Aya 159-160: Kama Ungekuwa Mkali
Maana
Kwa sababu ya rehma itokayo kwa Mwenyezi Mungu, umekuwa mpole kwao.
Katika Aya zilizotangulia Mwenyezi Mungu alikuwa akiwambia Masahaba wa Mtume (s.a.w); katika Aya hizi, Mwenyezi Mungu anamwambia Mtume wake mtukufu (s.a.w).
Yametangulia maelezo kwamba Waislamu walikwenda kinyume na amri ya Mtume (s.a.w) siku ya vita vya Uhud, na natija ilikuwa ni kushindwa wakamwacha Mtume kwenye shida, ambapo vita iliuma mchanga mpaka Mtume akajeruhiwa na maadui, akavunjwa meno ya mbele, ukachanika uso wake na ukawa unachuruzika damu. Wakati huo akiwa bado na uthabiti pamoja na watu wachache, akaita wale wanaokimbia lakini wasimwitike.
Baada ya kwisha vita waislamu walirudi kwa Mtume (s.a.w), lakini Mtume hakuwalaumu ingawaje walikuwa wakistahili hivyo. Bali aliyapuuza, akawapokea na akazungumza nao kwa upole. Haukuwa upole huu ila ni rehma kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Ikiwa Mwenyezi Mungu amemsifu Mtume wake kuwa ni mvunja ghadhabu kwa watu wake pamoja na ubaya wao, basi itakuwa yeye mwenyewe Mwenyezi Mungu ni zaidi. Imam Ali anasema, katika kumsifu Mwenyezi Mungu: "Ghadhabu haimshughulishi kuwacha rehma yake." Na katika dua zilizopokewa imesemwa: "Ewe ambaye rehma yake imetangulia ghadhabu yake."
Kisha Mwenyezi Mungu anabainisha hikma ya upole kwa Mtume wake mtukufu kwa kusema: Lau ungelikuwa mkali mwenye moyo mgumu bila shaka wangelikukimbia, na maadui wangelikucheka na ujumbe kwako usingelitimu na kuenea.
Kwa hakika makusudio ya kutumwa Mtume ni, kuongoza viumbe kwenye haki, nao viumbe hawawezi kumsikiliza isipokuwa yule mwenye upendo ambaye nafsi zao zinamtegemea, na nafsi haitegemei isipokuwa kwa aliye na moyo rahim; kama moyo wa Muhammad (s.a.w.w) ambao ulikunjuka kwa watu wote hata kwa wanyama. Alisema kuhusu wanyama: "mnapochinja chinjeni vizuri, anoe mmoja wenu kisu chake na ampe raha anayemchinja" Akasema tena: "Kuna malipo katika kumhudumia kila mwenye ini la joto." Hakika Mwenyezi Mungu alimsamehe Mumis kwa sababu alimwokoa mbwa asife na kiu."
Basi wasamehe katika mambo yanayokuhusu wewe ambapo walikuacha wakati wa dhiki na shida mpaka ukajeruhiwa. Na uwaombee maghufira katika haki inayomhusu Mungu Mtukufu pale walipomwasi na kuacha vita. Kauli yake hii Mwenyezi Mungu inafahamisha kimaana kuwa Yeye amekwisha wasamehe na kuwaghufuria, vyenginevyo asingemwamrisha Mtume wake hilo.
Na ushauriane nao katika mambo.
Arrazi anasema: Maulama wengi wamesema kuwa alif na lam hapa sio ya kijumla bali ni mahsusi tu, na kilichohusishwa katika Aya hii ni vita na kupambana na maadui. Kwa hivyo ushauri unahusika na vitu tu." wengine wakasema kuwa inakusanya mambo yote ya kidunia.
Kisha Razi akimnukuu Shafi anasema; kuwa mshawara hapa ni mapendekezo, sio wajibu, na kwamba hekima ya ushauri ni kuzituliza nyoyo zao tu. Kauli hii iko karibu na uzingatio. Kwa sababu, Maasum hawezi kutaka mwongozo kwa asiyekuwa Maasum.
Vyovyote itakavyokuwa ni kwamba dini kwa itikadi yake na sharia yake ni wahyi bila ya kuweko rai ya yeyote, hata Mtume mwenyewe ni mfikishaji tu na wala sio mtunga sharia. Na Mwenyezi Mungu amemwambia Mtume wake: "Huna lako jambo.." (3: 128) "Wewe ni muonyaji tu." (79:45)
Utakapoazimia, basi mtegemee Mwenyezi Mungu.
