read

Aya 116 - 117: Ukafiri Haufai Kitu

Maana

Hakika wale ambao wamekufuru, haitafaa kitu mali yao wala watoto wao kwa Mwenyezi Mungu.

Amesema Razi na mwenye Tafsir Al-Manar: "Wametofautiana wafasiri katika makusudio ya ambao wamekufuru. Kundi moja likasema kuwa ni baadhi ya makafiri. Wengine wakasema ni makafiri wote.”

Ama tuonavyo sisi ni kwamba, makusudio ni kila mwenye kukhalifu haki na kuipinga kwa masilahi yake na ya watoto wake, na kuhofia mali yake na utajiri - vyovyote atakavyokuwa, Mwislamu au kafiri. Ni kweli kuwa tamko la Aya linawahusu makafiri lakini sababu inayowajibisha ambayo ni kutofaa kitu, inaenea kwa wote wanoikhalifu haki kwa msukumo wa hawaa zao; nao ndio wale aliowataja Mwenyezi Mungu (s.w.t.) katika Aya kadhaa kuwa wameiuza haki kwa thamani duni.

Mfano wa wanavyovitoa katika maisha haya ya dunia, ni kama mfano wa upepo wenye baridi kali uliofikilia shamba la watu waliodhulumu nafsi zao, ukaliangamiza.

Yaani wale ambao wanachanganya utajiri wa halali na haramu na kuihalifu haki kwa ajili ya utajiri na kuutumia kwa ajili ya jaha, na starehe zao bila ya kujali dini au maadili, hakika matumizi ya hawa yameangamiza akili zao na kuharibu maadili yao, sawa na upepo wenye baridi kali unavyoangamiza shamba lililotayarishwa kuwa na mazao.

Kama watapata faida siku chache kwa kustarehe na kutosheleza uchu wao, basi watakuwa wamejipatia hasara na kuziuza nafsi zao kwa shetani; na wao watapa- ta adhabu ya milele huko akhera.
Na Mwenyezi Mungu hakuwadhulumu, lakini wanajidhulumu wenyewe, kwa sababu wamejiiingiza kwenye matamanio wao wenyewe kwa hiyari yao.

Imam Ali (a.s.) anasema: "Watu duniani ni aina mbili: Mtu aliyeiuza nafsi yake ikamwangamiza (yaani ameiuza nafsi yake kwenye matamanio na hawaa zake), na mtu aliyeinunua nafsi yake akaiacha huru. (Yaani aliyeinunua nafsi yake na kuisafisha na matamanio.)"

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَتَّخِذُوا بِطَانَةً مِنْ دُونِكُمْ لَا يَأْلُونَكُمْ خَبَالًا وَدُّوا مَا عَنِتُّمْ قَدْ بَدَتِ الْبَغْضَاءُ مِنْ أَفْوَاهِهِمْ وَمَا تُخْفِي صُدُورُهُمْ أَكْبَرُ ۚ قَدْ بَيَّنَّا لَكُمُ الْآيَاتِ ۖ إِنْ كُنْتُمْ تَعْقِلُونَ {118}

Enyi ambao mmeamini Msiwafanye wasiri wasiokuwa katika nyinyi. Hawazembei kuwaharibia. Wanapendelea yanayowapa mashaka. Imedhihiri chuki katika vinywa vyao, na wayafichayo vifuani mwao ni makubwa. Tumewabainishia ishara ikiwa nyinyi ni wenye akili.

هَا أَنْتُمْ أُولَاءِ تُحِبُّونَهُمْ وَلَا يُحِبُّونَكُمْ وَتُؤْمِنُونَ بِالْكِتَابِ كُلِّهِ وَإِذَا لَقُوكُمْ قَالُوا آمَنَّا وَإِذَا خَلَوْا عَضُّوا عَلَيْكُمُ الْأَنَامِلَ مِنَ الْغَيْظِ ۚ قُلْ مُوتُوا بِغَيْظِكُمْ ۗ إِنَّ اللَّهَ عَلِيمٌ بِذَاتِ الصُّدُورِ {119}

Hivyo basi! Nyinyi ndio hao muwapendao hali wao hawawapendi, nanyi mwaviamini vitabu vyote. Na wakikutana nanyi husema: Tumeamini, na wanapokuwa faraghani huwaumia vidole kwa hasira. Sema: Kufeni na hasira zenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa yaliyo vifuani.

إِنْ تَمْسَسْكُمْ حَسَنَةٌ تَسُؤْهُمْ وَإِنْ تُصِبْكُمْ سَيِّئَةٌ يَفْرَحُوا بِهَا ۖ وَإِنْ تَصْبِرُوا وَتَتَّقُوا لَا يَضُرُّكُمْ كَيْدُهُمْ شَيْئًا ۗ إِنَّ اللَّهَ بِمَا يَعْمَلُونَ مُحِيطٌ {120}

Ukiwagusa wema unawasononesha, na kama likiwapata baya wanalifurahia. Na kama mkisubiri na mkaogopa, basi hila zao hazitawadhuru kitu. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kuyazunguka wayatendayo.