read

Aya 17 – 18: Wafanyao Uovu Kwa Ujinga

Maana

Hakika toba ikubaliwayo kwa Mwenyezi Mungu ni ya wale tu wafanyao uovu kwa ujinga kisha wakatubia haraka.

Ujinga hapa ni kwa maana ya upumbavu wa kuacha uongofu na kufuata upotevu. Makusudio ya kutubia haraka ni kutubia mkosaji kabla ya kukaribiwa na mauti, kwani mauti yatakuja tu bila ya shaka yoyote, na kila kijacho ki karibu.

Maana kwa ujumla ni kuwa mwenye kufanya uovu, kisha akajuta na kutubia, basi Mwenyezi Mungu humkubalia toba yake na kumsamehe akawa kama hakufanya dhambi yoyote. Bali Mwenyezi Mungu atampa thawabu.

Unaweza kuuliza: Mbona dhahiri ya Aya inaonyesha kuwa ni wajibu kwa Mwenyezi Mungu kukubali toba ya wanaojuta na hali twajua kuwa Mwenyezi Mungu ndiye awajibishaye kwa mwengine lile alitakalo, lakini hakuna anayeweza kumwajibishia yeye kitu chochote. Kwa sababu hana wa kufanana naye?

Jibu: Makusudio sio kuwa mwenginewe anamwajibisha Mwenyezi Mungu kukubali toba; isipokuwa makusudio ni kwamba fadhila zake na utukufu wake vinawajibisha kukubali huku; kama vile unavyomwambia mtu mkarimu "Ukarimu wako unakulazimisha kutoa," Mwenyezi Mungu anasema: "Mola wenu amejilaz- imishia rehema …" (6:54)

Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu huwatakabalia toba zao.

Maadamu wanataka kweli kurudi kwenye safu za waumini bora. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa toba ya kweli na ya uongo,mwenye hekima, ya kukubali toba.

Na si toba ya wale ambao hufanya maovu mpaka mmoja wao akafikiwa na mauti akasema sasa mimi nimetubia.

Hakika Mwenyezi Mungu hukubali toba ya anayetubia kwa sharti ya kutubia kabla ya kudhihirikiwa na alama za mauti. Ama mwenye kutubia huku akiwa anachungulia kaburi, basi toba yake haitakubaliwa. Kwa sababu hiyo ni toba ya kuishiwa na kukata tamaa.

Unaweza kuuliza: Utasemaje kuhusu Hadith ya Mtume (s.a.w.) isemayo: 'Mwenye kutubia saa moja tu, kabla ya mauti yake, basi Mwenyezi Mungu humtakabalia na kwamba hata saa ni nyingi; mwenye kutubia na roho yake imefika hapa - akionyesha koo lake - basi Mwenyezi Mungu humtakabalia toba."

Jibu: Inabidi kuangalia vizuri riwaya hii kwa mambo haya yafuatayo:

Kwanza: Hadith hii inakhalifu Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Na imethibiti kutoka kwa Mtume (s.a.w.) kuwa amesema: "Kumekuwa kwingi kuzuliwa mambo katika uhai wangu na kutazidi baada ya kufa kwangu. Na atakayenizulia, basi na ajich- agulie makazi yake motoni. Ikiwajia Hadith kutoka kwangu, basi ilinganisheni na Kitabu cha Mwenyezi Mungu; yanayoafikiana na Kitabu cha Mwenyezi Mungu yachukueni na yanachohalifiana na Kitabu cha Mwenyezi Mungu basi msiyachukue."

Kwa ajili hiyo basi hatuikubali Hadith ya kukubaliwa toba wakati roho ikitolewa. Si ajabu kuwa baadhi ya viongozi wa Kibani Umayya na Bani Abbas waliwaambia wafuasi wao wakuu wawawekee Hadith hii, ili iwe ni hoja kwa wanaotawaliwa kwamba wao wanayo nafasi kwa Mwenyezi Mungu hata wakifanya dhuluma na ufisadi kiasi gani. Wao walikuwa na jopo la mafakihi waovu wa kuboresha vitendo vyao na kuifanya dini kulingana na matakwa ya ushetani.

