Aya 22 - 23:Walio Haramu Kuwaoa
Irabu
Yametangulia maelezo katika kufasiri Aya ya 3 ya sura hii kuwa herufi Ma pia hutumiwa kwa mwenye akili kama katika Aya hii: (Waliowaoa, baba zenu) kama ambavyo pia Man hutumiwa kwa asiyekuwa na akili; kama katika kauli yake Mwenyezi Mungu: Na wengine hutembea kwa matumbo yao (24:45) hapo ametumia neno Man kwa wanaotembea kwa matumbo ambao ni wanyama, hawana akili.
Watu wa 'Nahau' ni lazima wafuate Qur'an na wala sio kinyume. Ajabu ni kuwa wafasiri wengi wanafanya taawil katika Qur'an kwa sababu ya kauli ya watu wa Nahau, lakini hawabatilishi kauli ya watu wa Nahau kwa Qur'an.
Maana
Mwenyezi Mungu(s.w.t.) ameharamisha kuoa aina kadhaa za wanawake. Na uharamu wao uko mafungu mawili: Fungu la kwanza ni la uharamu wa milele, kwa maana ya kuwa hakuna mabadiliko; kama vile mtoto, dada, shangazi n.k. Fungu la pili ni lile la uharamu wa muda; kama vile mke wa mtu mwengine au dada wa mke n.k. Ufafanuzi ni kama ufuatavyo:
1. Wala msiwaoe waliowaoa baba zenu ila waliokwishapita.
Ilikuwa mtu anamuoa mke wa baba yake aliyekufa, ikiwa mke huyo si mama yake. Bali hata Umayya, babu wa Abu Sufiyan alimwacha mkewe, akamwoza mwanawe akiwa hai. Uislam umelikataza hilo kwa kulitilia mkazo na kulizingatia kuwa ni Uovu na chukizo na njia mbaya.
Mafakihi na wafasiri wameafikiana kuwa uharamu unaenea kwa wake wa mababu wa upande wa baba au mama; na kwamba uharamu huu unapatikana kwa kufungika ndoa tu, iwe kumepatikana kuingilia au la. Lakini wametofautiana kwa baba aliyezini na mwanamke, je utapatikana uharamu kwa mtoto wake? Shia Imamia, Hanafi na Hambal, wamesema ni haramu. Shafi akasema hakuna uharamu. Na Malik ana riwaya mbili.
2. Mmeharamishiwa mama zenu.
Yaani mumeharamishiwa kuwaoa mama zenu, wakiwemo nyanya zenu wa upande wa baba na mama
3. Na binti zenu
Na kuja chini; wajukuu na vitukuu, vilembwe na vinying'inya na kuendelea
4. Na dada zenu.
Dada na kaka hapa ni ndugu mdogo au mkubwa; ni sawa wawe ni baba mmoja au mama mmoja, atakuwa haramu. Lakini ni halali kuoa dada wa dada na dada wa kaka, akiwa siye dada.
Mfano wa hayo ni kuwa wewe una mtoto aitwaye Rauf, uliyezaa na mke mwingine ukamuoa mwanamke ambaye tayari amezaa na mume mwingine mtoto anayeitwa Hind, na Rauf naye akamuoa Hind.
Sasa wewe na mamake Hind mkizaa mtoto atakuwa ni kaka wa sehemu mbili, ni kaka wa Rauf kwa upande wa baba yake na kaka wa Hind kwa upande wa mama yake kwa hiyo Rauf atakaua ameoa dada wa dada yake na Hind ameolewa na kaka wa kaka yake.
5. Na shangazi zenu.
Shangazi ni kila mwanamke ambaye ni dada wa mtu ambaye nasaba yako inarejea kwake moja kwa moja au kupitia ngazi. Kwa hiyo shangazi yako ni dada wa baba yako ambaye amekuzaa wewe moja kwa moja. Shangazi wa baba yako ni dada wa babu yako ambaye amekuzaa wewe kupitia ngazi moja (baba yako) na shangazi wa babu yako ni dada wa baba wa babu yako ambaye amekuzaa wewe kupitia ngazi mbili (babu na baba) na kuendelea wote hao ni haramu.
Vilevile ni haramu shangazi wa mama yako. Kwa sababu yeye ni dada wa baba wa mama yako ambaye amekuzaa wewe kupitia ngazi moja (mama) na kuendelea. Ni halali kumuoa binti wa shangazi na wa ammi Kwa sababu yeye siye dada wa aliyekuzaa wewe. Bali ni binti wa kaka yake au dada yake.
6. Na khalati zenu
yaani dada za mama zenu. Ni kila mwanamke ambaye ni dada wa mtu ambaye nasaba yake inarejea kwako moja kwa moja au kupitia ngazi. Kwa hiyo khalat wako ni dada wa mama yako ambaye amekuzaa wewe moja kwa moja.Vilevile khalat wa mama yako ni dada wa nyanya yako ambaye amekuzaa wewe kupitia ngazi moja (mama yako) vile vile khalat wa baba yako hakuna tofauti isipokuwa huyu ni dada wa babu na yule ni dada wa nyanya. Pia khalat wa nyanya yako ni dada wa mama wa nyanya yako ambaye amekuzaa wewe kupitia ngazi mbili (mama na nyanya) na kuendelea. Wote hao ni haramu Hata hivyo ni halali binti wa Khalat na wa mjomba, kwa sababu yeye si dada wa aliyekuzaa bali ni binti wa kaka au dada yake.
