read

Aya 137 – 138: Zimepita Desturi

Maana

Hakika zimepita desturi nyingi kabla yenu.

Yametangulia maelezo kuhusu vita vya Uhud na walioshinda vita walikuwa ni washirikina. Kwa sababu wale waliokuwa wakilinda njia ya kupita adui waliiacha, adui akawazungukia kwa nyuma.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anawaambia katika Aya hii Masahaba wa Mtume Muhammad (s.a.w): Wajue habari za watu waliopita na yaliyowapata wale walioacha msimamo, ili wapate fundisho kwa hilo, na wasirudie tena waliyoyafanya katika Uhud ya kumwasi Mtume, kwa kuicha tupu njia ambayo waliamrishwa wabakie hapo vyovyote itakavyokuwa. Kwa hiyo, walipokhalifu, yaliwapata yalowapata umma uliotangulia ambao uliwakhalifu Mitume yao.

Basi tembeeni katika nchi na muangalie ulikuwaje mwisho wa wale waliokadhibisha.

Makusudio sio kutembea hasa, bali ni kujua hali ya waliopita kwa njia yoyote ile. Hakuna mwenye shaka kwamba ni jambo la faida kwa mwenye akili kufanya utafiti wa hali za watu na kuchunguza sababu zilizowadhoofisha ili apate funzo na kuongoka kwenye lile lenye masilahi. Kwa ajili hii, ndio akasema Mtukufu wa ayasemayo:

Huu ni ubainifu kwa watu na mwongozo na mawaidha kwa wamchao.

Hii ni ishara ya kutaja desturi nzuri, ambazo mwenye kuzifuata hufaulu na mwenye kuziacha hupata hasara. Hapana budi ubainifu uwe kwa watu wote, ili iwe ni hoja kwa aliyeasi, na mwongozo na mawaidha kwa mwenye kumcha Mungu. Kwani hiyo ndiyo njia pekee inayopambanua baina ya mwasi na mtiifu. Lau si ubainifu kusingelikuweko na utiifu wala uasi.

Ushenzi Wa 5 Juni

Mnamo mwaka 1387 A. H. watu wa Bahrain waliniita ili nikatoe mihadhara ya kidini kwa mnasaba wa mwezi Mtukufu wa Ramadhan.Nilikaa kwao karibu siku 25 ambapo nilitoa mihadhara 20; na vijana walikuwa wakinitupia maswali mbali mbali. Siku moja nikajiwa na ujumbe wakasema: Tuzungumzie sababu za tukio la 5 Juni, bila ya mtazamo wa kidini.

Nami ni kasema: Hakuna tofauti baina ya elimu na dini katika mtazamo wa kanuni na desturi inayotawala maisha.

Kwani matakwa ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) katika viumbe vyake na waja wake yanakwenda kwenye desturi za kielimu zilizonyooka na sababu za kawaida; bila ya kutofautisha baina ya waumini au makafiri.

Kwa mfano anayejua kuogelea, ataogelea mpaka ufukweni kwa amani hata kama ni kafiri, na asiyejua atazama hata kama ni Mumin, vile vile mwenye kujiandaa vizuri na adui yake atamshinda, ikiwa adui yake hayuko katika hadhari na maandalizi hata kama ni mlahidi.

Na mwenye kufanya uzembe akapuuza, basi hupata hasara hata kama ni katika mawalii na wakweli. Mwenyezi Mungu anasema kuwaambia Masahaba wa Mtume (s.a.w): "… Wala msizozane msije mkavunjika moyo na kupotea nguvu zenu …" (8:46)

Imam Ali (a.s.) anasema: "Hakika hao - akikusudia watu wa Muawiya - wameshinda kwa umoja wao kwenye batili. Na nyinyi - akiwakusudia watu wake - mmeshindwa kwa sababu ya kugawanyika kwenu kwenye haki yenu."

Kwa hivyo, haki haishindi kwa kuwa ni haki tu; na wala batili haishindwi kwa kuwa ni batili tu, bali kuna desturi katika maisha haya inayoendesha na kutawala jamii. Na Mwenyezi Mungu (s.w.t.) haiondoi au kubadilisha mwendo wake; sawa na ilivyo katika desturi ya maumbile.

Kwa hali hiyo basi, hakuna ajabu kwa wazayuni kuteka sehemu ya ardhi yetu, wakisaidiwa na wakoloni, maadamu sisi tumeghafilika, tukiwa tumegawanyika katika vijinchi ambavyo havina umoja wowote zaidi ya neno 'Uarabu.'

