read

Aya 100-103: Kuwatii Makafiri

Maana

Enyi mlioamini! Mtakapotii kikundi katika watu wa Kitabu, watawarudisha kuwa makafiri baada ya kuamini kwenu.

Katika Aya mbili zilizotangulia, Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewahadharisha watu wa Kitabu kuipinga haki pamoja na kuwazuia waumini na njia Yake Mwenyezi Mungu.
Katika Aya hii, Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anawahadharisha waumini wasiwasikilize makafiri katika watu wa Kitabu wanaojaribu kuwapoteza waumini na kuwafitini na dini yao.

Imepokewa Riwaya kwamba, sababu za kushuka Aya hii ni kuwa baadhi ya mayahudi walikusudia kuirudisha tena fitna iliyokuwepo baina ya kabila la Ansar na Khazraj wasiwe na umoja baada ya Mwenyezi Mungu kuwaweka pamoja kwenye Uislamu.
Kwa hiyo, makafiri wakawa wanawakumbusha uadui na mapigano waliyokuwa nayo wakati wa ujahiliya. Hasa siku ya vita ya Bughat ambayo Aus na Khazraj waliuana, na ushindi ukawa wa Aus. Mori ukawapanda wakawa karibu wapigane kama si kuwahi Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w).

Aya inafungamana na tukio hili, kama ambavyo inafungamana na jaribio la wahu- biri wa Kikristo wakati huu; na majaribio yote ambayo baadhi ya watu wa Kitabu na wengineo katika kutawanya umoja wa waislamu na kuwaepusha na dini yao, uzalendo wao, na uhuru wao na kuwa windo la kila mnyang'anyi.

Haya ndiyo wayafanyao wakoloni wa Kimagharibi kwa waarabu. Na kazi hiyo hawaifanyi peke yao, bali wanashirikiana na vibaraka duni ambao wanawatii na kuwafuata; na waliokufuru dini yao baada ya kuamini na kuiuza nchi yao.

Kwa hivyo basi, Aya inafungamana na vibaraka hawa na pia inafungamana na wanaohubiri fitina na ufisadi na wakapendelea ukafiri na upotevu. Ni sawa wawe ni katika watu wa Kitabu au wengineo; wa Mashariki na Magharibi.

Vile vile, Aya hii inafungamana na wanawake wetu wanavyoiga wanawake wa kimagharibi katika kujiremba na kujipodoa, na vijana wetu katika kudharau dini na mwendo wa dini. Vile vile desturi zote za madhara na haramu tulizoziiga kutoka kwa wageni.

Aya kwa dhahiri inakataza kuwatii makafiri katika kufuru na kurtadi. Lakini, linalosababisha hilo linaenea katika kila uigaji unaomkasirisha Mwenyezi Mungu na Mtume.

Na vipi mnakufuru na nyinyi mnaosomewa Aya za Mwenyezi Mungu na Mtume Wake mnaye.?

Yaani, haitakikani kwa Mwislamu kuathirika na kuwa katika upotevu wa wapoteza- ji, na kuwafuata makafiri katika desturi zao na hulka zao wakati ambapo yeye mwislamu anasoma Qur'an Tukufu na kumsikiliza Mtume Mtukufu, anayembain- ishia haki na kumuondolea kila shubha.

Anasema Nidhamuddin Al-Hasan Muhammad Annaisaburi katika Tafsir, Gharaibul-Qur'an: "Ama Kitabu kitabaki milele. Na Mtume (s.a.w) ingawaje amekwenda kwenye rehema ya Mwenyezi Mungu, lakini nuru yake imebaki. Kwa sababu, kizazi na warithi wake wanakaimu nafasi yake. Kwa sababu hii ndipo Mtume akasema: "Mimi ninawaachia vizito viwili ambavyo kama mkishikamana navyo hamtapotea: Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu."

Na mwenye kushikamana na Mwenyezi Mungu, basi ameongozwa katika njia iliyonyooka.

Kushikamana na Mwenyezi Mungu ni kushikamana na dini; dini mbele ya Mwenyezi Mungu ni uislamu, nayo ndiyo hasa njia iliyonyooka. Makusudio ni kuwa mwenye kushikamana na Mwenyezi Mungu kwa haki kabisa, hawezi wala hataweza kuuwacha uislamu kwa namna yoyote ya majaribio na hadaa zitakavyokuwa.

Unaweza kuuliza: Imekuja Aya isemayo "Hakika Mola wangu yuko juu ya njia iliyonyooka." (11:56) Na wewe unafasiri kuwa njia iliyonyooka ni uislamu. Kwa hiyo itakuwa Mwenyezi Mungu yuko kwenye dini ya kiislamu.

Jibu: Hakika njia iliyoonyooka ikinasibishwa kwa mja, inakusudiwa uislamu. Ama ikinasibishwa kwa Mwenyezi Mungu inakusudiwa uadilifu na hekima; yaani yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu anapanga mambo kwa uadilifu na hekima Yake.
Enyi mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu ipasavyo kumcha; wala msife isipokuwa mmekuwa waislamu.

