read

Aya 153-155: Mkawalipa Majonzi Kwa Majonzi

Maana

(Kumbukeni) mlipotoka mbio wala hamumtizami yeyote na hali Mtume anawaita nyuma yenu.

Msemo unaelekezwa kwa wale walioshindwa siku ya Uhud naye anawakumbusha walivyowaogopa washirikina na kukimbia kwao bila ya kumwangalia yeyote, na bila ya kuitikia mwito wa Mtume (s.a.w) wakati alipokuwa anawaita, akiwa amesimama nyuma yao huku akisema: "Njooni enyi waja wa Mwenyezi Mungu…Mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu…Atakayerudi Pepo ni yake… "Alifanya hivyo Mtume ili awatulize kuwa yeye yuko hai, baada ya mtu mmoja kupiga kelele kwamba Muhammad ameuawa, na nyoyo za waislamu kutaharuki.

Akawalipa majonzi kwa majonzi.

Mtume aliwaamrisha wapiga mishale wasiondoke kwenye jabali kwa hali yoyote, wakaasi na kukhalifu amri yake. Mtume (s.a.w) akapata majonzi kwa hilo. Kwa hiyo Mwenyezi Mungu akawalipa wao majonzi ya kushindwa badala ya majonzi ya Mtume. Majonzi ya kwanza ni yale waliyoyapata Masahaba walioshindwa, na majonzi ya pili ni yale aliyoyapata Mtume.

Inasemekana kuwa majonzi yote mawili waliyapata Masahaba, na kwamba majonzi yalikuwa mengi; kama vile kuuawa ndugu zao, kushindwa na washirikina na majuto ya kuasi kwao.

Ili msihuzunike kwa mliyoyakosa,

Ambayo ni manufaa na ngawira.

Wala kwa yaliyowasibu,

Ambayo ni majeraha na kushindwa. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu amewaonyesha uchungu wa kuuliwa na kushindwa ili mjizoeze muweze kuvumilia shida na mashaka, na kuwa na subira juu ya twa'a ya Mwenyezi Mungu kwa hali yoyote itakavyokuwa natija, wala msi- huzunike kutokana na kukosa ngawira au masaibu yaliyowapata.

Yametangulia maelezo kwamba wapiga mishale waliacha sehemu zao kwa tamaa ya ngawira, jambo ambalo lilisababisha kushindwa kwa waislamu. Kwa hiyo, Mwenyezi Mungu anatanabahisha kuwa wachukue funzo kutokana na kushindwa huku na wala wasimkhalifu tena Mtume.

Na Mwenyezi Mungu ana habari za mnayoyatenda,

Maana yako wazi, na makusudio ni kuhimiza twa'a na kukaripia maasi.

Kisha baada ya majonzi akawateremshia utulivu, usingizi.

Waliokuwa pamoja na Mtume siku ya Uhud wamegawanyika sehemu mbili, kuna wale waliokuwa waumini wa kweli walioona uhakika kuwa uislamu utashinda tu, na kuwa Mwenyezi Mungu ataudhihirisha kuliko dini zote, kwa vile Mtume amewaelezea hilo. Ama kushindwa katika vita moja au zaidi hakuwatoi katika uislamu. Ambao walikuwa wakiitakidi hivi ndio wanaoambiwa: 'kisha baada ya majonzi akawateremshia utulivu' - usingizi. Kulala wakati wa misukosuko ni neema kubwa inayosahihisha masaibu mengi.

Uliofunika kundi katika nyinyi.

Ni kundi hili hili tulilolitaja ambalo watu wake walikuwa na busara katika imani. Kundi la pili, katika waliokimbia siku ya Uhud, ni wanafiki ambao Mwenyezi Mungu
amewataja kwa sifa hizi zifuatazo.

1). Na Kundi Jingine Limeshughulishwa Na Nafsi Zao.

Kundi hili halifunikwi na usingizi ili wapate mfazaiko. Wafasiri wamesema watu hao ni Abdullah bin Ubayya, Mut'ib bin Qushairy na wafuasi wao. Aya hii inafahamisha kwamba imani kamili inahitaji mtu kujishughulisha na mambo ya waisla- mu, asipofanya hivyo huyo ni mpungufu wa imani. Kuna Hadith isemayo: "Asiyejishughulisha na mambo ya waislamu basi si mwislamu."