Yaani ukiazimia kufanya jambo kutokana na ushauri au usiokuwa ushauri, basi litekeleze kwa kufanya maandalizi kwa kutegemea msaada wa Mwenyezi Mungu katika kufaulu na kushinda.
Akiwasaidia Mwenyezi Mungu, hapana wa kuwashinda.
Msaada wake Mwenyezi Mungu Mtukufu unakuwa pamoja na kutekeleza sababu alizozijaalia Mwenyezi Mungu kuwa ni njia ya kufikia ushindi, ambazo pamoja na kumtegemea Mwenyezi Mungu, ni kukamilika maandalizi ambako Mwenyezi Mungu amekudokeza pale aliposema: "Na waandalieni nguvu muwezavyo" (8:60)
Na kama akiwaacha ni nani tena atakayewasaidia baada yake?
Mwenyezi Mungu huwaacha wale ambao hawana mjumuiko wa kheri. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: "Wala msizozane, msije mkalegea na kupoteza nguvu zenu." (8:46)
Kwa ufupi ni kwamba kukamilisha maandalizi bila ya ikhlas hakuna faida yoyote, kama ilivyokuwa kwa Waislamu siku ya vita vya Hunain: "Na siku ya Hunain, ulipowapandisha kichwa wingi wenu, lakini haukuwafaa kitu, na ardhi ikawa finyu juu yenu ingawaje ni pana, kisha mkageuka mkarudi nyuma." (9:25)
Kama ambavyo ikhlas nayo bila ya maandalizi haifai kitu. Mwenye kutekeleza yote mawili (maandalizi na kumtegemea Mwenyezi Mungu), basi hana wa kumshinda. Kwa sababu Mwenyezi Mungu yuko pamoja naye; "panga na utawakali."
Siri Ya Utukufu Wa Muhammad
Abdullah, baba yake Mtume, alisafiri kwenda Sham (Syria ya sasa) kibiashara wakati mama yake akiwa na mimba yake. Katika safari ya kurudi, Abdullah aliwapitia wajomba zake wa ukoo wa Najjar waliokuwa Madina, akaugua huko na kufariki. Kwa hivyo akafariki akiwa fakiri bila ya kumwachia mwanawe kitu cho- chote zaidi ya ngamia watano, kondoo wachache na mjakazi wa kihabeshi aliyekuwa akiitwa Ummu Ayman ambaye alikuwa ni mmoja kati ya walezi wake. Mtume (s.a.w) alizaliwa Makka mwezi wa Rabi-ul-Awwal (mfungo sita), mwaka wa ndovu, sawa na mwezi wa Agosti 570A.D. kama ilivyotajwa.
Kunyonyeshwa Kwake Na Malezi Yake
Mtume alinyoyeshwa na Thuwayba kisha akanyonyweshwa na Halima Saadiya. Mama yake alifariki akiwa na miaka 6 na babu yake alifariki akiwa na miaka 8. Kisha akalelewa na ami yake, Abu Talib na akamkinga hadi pumzi yake ya mwisho. Aliishi naye miaka 42. Mtume aliishi miaka 63 ambayo 53 aliimalizia Makka na 10 Madina.
Wasifu
Kiumbo alikuwa si mrefu si mfupi, alikuwa na kichwa kipana. Uso wa duara na mpana. Nyusi zake zilikuwa ziko karibu kuungana, katikati yake palijitokeza mshipa, ambao anapokasirika hufura na kuwa mwekundu.
Vilevile alikuwa na macho meusi na kope ndefu. Pua iliyochongoka, mwenye meno mazuri, ndevu nyingi na kifua kipana. Pia alikuwa na mikono mirefu, na alikuwa na weupe uliochanganyika na wekundu, na alikuwa na mwili mkakamavu.
Akasirikapo, uso wake huiva na anapohuzunika mara nyingi hushika ndevu zake. Alipokuwa akizungumza huashiria kwa kiganja chake chote na anapostaajabu hukigeuza. Anapozama katika mazungumzo hupiga dole lake gumba la kushoto kwenye kiganja chake cha kulia.
Akiona jambo linalomchukiza alikuwa akigeuza uso wake na anapochemua (kupiga chafya) hujifunika. Alikuwa akicheka mpaka yakaonekana magego yake na alikuwa mwingi wa tabasamu.
Alikuwa hakatai chakula kinachopatikana wala hakalifishi kinachokosekana. Na kama hapati chakula, huvumilia mpaka kufikia hatua ya kufunga jiwe tumboni mwake kwa sababu ya njaa.