Kila mwenye kufanya ya wajibu na kujiepusha na mambo ya haramu, basi ndio amemcha Mwenyezi Mungu ipasavyo kumcha. Haya ndiyo maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu: "Mcheni Mwenyezi Mungu muwezavyo" (64:16)
Kwa sababu, lisilowezekana halikalifiwi na sharia. Na kila lisilowezekana kukalifiwa, basi liko nje ya kumcha Mwenyezi Mungu. Ama kauli yake Mwenyezi Mungu "Msife isipokuwa mmekuwa waislamu;" ni kukataza kuacha uislamu na kuamrisha kuwa imara nao mpaka siku ya kifo.

Na shikamaneni na kamba ya Mwenyezi Mungu nyote wala msifarikiane.

Kamba ni maarufu; na makusudio yake hapa ni uislamu. Maana ya Aya nzima, ni kuwa maadam waislamu ni wafuasi wa dini moja, Mtume mmoja na Kitabu kimoja, basi ni juu yao wote kuuchunga mfungamano huu wa kidini ambao ndio wenye nguvu zaidi kuliko mfungamano wa nasaba, na kuwa na hima nao; wala wasigawanyike vikundi.

Unaweza kuuliza: Je, mwito huu wa muungano wa kidini si aina ya ubaguzi wa dini?

Jibu: Hapana, mwito huu wa mshikamano wa wafuasi wa dini moja ni sawa na mwito wa mshikamano wa wanachama wa chama kimoja, au wa wafamilia moja. Mshikamano huu haulazimishi kuwabagua wengine.

Bali ni kinyume na hivyo katika uislamuu, ambapo unatoa mwito wa kuwapenda na kuwahurumia watu wengine bila ya kuangalia dini zao, fikra zao au kabila zao. Kwa hivyo basi undugu wa Kiislamu ni nguzo ya udugu wa kibinadamu.

Kwa ujumla ni kwamba kundi ambalo ni wajibu kusaidiana nalo, ni lile lililojiku- sanya na kusaidiana katika jambo lililo na radhi ya Mwenyezi Mungu na masilahi ya watu. Ama kukutana kusikokuwa na faida yoyote ya kuridhisha hakutakikani.

Imam Ali (a.s.) anasema: "Utengano ni kwa watu wa batili hata wakiwa wengi. Na kuungana ni kwa watu wa haki hata wakiwa wachahe." Na hiyo ndiyo tafsir ya Hadith mashuhuri: "Msaada wa Mwenyezi Mungu uko pamoja na wengi." Yaani kuwahusu wanaojumuika na kusaidiana kwa jambo la haki. Ama ikiwa ni kwa jambo la batili; basi hawatakuwa na yeyote zaidi ya shetani.

Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu juu yenu mlipokuwa maadui naye akaziunganisha nyoyo zenu; hivyo kwa neema yake mkawa ndugu.

Mwenyezi Mungu anawakumbusha waislamu wa kwanza vile walivyokuwa na misukusuko ya vita, bughudha na vita vya kuendelea, kama vile vita vya Aus na Khazraj vilivyodumu kwa muda wa miaka mia moja na ishirini, kama ilivyoelezwa kwenye Tafsir Tabari. Basi Mwenyezi Mungu akaziunganisha nyoyo zao kwa baraka ya uislamu mpaka wakawa ni ndugu wanaohurumiana na kunasihiana.

Jafar bin Abu Talib katika mazungumzo yake na Najjash alimwambia: "Tulikuwa watu wa ujahilia (ujinga) tukiabudu masanamu, tukila mizoga, tukifanya maovu, kuvunja undugu, kumfanyia uovu jirani na mwenye nguvu akimuonea mnyonge.

Tulikuwa hivyo mpaka Mwenyezi Mungu akatuletea Mtume atokanaye na sisi; tunayemjua nasaba yake, ukweli wake, uaminifu na usafi wake.

Akatulingania kwa Mwenyezi Mungu ili tumwabudu yeye peke yake na tuachane na kuabudu wasiokuwa Yeye - mawe na masanamu. Akatuamrisha kusema kweli, kutekeleza amana, kuunga undugu, kumfanyia wema jirani na kujizuia na haki za watu na damu (zao).

Akatukataza kufanya maovu, kusema uongo, uzushi, kula mali ya yatima na kuwavunjia heshima wanawake wanaojistahi. Akatuamrisha tumwabudu Mwenyezi Mungu na kutomshirikisha na chochote. Pia akatuamrisha kuswali, kutoa Zaka na kufunga."

Na mlikuwa ukingoni mwa shimo la moto naye akawaokoa nalo.

Yaani mlikuwa karibu na moto wa Jahannam, kwa ukafiri wenu, Mwenyezi Mungu akawaokoa nao kwa baraka ya Muhammad (s.a.w).

وَلْتَكُنْ مِنْكُمْ أُمَّةٌ يَدْعُونَ إِلَى الْخَيْرِ وَيَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنْكَرِ ۚ وَأُولَٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ {104}

Na liwepo miongoni mwenu kundi lenye kulingania kwenye heri, na kuamrisha mema na kukataza maovu. Na hao ndio wenye kufaulu