Pili: Fikra ya kukubaliwa toba wakati wa kufa ni hadaa ya kufanya madhambi na hii ni kazi ya shetani sio ya Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema.

Tatu: Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anakubali amali ya aliyeifanya kutokana na matakwa yake na uhuru wake kamili tu. Kwa dhahiri ni kwamba mtu anakuwa huru tu, ikiwa atafanya amali akiwa na uwezo wa kufanya na kuacha. Ama ikiwa anaweza kufanya tu, lakini hana uwezo wa kuacha; au anaweza kuacha tu bila ya kuwa na uwezo wa kufanya, basi atakuwa ni mwenye kuendeshwa bila ya hiyari.

Hivi ndivyo ilivyo kwa kutubia wakati wa mauti kwani ilivyo ni kwamba mtubiaji katika hali hii ya mauti, huwa hawezi kufanya dhambi na maasi, sawa na atakavyoshindwa kesho yule atakayesema:
Mola wetu! Tuondolee adhabu hii hakika sisi ni wenye kuamini …" (44:12)

Ikiwa Mwenyezi Mungu atamkubalia toba anayechungulia kaburi, basi itatakikana pia amkubalie anayeadhibiwa motoni. Kwa hivyo ndipo Mwenyezi Mungu akawafanya sawa na kuwaunganisha pamoja pale aliposema: "Wala wale ambao hufa wakiwa makafiri."

Yaani pia Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hakubali toba ya wale wanaokufa wakiwa makafiri, na wala hawajuti mpaka waone adhabu Siku ya Kiyama, bali pia hawakubaliwi wakiwa njiani kuendea Siku hii ya Kiyama; kama isemavyo Qur'an: "Hata yanapomfikia mmoja wao mauti, husema: Mola wangu! Unirudishe ili nifanye mema katika yale niliyoyaacha. Hapana! Hakika hilo ni neno tu analolisema; na nyuma yao kuna kizuizi mpaka siku watakapofufuliwa." (23: 99-100)

Ni kweli kuwa kimtazamo wa kiakili inawezekana kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu awasamehe wenye dhambi hata kama hawakutubia kwa ukarimu wake tu. Lakini hilo ni jambo jengine na kukubaliwa toba wakati wa kufa ni jambo jengine.

Toba Na Maumbile

Toba ni tawi litokanalo na kuwepo dhambi. Kwa sababu ni kutaka kusamehewa hizo dhambi. Na mtu haepukani na dhambi iwe ndogo au kubwa, isipokuwa aliyehifadhiwa na Mwenyezi Mungu (Maasum). Imenasibishwa kwa Mtume (s.a.w.) kauli hii: "Ukighufiri unaghufiri dhambi zote, kwa mja wako mja yeyote."

Mwenyezi Mungu amewajibisha toba kwa mwenye dhambi, kama vile alivyowajibisha Saumu na Swala. Miongoni mwa Aya zinazofahamisha wajibu ni Aya hii tunayoifasiri. Na pia Aya hizi zifuatazo: "Enyi mlioamini tubuni kwa Mwenyezi Mungu toba ya kweli." (66:8)

"Na kwamba mwombeni msamaha Mola wenu na mtubie kwake." (11:3) "Na wasiotubia, basi hao ndio madhalimu." (49:11)

Kwa hakika hasa wajibu wa kutubia hauhitaji dalili; kwa sababu ni katika maswala ambayo yanakuwa na dalili pamoja. Kila mtu kwa maumbile yake anatambua kuwa mkosaji lazima aombe msamaha kwa kosa lake na pia kumtaka msamaha yule aliyemkosea.

Na hilo limekuwa ni jambo la kawaida la kimataifa hata kama kitendo kimefanyika kimakosa na bila ya kukusudia. Ndege ikiingia anga ya nchi nyingine au mashua ikiingia bahari ya nchi nyingine bila ya ruhusa, basi ni lazima itangaze kuomba msamaha wake vingenevyo italaumiwa na kanuni.

