read

Aya 128 – 129: Huna Lako Jambo

Maana

Huna lako jambo.

Huenda waislamu kwa sababu ya kumtukuza Mtume wa Mwenyezi Mungu, wakadhani kwamba ametia mkono katika yaliyotokea Badr au wangeshindwa. Ndipo Mwenyezi Mungu akayaondoa mawazo haya kwamba mambo yote ni ya Mwenyezi Mungu peke Yake. Hakika Qur'an imesisitiza sana katika Aya kadhaa kwamba Muhammad (s.a.w) ni mtoa bishara na muonyaji tu; ni mfikishaji wa hukmu za Mwenyezi Mungu kwa waja Wake. Sio mbali kuwa hekima ya kukaririka huku na kutilia mkazo ni kwamba waislamu wasiingie ndani sana kuhusu Mtume wao kama walivyofanya wakristo kumhusu Bwana Masih (a.s.).

Au awatakabalie toba yao au awaadhibu, kwa sababu wao ni madhalimu.

Kauli hii inaungana na ile iliyosema au awadhalishe, yaani amri yote ni ya Mwenyezi Mungu; ama awatakabalie toba watakaposilimu au awaadhibu waking'ang'ania ukafiri, kwa sababu wao wanastahili adhabu kwa dhuluma yao; yaani ukafiri wao.

Na ni vya Mwenyezi Mungu viliyomo mbinguni na vilivyomo ardhini.

Ambaye ana ufalme wa mbingu na ardhi ni hakika kuwa na amri zote wala hakuna chochote anachoshirikiana na mwengine.

Humsamehe amtakaye na humwadhibu amtakaye.

Mara nyingi tumetaja kwamba akili inahukumu kuwa kafiri anastahili adhabu, laki- ni sio kuwa analazimika nayo; bali Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anaweza kumsamehe. Kwa ajili ya hekima fulani hata kama anastahili adhabu; sawa na unavyomsamehe anayekufanyia uovu au kumsamehe unayemdai. Na rehema na usamehevu kutokana na Mwenyezi Mungu ndio zaidi kutokana na fadhila Yake na ukarimu Wake.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَأْكُلُوا الرِّبَا أَضْعَافًا مُضَاعَفَةً ۖ وَاتَّقُوا اللَّهَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ {130}

Enyi ambao mmeamini msile riba ziada juu ya ziada. Na mcheni Mwenyezi Mungu ili mpate kufaulu.

وَاتَّقُوا النَّارَ الَّتِي أُعِدَّتْ لِلْكَافِرِينَ {131}

Na uogopeni moto ambao umeandaliwa makafiri.

وَأَطِيعُوا اللَّهَ وَالرَّسُولَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ {132}

Na mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume ili mpate kurehemiwa.

وَسَارِعُوا إِلَىٰ مَغْفِرَةٍ مِنْ رَبِّكُمْ وَجَنَّةٍ عَرْضُهَا السَّمَاوَاتُ وَالْأَرْضُ أُعِدَّتْ لِلْمُتَّقِينَ {133}

Na harakisheni kuomba msamaha kwa Mola wenu na pepo ambayo upana wake ni mbingu na ardhi imeandaliwa wamchao.