Aya 3-4: Mkihofia Kutofanya Uadilifu Basi Ni Mmoja.
Nahau
Makusudio ya herufi Ma hapa ni wanawake. Wafasiri wamekanganywa kuhusu maana yake. Wengine wamefasiri kwa jinsi ya wanawake; wengine, kwa sifa na kuna wengine waliofasiri kwa kitu. Siri ya kubabaika kwao ni kauli ya watu wa Nahau kwamba herufi Ma ni ya kisichokuwa na akili na Man ndiyo ya mwenye akili. Lakini kimsingi ni kuwa Qur'an ni hoja juu ya watu wa Nahau, na wala watu wa Nahau si hoja juu ya Qur'an. Qur'an imetumia herufi Ma kwa mwenye akili katika Aya nyingi.
Kama vile: "Na (kwa) mbingu na aliyeziweka." (91:5). Nyingine: "Wala nyinyi hamuabudu yule ninayemuabudu" Au kama ilivyotumia Man, kwa kisicho na akili. "Na wengine huenda kwa matumbo yao" (24:45)
Ndio ni kweli kwamba aghlabu ni kutumiwa Ma kwa kisicho na akili na Man kwa mwenye akili, lakini kuwa aghlabu ni kitu kingine na kutowezekana ni kitu kingine.
Maunganisho ya wawili wawili na watatu watatu na wanne wanne, yamekuja kwa 'na' na wala sio 'au'. Kwa sababu kila mtu aweza kuwa na hiyari ya idadi anayotaka katika hii iliyotajwa. Lau ingeliunganishwa kwa au ingelikuwa maana yake atakayechagua wawili ndio hao hao, hawezi kuongeza, na mwengine aweze kuchagua watatu tu na pia mwengine achague wane.
Maana
Na kama mkihofia kutowafanyia usawa mayatima, basi oeni mnaowapenda katika wanawake, wawili wawili na watatu watatu na wanne wanne.
Msingi wa kuoa wake zaidi ya mmoja hadi kufikia wane umethibitishwa kisheria kwa hukumu ya Qur'an na Hadith na ijmai kwa kauli na vitendo. Bali msingi huu unajulikana kuwa ni katika dharura za dini. Lakini haukuhalalishwa moja kwa moja, bali umewekewa masharti ya kuuhalalisha kwa dharura ya dini vilevile.
Hapa kuna swali linalojitokeza; kwamba maana yaliyo wazi katika Aya hii ni kwam- ba mwenye kuogopa kutofanya uadilifu katika mayatima basi aoe wake wawili, watatu na wane, na kwamba akifanya hivyo hakutobakia dhuluma yoyote.
Bila shaka, kama maana yangekuwa haya, ingekuwa sawa na maneno ya kubobokwa, kwani hakuna mfungamano wote kati yake, na Qur'an zimepamban- uliwa Aya zake kutoka kwa Mwenye Hekima aliye Mjuzi?!
Jibu la swali hili liko wazi na ni jepesi, isipokuwa kutofautiana majibu ya wafasiri na kugongana kwao, kumemwacha msomaji gizani.
Kwa ufupi ni kuwa maneno tangu mwanzo yanahusiana na waliousiwa (mawasii) mayatima, ambao ndio waliokusudiwa katika kauli ya "na wapeni mayatima mali zao wala msibadilishe kibaya kwa kizuri wala msile mali zao."
Baada ya kuambiwa haya wenye kufungamana na mali ya yatima, ndipo Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akawaambia mawasii jambo jengine litakalofungamana na ndoa ya mayatima ambalo ni "Kama mkihofia kutofanya usawa katika mayatima:…Yaani katika ndoa ya mayatima.
Neno 'ndoa' limefahamika kutokana na neno basi 'oeni' Huo ni mlango wa kuondoa cha kwanza kinachofahamishwa na cha pili; kama wasemavyo watu wa Nahau.
Kukadiria kwake ni: Ama mambo yanayohusu kuoa wanawake katika mayatima, basi ni juu yenu enyi mawasii, kama mkiwaoa msiwanyime haki zao.
Na kama mkihofia kutowafanyia haki kwa kuangalia kuwa wao wako peke yao, hakuna yeyote atakayewatetea, basi waacheni na muoe wengine, Mwenyezi Mungu amewapa nafasi kwa mayatima kama vile alivyowahalalishia wengineo kuoa mmoja, wawili, watatu au wane. Lakini vilevile kwa misingi ya usawa na kama mkihofia kutofanya usawa kwa zaidi ya mmoja, basi oeni mmoja.