Hata hivyo, zamu ya kwanza inaweza kuwa kwa upande wa batili, lakini mwisho inakuwa kwa mwenye kusubiri na kumcha Mungu.

Kwa sababu namna yoyote itakavyokuwa batili itakosa nguvu na sifa zitazoiwezesha kuendelea. Wakati wowote ule haki itakapopata wa kuipigania ambao wanaiamini na kujitolea mhanga kwa ajili yake, basi batili itatokomea tu.

Jambo lenye matumaini ni kwamba waarabu hawakusalimu amri, bali misukosuko na kushindwa kumewakomaza. Wakoloni walifikiri kwamba urefu wa njia utawadhoofisha waarabu na kwamba kuzikalia kimabavu ardhi zao kutawafanya wanyenyekee. Lakini imeonekana kuwa wamekosea, na hakuna kitu kwa waarabu ila subira na bidii, iwe njia ni ndefu au fupi, nyepesi au nzito.

Unaweza kuuliza: Umesema kuwa matakwa ya Mwenyezi Mungu yanapita kwenye desturi iliyozoelekea; lakini mbona Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwaangamiza watu wa Nuh kwa tufani, watu wa Hud kwa upepo usiozuilika, watu wenye ndovu aliwamwagia mawe ya udongo mkavu, na Madain ya Lut ikaigeuza chini juu, yote hayo ni kwa sababu ya kuasi tu na kuihalifu haki; kama ilivyoelezwa katika Kitabu chake Kitukufu.

Jibu: Hekima ya Mwenyezi Mungu imepitisha matukio hayo ni maalum kupitia kwa Mitume waliotangulia tu na wala haikuendelea na kuenea kwa makafiri wote, kwa hiyo kutumia kipimo kwenye hilo ni nadra.

Swali la pili: Kwa nini haki isishinde katika hali zote, maadamu Mwenyezi Mungu anaitaka na anawataka watu wa haki, akichukia batili na wafuasi wake?

Jibu: Lau haki ingelishinda katika hali zote, watu wote wangelifuata kwa kupenda ushindi na kuchukia batili na ingelikuwa uzito kupambanua baina ya habithi ambaye anafuta haki kwa kukusudia manufaa na biashara, na mwema ambaye anafuata haki kwa njia ya haki na anayevumilia shida na matatizo. Zaidi ya hayo ni kwamba sababu hazijulikani ila baada ya kushindwa.

Pili, lau matatizo angeyapeleka kwa wabatilifu daima na milele na kuwaepushia wenye haki, basi taklifa, thawabu na dhambi zingelibatilika vile vile. Kwa sababu kufuata haki katika hali hii kungelikuwa ni kwa nguvu na kushindwa, si kwa matakwa na hiyari.
Kwa ufupi ni kwamba ni juu ya mwislamu kuizingatia vizuri maana ya Aya za Qur'an na kuzifanya ni kipimo cha itikadi yake, picha yake ya kushindwa na kushinda, na nguvu na udhaifu, na kwamba kila kimoja katika mawili hayo yana njia yake mahsusi.

وَلَا تَهِنُوا وَلَا تَحْزَنُوا وَأَنْتُمُ الْأَعْلَوْنَ إِنْ كُنْتُمْ مُؤْمِنِينَ {139}

Wala msidhoofike wala msihuzunike kwani nyinyi ndio mlio juu ikiwa nyinyi ni waumini.

إِنْ يَمْسَسْكُمْ قَرْحٌ فَقَدْ مَسَّ الْقَوْمَ قَرْحٌ مِثْلُهُ ۚ وَتِلْكَ الْأَيَّامُ نُدَاوِلُهَا بَيْنَ النَّاسِ وَلِيَعْلَمَ اللَّهُ الَّذِينَ آمَنُوا وَيَتَّخِذَ مِنْكُمْ شُهَدَاءَ ۗ وَاللَّهُ لَا يُحِبُّ الظَّالِمِينَ {140}

Kama mmepata jeraha, basi kuna kaumu wamekwishapata jeraha kama hilo, na siku za namna hii tunawaletea watu kwa zamu. Na ili apate kuwajua Mwenyezi Mungu ambao wameamini katika nyinyi na afanye miongoni mwenu mashahidi. Na Mwenyezi Mungu hawapendi madhalimu.

وَلِيُمَحِّصَ اللَّهُ الَّذِينَ آمَنُوا وَيَمْحَقَ الْكَافِرِينَ {141}

Na ili awatakase Mwenyezi Mungu ambao wameamini na awaangamize makafiri.