingine isemayo: "Na miongoni mwao wako waliomwahidi Mwenyezi Mungu: akitupa katika fadhila zake, hakika tutatoa sadaka na tutakuwa miongoni mwa watu wema. Lakini alipowapa katika fadhila zake walizifanyia ubakhili na wakageuka na huku wakipu- uza."(9:75 - 76)

Mwenye akili na uzoevu huituhumu nafsi yake wala halitilii mkazo kwa mawazo kila linalomtokea, kwa kuhofia kuwa bendera inayofuata upepo; kama ambavyo mumin wa kweli anabaki kuwa thabiti katika tabu na raha; maneno yake hufuatana na vitendo vyake katika hali zote na yote huyaelekeza kwa Mwenyezi Mungu peke yake.

Yamekuja maelezo katika tafsir ya Aya isemayo: "Na yeye ndiye ambaye amewaumba katika nafsi moja kuna (iliyo) mahali pa milele na mahali pa muda." (6:98) kuwa, mahali pa milele ni imani iliyo thabiti, na mahali pa muda ni imani ya kuazima, na hakuna kitu kinachofahamisha imani potofu kuliko kugongana kauli na vitendo.

Ndio maana zikawa kauli za Mitume na Maimamu watakatifu ndio vitendo vyao hasa. Na vitendo vya wanafiki viko mbali na kauli zao.

وَمَا مُحَمَّدٌ إِلَّا رَسُولٌ قَدْ خَلَتْ مِنْ قَبْلِهِ الرُّسُلُ ۚ أَفَإِنْ مَاتَ أَوْ قُتِلَ انْقَلَبْتُمْ عَلَىٰ أَعْقَابِكُمْ ۚ وَمَنْ يَنْقَلِبْ عَلَىٰ عَقِبَيْهِ فَلَنْ يَضُرَّ اللَّهَ شَيْئًا ۗ وَسَيَجْزِي اللَّهُ الشَّاكِرِينَ {144}

Hakuwa Muhammad ila ni Mtume; wamekwisha pita Mitume kabla yake. Je, akifa au akiuliwa mtarudi nyuma? Na atakayerudi nyuma hatamdhuru kitu Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu atawalipa wenye kushukuru.

وَمَا كَانَ لِنَفْسٍ أَنْ تَمُوتَ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّهِ كِتَابًا مُؤَجَّلًا ۗ وَمَنْ يُرِدْ ثَوَابَ الدُّنْيَا نُؤْتِهِ مِنْهَا وَمَنْ يُرِدْ ثَوَابَ الْآخِرَةِ نُؤْتِهِ مِنْهَا ۚ وَسَنَجْزِي الشَّاكِرِينَ {145}

Na nafsi haiwezi kufa ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu kama ilivyoandikwa ajali yake. Na anayetaka malipo ya dunia tutampa humo na anayetaka malipo ya akhera tutampa huko; na tutawalipa wenye kushukuru.

وَكَأَيِّنْ مِنْ نَبِيٍّ قَاتَلَ مَعَهُ رِبِّيُّونَ كَثِيرٌ فَمَا وَهَنُوا لِمَا أَصَابَهُمْ فِي سَبِيلِ اللَّهِ وَمَا ضَعُفُوا وَمَا اسْتَكَانُوا ۗ وَاللَّهُ يُحِبُّ الصَّابِرِينَ {146}

Ni manabii wangapi waliopigana pamoja nao waumin wengi, nao hawakulegea kwa yale yaliyowasibu katika njia ya Mwenyezi Mungu, wala hawakudhoofika, wala hawakudhalilika. Na Mwenyezi Mungu anawapenda wanaosubiri.

وَمَا كَانَ قَوْلَهُمْ إِلَّا أَنْ قَالُوا رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا ذُنُوبَنَا وَإِسْرَافَنَا فِي أَمْرِنَا وَثَبِّتْ أَقْدَامَنَا وَانْصُرْنَا عَلَى الْقَوْمِ الْكَافِرِينَ {147}

Halikuwa neno lao, ila ni kusema: Ewe Mola wetu! Tughufirie dhambi zetu na kupita kwetu kiasi katika mambo yetu na uimarishe miguu yetu na utunusuru juu ya watu makafiri.

فَآتَاهُمُ اللَّهُ ثَوَابَ الدُّنْيَا وَحُسْنَ ثَوَابِ الْآخِرَةِ ۗ وَاللَّهُ يُحِبُّ الْمُحْسِنِينَ {148}

Mwenyezi Mungu akawapa malipo ya duniani na malipo ya akhera na Mwenyezi Mungu anawapenda watendao mema.