Kwa hivyo basi, kila Aya au mapokezi yanayofahamisha wajibu wa toba, ni uthibitisho wa hukumu ya kimaumbile na wala sio sharia mpya.

Basi mwenye kufanya dhambi na asitubie atakuwa amefanya uovu mara mbili. Kwanza amefanya dhambi, Pili, kuacha kutubia. Hali mbaya zaidi ni kuacha toba na kuiharibu kwa kurudia dhambi baada ya kumwahidi Mwenyezi Mungu kutekeleza twaa na kufuata amri. Mwenyezi Mungu anasema: "Mwenyezi Mungu amekwishayafuta yaliyopita; lakini atakayefanya tena Mwenyezi Mungu atampa adhabu," (5:95)

Hadith inasema: "Mwenye kuendelea na dhambi na huku anataka msamaha basi ni kama mwenye kucheza shere."

"Mwenyezi Mungu atawalipa shere zao na kuwaacha katika upotofu wao wakitan- gatanga ovyo." (2:15)

Dhambi inathibiti kwa kuacha aliyoyaamrisha Mwenyezi Mungu au kutenda aliy- oyakataza kwa makusudi na kung'ang'ania.' Kwa dhahiri ni kwamba hukumu za kiakili ndizo hukumu za Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kwa sababu anafikisha huku- mu zake kwa njia mbili: Akili na kwa ulimi wa Mtume wake. Natija ya mwisho ni kwamba hakuna dhambi wala adhabu bila ya ubainifu kama wasemavyo mafakihi waislamu; au bila ya maandishi kama wasemavyo wanasheria.

Kutokana na maelezo hayo yaliyotangulia, inatubainikia kuwa mtu anakuwa ni mwenye dhambi na mwasi ikiwa ameyafanya aliyokatazwa na Mwenyezi Mungu au kuacha aliyoamrishwa na Mwenyezi Mungu kwa makusudi na kujua. Lakini kama atafanya au kuacha kwa kusahau, au kulazimishwa au kwa kutojua kusikokuwa kwa uzembe na kupuuza, basi hatahisabiwa kuwa ni mwenye dhambi; na hakutakuwa na sababu za kuwajibisha toba. Mwenyezi Mungu anasema: "Mwenye kutubia baada ya dhulma yake." (5:39)

Kwa sababu kila mwenye kufanya dhambi basi amejidhulumu mwenyewe kwa kujiingiza kwenye hisabu na adhabu.

Toba ni kujuta mwenye dhambi aliyoyafanya na kutaka msamaha na maghufira kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kutorudia dhambi mara ya pili. Akirudia basi toba imebatilika na atahitajia kuweka upya ahadi madhubuti zaidi na moyo mnyenyekevu.

Imam Zainul-abiddin (a.s.) anasema: "Ikiwa kujuta ni toba basi mimi ni wa mwan- zo wa wenye kutubia. Na ikiwa kuacha kukuasi ni kurejea kwako, basi mimi ni wa mwanzo wa wenye kurejea kwako. Na ikiwa kutaka maghufira ni kuondolewa dhambi, basi mimi ni wa mwanzo wa wenye kutaka maghufira."

Makusudio ya kutaka maghufira ni kufanya kwa vitendo sio kwa maneno. Kabla ya chochote kwanza aanze kurudisha haki za watu alizozidhulumu. Ikiwa amem- nyang'anya mtu shilingi basi airudishe; na ikiwa amewambia maneno mabaya au kumfanyia vitendo vibaya, basi amwombe msamaha. Kisha alipe faradhi zilizom- pita; kama vile Hija, Saumu na Swala.

Siku moja Amirul-muminin Ali (a.s.) alimsikia mtu mmoja akisema: "Namtaka maghufira Mwenyezi Mungu." Imam Akasema: "Unajua kutaka maghufira? Hiyo ni daraja ya juu, na inakuwa katika maana sita."