2). Wakimdhania Mwenyezi Mungu Dhana Ya Kijinga Isiyo Ya Haki.

Kila anayekata tamaa kwa rehma ya Mwenyezi Mungu au akamdhania Mwenyezi Mungu kwamba amefanya yasiyotakikana kuyafanya ameleta dhana ya kijinga. Miongoni mwao ni wale waliosema siku ya Uhud, kwamba Muhammad angelikuwa Mtume, asingeshindwa na washirikina, hawajui au wanajitia kutojua kuwa vita ni kushinda na kushindwa na kwamba mambo huangaliwa mwisho wake.

3). Wakisema: Je, Tuna Chochote Katika Jambo Hili?

Yaani hatuna chochote, na Mwenyezi Mungu akamwamrisha Mtume wake kuwa- jibu kuwa hamna chochote kwa ajili yenu wala kwa mwengine, isipokuwa ni kwa Mwenyezi Mungu peke yake:

"Waambie mambo yote ni ya Mwenyezi Mungu ."

Sisi letu ni kusikiliza na kutii tu. Aya hii iko katika mfano wa Aya ya 128 ya Sura hii.

Huficha katika nafsi zao uongo na unafiki ambalo hawakudhihirishii wewe kama vile kuwa wao husema, lau ingelikuwa tunalolote katika jambo hili tusingeliuliwa hapa.

Yaani, lau tungelikuwa na kitu katika jambo hili tusingelitoka kwenda kupigana, na kama tungelitoka tungelipigana vizuri bila ya kuuliwa yeyote hapa; yaani, katika Uhud.

Kauli ya wanafiki kusema: 'Je tuna chochote katika jambo hili?' Kisha kusema: 'Lau tungelikuwa na kitu katika jambo hili.' Inafanana na mtu anayesema: 'Sina pesa, lau ningelikuwa nazo ningelifanya hivi na hivi.'

Waambie lau mngelikuwa nyumbani mwenu wangetoka ambao wameandikiwa kuuawa wakaenda katika maangamivu yao.

Hili ni jibu la aliyesema: 'Lau tungelikuwa na kitu tusingeliuawa.' Njia ya majibu ni kwamba, hadhari haiondoi kadari na kwamba mpangilio hauzuwii makadirio, ni sawa jambo la vita liwe lenu au lisiwe. Umekwisha tangulia ufafanuzi katika kufasiri Aya ya 145 ya Sura hii, kifungu 'Ajali imeandikwa.'

Na ili Mwenyezi Mungu ayajaribu yaliyomo vifuani mwenu na ayasafishe yaliyomo nyoyoni mwenu. Na Mwenyezi Mungu anayajua yaliyomo vifuani.

Hekima ya janga la siku ya Uhud ni upambanuzi wa kutambua mumin na mnafiki na kudhihirisha hakika yao kwa watubiao kwa Mwenyezi Mungu, kwa sababu Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa yaliyo katika nyoyo.

Kwa hivyo, mu'min anazidi imani kwa misukosuko na vile vile kwa malipo na thawabu. Na mnafiki anafichuka.

Siri Ya Kushindwa

Zaidi ya hayo yote ni kwamba lau mtu angeliishi maisha yake yote bila ya matatatizo na shida yoyote, ingelikuwa ni jambo la kushangaza katika akili za watu. Matatizo ndiyo yasafishayo nafsi na kuzikomaza, na kuvumilia shida kunamfikisha mtu kwenye malengo yake.

Uzoefu umeonyesha kuwa hakuna mpinganaji yoyote au mwanasiasa, mfanya biashara, mwanachuoni, mwana fasihi, mfanyi kazi, au mkulima, aliyefanikiwa katika malengo yake, isipokuwa kwa uthabiti na kuvumilia shida.

Lau tutafanya utafiti ili tujue siri ya kutofaulu katika maisha, tutaona kuwa ni udhaifu, kuhofia urefu wa njia na kutovumilia tabu na matatizo.

