Aya 110-111: Umma Wa Muhammad
Maana
Mmekuwa ni umma bora mliotolewa kwa watu, mnaaamrisha mema na kukataza maovu na mnamwamini Mwenyezi Mungu
Kuna njia kadhaa kuhusu Aya hii, kama ifuatavyo:
1) Katika makusudio ya umma, hakuna mwenye shaka kuwa makusudio ya umma hapa ni Umma wa Muhammad (s.a.w), kwa dalili ya mfumo wenyewe wa maneno ulivyo na mtiririko wa misemo inayoelekezwa kwa waumini; kama vile; "Enyi ambao mmeamini mcheni Mwenyezi Mungu. Na shikamaneni na kamba ya Mwenyezi Mungu. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu kwenu …" Mpaka kufikia kauli yake Mwenyezi Mungu: "Mmekuwa ni umma bora."
2) Je, makusudio ni waislamu wote katika wakati wote, au ni kuwahusu wale walio kuwa katika siku za kwanza za uislamu kama vile Masahaba na waliofuatia (tabiina)?
Jibu:Kuainisha makusudio ya umma hapa, kunahitaji kujua makusudio ya herufi kana (kuwa) ambayo ilivyo ni kuwa inahitaji isimu na habari yake. Pia hiyo kana inafahamisha kufanyika kitendo wakati uliopita, lakini haielezi ni wakati gani kimefanyika hicho kitendo wala kuwa kinaendelea au la.
Isipokuwa hilo linaweza kufahamika kutokana na vitu vingine vilivyo pamoja nayo kimaneno au hali ilivyo. Kwa mfano kusema, Zaid alikuwa ni mwenye kusimama. Hapo inachukuliwa kutendeka tendo la kusimama na kuisha bila kuendelea. Yaani Zaid, hakuwa ni mwenye kusimama, basi akasimama kipindi fulani bila ya kuen- delea kusimama maisha. Lililofahamisha hilo ni neno mwenye kusimama, yaani hawezi kusimama maisha.
Lakini kama tukisema Mwenyezi Mungu amekuwa ni Mwingi wa maghufira Mwenye kurehemu, hapo hali inafahamisha kudumu kwa tendo lenyewe, kwa sababu rehema na maghufira haviepukani na dhati yake Mwenyezi Mungu, na dhati yake Mwenyezi Mungu Mtukufu ni ya milele na milele.
Kwa kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameufungamanisha ubora wa umma na kumwamini kwake, na kuamrisha mema na kukataza maovu, basi maana ya Aya yanakuwa ni: Enyi waislamu! Msiseme tu sisi ni umma bora mpaka muamrishe na kukataza maovu; na kwamba sifa hii ya ubora itawaondokea mara tu mnapopuuza hilo.
Kwa hivyo basi kana hapa inakuwa ni kamilifu, sio pungufu; yaani haihitaji khabar. Kwa maana hayo makusudio ni waislamu wote1
3).Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu 'mliotolewa kwa Watu' inafahamisha kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amemleta Muhammad na umma wake (s.a.w) ushinde umma zote za mwanzo ukiwa umechukua Kitabu cha Mwenyezi Mungu mkono mmoja na Hadith za Mtume kwenye mkono mwingine, huku ukiwalingania vizazi vishikamane na vitu viwili hivyo na kuvitegemea kwa itikadi, sharia na maadili.
Kwa sababu ndio marejeo pekee yanayoweza kuhakikisha ufanisi wa mambo yote, kudhamini maisha ya kila mtu na kufungua uwanja wa wenye uwezo wa kufanya ijitihadi kwa misingi ya usawa, amani na uhuru wa watu wote.2
Aya hii katika madhumuni yake inaafikiana na Aya isemayo: "Tumewafanya ni umma wa wastani, ili muwe mashahidi juu ya watu na Mtume awe shahidi juu yenu." (2:143)
Ikiwa waislamu hawatafanya harakati zozote za kulingania kwenye kheri au kuamrisha mema na kukataza mabaya, basi sifa za uongozi zitawaondokea na watakuwa na haja ya kiongozi atakayewaamrisha mema na kuwakataza maovu.
Ulikuwepo wakati ambapo waislamu walikuwa na harakati hizi. Wakati huo walikuwa wakistahili kuwa viongozi wa umma zingine; kisha wakapuuza; wakaendelea hivyo mpaka wakawa wanakataza mema na kuamrisha maovu; kama tuonavyo sasa.
