Aya 130 – 133: Msile Riba
Maana
Enyi ambao mmeamini! Msile riba ziada juu ya ziada. Na mcheni Mwenyezi Mungu ili mpate kufaulu.
Wafasiri wametaja njia nyingi za kuiunganisha Aya hii na iliyo kabla yake. Nasi tumeshawahi kueleza mara nyingi kwamba miongoni mwa desturi ya Qur'an ni kuchanganya baadhi ya hukumu na hukumu nyingine. Zaidi ya hayo ni kwamba Aya zake zimeteremshwa kwa vipindi na kwa matukio mbali mbali.
Wametoa dalili baadhi kwa Aya hii kwamba riba iliyo haramu ni riba iliyo maradufu. Ama isiyokuwa maradufu, basi si haramu; kutokana na neno ziada juu ya ziada.
Ilivyo hasa ni kwamba riba ni haramu kwa mafungu yake yote na daraja zake zote. Umaradufu si sharti la ukatazo, isipokuwa ni kuonyesha vile walivyokuwa wakifanya riba wakati wa ujahiliya. Zaidi ya hayo, ni kuweko Hadith na kuweko 'ijma', kwamba riba chache ni haramu kama ilivyo nyingi. Chochote ambacho wingi wake ni haramu, basi uchache wake pia ni haramu; iwe ni riba au si riba.
Mwenye Tafsir Al-Manar amerefusha ufafanuzi alipofasiri Aya hii. Mwisho akamalizia kuwa riba iko mafungu mawili: Fungu la kwanza, ni riba ya muda; kwa mfano kushindwa mtu kulipa deni lake katika muda wa deni, wakaafikiana mdai na mdaiwa kuwa aongeze muda wa kulipa na aongeze mali.
Yaani kila unapozidi muda ndipo mali ya kulipa inavyozidi. Akaendelea kusema mwenye Al-Manar: "Aina hii ya riba ni haramu hiyo yenyewe".
Fungu la pili, ni riba ya ziada kwa mfano kutoa mtu shillingi 100 kwa kutaka kulipwa shillingi 110. Anasema mwenye Al-Manar kuwa riba hii, yenyewe sio haramu, isipokuwa ni haramu kwa sababu ya kufikia haramu; yaani kwa kuhofia kuwa riba ya muda ambayo ni haramu.
Kwa maneno mengine ni kuwa riba ya muda ni haramu, kama lengo na riba ya ziada ni haramu kama njia ya kufikia lengo.
Kisha akaendelea kusema: "Riba ya ziada ni halali kwa dharura, bali hata kwa kuwa na haja; kama alivyosema Ibn Al-qayyim."
Hebu tuangalie maelezo yafuatayo:
(i) Imethibiti katika Qur'an na Hadith kwamba aina zote za riba ni haramu bila ya kutofautisha kuwa ni muda au la.
(ii) Kusema: "Bali kwa haja pia," ni katika kuteleza kwa kalamu. Kwani, ni dharura tu ndiyo ihalalishayo haramu. Ama haja hapana. Kuna tofauti kati ya haja na dharura, ni kwamba haja mtu anaweza asihitaji, japokuwa kwa kuivumilia. Ama dharura ni lazima kutekelezwa tu.
(iii) Dharura hapa haiwezi kupatikana kabisa. Si kwa mpokeaji wala kwa mtoaji. Mpokeaji riba, hana dharura yoyote. Kwa sababu anacho kitu cha kujisaidia japokuwa kwa siku moja (ndio maana akakopesha), ama yule mtoaji riba, ikiwa dharura imemfanya akope, basi haiwezi kumfanya atoe (yeye mwenyewe hana ndio maana akakopa). Na hilo si halali hata kama ataweka sharti, kwa sababu, sharti limebatilika. Na kama akichukua kwa nguvu, basi si halali kwa mchukuaji. Kwa sababu huko ni kula mali kwa batili.
(iv) Hebu tuseme, dharura inawezekana kwa anayepokea riba; itakuwa imeondoa hukmu tu, lakini maudhi hayajaondoka. Kwa mfano mwenye njaa ya kushikika akiiba mkate bila shaka atakuwa ameondokewa na hukmu ya kupata dhambi lakini maudhui ya kurudisha thamani ya mkate bado yapo. Yaani analo jukumu la kumlipa mwenye mkate atakapokuwa na uwezo. Na mwenye kuhalalisha kuchukua riba kwa dharura hawezi kuwajibisha kuirudisha kwa mwenyewe ikiondoka shida.
Tumezungumza kwa ufafanuzi kuhusu riba katika Aya ya 275 Sura ya Baqara
Na mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume ili mpate kurehemiwa.
Hapa kuna ufahamisho wa mambo mawili: Kwanza, kula riba ni kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume. Pili: mtu hapati rehema ya Mwenyezi Mungu kwa hali yoyote.
Na harakisheni kuomba msamaha kwa Mola wenu na pepo ambayo upana wake ni mbingu na ardhi; imeandaliwa wamchao Mungu.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kukataza kula riba, kuhadharisha na moto na kutoa mwito wa taqwa na kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume; baada ya yote haya ameamrisha kufanya haraka mambo ya kheri ambayo yanawajibisha radhi ya Mwenyezi Mungu na pepo yake. Heri na mambo mema zaidi ni kuhurumiana, kusaidiana na kutoa mali kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mtukufu; kama itakavyoeleza Aya ifuatayo: Ama kauli Yake: Upana wake ni mbingu na ardhi; ni fumbo la ukubwa.
الَّذِينَ يُنْفِقُونَ فِي السَّرَّاءِ وَالضَّرَّاءِ وَالْكَاظِمِينَ الْغَيْظَ وَالْعَافِينَ عَنِ النَّاسِ ۗ وَاللَّهُ يُحِبُّ الْمُحْسِنِينَ {134}
وَالَّذِينَ إِذَا فَعَلُوا فَاحِشَةً أَوْ ظَلَمُوا أَنْفُسَهُمْ ذَكَرُوا اللَّهَ فَاسْتَغْفَرُوا لِذُنُوبِهِمْ وَمَنْ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ إِلَّا اللَّهُ وَلَمْ يُصِرُّوا عَلَىٰ مَا فَعَلُوا وَهُمْ يَعْلَمُونَ {135}
أُولَٰئِكَ جَزَاؤُهُمْ مَغْفِرَةٌ مِنْ رَبِّهِمْ وَجَنَّاتٌ تَجْرِي مِنْ تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا ۚ وَنِعْمَ أَجْرُ الْعَامِلِينَ {136}