7. Na binti wa kaka na binti wa dada
Na kuendelea chini
8. Na mama zenu waliowanyonyesha na dada zenu wa kunyonya.
Wameafikiana kwa kauli moja kuitumia Hadith hii: "Ni haramu kwa kunyonyesha yale yaliyo haramu kwa nasaba." Kwa hivyo kila mwanamke aliye haramu kumuoa kwa nasabu atakuwa haramu pia kwa kunyonya, awe ni mama, dada au binti. Vile vile shangazi, khalat, binti wa kaka au binti wa dada.
Wametofautiana katika idadi ya kunyonyesha inayowajibisha uharamu. Shia Imamia wamesema ni manyonyesho kumi na tano kamili, ambayo hayakuingiliwa kati na nyonyesho la mwanamke mwengine. Au kunyonya mtoto mchana mmoja na usiku wake kwa sharti ya kuwa lishe yake katika muda huu iwe ni maziwa ya huyo mwanamke tu.
Shafii na Hambal wamesema, hapana, yawe ni manyonyesho matano kwa uchache. Hanafi na Malik wamesema kuwa uharamu unapatikana kwa kunyonyesha tu, kuwe kwingi au kuchache. Kuna masharti mengine ya kunyonyesha tumeyataja kwa ufafanuzi katika kitabu
Ahwalush-Shakhsiyya Alal-madhahibil Khamsa.
9. Na mama wa wake zenu.
Wameafikiana kuwa mama wa mke (mama mkwe) na kuendelea juu, ni haram mara tu ukifunga ndoa na binti yake hata kama hukumwingilia.
Amekua pekee yule aliyesema kuwa kufunga ndoa tu, hakuharamishi mama mkwe mpaka aingili- we binti na akatoa dalili kwa Aya hii pale alipolifanya neno ambao mmewaingilia kuwa ni sifa ya mama za wake na wana wa kambo. Lakini mafakihi wamempinga kwa kauli hii kuwa sifa inamrudia aliye karibu zaidi na kwa Hadith sahihi kutoka kwa Mtume Mtukufu (s.a.w.). Aina zote hizo zilizotajwa ni haramu milele.
10. Na binti zenu wa kambo walio katika ulinzi wenu, waliozaliwa na wake zenu mliowangilia, iwapo hamkuwaingilia hapana vibaya juu yenu.
Wameafikiana kuwa binti wa mke hawi haramu kwa kufunga ndoa tu na mama yake bila ya kumwingilia. Kwa hivyo inajuzu kwake kumtaliki mama kabla ya kumwingilia kisha kumuoa binti yake. Walio katika ulinzi wenu, haina maana kuwa wasio katika ulinzi wenu ni halali. Kwani binti wa kambo ni haramu tu hata kama hayuko chini ya ulinzi wa baba wa kambo. Imetajwa ulinzi kwa kubainisha kuwa aghlabu inakuwa hivyo.
Hanafi na Malik wamesema kugusa na kutazama kwa matamanio kunawajibisha uharamu, sawa na kuingilia. Shia Imamiya, Shafi na Hambal wamesema hakuna uharamu ila kwa kuingilia wala kugusa na kutazama hakuna athari ya kusababisha uharamu hata ikiwa ni pamoja na matamanio.
Wameafikiana kuwa hukumu ya kumwingilia mwanamke kwa kutatizika ni kama hukumu ya kuingilia kwa ndoa sahih katika yaliyotajwa. Maana ya kuingilia kwa kutatizika ni kuingiliana mwanamke na mwanamume kwa kufikiria kuwa ni mke na mume washaria, halafu ikabainika kuwa ni watu kando.
11. Na wake wa watoto wenu waliotoka katika migongo yenu
Wameafikiana kuwa mke wa mtoto na wa mjukuu, na kuendelea chini, ni haramu kwa baba, babu na kuendelea juu, hata kwa kufunga ndoa tu bila ya kumwingilia. Neno "kutoka katika migongo yenu," ni mtoto wa kumzaa mwenyewe, si mtoto wa kupanga yaani asiwe wa kulea. Ama mtoto wa kunyonya hukumu yake ni kama hukumu ya mtoto wa kumzaa, kutokana na Hadith: Ni haram kwa kunyonya yaliyo haramu kwa nasaba.
12. Na kukusanya kati ya dada wawili isipokuwa wale waliokwishapita.
Wameafikiana katika uharamu wa kukusanya dada wawili. Lakini kama mume akifarikiana na mkewe kwa kifo au talaka, basi inajuzu kumwoa dada yake.
Imamia na Shafii wanasema kuwa mtu akimwacha mkewe talaka rejea, basi hai-juzu kufunga ndoa na dada yake mpaka eda ishe. Ama ikiwa ni talaka isiyokuwa rejea, basi inajuzu kumwoa dada yake katikati ya eda. Kwa sababu ni talaka isiyo na uwezekano wa kurejeana.
Madhehebu mengine yamesema kuwa haijuzu kufunga naye ndoa ila baada ya kwisha eda, bila ya kutofautisha talaka rejea na nyengineyo.