Basi Imam akayataja ikiwa ni pamoja na kuazimia kutorudia dhambi, kurudisha haki za viumbe na kulipa faradhi nk. Yakitekelezeka hayo kwa anayetubia basi atakuwa miongoni mwa aliowahusu Mwenyezi Mungu kwa kauli yake: "Na hakika mimi ni mwingi wa kumsamehe anayetubia na akaamini na akatenda mema, tena akaongoka ". (20:82)

Yaani kuendelea na uongofu ambao ni imani na amali njema.

Hadith inasema: "Mwenye kutubia ni kama asiyekuwa na dhambi," Bali anakuwa katika watu wema: Mwenyezi Mungu anasema: "… Tubieni kwake atawastarehesha starehe njema." (11:3)

Na akasema tena: "… Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wanaotubia …" (2:222)

Mtume (s.a.w.) amesema: "Mwenye kujiona kuwa ni muovu basi yeye ni mwema." Ama siri ya kuwa mwema mtubiaji na ukubwa wa utukufu wa daraja yake mbele ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ni kule kujitambua mwenyewe na kuihisabu nafsi yake na kila aibu na upungufu na kuipigania hiyo nafsi jihadi kwa ukamilifu na utiifu. Hii ndiyo jihadi kubwa aliyoieleza Mtume (s.a.w.). Walikwisha sema Mitume na wenye hekima: "Jitambue," Makusudio yao ni kuwa mtu azitambue aibu zake na ajisafishe.
Pengine mtu anaweza kusema kuwa mtu hupitia mikondo mingi; kama vile wazazi wake, shule, jamii yake mazingira na mengineyo yanayoathiri utu wake bila ya kuweza kuyaepuka. Kwa hiyo basi mtu hawezi kuambiwa kuwa ana dhambi au ni mwovu. Kwa sababu dhambi ni ya jamii na ya mazingira, Ikiwa hakuna dhambi basi maudhui ya kutubia yanafutika kabisa.

Jibu: Ni kweli kuwa mazingira ya mtu yanamwathiri, lakini vile vile ni kweli kuwa matakwa ya mtu yanaathiri mazingira. Kwa sababu mtu na mazingira ni uhakika unaonekana, na kila kitu chenye uhakika unaonekana hakina budi kuwa na athari, vyinginevyo kitakuwa si chochote. Kwa hivyo basi mtu anaweza kuyaathiri mazin- gira yake, bali anaweza kuyageuza akiwa ni jasiri.

Mazingira anayoishi binadamu huwa yanamsababishia mtu kupendelea kuona natija yake na matunda yake. Kwa hivyo basi ni juu ya mtu kuangalia na kuyachunguza matunda haya na hayo mapendeleo. Ikiwa yana mwelekeo mzuri, basi apate msukumo, vinginenvyo itambidi aachane nayo. Na hili sio jambo gumu. Lau binadamu angekuwa hana uwezo wa kuyakabili mazingira, asingeliambiwa kwamba ni mwema au ni mbaya; na pia kusingekuwapo na adhabu au thawabu,. Vile vile kusingekuwako na njia ya kuelezea kuweko dini, hulka njema, sharia au kanuni.

Swali la pili: Umesema kwamba toba ni tawi la dhambi, ambapo tunajua kuwa Mitume na Maimam walikuwa wakitubia kwa Mwenyezi Mungu wakati wao wako mbali na dhambi.

Jibu: Mitume na Maimam wametwahirishwa na uchafu na maasi, hilo halina shaka. Lakini wao kutokana na walivyomjua Mwenyezi Mungu na kumwogopa sana, walijiona kama wana dhambi. Kwa hivyo walitubia dhambi ya kuwazia tu, wala haiko.