Kwa maelezo hayo ndio maneno ya Aya yatakuwa yanaungana vizuri, sawa na kumwambia mwenzako. "Ikiwa huli aina hii, kwa sababu unakula sana na kuogopa kuvimbiwa, basi kula aina nyingine, lakini pia usile sana na utajitia kwenye madhara." Kila tamko tutakalo likadiria kwa maana hayo tuliyoyataja, basi yanakubalika nayo.
Imezoeleka kuwa Qur'an inafupisha maneno sana, na kuacha kutaja kila ambacho msomaji anaweza kukifahamu kwa ishara tu. Ikiwa yaonekana wafasiri watakuwa wanababaika, basi hiyo inafahamisha kuwa Aya hii ni ya mkato sana .(hivyo, inababaisha zaidi).
Mkihofia kutofanya uadilifu basi ni mmoja.
Makusudio ya usawa ni uadilifu (usawa) katika mavazi, mahali pa kuishi na mengineyo katika mambo ambayo yako ndani ya uwezo wa mtu. Ama yale ambayo yako nje ya uwezo wake; kama vile moyo kumpenda mmoja zaidi, basi hayalazimishwi usawa.
Kwa hivyo basi, ndio tunapata tofauti kati ya Aya hii na ile isemayo: "na hamtaweza kufanya uadilifu baina ya wake (wenu) hata mkijitahidi vipi."(4:129)
Makusudio ya uadilifu katika Aya kwanza ni uadilifu katika kukidhi mahitaji yake, na katika ya pili ni uadilifu wa mapenzi ya moyo.
Unaweza kuuliza: Hakika Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewajibisha kutosheka na mke mmoja tu, ikiwa kunahofiwa dhuluma katika zaidi ya mmoja. Na kwa dhahiri ni kwamba hofu ya kinafsi mara nyingi hukosea kuliko kupata.
Na tumewashuhudia wanaume wengi wanashindwa na matamanio na kuongeza wake halafu wanakabiliwa na matatizo. Kwa hiyo sharti hili si sawa.
Jibu: Mushkeli huu hauepukiki, kama tutakusudia kuhofia hali ya nafsi. Ama ikiwa ni kuhofia hali ya nafasi ya mtu na afya yake, kwamba yeye anaweza zaidi ya mmoja, basi swali halitokuwa na haja.Vitu vya kimaada vya kidhahiri inawezekana kuvidhibiti kwa wepesi; wala katika sheria ya kiislamu hakuna kukadiria hali mahsusi ya mtu anayetaka kuoa wake wengi; kama ilivyo hivi sasa katika baadhi ya miji ya kiislamu.
Hilo ni karibu zaidi na kutofanya dhuluma.
Yaani kuwa na mke mmoja ni karibu zaidi na uadilifu na ni mbali zaidi na kufanya dhuluma. Hii ni ishara ya kuonyesha kuwa, ni juu ya mume kutosheka na mke mmoja, kwa sababu kuwa na zaidi ya mmoja kunaleta matatizo.
Katika Tafsir Al-Bayadhawi amesema kuwa baadhi ya wafasiri wamefasiri neno la tau'uluu kutoka neno I'yal ulezi mwingi; kwa maana ya kuwa ni bora mume asioe wake wengi ili asipate tabu na mashaka kwa ajili ya hao wake na watoto.
Mwenye Tafsir Al-Manar amesema kauli hii ndiyo yenye nguvu zaidi. Na amesema Imam Ali: "Ulezi mchache ni moja ya nafuu".
Wapeni wanawake mahari yao hali ya kuwa ni zawadi.
Makusudio ya zawadi hapa ni ile ambayo Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameilazimisha kwa mume. Maana yake ni wapeni wanawake mahari yao, kwa sababu Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameyalazimisha kuwa ni zawadi sio kununua starehe. Kwa sababu wote wawili wanastarehe.
Kama wakiwatunukia kitu katika hayo mahari yao, basi kuleni kwa raha na kunufaika.
Mahari ni mali ya mke, anaweza kuitumia vile anavyotaka, wala haifai mume au mtu mwengine yeyote kumwingilia kwenye mahari; kama asemavyo Mwenyezi Mungu: "…Na mkawa mmempa mmoja wao chungu ya mali, basi msichukue kitu katika hiyo (mali)." Ila ikiwa atatoa ruhusa na kwa radhi yake sawa na mali nyingine.
Ndoa Ya Mitala (Wake Wengi)
Uislamu umeweka sharia ya kuoa wake wengi kwa sharti. Hilo halina shaka, wala silo la kufanyiwa utafiti na Ijtihadi. Lakini mlango wa Ijthadi ulio wazi katika kufasiri sharti ya mwenye kutaka kuoa wake wengi, Mujtahid anaweza kusema: Makusudio ya kuhofia ni vile tu mume kufikiria kufanya dhuluma na kutofanya usawa kwa wake wengi. Kwa hiyo, kwa mujibu wa Mujtahdii huyu itakuwa hai- wezekani kuoa wake wengi isipokuwa kwa nadra. Kwa sababu mafikirio haya yako kwa wengi, na yanatiliwa mkazo na ufisadi tunauona katika majumba mengi yaliyo na mke zaidi ya mmoja.