Alikuwa anaweza kukaa mwezi mzima bila ya kupa- ta mkate. Siku moja alimtuma mtu kwenda kumkopea kwa myahudi mmoja, yule myahudi akakataa na akasema: "Muhammad hana shamba wala mifugo, ni nani atakayelipa?"
Vilevile Mtume hakuwa na kanzu, juba au shuka zaidi ya moja kwa wakati mmoja. Pia hakuwa na viatu zaidi ya jozi moja. Alikuwa na mkeka anaoulalia usiku na kuukalia mchana, mpaka akafanya alama mbavuni. Na alikuwa na mto wa ngozi uliojazwa ndifu.
Wakati wa kulala alikuwa akiweka mkono wake chini ya shavu lake na hulalia upande wake wa kulia. Alikuwa akijishonea viatu na kanzu yake inapopasuka, na alikuwa akipanda punda.
Ingawaje utajiri wa Bara-arabu ulikuwa kwenye madaraka yake lakini alikuwa akitoa kila kinachomfikia akiwa ni mtu asiyeogopa ufukara, kama alivyosifiwa na bedui mmoja.
Mtume Na Ufukara
Lakini yote hayo hayana maana kwamba yeye alikuwa akiupenda ufukara na kuuridhia. Hapana! Bali alikuwa akiomba kuhifadhiwa nao na akisema: "Ewe Mwenyezi Mungu! Ninataka hifadhi kwako kutokana na ufukara, uchache wa mali na udhalili. Na ninataka hifadhi kwako na kushindwa na uvivu. Na ninataka hifadhi na kudhulumu au kudhulumiwa."
Mtume hakuwa akiupenda ufukara na kuuridhia, lakini maadamu alikuwa akiishi katika jamii fakiri, basi njia bora ni kuishi upande wa ufakiri na kuwa sawa nao katika ulaji, mavazi na mahali pa kuishi. Wala hakuna kosa kubwa na dhulma kuliko kuwa kiongozi ameshiba na raia wake mmoja ana njaa.
Amirul-Muminiin Ali anasema: "Hakika Mwenyezi Mungu amewafaradhishia Maimamu waadilifu kujipima kwa kuwa sawa na watu ili maumivu ya ufukara yasimwathiri yakammaliza."
Amesema tena: "Je, nitosheke kuitwa Amirul-Mu'miniin (Kiongozi wa Waumini) na wala sishirikiani nao katika hali ngumu ya maisha."
Utaratibu Wa Mwito Wake
Kwanza aliwaonya jamaa zake walio karibu. Hapo ni wakati iliposhuka Aya: "Na waonye jamaa zako walio karibu." (26:214) Basi akawafanyia chakula na akawaalika.
Miongoni mwa maneno aliyowaambia ni, "Ni nani atakayekuwa msaidizi wangu katika jambo hili, awe ndugu yangu, wasii wangu na khalifa wangu kwenu?" wote wakanyamaa isipokuwa Ali bin Abu Talib aliyesema: "Mimi, ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu." Basi akamshika shingoni kwake akasema: "Huyu ni ndugu yangu, wasii wangu na khalifa wangu kwenu, kwa hiyo msikilizeni na mumtii."
Watu wakanyanyuka huku wakicheka na kumwambia Abu Talib: "Umeamrishwa umsikilize na umtii mwanao mwenyewe!" Kisha Mtume akawalingania watu wake - Waarabu, kisha akamlingania kila mtu wa mwanzo hadi wa mwisho. Mwenyezi Mungu anasema; "Na hatukukutuma ila kwa watu wote." (34: 28)
Ama Mitume wengine walipelekwa kwa watu wao tu au watu wa zama zao tu. Ndio maana Nuh, Ibrahim, Hud, Swaleh, Musa na wengineo, walikuwa waki- waambia watu wanaowalingania kwenye imani kwa kutumia neno: "Enyi watu wangu."
Ama Muhammad (s.a.w) aliwaambia watu wote wa kila zama na kila miji, wa aina tofauti na lugha tofauti, kwa kusema: "Enyi watu! Mimi ni mjumbe wa Mwenyezi Mungu kwenu nyote." (7: 158)
Pia Mtume aliwaandikia barua wafalme wa duniani, akiwemo Kisra na Kaizari na akawatumia ujumbe wake akiwalingania kwenye imani kuhusu risala yake.