Na hiyo ni athari katika athari za kuhifadhiwa kwao na utukufu wao. Kwa sababu, mtukufu hajioni kuwa ni mtukufu, bali hajioni ni chochote kwa Mwenyezi Mungu, daima anajituhumu kuwa si mkamilifu katika kumtii Mwenyezi Mungu na kumwabudu. Kwa ajili hiyo ndipo humuomba msamaha na kumtaka msaada kwa mwisho mzuri kinyume na "Wale ambao bidii yao imepotea bure katika maisha ya dunia na wao wanafikiri kwamba wanafanya vizuri." (18:104)

Bora zaidi ya niliyoyasoma kuhusu maudhui haya ni kipande cha dua ya uokofu (munajat) ya Imam Zainul-abidin (a.s.) akiwa anamtaka Mwenyezi Mungu ampelekee mja mwema anayetakabaliwa dua ili mja huyu amwone Imam akiwa na hali mbaya ya kumwogopa Mwenyezi Mungu; aweze kuathirika na kumhurumia Imam amwombee kwa Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu aitakabalie dua ya mja huyu mwema. Hapo Imam aweze kuokoka na hasira ya Mwenyezi Mungu na machukivu yake. Na afuzu kwa kupata radhi Yake na maghufira Yake.

Haya ndiyo aliyoyasema Imam, namnukuu: "Huenda mmoja wao kwa rehema yako akanihurumia kwa msimamo wangu mbaya, akanionea huruma kwa hali yangu mbaya akaniombea dua inayosikilizwa zaidi kwako kuliko dua yangu; au uombezi (shafaa) unaotegemewa zaidi kwako kuliko uombezi wangu ambao utakua ni sababu ya kuokoka kwangu na ghadhabu yako na kufuzu kwangu kwa radhi yako."

Imam Zainul-abidin aliyasema haya siku ambayo hakuweko yeyote duniani anayekurubia sifa moja katika sifa zake adhimu. Hapo ndipo inapokuwa siri ya utukufu.

Baada ya maelezo yote haya ni kwamba toba ina maelezo mengi ambayo yanaweza kupanuliwa katika kitabu mbali kinachohusu toba tu. Huenda tukayarudia tena katika mahali patakapo nasibu.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا يَحِلُّ لَكُمْ أَنْ تَرِثُوا النِّسَاءَ كَرْهًا ۖ وَلَا تَعْضُلُوهُنَّ لِتَذْهَبُوا بِبَعْضِ مَا آتَيْتُمُوهُنَّ إِلَّا أَنْ يَأْتِينَ بِفَاحِشَةٍ مُبَيِّنَةٍ ۚ وَعَاشِرُوهُنَّ بِالْمَعْرُوفِ ۚ فَإِنْ كَرِهْتُمُوهُنَّ فَعَسَىٰ أَنْ تَكْرَهُوا شَيْئًا وَيَجْعَلَ اللَّهُ فِيهِ خَيْرًا كَثِيرًا {19}

Enyi ambao mmeamini! Si halali kwenu kuwarithi wanawake kwa nguvu; wala msiwataabishe kwa kutaka kuwanyang'anya baadhi ya mlivyowapa, ila watakapofanya uchafu ulio wazi. Na kaeni nao kwa wema; na kama mkiwachukia basi huenda mkachukia kitu na Mwenyezi Mungu amejaalia heri nyingi ndani yake

وَإِنْ أَرَدْتُمُ اسْتِبْدَالَ زَوْجٍ مَكَانَ زَوْجٍ وَآتَيْتُمْ إِحْدَاهُنَّ قِنْطَارًا فَلَا تَأْخُذُوا مِنْهُ شَيْئًا ۚ أَتَأْخُذُونَهُ بُهْتَانًا وَإِثْمًا مُبِينًا {20}

Na mtakapotaka kubadilisha mke mahali pa mke na mkawa mumempa mmoja wao rundo la mali, basi msichukue katika mlichowapa. Je, mnakichukua kwa dhulma na kwa makosa yaliyo wazi?

وَكَيْفَ تَأْخُذُونَهُ وَقَدْ أَفْضَىٰ بَعْضُكُمْ إِلَىٰ بَعْضٍ وَأَخَذْنَ مِنْكُمْ مِيثَاقًا غَلِيظًا {21}

Mtachukuaje na hali mmeingiliana na hali wao wamechukua kwenu agano madhubuti?