Qur'an pia imekwishalidokeza hilo kwa kusema "Hilo ni karibu zaidi na kutofanya dhuluma." Yaani kutosheka na mmoja ni karibu na uadilifu na ni mbali na kufanya dhuluma. Kwa hiyo kufungamanisha kujuzu kuoa zaidi ya mke mmoja, na kusiwe na uonevu na ufisadi ni sawa na kufungamanisha na muhali (jambo lisilo wezekana) kulingana na inavyotokea mara kwa mara.
Jambo la kushangaza ni kwamba wale ambao wana uwezekano wa kuwafanyia uadilifu wake wengi na hali ya afya na mali zinawaruhusu, hawapendelei kuoa mke zaidi ya mmoja na wanaogopa hata kama wanatamani kufanya hivyo. Lakini wale ambao hawatarajiwi kufanya uadilifu kwa namna yoyote ile na kuharibu jamii na kizazi chao kwa kuoa wake wengi, hawa wanajipiga moyo konde kwa kuoa mke zaidi ya mmoja. Na jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba wanavyuoni wa kidini wanapitisha ndoa za watu hawa, bila ya kusita na hata kuuliza na kupata jawabu, kama kwamba kuoa mke zaidi ya mmoja kumehalalishwa hivi hivi tu, bila ya sharti lolote.
Zaidi ya hayo, kuoa mke zaidi ya mmoja si katika wajibu wala sunna katika sharia ya kiislam, isipokuwa uislam umeruhusu kwa mambo maalum na masilahi mahsusi. Lakini maadui wa dini wamewachukulia wale vinukamito (wapendao kuoa sana) ambao hawajali masharti yoyote kuwa ni njia ya kutia ila na kuufedhehi uislam; kama ilivyo kawaida yao kutoa hoja kwa vitendo vya watu kuwa ndio vitendo vya dini na itikadi. Lau kama wangekuwa ni watu wa usawa basi wangelifanya kinyume, na kuitolea hoja dini juu ya watu wafanyao makosa na siyo dini.
Wakati uislam unashartiza mume asioe zaidi ya mke mmoja ila baada ya kuhakik- isha kuwa hakutakuweko ufisadi na dhuluma, huko kwenye miji ya Ulaya na Marekani kuna baadhi ya miji wanawake mara nyingi wanatembea na waume wa nje wanaowataka bila ya sharti lolote tena pengine mumewe akiwa anajua.
Zaidi ya hayo, bunge la Uingereza mwaka uliopita lilipitisha sheria ya kulawiti na ikaungwa mkono na baadhi ya wakuu wa dini; mji wote ukajaa furaha kwa kuwa wamewahi wao kuendelea na kuwa na mwamko wa kisasa.
Miongoni mwa maajabu ni kwamba Kusini mwa India na sehemu za mpaka wa Kaskazini wanaruhusu mke kuwa kwenye ndoa na zaidi ya mume mmoja; na utaratibu huu bado unaendelea hadi leo.1
وَلَا تُؤْتُوا السُّفَهَاءَ أَمْوَالَكُمُ الَّتِي جَعَلَ اللَّهُ لَكُمْ قِيَامًا وَارْزُقُوهُمْ فِيهَا وَاكْسُوهُمْ وَقُولُوا لَهُمْ قَوْلًا مَعْرُوفًا {5}
وَابْتَلُوا الْيَتَامَىٰ حَتَّىٰ إِذَا بَلَغُوا النِّكَاحَ فَإِنْ آنَسْتُمْ مِنْهُمْ رُشْدًا فَادْفَعُوا إِلَيْهِمْ أَمْوَالَهُمْ ۖ وَلَا تَأْكُلُوهَا إِسْرَافًا وَبِدَارًا أَنْ يَكْبَرُوا ۚ وَمَنْ كَانَ غَنِيًّا فَلْيَسْتَعْفِفْ ۖ وَمَنْ كَانَ فَقِيرًا فَلْيَأْكُلْ بِالْمَعْرُوفِ ۚ فَإِذَا دَفَعْتُمْ إِلَيْهِمْ أَمْوَالَهُمْ فَأَشْهِدُوا عَلَيْهِمْ ۚ وَكَفَىٰ بِاللَّهِ حَسِيبًا {6}
- 1. Kumbuka 'leo' hii 'mwaka jana' ni wa mwaka 1967 kilipoandikwa kitabu hiki - mfasiri