Aya 149-151: Mkiwatii Ambao Wamekufuru
Lugha
Makusudio ya neno sultan ni hoja, limetumika neno hilo kwa vile hoja ina nguvu za kuikinga batili.
Maana
Enyi ambao mmeamini! Mkiwatii ambao wamekufuru watawarudisha nyuma.
Sheikh Maraghi katika kufasiri Aya hii anasema: "Makusudio ya 'ambao wamekufuru' ni Abu Sufyan, kwa sababu yeye ndiye mzizi wa fitina."
Kila mtu, awe na haki au batili, anataka watu wote wawe upande wake. Tofauti ni kwamba twaa ya mbatilifu ni hasara na madhara. Na twaa ya mwenye haki ni faida na manufaa, kwa ajili hii ndipo Mwenyezi Mungu akawahadharisha waumini na makafiri.
Bali Mwenyezi Mungu ndiye mlinzi wenu naye ndiye bora wa wasaidizi.
Mu'min hafikirii kumtii kafiri na kumpenda wala hababaishwi na hadaa zake au kumfanya ni mlinzi, isipokuwa Mungu tu peke yake ndiye anayemnusuru na maadui. Na ambaye Mwenyezi Mungu ndiye msaidizi wake, hatahitajia rafiki wala msaidizi mwingine.
Tutatia hofu katika nyoyo za ambao wamekufuru kwa sababu ya kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kitu ambacho hakukiteremshia hoja.
Yaani, enyi waislamu! Msiwaogope washirikina kwa sababu ya wao kuwashinda katika vita vya Uhud, kwani Mwenyezi Mungu atatia hofu katika nyoyo zao kutokana na nyinyi, kwa sababu wao wamemfanya Mwenyezi Mungu kuwa ana washirika bila ya dalili yenye mwelekeo, isipokuwa ni kwa kufuata tu.
Inasemekana kuwa Abu Sufian na washirikina wenzake walipoondoka Uhud kuelekea Makka, walisema: "Tumefanya vibaya sisi; tumewaua mpaka wakabakia wanyonge halafu tukawaacha, tuwarudieni! Tuwamalize" Walipoazimia hivyo Mwenyezi Mungu akawatia hofu, mpaka wakaacha yale waliyoyakusudia." Ni sawa sababu hii iwe ndiyo ya kushuka Aya au la, lakini tamko la Aya halikatai hayo.
وَلَقَدْ صَدَقَكُمُ اللَّهُ وَعْدَهُ إِذْ تَحُسُّونَهُمْ بِإِذْنِهِ ۖ حَتَّىٰ إِذَا فَشِلْتُمْ وَتَنَازَعْتُمْ فِي الْأَمْرِ وَعَصَيْتُمْ مِنْ بَعْدِ مَا أَرَاكُمْ مَا تُحِبُّونَ ۚ مِنْكُمْ مَنْ يُرِيدُ الدُّنْيَا وَمِنْكُمْ مَنْ يُرِيدُ الْآخِرَةَ ۚ ثُمَّ صَرَفَكُمْ عَنْهُمْ لِيَبْتَلِيَكُمْ ۖ وَلَقَدْ عَفَا عَنْكُمْ ۗ وَاللَّهُ ذُو فَضْلٍ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ {152}