Leo vijana wamekuwa wanajivua kabisa na dini na hulka njema. Wakimwona mtu anaswali au kufunga husema kwa dharau: "Bado kuna Swala na Saumu katika karne ya ishirini?"
Mwenye Tafsir Al-Manar, katika kufasiri Aya hii, anasema: "Kwa kweli hasa ninasema, haukuzimika ubora wa umma uliotolewa kwa watu, mpaka pale ulipoacha kuamrisha mema na kukataza mabaya.
Na haukuacha hivyo kwa kupenda au kupuuza amri ya Mwenyezi Mungu, bali ni kwa kulazimishwa na ufedhuli wa Wafalme wa bani Umayya na waliofuata nyayo zao."
Kwa msingi vitu hutajwa kwa kinyume chake; kama ambavyo hutajwa kwa kifani chake, basi tutaleta Hadith tukufu aliyoitaja Hafidh Muhibbudin Attabari, amesema: "Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w) 'Mfano wa Ahlu bait wangu, ni kama safina ya Nuh mwenye kuipanda ataokoka, na mwenye kushikamana nayo ataokoka, na mwenye kuachana nayo ataghariki'".
Ama Hadith ya "Mimi nawaachia vizito viwili: Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Kizazi changu - Ahlul bait wangu," imepokewa na wapokezi 35 katika Masahaba.
Na lau wangeliamini watu wa Kitabu, ingelikuwa heri kwao.
Yaani lau watu waliopewa Tawrat na Injil, wangelimwamini Muhammad (s.a.w) ingelikuwa imani yao hiyo ni heri yao katika muda wa sasa na ujao.
Katika wao kuna wanaoamini na wengi wao ni wafasiki.
Yaani katika watu wa Kitabu kuna waliomwamini Muhammad (s.a.w); kama vile Abdullah bin Salam na watu wake, na wengineo katika wanaswara, na wengi wao walibaki katika ukafiri.
Neno Fasiq na Kafir yanapokezana maana, hutumiwa Fasiq kwa maana ya Kafiri na Kafir kwa maana ya Fasiq. Na Fasiq hapa ina maana ya kafiri.
Hawatawadhuru, isipokuwa kuwaudhi tu, na wakipigana nanyi watawakimbia
Madhara yako aina mbili: Kwanza, ni kiasi cha huzuni na kusikia uchungu tu, ambako kadiri siku zinavyokwenda nayo yanafutika; kama vile inavyotokea katika nafsi kwa kusikia habari mbaya. Pili, ni yale yanayogusa maisha na kuyumbisha; kama vile madhara yaletwayo na dola ya Israil ndani ya nchi ya Waarabu.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewabashiria maswahaba wa Mtume (s.a.w) kwamba watu wa Kitabu: Hawatawadhuru isipokuwa kwa maneno tu, kama vile uzushi na mabezo.
Ama katika uwanja wa vita, nyinyi ndio washindi. Amesema kweli Mwenyezi Mungu katika kiaga chake. Aliwapa ushindi waislamu wa mwanzo kwa wakristo na wengineo.
ضُرِبَتْ عَلَيْهِمُ الذِّلَّةُ أَيْنَ مَا ثُقِفُوا إِلَّا بِحَبْلٍ مِنَ اللَّهِ وَحَبْلٍ مِنَ النَّاسِ وَبَاءُوا بِغَضَبٍ مِنَ اللَّهِ وَضُرِبَتْ عَلَيْهِمُ الْمَسْكَنَةُ ۚ ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ كَانُوا يَكْفُرُونَ بِآيَاتِ اللَّهِ وَيَقْتُلُونَ الْأَنْبِيَاءَ بِغَيْرِ حَقٍّ ۚ ذَٰلِكَ بِمَا عَصَوْا وَكَانُوا يَعْتَدُونَ {112}
- 1. Maelezo haya yanafahamika zaidi kwa wajuao Nahau- Mtarjumu
- 2. Wajuzi wametunga vitabu kadhaa kuhusu maudhui haya. Baadhi ya watungaji ni watu wa nje, vingi katika hivyo vinatekeleza lengo; chenye faida zaidi - kwa maoni yangu - ni kijitabu cha Dkt Abdul-Wahid Wafi kiitwacho Al-musaawat fil-Islam. Ingawaje ni kidogo lakini kina mada nyingi na dalili nzito.