Nayasema haya nikiwa mimi mwenyewe nimefanya majaribio kutokana na uvu- milivu nimefikia ambayo sikuwa hata nikiyaota Al-hamdulillah. Nimejaribu nikawa na yakini kuwa subira inafanya miujiza na kwamba werevu bila ya subira na uvumilivu haufai chochote.

Hakika wale waliogeuka siku yalipokutana makundi mawili, shetani ndiye aliyewatelezesha kwa sababu ya baadhi ya waliyoyafanya. Na Mwenyezi Mungu amekwishawasamehe; hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira, mpole .

Wengi wamesema kuwa Aya hii inawahusu wapiga mishale walioamrishwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w) wabakie sehemu zao ili kuwakinga waumini kwa upande wa nyuma, kisha wakaondoka wakidhania kuwa washirikina wameshindwa. Lakini Aya haikuwataja wapiga mishale na wengineo walioshindwa siku ya Uhud.

Hata hivyo kuenea kwake kunahusu waumini na wala si kwa wanafiki, kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu, amekwisha wasamehe kwa sababu Mwenyezi Mungu hawasamehi wanafiki wananong'ania unafiki wao ambao ni mbaya zaidi kuliko ushirikina wa waziwazi.

Kwa ufupi ni kwamba aliyeshindwa siku ya Uhud hana shaka na Mwenyezi Mungu na Mtume wake, isipokuwa alikimbia ama kwa tamaa au kutokua na subira na mshikamano, na mengineyo ambayo hawezi kujiepusha nayo asiyekuwa Masum, na ambayo hayana mfungamano na unafiki au shaka yoyote. Haya aliyasamehe Mwenyezi Mungu, hata kama ndiyo yaliyoleta yaliyotokea.

Imesemekana kwamba kauli ya Mwenyezi Mungu: Shetani ndiye aliyewatelezesha, kwa baadhi ya waliyoyafanya; ni kwamba Shetani aliweza kuwatelezesha kwa sababu ya dhambi walizozifanya kabla ya Uhud. Lakini haya ni kiasi cha kudhani tu. Lililo karibu zaidi ni kwamba kufanya, hapa ni ishara ya pupa yao na kutokuwa na subira.

Shetani alipoona hivi akaitumia nafasi na kuwahadaa kuwa wameshinda na kuwapofua kuwa mambo ni salama. Na wafasiri wote, watu wa sera na historia wameafikiana kuwa Imam Ali bin Abu Talib (a.s.) alikuwa ni mmoja wa waliobaki bila ya kukimbia.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَكُونُوا كَالَّذِينَ كَفَرُوا وَقَالُوا لِإِخْوَانِهِمْ إِذَا ضَرَبُوا فِي الْأَرْضِ أَوْ كَانُوا غُزًّى لَوْ كَانُوا عِنْدَنَا مَا مَاتُوا وَمَا قُتِلُوا لِيَجْعَلَ اللَّهُ ذَٰلِكَ حَسْرَةً فِي قُلُوبِهِمْ ۗ وَاللَّهُ يُحْيِي وَيُمِيتُ ۗ وَاللَّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ {156}

Enyi mlioamini msiwe kama wale waliokufuru na wakawasema ndugu zao, waliposafiri katika nchi au walipokuwa vitani: lau wangelikuwa kwetu wasingekufa na wasingeliuawa; ili Mwenyezi Mungu ayafanye hayo kuwa majuto katika nyoyo zao. Na Mwenyezi Mungu anahuisha na kufisha na Mwenyezi Mungu anaona mnayoyatenda.

وَلَئِنْ قُتِلْتُمْ فِي سَبِيلِ اللَّهِ أَوْ مُتُّمْ لَمَغْفِرَةٌ مِنَ اللَّهِ وَرَحْمَةٌ خَيْرٌ مِمَّا يَجْمَعُونَ {157}

Na kama mkiuawa katika njia ya Mwenyezi Mungu au mkifa, basi maghufira na rehma kutoka kwa Mwenyezi Mungu ni bora kuliko yale wanayoyakusanya.

وَلَئِنْ مُتُّمْ أَوْ قُتِلْتُمْ لَإِلَى اللَّهِ تُحْشَرُونَ {158}

Na kama mkifa au mkiuawa, nyote mtakusanywa kwa Mwenyezi Mungu.