Siri Ya Utukufu Wake
Muhammad (s.a.w) alikuwa ni mwanaadamu; yeyote atakayemsifu kwa sifa ya muumbaji, mwenye kuruzuku, basi atakuwa amemkufuru Mwenyezi Mungu. Lakini watu wote kuanzia Adam mpaka mtoto wake wa mwisho, sio kama Muhammad, mtukufu zaidi katika wao, ni yule atakayethibitishwa utukufu na ubora wake na Muhammad. Ni sawa awe amethibitishiwa kwa nukuu na kuelezwa jina au kwa sifa ya kijumla, kama kusema: mbora wa watu ni yule anayewanufaisha zaidi watu.
Ama siri ya utukufu wa Muhammad ni kwamba yeye alikuwa akibeba matatizo ya watu wote. Alikuwa pamoja na mayatima na wajane na kuwatekelezea mahitaji yao. Hakuna yeyote awe rafiki au adui ila atamshughulikia na kumhurumia, kumpa usaidizi.
Maneno yangu haya hayatokani na ushabiki au malezi na mazingira la! Bali yana- tokana na kauli ya Mwenyezi Mungu aliposema: "Na hatukukutuma wewe ila ni rehma kwa viumbe." (21:107)
Maana yake ni kuwa huruma zake, na kushughulikia kwake watu hakuko kwa jamaa zake, au marafiki zake tu bali kumeenea kwa watu wote, maadui na marafiki, kama maji na hewa. Watu walimvunja meno, wakamjeruhi uso, lakini alisema: "Ewe Mwenyezi Mungu waongoze watu wangu hakika wao hawajui." Hakutosheka kuwaombea uongofu lakini aliwatakia udhuru kwa ujinga wao na kutofahamu.
Hakuna ajabu ikiwa Muhammad hakukasirika kwa ajili ya nafsi yake au kuzuia nafsi yake na anasa za dunia, isipokuwa ajabu ni kufanya kinyume na hivyo.
Tabia hiyo ni lazima kwa yule aliyepelekwa kwa ajili ya kutimiza tabia tukufu na kuwalingania watu wote kumsadikisha na kuamini risala yake. Wala hakuna maana ya kusadikisha isipokuwa kusadikisha uadilifu na wema, wala kumwamini yeye isipokuwa kuamini haki na utu, sio yeye mwenyewe.
Siku moja mtu mmoja alimwita hivi: "Ewe bwana wetu, mtoto wa bwana wetu. Mbora wetu na mtoto wa mbora wetu!" Mtume akasema: "Asiwachezee shetani, mimi ni Muhammad mja wa Mwenyezi Mungu, na Mtume wake. Wallahi sipendi wanitukuze zaidi ya cheo changu."
Masahaba zake walikuwa wanapomuona hawamsimamii ingawaje ni kipenzi chao, kwa sababu walikuwa wanajua kuwa hapendi kusimamiwa. Pia alikuwa akichukia kutembea na mtu akiwa nyuma yake, hivyo humshika mkono na kumvuta ubavuni mwake ili watembee pamoja.
Hii ndiyo hulka ya Muhammad (s.a.w.). Ndio ni kweli kuwa watu wote si kama yeye, lakini hulka zake ndio kioo cha hakika ya uislamu. Yeyote mwenye kulinga- nia uislamu na asifuate mwendo wa Mtume wake, basi ni mdanganyifu, ni sawa atambue hivyo au asitambue au hata akijiona, na watu wakimwona yeye ni mtukufu zaidi.
وَمَا كَانَ لِنَبِيٍّ أَنْ يَغُلَّ ۚ وَمَنْ يَغْلُلْ يَأْتِ بِمَا غَلَّ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۚ ثُمَّ تُوَفَّىٰ كُلُّ نَفْسٍ مَا كَسَبَتْ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ {161}
أَفَمَنِ اتَّبَعَ رِضْوَانَ اللَّهِ كَمَنْ بَاءَ بِسَخَطٍ مِنَ اللَّهِ وَمَأْوَاهُ جَهَنَّمُ ۚ وَبِئْسَ الْمَصِيرُ {162}
هُمْ دَرَجَاتٌ عِنْدَ اللَّهِ ۗ وَاللَّهُ بَصِيرٌ بِمَا يَعْمَلُونَ {163}
لَقَدْ مَنَّ اللَّهُ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ إِذْ بَعَثَ فِيهِمْ رَسُولًا مِنْ أَنْفُسِهِمْ يَتْلُو عَلَيْهِمْ آيَاتِهِ وَيُزَكِّيهِمْ وَيُعَلِّمُهُمُ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَإِنْ كَانُوا مِنْ قَبْلُ لَفِي ضَلَالٍ مُبِينٍ {164}